Wednesday, October 11, 2017

SIMULIZI, TAMAA MBELE MAUTI NYUMA SEHEMU YA 2

TAMAA MBELE, MAUTI NYUMA 2 inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya mabasi ya Raqeeb Luxury Coach ifanyazo safari zake Tanga Arusha na Arusha Tanga kila siku, kwa mawasiliano, 0655 902929

ILIPOISHIA

Dastan alilipita gari hilo na kwenda kusimama mbele, mahali ambapo palikuwa na kiza kilichotokana na mti wa muarubaini uliokuwa umeota pembeni mwa barabara.

Ili aweze kuwaona vizuri, aliigeuza pikipiki yake ielekee upande ule aliotokea na kuendelea kuwatupia macho watu hao.

Aliwaona wawili hao wakishuka kwenye gari na msichana akafungua mlango wa ile nyumba na kuingia ndani na mtu huyo.

Dastan aliendelea kusubiri kuona kama wangetoka tena. Ukapita muda mrefu. Wakati inakaribia kuwa saa tano usiku Dastan aliona taa ya mbele ya nyumba hiyo ikizimwa, kukawa kiza. Lakini kulikuwa na mwanga hafifu uliotoka katika nyumba za jirani.

Baadaye Dastan alimuona yule msichana ametoka peke yake. Akaangalia kila upande. Mtaa huo ulikuwa kimya na hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akipita.

SASA ENDELEA

Msichana akarudi ndani. Baada ya muda kidogo alitoka tena sasa akiwa anamburuza chini yule jamaa aliyeingia naye ambaye upande wake wa kichwani ulikuwa umetapakaa damu.

Alikuwa amemshika mabega yake akimburuza na kutoka naye nje. Aliendelea kumburuza hadi kwenye gari lake. Akafungua boneti la nyuma la gari lake. Akajaribu kuubeba mwili wa mtu huyo ambao haukuonesha dalili yoyote ya kuwa hai, akautia kwenye boneti la gari kisha akalifunga.

Baada ya hapo msichana huyo alikwenda kufunga mlango wa nyumba kisha akajipakia kwenye gari na kuondoka.

Gari hilo lilikuwa linakwenda  upande ule aliokuwa Dastan. Dastan aliwasha pikipiki akaigeuza na kuiondoa haraka kuelekea kule kule lilikoelekea gari hilo.

Alikuwa amelitangulia gari hilo ambalo halikuwashwa taa za mbele. Dastan naye hakuwasha taa za mbele wala nyuma. Alihofia kuwa kama msichana huyo angemuona angegundua kuwa alikuwa anamchunguza.

Dastan aliuvuka mtaa uliokuwa mbele akaendelea kwenda huku mara moja moja akitazama nyuma.

Akaliona gari hilo likikata upande wa kulia nyuma yake. Ulikuwa ni ule mtaa aliouvuka. Dastan akaigeuza pikipiki na kulifuata. Alikata upande ulioelekea gari hilo akaliona limesimama chini ya vivuli vya miti. Upande wa kulia wa mahali liliposimama kulikuwa na makaburi yaliyokuwa yamezungushiwa ukuta.

Dastan naye akasimamisha pikipiki yake pembeni mwa barabara kwenye kivuli cha mti.

Alimuona yule msichana akifungua boneti la nyuma la gari lake akautoa mwili wa yule  mtu na kuutupa chini. Baada ya kulifunga boneti aliuburuza ule mwili hadi kwenye ule ukuta uliozunguka makaburi akauacha mwili huo  na kurudi kwenye gari. Akaliwaha na kuondoka.

Gari hilo lilipoondoka Dastan aliiendesha pikipiki hadi mahali hapo akaumwilika ule mwili kwa taa za pikipiki yake na kugundua kuwa alikuwa ni yule jamaa aliyeondoka na yule msichana kule hoteli na kutokana na damu iliyokuwa imeenea kichwani mwake alihisi alikuwa ameshakufa.     

Dastan alishuha pumzi akatazama barabarani kuona kama angeliona tena lile gari la msichana lakini hakuliona tena. Akaondoka mahali hapo.

                                           **********

Dastan Seseko alikuwa fundi maarufu wa kompyuta. Ofisi yake ilikuwa mtaa wa barabara nane mkabala na barabara ya Taifa. Alikuwa akishirikiana na fundi mwenzake Ali Msela.

Wote wakiwa vijana waliohitimu kutoka chuo cha Veta na kuamua kujiajiri wenyewe, walikuwa wanatoka katika familia tofauti. Ali alikuwa anatoka katika familia ya kawaida yenye baba na mama akiwa na asili ya Tanga.

Dastan alitoka katika kituo kimoja cha yatima  mjini humo ambacho mbali ya kumlea tangu alipokuwa mdogo pia kilimpatia elimu kuanzia ya msingi, ya sekondari hadi Chuo cha Veta. Hakuwa akimjua baba yake wala mama yake.

Dastan alipomaliza msomo ya Veta ndipo alipoanza kujitegemea mwenyewe na kupangisha chumba eneo la Chumbageni.

Tangu alipoanza kujiajiri mwenyewe akishirikiana na Ali Msela aliyekutana naye Veta, Dastan aliona maisha yake yalikuwa yakielekea kuwa mazuri. Kipato alichokuwa anapata kilitosha kumuwezesha kimaisha.

Baada ya kuona alikuwa amefikia umri wa kuwa na mke, Dastan  alianza kutafuta mchumba. Akiwa katika harakati hizo ndipo alipokutana na msichana aliyeona kuwa angefaa kuwa mke wake.

Lakini katika kumfuatilia akakutana na tukio ambalo  hakukitegemea.


Tangu siku ile Dastan alijiambia suala la kuchagua mchumba si la kuchukulia kimzaha. Kwa mtindo aliokuwa ameutumia angeweza kujikuta anapoteza maisha yake kama alivyomuona mwenzake ambaye aliingia nyumbani kwa yule msichana akiwa mzima na kutoka akiwa maiti.

Wiki moja baada ya tukio hilo Dastan alikuwa amekaa katika chumba chake cha kazi akishughulikia kompyuta iliyokuwa na tatizo la kuwekewa program.

Mwenzake Ali alikuwa akiunganisha nyaya za kompyuta nyingine.

Ghafla waliona gari likisimama mbele ya duka lao. Akashuka msichana ambaye Dastan alipomuona tu, moyo wake ulishituka. Alikuwa ni yule msichana aliyemuua mtu wiki moja iliyopita. Alikuwa ameshika laptop mkononi.

Mara tu baada ya kushuka kwenye gari alitembea kuelekea kwenye mlango wa duka hilo. Dastan alikuwa akimkodolea macho.

Alipoingia ndani ya duka hilo aliwasalimia kisha akaiweka laptop yake juu ya meza kubwa aliyokuwa kando ya mlango.

“Lapto yangu ina tatizo” akasema huku akimtazama Dastan aliyekuwa upande wa pili wa meza hiyo.

“Ina tatizo gani?” Dastan alimuuliza huku akimtazama kwa macho ya tashiwishi.

“Haiwaki, sijui ni kwanini?”

Dastan aliikamata laptop hiyo akaifungua na kujaribu kuiwasha. Laptop haikuwaka.

“Itabidi tufungue tujue tatizo lake. Tuachie tutaishughulikia”

“Nije muda gani?”

“Njoo kesho, kwa muda huu tuna kazi  tulizokwisha zianza”

“Kesho, nije saa ngapi?”

“Njoo saa sita mchana”

“Sawa. Nitakuja muda huo”

Msichana akageuka na kuondoka. Dastan alimsindikiza kwa macho hadi alipokuwa anaondoka na gari lake. Alitaka kumueleza mwenzake kuhusu aliyoyashuhidia kwa msichana huyo wiki moja iliyopita lakini akanyamaza.

Kilichomfanya abaki kimya ni kuwa kulikuwa na taarifa ya polisi katika vyombo vya habari iliyoeleza juu ya kupatikana kwa mtu aliyekutwa ameuawa kando ya eneo la makaburi katika mtaa mmoja wa eneo la Bombo.

Taarifa hiyo ambayo ilitolewa kwenye vyombo vya habari siku tatu baada ya tukio lile, ilieleza kwamba mtu huyo asiyefahamika ambaye alikutwa asubuhi akiwa ameuawa alikuwa na jaraha kichwani lilionesha kuwa alipigwa na kitu chenye ncha kali.

Dastan aliogopa kueleza kuwa aliliona tukio hilo kwa vile mtuhumiwa mwenyewe alikuwa hajakamatwa, akaamua kunyamaza kimya.

Mara tu michana huyo alipoondoka, Dastan aliifungua ile laptop na kugundua kuwa ilikuwa na tatizo dogo. Kulikuwa na kiwaya kilichokuwa kinasambaza umeme kwenye mashine yake, kilikatika. Alikiunganisha na laptop ikawaka hapo hapo.

Latop ilipowaka Dastan aliingia katika chumba cha ndani na kuanza kuipekua. Alikuta taarifa mbali mbali za kidaktari pamoja na picha zilizoonesha maeneo mbali mbali ya ndani ya mwili wa mwanaadamu ambayo yalikuwa yakielezewa kitaalamu.

Dastan alijiuliza yule msichana anafanya kazi gani? Kwanini laptop yake ina maelezo ya kidaktari na ina picha za viungo vya binaadamu?

Akafikiria kwamba huenda msichana huyo alikuwa akiua watu na kuchomoa viungo vya ndani ambavyo huviuza.

Baada ya kuoma taarifa hizo ambazo hata hivyo hakuweza kuzielewa, Dastan aliizima laptop akaiweka na kwenda kuendelea na kazi yake.

Siku ya pili yake saa sita mchana msichana akawasili tena. Laptop yake ilikuwa juu ya meza.

Baada ya kuwasalimia mafundi hao, alimuuliza Dastan.

“Laptop yangu ipo tayari?”

“Ipo tayari” Dastan alimjibu kwa kumchangamkia.

Aliifungua ile laptop akaiwasha. Msichana alipoona laptop yake inawaka alitabasamu.

Dastan alidhani msichana angemuuliza ilikuwa na tatizo gani, swali ambalo mafundi wengi hawalipendi. Lakini msichana hakuuliza swali hilo.

Aliishika laptop yake na kuingia kwenye program ambazo alitaka kuzijaribu. Aliporidhika akaizima.

“Ni kiasi gani?” akauliza.

Dastan akamtazama. Alimuhisi alikuwa msichana mrembo na mwenye ubinaadamu wa hali ya juu.

Wakati akimtazama, Dastan alikumbuka kwamba siku chache zilizopita msichana huyo aliua mtu na kwenda kuutupa mwili wake kwenye eneo la makaburi.

Akajiambia pengine urembo wake na ubinaadamu wake ulionekana kwa nje tu, kwa ndani yake alikuwa msichana katili na dhalimu.

Dastan alitaka amwambie ampe shilingi elfu ishirini lakini akabadili mawazo.

“Nipe elfu kumi” akamwambia.

Msichana alifungua mkoba wake akachomoa noti ya shilingi elfu kumi akampa Dastan.

“Asante”

Msichana allichukua laptop yake akawaaga mafundi hao na kuondoka. Dastan aliendelea kumtazama msichana huyo hadi alipojipakia kwenye gari yake na kuondoka.

Hata baada ya msichana kuondoka, Dastan aliendelea kujiuliza ni kitu gani kilitokea siku ile kati ya yule jamaa aliyeuawa na msichana huyo.

Akajiuliza tena kama watu hao walikuwa wakijuana au walikutana siku ile kwa mara ya kwanza.

“Inawezekana kwamba walikuwa wanajuana, isingekuwa rahisi kwa msichana kumpeleka nyumbani kwake mwanaume aliyekutana naye siku hiyo hiyo” Dastan akajiambia.

Hata kama walikuwa wakijuana, Dastan aliendelea kujiambia, Ni mtafaruku gani uliwatokea hadi msichana huyo alimuua mwenzake?

Zikapita tena wiki mbili. Siku hiyo Dastan aliamka asubuhi na kuona mwili wake ukimuuma na pia alikuwa akisikia kizunguzungu. Akahisi kwamba alikuwa na malaria.

Alipomudu kuinuka kitandani ilikuwa saa tatu. Wakati anavaa baada ya kuoga, mwenzake alimpigia simu.

“Habari ya asubuhi Dastan?” Ali alimsalimia baada ya Dastan kupokea simu.

“Nzuri. Sikuamka vizuri leo, najisikia kuumwa”

“Oh nini zaidi?”

“Nahisi nina malaria, huenda nisifike kazini leo”

“Sasa nenda kapime, kama ni malaria upate matibabu”

“Nikitoka hapa nakwenda hospitali”

“Sawa. Utanijulisha itakavyokuwa”

Baada ya kuzungumza na Ali, Dastan alitoka akapanda pikipiki yake na kuelekea katika zahanati moja iliyokuwa barabara ya kwanza.

Aliegesha pikipiki nje akaingia ndani. Alisubiri watu wawili waliokuwa katika msitari wa kuingia katika chumba cha daktari. Watu hao waliposhughulikiwa akaingia.

Mshangao alioupata Dastan ulionekana wazi usoni kwake. Yule msichana aliyekuwa akimuwazia akilini mwake ndiye aliyekuwa daktari!

“Hujambo bibie?” akamsalimia.

“Sijambo, karibu ukae” Msichana akamkaribisha kisha akaongeza.

“Nakukumbuka fundi wangu wa laptop”

Dastan akatabasamu.

“Nafurahi kuwa umenikumbuka, sikujua kama wewe ni daktari”

“Mimi ni daktari na niko hapa. Una tatizo gain?”

Dastan akamueleza alivyojisikia.

“Inawezekana una malaria lakini nenda ukapime kwanza. Tunapimia chumba cha tatu. Baada ya kupima utarudi tena hapa”

“Sawa” Dastan alimjibu na kutoka.

Aliingia chumba cha tatu na kushughulikiwa tatizo lake. Kipimo chake kilionesha kuwa alikuwa na vidudu vine vya malaria. Baada ya kuandikiwa cheti alirudi tena katika chumba cha daktari.

“Hebu nione cheti chako” msichana alimwambia alipomuona akiingia.

Dastan alimpa cheti hicho kisha akaketi..

“Una vidudu vinne” Msichana alimwambia na kuongeza.

“Nitakuandikia dawa ambazo utatumia kwa siku tatu”

Msichana aliandika cheti kingine akamwambia Dastan.

“Jina lako tafadhali”

“Naitwa Dastan Seseko”

Itaendelea kesho hapahapa tangakumekucha usikose uhondo huu, KUMEKUCHA UPYA

No comments:

Post a Comment