Tuesday, October 17, 2017

SIMULIZI, TAMAA MBELE MAUTI NYUMA SEHEMU YA 7

TAMAA, MAUTI NYUMA 7

ILIPOISHIA

“Patel amekamatwa. Anatumiwa kusafirisha meno ya tembo nchi za nje”

“Kumbe yule bwana anafanya magendo ya meno ya tembo?”

“Nilikuwa nikisikia hivyo lakini leo ndio nimethibitisha”

“Sasa kesho mtakwenda kazini?”

“Tutakwenda. Kama duka halitafunguliwa tutarudi”

“Mimi sitaki kazi tena, nitatafuta mahali pengine. Kama tajiri mwenyewe ameshakamatwa sidhani kama tutakuwa  na ajira tena”

Lwanzo akawa amejiachisha kazi. Miezi michache baadaye akasikia kwamba tajiri yao huyo aliyekamatwa alihukumiwa na mahakama kifungo cha miaka kumi na mitano jela.

Wakati huo alikuwa bado ameficha zile dola. Baada  ya hapo ndipo alipoanza kuzitumia.

Kwanza alinunua mashamba ya mirungi huko Meru kisha akanunua magari mawili ya kusafirishia mihadharati hiyo kutoka Meru hadi jijini Nairobi na Mombasa.

SASA ENDELEA

Biashara hii ilimuinua mara moja. akanunua hoteli mbili. Alifungua maduka karibu kumi ya vifaa vya ujenzi na alinunua mabasi madogo ishirini aliyoyafanya daladala.

Mwenyewe alinunua nyumba ya kifahari ya ghorofa moja aliyokuwa akiishi. Pia alinunua gari la heshima la kutembelea.

Hakumsahau mwenyeji wake Omondi. Alimuachia zile daladala ishirini azisimamie yeye. Lwanzo alikuwa akichukua hesabu tu kutoka kwa Omondi.

Maisha ya Lwanzo yakawa yamebadilika sana. Alipokuja Nairobi kutoka Congo alikuwa mtu asiyefahamika. Lakini baada ya kupata utajiri akawa maarufu na kufahamika na wengi.

Omondi alipokuwa ameajiriwa kwa tajiri wa kihindi maisha yake yalikuwa duni thamani. Alipopatiwa kazi ya kusimamia magari ya Lwanzo na yeye aliinuka na kuonekana  mtu miongoni mwa watu.

Aliweza kujenga nyumba yake mwenyewe na kuwapeleka watoto wake katika shule za maana. Alimshukuru sana Lwanzo kwa kuweza kuyabadili maisha yake.

Siku moja Lwanzo alikuwa akipita na gari lake katika barabara moja jijini Nairobi. Alimkosakosa msichana mmoja aliyekuwa anavuka barabara bila kutazama magari. Alifanikiwa kumkwepa lakini pikipiki ikamkumba msichana huyo na kumtupa chini.

Mguu wake ukawa unavuja damu. Mwenye pikipiki hakutaka taabu na trafiki wa Nairobi. Alijua fika kwamba kosa halikuwa lake lakini trafiki wangembana yeye ili atoe pesa, akaamua kukimbia.

Kutokana na ubinaadamu wake Lwanzo alifunga breki akasimamisha gari. Alimfuata yule msichana ambaye bado alikuwa amelala chini akigwayagwaya , akamuuliza.

“Umeumia sana?”

“Mguu wangu unatoka damu” msichana alisema akiwa ameushikilia mguu wake.

“Inuka nikupeleke hospitali”

Msichana alijaribu kuinuka. Aliposhindwa Lwanzo alimsaidia kumuinua.

Akamkokota kuelekea lilipokuwa gari lake, akampakia na kwenda naye hospitali ya pesa.

Mguu wa msichana huyo ulipigwa picha na kugundulika kuwa ulikuwa umetenguka ukawekwa sawa na kuvalishwa plasta ngumu.

Pale palipokuwa na jeraha lililokuwa linavuja damu palisafishwa na kuwekwa plasta. Gharama zote alizilipia Lwanzo.

“Unaishi wapi nikupeleke?” Lwanzo akamuuliza wakati akimpakia tena kwenye gari.

“Pale nilipogongwa nilikuwa ninakwenda mahakamani lakini sasa nimeshachelewa”

“Ulikuwa na kesi?”

“Ndiyo nilikuwa na kesi na tarehe yake ilikuwa ni leo”

“Sasa acha nikufikishe mahakamani ili utoe taarifa kuwa ulipata ajali, vinginevyo unaweza kukabiliwa na kesi nyingine ya kudharau mahakama”

“Sawa. Nipeleke”

Wakati Lwanzo akimpeleka msichana huyo mahakamani alimuuliza.

“Umeshitakiwa kwa kosa gani?”

“Kosa la kuonewa tu na mwanaume. Amekwenda kunishitaki kuwa nilimuibia pesa zake shilinhgi laki tano (sawa na milioni kumi za Tanzania) wakati haikuwa kweli. Nilikamatwa kwa kudhalilishwa nikawekwa ndani siku mbili, siku ya  tatu nikapelekwa mahakamani. Ndipo nikapatiwa dhamana”

“Huyo mtu aliyekushitaki ni nani?”

“Mjinga mmoja. Alikuwa mchumba wangu halafu nikajakumfumania na rafiki yangu wa chanda na pete nikavunja uchumba. Sasa hicho ndicho kilichomuudhi. Yule msichana anaendelea naye mpaka leo na mimi simtaki tena

“Alisema ulimuibia wapi pesa hizo?’

“Kwanza alishaniambia kuwa atanikomoa. Kuna siku nilikwenda nyumbani kwake kuchukua nguo zangu zilizokuwa kwake, yeye hakuwepo lakini mwanamke wake alikuwepo, tukagombana sana. Kwa vile mwenyewe hakuwepo sikuchukua kitu lakini siku ya pili yake akaniletea polisi nyumbani kwangu akidai kuwa nilimuibia shilingi laki tano. Yaani lengo lake anifunge”

“Huyo jamaa ni mpumbavu, akishakufunga atapata faida gani?”

“Si bado ananitaka na mimi simtaki tena. Sasa anataka kunikomoa”

“Huyo rafiki yako bado anaendelea naye?”

“Bado yuko naye”

“Abaki na huyo, kwanini anataka kukukomoa wewe?”

“Ni mwanaume mjinga na mpumbavu, yaani najuta kumfahamu. Yeye ndio amesababisha nigongwe na pikipiki kwa sababu nina uchungu mpaka sijielewi”

“Tulia. Nitakusaidia”

Msichana huyo aliposikia kauli hiyo ya Lwambo aliugeuza uso wake akamtazama usoni.

“Utanisaidiaje kakaangu?” akamuuliza.

“Nitakuwekea wakili”

“Wakili atakuwa na gharama kubwa”

“Ninajua”

Msichana akanyamaza kimya.

Lwanzo alimfikisha mahakamani. Alishuka naye kwenye gari na kuingia naye kwenye jengo la mahakama. Msichana akajitambulisha kwa makarani wa mahakama. Akaambiwa kwamba kesi yake imeahirishwa tena hadi kesho yake.

“Mdhamini wako ametakiwa hadi kesho akufikishe mahakamani vinginevyo atakabiliwa na adhabu” Msichana huyo aliambiwa.

“Nilipata ajali wakati nakuja mahakamani. Mnaona mguu wangu huu, ndio kwanza natoka hospitalini”

“Umefanya vizuri kuwahi kuja kutupa taarifa. Hakimu ameandika kuwa umedharau mahakama. Hilo ni kosa jingine. Sasa njoo kesho, kesi yako itaendelea”

“Sawa. Nnitakuja kesho”

Lwanzo akatoka na msichana huyo na kumpakia kwenye gari lake.

“Sasa twende tukamuone mwanasheria” Lwanzo akamwambia msichana huyo mara tu alipoliwasha gari.

“Asante kaka yangu”

Wakati gari likiwa kwenye mwendo Lwanzo alimuuliza msichana huyo.

“Hatujajuana vizuri, mimi naitwa Lwanzo Sseseko, wewe unaitwa nani?”

“Mimi naitwa Herieth, natokea Kiambu”

“Ndugu zako wako wapi?”

“Sitaki nikufiche, mimi sina ndugu yeyote hapa Nairobi. Nilikuwa na rafiki tu na ndiye huyo aliyenisaliti”

“Una maana kwamba ndugu zako wako Kiambu?”

“Huko pia karibu ndugu wote walishakufa. Wazazi wangu ndio sikuwajua kabisa. Walikufa nikiwa mdogo sana”

Pole sana. Ulikuja lini hapa Nairobi?”

“Kama miaka mitatu iliyopita. Na kilichonileta hapa ni kutafuta kazi. Ndiyo nikakutana na huyo rafiki yangu aliyenitafutia kazi ya baa”

Lwanzo aligeuza uso wake haraka akamtazama msichana huyo.

“Unafanya kazi baa?” akamuuliza.

“Ndiyo, nilikuwa nafanya baa hata huyo rafiki yangu anafanya hapo hapo”

“Mbona unasema ulikuwa, una maana hivi sasa hifanyi tena”

“Nimeacha baada ya huyo rafiki yangu kumchukua mchumba wangu. Hatuwezi kufanya kazi pamoja kwa sababu tumeshakuwa maadui”

“Kwa hiyo hivi sasa umeacha?”

“Nimeacha lakini natafuta mahali pengine. Siwezi kuacha kabisa. Kodi ya chumba nitalipa na nini. Mwanaume niliyekuwa nikimtegemea amechukuliwa na rafiki yangu”

itaendelea kesho Usikose Uhondo huu hapahapa Usikupite

No comments:

Post a Comment