Saturday, October 14, 2017

SIMULIZI, TAMAA MBELE MAUTI NYUMA SEHEMU YA 4

HADITHI hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni za mabasi ya Freys luxury Coacha na Raqeeb Luxury zifanyazo safari zake Tanga, hadi Singida kupitia Moshi, Arusha, Babati kila siku, na hufanya hivyo kila siku kuanzia Singida, kwa mawasiliano piga simu, 0622 292990

TAMAA MBELE, MAUTI NYUMA 4

ILIPOISHIA

“Ulisomea wapi ufundi wa kompyuta?”

“Nilisoma Veta”

“Hivi sasa unaishi wapi?”

“Ninaishi Chumbageni”

“Maisha yanakwendaje?”

“Kwa kweli yanakwenda vizuri”

“Uliwahi kuelezwa historia ni kwanini wewe umekuwa katika kituo kile cha kulelea yatima?”

“Nilielezwa. Kwa kweli ni historia ya kuhuzunisha”

Dastan akamueleza historia yake.  Alimwambia yeye na mdogo wake wa kike walifikishwa katika kituo hicho wakiwa wadogo sana.

Dastan aliambiwa alifikishwa katika kituo hicho akiwa na umri uliokadiriwa kuwa miaka mitano na mdogo wake akiwa na umri wa miaka mitatu.

Aliyewapeleka katika kituo hicho ni afisa ustawi wa jamii ambaye aliwaeleza viongozi wa kituo hicho kuwa mwanamke aliyekuwa na watoto hao alifariki dunia kwa ajali ya gari.

SASA ENDELEA

Aliwaeleza kwamba mwanamke huyo akiwa na watoto hao walishuka kutoka katika basi lililotoka Nairobi nchini Kenya na walipanda teksi ambayo ilipata ajali ya kugongwa na lori.

Mwanamke huyo na watoto hao walikimbizwa hospitalini lakini saa chache baadaye mwanamke huyo alifariki dunia.

Kabla ya kufa aliwahi kutoa maelezo kuhusu mahali alikokuwa akitoka na watoto hao. Alisema yeye alikuwa Mtanzania na watoto hao alikuwa akiwalea huko Nairobi akiwa mfanyakazi wa ndani kwa mtu mmoja aliyemtaja kwa jina la James Omondi

Alisema watoto hao alipewa na mtu huyo awalee na kuwafanya kama watoto wake.

Aliwatajia majina ya watoto hao. Mtoto wa kiume alikuwa Dastan lwanzo Seseko na wa kike Hilda Lwanzo Seseko.

Juhudi za  maafisa wa ustawi wa jamii kumpata James Omondi kutoka Nairobi ili atoe maelezo kuhusu watoto hao zilishindikana na hivyo watoto hao wakapelekwa kituo cha kulelea yatima kilichoko Kange nje kidogo ya jiji la Tanga.

“Kwa hiyo baada ya wewe kuondoka katika kituo hicho, mdogo wako yuko wapi?” Msichana huyo akamuuliza Dastan.

“Mdogo wangu tulitengana tangu tukiwa wadogo na sijamuona tena” Dastan alimwambia.

“Mlitengana vipi?”

“Niliambiwa  kuwa miezi michache tu baada ya kufikishwa katika kituo kile, mdogo wangu alichukuliwa na tajiri mmoja kwa nia ya kwenda kumlea na kumpatia elimu. Na atakuwa amekulia huko huko na kwa sasa si rahisi kumjua tena”

“Lakini bila shaka utakuwa una hamu ya kumuona mdogo wako?”

“Lazima. Si najua mtu ni ndugu yake”

“Nafurahi kukufahamisha kuwa mimi ndiye mdogo wako Hilda Lwanzo Seseko”

Mwili wa Dastan ulisisimka, akamkazia macho msichana huyo kama vile ndio kwanza alikuwa anamuona.

“Wewe ni Hilda?” akamuuliza kwa mshangao.

Msichana alifungua pochi yake akatoa kitambulisho chake na kumpa Dastan.

Dastan alikitazama na kuiona picha ya msichana pamoja na jina lake Hilda Seseko.

Akajikuta akiinuka kwenye kiti na kumfuata msichana huyo akiwa ameichanua mikono yake. Msichana akasimama, wakakumbatiana.

Baada ya hapo Dastan alirudi kwenye kiti.

“Kilichonitambulisha ni pale hospitali uliponitajia jina lako” Msichana alimwambia.

“Sasa ulinijuaje wakati ulichukuliwa ukiwa  mdogo?”

“Ni hivi karibuni tu nilipogundua. Wale watu walionilea ndio niliokuwa nikijua ni wazazi wangu. Walinichukua mimi kwa sababu hawakujaliwa kupata mtoto. Baba alitangulia kufariki akabaki mama. Mama naye akapata ugonjwa wa moyo

“Siku chache kabla  ya mama  kufa akaniammbia kuwa wao hawakuwa wazazi wangu halisi bali ni wazazi wa kunilea tu, akanipa historia yote. Kule walikonichukua waliambiwa kuwa nilikuwa na ndugu yangu wa kiume anaitwa Dastan Lwanzo Seseko. Hapo ndipo nilipokujua”

“Sawa. Kwa hiyo wazazi waliokulea wote wameshafariki?”

“Mama alikufa mwaka jana wakati tayari nimeshaanza kazi ya udakatari. Baba alikufa wakati nikiwa chuo nikisomea udaktari”

“Sasa kwanini hukurudi tena kwenye kituo kuniulizia kaka yako?”

“Kilichotokea ni kwammba wale wazazi wangu walinificha wakati wote kuniambia ukweli huo. Mimi nilijua wao ndio wazazi wangu. Kwa hiyo sikujua kama nilikuwa na ndugu huko hadi mama aliponifichulia”

“Na alipokufichulia kwanini hukuja kuniulizia?”

“Kwanza mama aliponieleza nililia sana. Halafu nilikuja katika kile  kituo kukuulizia. Kumbukumbu zikaonesha kwamba kweli nilitoka katika kituo kile, lakini wewe ulikuwa umeshaondoka na haawakujua uko wapi”

Dastan na msichana huyo waliletewa chakula walichokuwa wameagiza wakaosha mikono na kuanza kula.

“Mimi baada ya kumaliza masomo ya Veta nilifungua duka langu la ufundi wa kompyuta pale barabara ya nane nikishirikiana na mwenzangu ambaye ulinikuta naye siku ile” Dastan akamwambia msichana huyo.

“Nilikuwa nikikuwaza sana. Nilikuwa sijui kaka yangu unaishi maisha gain. Leo hii najisikia kuwa na furaha isiyo kifani”

“Uliniambia unaishi eneo la Bombo, ile nyumba unayoishi ni ya nani?”

“Ni yangu. Niliirithi kwa wale wazee walionilea, hawakuwa na mtoto mwingine wa kuwarithi. Tukitoka hapa tutakwenda nyumbani kwangu ukapaone”

Lile tukio la siku ile la yule mtu aliyeuawa na Hilda bado lilikuwa likizunguka akilini kwa Dastan.

“Kuna kitu kimoja nataka kukuuliza Hilda”

“Kitu gani?”

“Kuna siku moja ulikuja hapa hoteli mida kama hii halafu nilikuona wewe ukiondoka na jamaa mmoja. Mimi niliwafuatilia kwa pikipiki yangu. Niliwaona mkiingia katika nyumba moja katika eneo la Bombo, baadaye nikaona unamburuza yule mtu na kumpakia kwenye buti ya gari na kwenda kumuacha katika eneo la makaburi nyuma ya ule mtaa”

Msichana akagutuka.

“Kumbe uliona?”

“Nilikuona na nilipata hofu sana”

Msichana alinyamaza kimya kwa sekunde kadhaa kisha alisema.

“Yule mtu nilikutana naye kwa mara ya kwanza katika eneo la stendi. Alionesha kama alitaka tuwe marafiki. Lakini kadiri nilivyomzoea nilianza kugundua hakuwa mtu mwema na pia niligundua alikuwa anatoka Kenya.

“Kuna siku aliniambia dhamira yake. Aliniambia wazi kuwa alikuwa anamtafuta Dastan Lwanzo Seseko wakati tayari nilishaambiwa kuwa kuna kaka yangu anaitwa Dastan Lwanzo Seseko ambaye sijui aliko.

“Siku ile alikuwa amelewa na alinieleza kinaganaga kwamba anamtafuta Dastan amuue na kwamba alitumwa kutoka Nairobi na tajiri mmoja anayeitwa James Omondi.

“Aliniambia yeye ni Mkenya lakini ameshafika mara kadhaa hapa Tanzania na si mgeni wa jiji la Tanga. Nikamuuliza ni kwanini huyo Omondi amekutuma umuue huyo mtu, akanieleza kisa kirefu. Nisikilize kwa makini kaka yangu.

“Aliniambia alivyosikia kutoka kwa baadhi ya watu wanaomjua Omondi, mali aliyokuwa nayo Omondi si yake. Ni mali aliyotakiwa awarithishe Dastan na mdogo wake wa kike watakapofikia umri wa miaka kumi na minane.

“Lakini yeye aliwaondoa kwa hila Dastan na mdogo wake kutoka Nairobi na kuwapeleka Tanzania walelewe huko ili wakiwa wakubwa wasijue kuwa kuna mali wanayotakiwa kurithishwa.

“Hivi karibuni Omondi alipata habari kuwa Dastan ambaye ni wewe uko Tanga na wakati wowote unaweza kwenda Nairobi kudai hizo mali. Hapo ndipo Omondi alipotuma mtu kutoka Nairobi aje akuue.

“Ingawa wakati ule nilikuwa sijui uko wapi lakini baada ya kunieleza zile habari ndipo nilipomchukua nyumbani kwangu. Nilimpiga na chupa kichwani ili nimuue yeye kabla ya kuja kukuua wewe, kwa vile nilishajua kwamba wewe ni ndugu yangu na nilikuwa na tamaa kwamba iko siku tungeweza kukutana”

Hapo nikashusha pumzi ndefu.

Kumbe mimi ndiye niliyetakiwa kuuawa!

Kumbe Hilda alimuua mtu yule ili kuniokoa mimi!

Nilikuwa namtuhumu kwamba ni msichana muuaji kumbe sivyo!
Dastan alikuwa akiwaza akilini mwake.

“Sasa nimekuelewa vizuri. Lakini nikwambie licha ya kutojua kwamba wewe ni damu yangu sikumueleza mtu yeyote kuhusu tukio lile, nilinyamaza kimya” Nikamwambia Hilda.

“Ni kwa sababu ya damu. Damu nzito kuliko maji”

“Ni kweli. Sasa  kuna swali nimekuwa nikijiuliza. Huyo Omondi ni nani. Mimi pia nilielezwa kwamba huyo mama aliyetuleta hapa Tanzania alikuwa mfanyakazi wa nyumbani kwa Omondi na yeye ndiye aliyetutoa sisi tuje huku tulelewe na huyo mama. Halafu kumbe ametuma mtu aje aniue”

“Bahati nzuri yule mtu aliingia mikononi mwangu”

“Nashukuru sana kwa kuokoa maisha yangu. Pengine angenigundua na angeniua. Huyo mtu atakuwa ni jambazi”

“Zake zimeshakwisha. Nimekuwa nikijiuliza hizo mali alizonazo Omondi zinatuhusu vipi sisi”

“Mimi nashukuru kuwa tumekutana na tumejuana. Tunayo sababu sasa ya kutafuta asili yetu, kuwajua wazazi wetu na kumjua huyu Omondi pamoja na hizo mali”

“Ukiangalia hili jina la Lwanzo Seseko ambalo bila shaka ni la baba yetu, asili yake ni Congo. Bila shaka wazazi wetu ni watu wa Congo”

“Lakini tunaelezwa kuwa tulitokea Nairobi tukiwa wadogo. Omondi naye yuko Nairobi. Katika historia yetu fupi, lwanzo Seseko hatajwi, anatajwa Omondi. Kuna haja ya kuanza kufanya  utafiti”

Walikuwa wameshamaliza kula. Waliosha mikono. Hilda akalipa bili yote kisha wakatoka.

“Twende nyumbani” Hilda alimwambia Dastan akiwa amehamasika.

“Ile nyumba yako ninaifahamu. Panda gari yako, mimi nakuja na pikipiki”

“Sawa”

Hilda alikwenda kujipakia kwenye gari lake na Dastan alipanda pikipiki, wakaondoka.


ITAENDELEA kesho Usikose Uhondo huu hapahapa Kumekucha

No comments:

Post a Comment