RIWAYA
KAMA UNATAKA FEDHA ZA MAJINI
4
ILIPOISHIA
Pia nilikuta chupa ambayo
ndani yake mlikuwa na yai zima lililoandikwa maandishi ya kiarabu kwa wino
mwekundu. Pia mlikuwa na talasimu iliyokuwa na picha ya mtu. Sikuweza kujua
lile yai liliingia vipi ndani ya ile chupa wakati mdomo wa chupa ulikuwa na uwazi
mdogo sana.
Mbali ya ile chupa kulikuwa
na kipande cha ubao mweusi uliokuwa na maandishi ambayo sikuweza kutambua
yalikuwa ya lugha gani, Kigiriki si Kigiriki, Kichina si Kichina! Pia kulikuwa
na vikorokoro vingine ambavyo sikuweza kuvielewa. Vitu hivyo kwa kweli
vilinishangaza.
Baada ya kuviangalia kwa
dakika kadhaa nilivirudisha ndani ule mkoba.
Nilichukulia kwamba
wazee wa zamani walikuwa na vikorokoro
vingi vya kiasili walivyokuwa wanavihifadhi kwa imani mbalimbali. Na kwa kweli
nisingeweza kujua baba yangu alikuwa amehifadhi vitu vile kwa sababu gani.
Nikaamua kuurudisha ule mkoba
mvunguni nilikoutoa. Mkoba huo haukushughulisha sana akili yangu. Akili yangu ilikuwa
imeshughulishwa zaidi na zile pesa. Nilipotoka pale chumbani nilitaka kurudi tena
chumbani mwangu nizitazame tena zile pesa kwenye lile sanduku la chuma lakini
nikajizuia. Niliona kama nilikuwa ninafanya jambo la kitoto.
SASA ENDELEA
Kwa vile sikuwa na kazi
nyingine ya kufanya nikaamua kukaa barazani mwa ile nyumba yetu na kupanga
mambo yangu. Jambo la kwanza nililolipanga ni jinsi ya kuondoka na zile pesa
kwenda nazo Dar.
Utata ulikuwa ni namna
nitakavyoweza kusafiri kwenye basi nikiwa na sanduku hilo
zito bila watu kujua kama lilikuwa na kiasi
kingi cha pesa.
Nilijiambia kwa vyovyote vile
lazima ningetiliwa mashaka na abiria wenzangu na kama sanduku hilo litafikishwa polisi na kufunguliwa,
polisi wangeshuku kuwa nilikuwa jambazi kwani wasingeamini kuwa pesa zile
nimezirihi kutoka kwa baba yangu.
Nikazidi kujiambia kuwa hata kama nitafika Dar na pesa hizo, nisingeweza kuzihifadhi
benki kwani nisingeweza kujieleza nimezipata wapi. Mwisho wake ningeangukia
mikononi mwa polisi na kutakiwa nijieleze vizuri.
Usiku ulipowadia nilikwenda
kula kwa mama lishe kwa vile nyumbani nilibaki peke yangu. Baada ya kula
chakula nikarudi nyumbani kulala.
Hata huo usingizi wenyewe
haukunijhjia. Nilikuwa nikiwaza zile pesa tu. Nakumbuka nilitazama saa yangu na
kuona ilikuwa
saa nane usiku nikatoka uani
kujisaidia kisha nikarudi kulala. Safari hii nilipofumba macho yangu tu
usingizi ukanichukua hapo hapo.
Vile napata usingizi tu ikanijia ndoto ya ajabu.
Nilimuota mwanamke mmoja wa kiarabu amekaa kwenye kiti kilichokuwa mle
chumbani.
Alikuwa mzuri sana. Mavazi yake ndiyo
yaliyonishitua. Alikuwa amevaa shuka nyeupe tupu huku miguu yake ikiwa
pekupeku. Kichwani alikuwa amejifunga kilemba cha rangi nyekundu.
Wakati namtazama huku
nikijiuliza mwanamke yule ametokea wapi, aliniuliza.
“Unanijua mimi?”
“Sikujui” nikamjibu.
“Mimi ndiye niliyekuwa mke wa
baba yako. Mimi ni mwanamke wa kijini. Jina langu ni Maimuna. Kwetu ni Kisima
cha Giningi Zanzibar”
Akaendelea kuniambia.
“ Baba yako alifika mahali
hapo kutafuta fedha za majini. Akakutana na Baba yetu aliyekuwa akitufuga, mzee
Habibu Sultani wakakubaliana kwamba ili baba yako apate fedha za majini
aozeshwe mke wa kijini miongoni mwa majini wanaokalia mali”
Huku nikimsikiliza kwa makini
mwanamke huyo aliendelea.
“Mzee Sultani akaniozesha
mimi kwa baba yako baada ya baba yako kukubaliana na masharti yetu. Masharti
yetu yalikuwa kwa kunioa mimi yeye atapata fedha za majini na atakuwa tajiri
lakini lazima amtoe kafara mke wake aliyekuwa naye awe dondocha. Na baada ya
miaka kumi amtoe kafara mtoto wake au mjukuu wake naye pia awe dondocha”
Wakati nikielezwa hayo nilikuwa
nimeduwaa nikimsikiliza mwanamke huyo ambaye aliendelea kunieleza.
“Sharti letu jingine lilikuwa
lazima amtaje mrithi wake ili nimjue mapema. Baba yako akakutaja wewe na ndio
sababu alipokaribia kufa alikwambia urithi wako uko mvunguni mwa kitanda.
“Zile pesa zilizomo kwenye
lile sanduku ni pesa zangu. Kila siku zinaongezeka. Zile hazizishi, utatumia
mpaka unakufa. Baada ya baba yako kutimiza
masharti yetu nilianza kumuingizia zile pesa kwenye sanduku mpaka hivi
sasa limejaa. Alimfanya mke wake dondocha na juzi juzi tu alimfanya dondocha
mjukuu wake, yaani mtoto wako”
“Ninavyojua mimi ni kuwa mama
yangu alikufa na mwanangu pia alikufa mwenyewe” nikamwambia mwanamke huyo.
“Hivyo ndivyo ilivyoonekana
kuwa watu hao wamekufa lakini hawakufa, wako hai. Ni kama vile wamechukuliwa
msukule. Mama yako na mwananao wako kule kwenye pango ambako baba yako alitaka
kukupeleka siku ile usiku lakini akafikwa na umauti.
“Watu hao wapo hai, wanaishi
katika pango lakini si wazima. Wote wawili ni mataahira wanaohitaji
kuhududumiwa kwa chakula. Chakula chao ni uji wa mapumba ya mahindi
uliochanganywa na asali ya nyuki. Baba yako alikuwa akiwapelekea uji huo saa
nane usiku kila siku. Wanakula usiku tu”
Mwanamke huyo alinyamza
akanitazama kabla ya kuendelea.
“Kwa vile wewe umerithi zile
pesa utanirithi na mimi na utawarithi na wale madondocha, yaani utakuwa
unawatazama wewe na kuwapa chakula chao kila siku.
“Na mimi kila wiki utakuwa
unaniingilia kimwili kama mke wako. Siku
unayopenda utakwenda kwenye kaburi lolote utavua nguo na kubaki uchi saa nane
usiku halafu mimi nitakuja hapo”
“Je kama nitakataa?”
nikamuuliza yule jini baada ya maelezo yake kunitia hofu.
“Huwezi kukataa. Hayo ndiyo masharti
ya sisi na baba yako. Lazima urihi zile pesa na ni lazima ukubaliane na yote
niliyokueleza” Mwanamke huyo aliniambia na kuongeza.
“Kingine nilichotaka
kukueleza ni kuwa kama vile ambavyo baba yako
alimtoa kafara mke wake na wewe utatakiwa umtoe kafara mke wako ili mama yako
aweze kufa kwa sababu muda wake umekwisha”
Loh! Yalikuwa maneno
yaliyonitisha sana.
Nimtoe kafara mke wangu awe dondocha? Na ni kwa sababu gani hasa? Kama ni pesa za majini aliyezitaka ni baba yangu ambaye
ameshakufa, mimi zinanihusu nini?
Hapo nikatikisa kichwa
kukataa.
“Sikubaliani na mashrti hayo.
Mimi siwezi kumtoa kafara mke wangu, siwezi kufanya ukatili huo”
“Huwezi nini, wakati hayo ni
makubaliano ya sisi na baba yako. Baba yako alituambia wewe utarithi pesa zile
na utatimiza mashrti tutakayokupa” Mwanamke huyo akaniambia kwa mkazo.
Nikaendelea kutikisa kichwa.
“Huwezi
kukataa kitu hapa. Kama umerithi zile pesa lazima utimize masharti
hayo. Kama utakataa tutamchukua wenyewe mke wako. Sasa nenda
kawape chakula wale madondocha, hawajakula tangu baba yako alipokufa”
Hapo hapo nikashituka
usingizini.. Nikatazama huku na huku, sikumuona
yule mwanamke aliyekuwa akiniambia maneno hayo.
Jasho lilikuwa limenisambaa
mwili mzima. Nikanyanyuka na kuketi kitandani.
Nikagundua kuwa nilikuwa
ninaota lakini huenda ndoto yenyewe ilikuwa
na ukweli unaotisha.
Kwa ndoto ile niligundua
marehemu baba yangu alikuwa akiishi na yule jini mwanamke ambaye alitaka
nimrithi.
Pia niligundua kuwa baba
yangu alikwenda eneo la Kisima cha Giningi huko Zanzibar kutafuta pesa za majini ndipo
alipokutana na Habib Sultan ambaye alimmilikisha yule jini pamoja na kumpa
masharti ya kupata utajiri.
Kumbe baba yangu alikuwa
akimiliki pesa za majini! Na pia alikuwa akiishi na mke wa kijini! Ndio maana
baada ya kufa mama yangu, baba hakuoa mke mwingine hadi mwenyewe alipofariki.
Lakini habari nyingine
iliyonishitua ni kuhusu kuwa hai kwa mama yangu na mwanangu Abdul. Nilichokuwa
ninakifahamu na kila mtu anakifahamu ni kuwa mama yangu alikufa, tena alikufa
baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Na kuhusu mwanangu ni hivyo
hivyo. Nilichokuwa ninakifahamu ni kuwa mwanangu alikufa.
Sasa ile habari kuwa watu hao
wako hai wamegeuzwa madondocha, ilinishitua sana.
Lakini wakati nafikiria zile
pesa, nikakumbuka kwamba mke wangu naye alikuwa kwenye hatari ya kufanywa
dondocha bila kutaka mimi mwenyewe.
Pesa zilikuwa tamu lakini
masharti yake yalikuwa magumu. Sikuweza
kujua marehemu baba yangu aliupata wapi ujasiri wa kuyakubali masharti yale.
Kusema kweli baada ya kuamka sikulala tena hadi asubuhi
kulipokucha. Baada ya kuoga na kuvaa nilichukua sime nikatoka kuelekea kule
kwenye pango ambako niliambiwa mama yangu na mwanangu walikuwa wamewekwa.
Nilifika hadi pale mhali
ambapo baba yangu alianguka na kufa
nikaendelea kwenda hadi nikaona ule mti ambao baba yangu aliniambia. Nikakata
kushoto. Baada ya mwendo mfupi nikakuta kichaka ambacho nilishuku ndio kile
nilichoambiwa kuwa ndani yake kuna pango.
Kitu kilichonipa moyo na
kuona kuwa mahali hapo palikuwa na watu nilisikia sauti za watu wanaolalamika.
Nikaingia ndani ya kile kichaka, nikaona pango.nililokuwa limezibwa kwa jiwe
kubwa. Sauti nilizokuwa ninazisikia zilikuwa zinatoka ndani ya pango hilo.
Nikaliondoa lile jiwe na
kulisukuma kando. Mlango wa pango ukawa wazi. Nikashika sime yangu mkononi na
kuingia. Mwanga wa jua ulikuwa umejipenyeza hadi ndani ya pango hilo na hivyo niliweza
kuona vyema.
Vile naingia tu, zile sauti
zikazidi. Nikamuona mama yangu na mwanangu wamewekwa chini kama
walemavu wakilia njaa. Walikuwa weusi kama waliopakwa lami na walikuwa
wamekonda sana kiasi kwamba walikuwa wanatisha
na kuonekana kama vinyago.
Walikuwa wamenikodolea macho
huku wamefungua midomo yao
kuashiria kuwa walikuwa wanataka kula. Kwa kweli walinitia huruma sana. Mambo yale
yalifanywa na baba yangu aliyekuwa ameshakufa lakini kama
angekuwa hai ningekwenda kumpiga sime nikamuua kwa hasira.
Baada ya kumuona mama yangu
na mwanangu wanavyolalamikia njaa, nikakumbuka kwamba nilikwenda kizembe mahali
hapo. Sikuwachukulia chakula chao nilichoagizwa. Nikageuka na kutoka mbio.
Nilirudi nyumbani nikawatayarishia
uji wa mapumba ya mahindi kama nilivyoagiwa kisha nikautia uji huo asali ya nyuki.
Sikuona vibaya kuwapelekea uji wa mapumba ya mahindi kwa sababu ni mzuri na
mimi mwenyewe niliwahi kuunywa mara nyingi.
Uji ulipoiva niliutia kwenye
chupa ya chai nikachukua vikombe viwili na kutoka mbio kurudi kule pangoni.
Niliingia kwenye lile pango
nikawamiminia uji kwenye vile vikombe na kuwapa. Walikuwa hawawezi kunywa
wenyewe. Walikuwa kama watu waliopooza. Ilibidi niwanyweshe. Uji ulikuwa moto
lakini walikunywa hivyo hivyo kwa sababu ya njaa.
Je nini kitatokea? Usikose kufuatilia kesho hapahapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment