HADITHI hii inakuja kwa hisani kubwa ya kampuni ya mabasi ya Abiria ya Raqeeb Luxury Coach ifanyayo safari zake kati ya Tanga na Arusha kila siku, siku mara 6 kuanzia saa 2 hadi saa 6, ofisi zao zoko barabara ya 12 Ngamiani Tanga mkabala na kituo cha mafuta cha Tapco, unaweza kuwasaliana nao kwa simu no, 0655 902929
TAMAA MBELE, MAUTI NYUMA…
(1)
NA FAKI A FAKI
Mbinguni kuna nyota tatu zilizofuatana katika mstari mmoja.
Ukitazama angani wakati wa usiku unaweza kuziona. Wahenga wanasema nyota hizo
zinaashiria kuwa tamaa kwa binaadamu iko mbele, mauti yako nyuma na binaadamu
yuko katikati.
Wakati binaadamu anaikimbiza tamaa na yeye anakimbizwa na
mauti!
Nyota hizo zinawakilisha ukweli kwamba siku zote binaadamu
anaongozwa na tamaa. Lakini amesahau kuwa mauti nayo yako nyuma yake!
SASA ENDELEA.
Shangwe Mpya ilikuwa moja ya hoteli maarufu jiji Tanga.
Haikuwa maarufu kwa sababu ya mandhari yake ya kupendeza au kuwa katika mtaa
ambao ni maarufu, ilikuwa maarufu kwa sababu ilikuwa hoteli ya miaka mingi.
Ilikuwa hoteli ya ghorofa moja tu iliyokuwa katika barabara
ya Eckenford. Pengine ilikuwa hoteli ambayo haikuvutia wageni kwani idadi ya
wageni waliofika katika hoteli hiyo haikuwa kubwa.
Hoteli
ya Shangwe Mpya ilivutia zaidi wenyeweji wa Tanga.
Sababu kubwa ni kuwa kulikuwa na vyakula vya kiasili na bei yake ilikuwa
nafuu sana. Pengine hilo ndilo lililofanya hoteli ya Shangwe Mpya kuwa
maarufu
sana.
Saa moja usiku Dastan Seseko aliisimamisha pikipiki yake
mbele ya hoteli ya Shangwe. Akaiegesha kwenye eneo la kuegesha pikiki na
kuelekea kwenye mlango wa kuingia hotelini humo.
Ilikuwa kawaida yake kwenda kula chakula cha jioni kila
ifikapo saa mbili usiku lakini usiku huo aliwahi kufika. Alikuwa na sababu moja
kubwa iliyomfikisha mapema mahali hapo.
Kwa siku tatu mfululizo kila alipofika hotelini hapo alikuwa
akikutana na msichana mmoja aliyekuwa akienda kula chakula cha jioni. Lakini
mara zote hizo Dastan anapofika, msichana huyo huwa ameshamaliza kula na
kutoka.
Hivyo usiku huo Dastan alifika mapema zaidi kuliko muda wake
ili aweze kumuona vyema msichana huyo.
Dastan aliingia katika eneo la wazi la hoteli ambalo
lilitapakaa viti na meza kwa ajili ya wateja.
Kwanza alizungurusha macho katika eneo hilo ambalo halikuwa na watu wengi muda huo.
Baada ya kutomuona msichana aliyekuwa akimtaka alitafuta meza ya pembeni na
kwenda kuketi.
Aliagiza nyama choma na juisi kisha akayaelekeza macho yake
kwenye mlango wa kuingia katika eneo hilo.
Aliamini kuwa msichana aliyesababisha afike mahali hapo
mapema angewasili wakati wowote.
Dastan alikumbuka siku ya kwanza alipomuona msichana huyo
alistushwa na umbile lake
pamoja na sura yake
jamali. Akajiambia hakuwahi kukutana na msichana aliyeugusa moyo wake kiasi
kile kama ilivyokuwa kwa msichana huyo.
Siku ya pili alimuona tena akitoka. Alipomtazama
alijiridhisha kuwa mawazo yake yalikuwa sahihi. Msichana huyo alikuwa mrembo na
mwenye mvuto.
Siku ya tatu alikutana
naye tena. Bahati mbaya siku zote hizo hakupata muda wa kutosha angalau
wa kumsalimia.
Ulikuwa ni upumbavu ambao ungeweza kumnasa mwanaume yeyote
anayekutana na msichana mrembo. Dastan alitaka kuzungumza naye na amueleze kuwa
alikuwa amempenda.
Wakati Dastan analetewa nyama choma aliyoagiza pamoja na bilauli
ya juisi akamuona msichana huyo akiingia. Moyo wake ulishituka kidogo akaacha
kuitazama sahani ya nyama choma na kumuangalia msichana huyo huku vyakela vyote alivyoagiza akivipiga pindu na kumwagika chini.
Alitamani aende akaketi katika meza aliyoketi yeye lakini
ilikuwa sivyo. Msichana alikwenda kukaa katika meza nyingine.
Wakati Dastan akiendelea kumtazama huku akisifia uzuri wake
alijiambia baada ya muda kidogo ataamisha makazi kwenye meza ya msichana huyo
ili aweze kuzungumza naye.
Msichana aliletewa nyama choma na ndizi za kuchoma. Wakati
anaanza kula, kuna jamaa aliingia na kwenda kukaa katika meza aliyokaa msichana
huyo. Kitendo hicho kilimkera Dastan na kumfanya ajilaumu kwa kuchelewa kwenda
kuketi yeye.
Baada ya muda kidogo aliwaona wawili hao wameingia katika
mazungumzo. Dastan alikuwa akiumia kimoyomoyo huku akienndelea kujilaumu.
Lakini baadaye kidogo alipata shaka kwamba watu hao huenda
walikuwa wanajuana kwani baada ya
kumaliza kula waliondoka pamoja.
Dastan alikuwa amemaliza kula kitambo baada ya kuagiza mlo mwengine baada ya ule wa awali kuupiga pindu. Baada ya kulipa bili
yake aliinuka na kuwafuata nje.
Aliwaona wakijipakia kwenye gari la msichana na kuondoka.
Kihoro kilikuwa kimemshika Dastan. Na yeye akawasha pikipiki
yake na kuwafuata.
Gari hilo
lilikamata barabara ya Eckenford, baadaye lilikata kushoto likaingia eneo la
Bombo. Dastan alikuwa bado akiwafuata nyuma.
Walilivuka daraja la Mkwakwani kisha wakakata kulia. Dastan
naye alikata kulia. Gari hilo
baada ya kuumaliza mtaa huo, lilikata kushoto na kusimama mbele ya nyumba moja
iliyokuwa upande wa kulia wa barabara.
Dastan alilipita gari hilo
na kwenda kusimama mbele, mahali ambapo palikuwa na kiza kilichotokana na mti
wa muarubaini uliokuwa umeota pembeni mwa barabara.
Ili aweze kuwaona vizuri, aliigeuza
pikipiki yake ielekee upande ule aliotokea na kuendelea kuwatupia macho watu
hao.
Aliwaona wawili hao wakishuka kwenye gari na msichana
akafungua mlango wa ile nyumba na kuingia ndani pamoja na mtu huyo.
Dastan aliendelea kusubiri kuona kama
wangetoka tena. Ukapita muda mrefu. Wakati inakaribia kuwa saa tano usiku,
Dastan aliona taa ya mbele ya nyumba hiyo ikizimwa, kukawa kiza. Lakini
kulikuwa na mwanga hafifu uliotoka katika nyumba za jirani.
Baadaye Dastan alimuona yule msichana ametoka peke yake.
Akaangalia kila upande. Mtaa huo ulikuwa kimya na hakukuwa na mtu yeyote
aliyekuwa akipita.
ITAENDELEA kesho hapahapa tangakumekucha, KUMEKUCHA UPYA
No comments:
Post a Comment