RIWAYA
KAMA UNATAKA FEDHA ZA MAJINI
5
ILIPOISHIA
Vile naingia tu, zile sauti
zikazidi. Nikamuona mama yangu na mwanangu wamewekwa chini kama
walemavu wakilia njaa. Walikuwa weusi kama waliopakwa lami na walikuwa
wamekonda sana kiasi kwamba walikuwa wanatisha
na kuonekana kama vinyago.
Walikuwa wamenikodolea macho
huku wamefungua midomo yao
kuashiria kuwa walikuwa wanataka kula. Kwa kweli walinitia huruma sana. Mambo yale
yalifanywa na baba yangu aliyekuwa ameshakufa lakini kama
angekuwa hai ningekwenda kumpiga sime nikamuua kwa hasira.
Baada ya kumuona mama yangu
na mwanangu wanavyolalamikia njaa, nikakumbuka kwamba nilikwenda kizembe mahali
hapo. Sikuwachukulia chakula chao nilichoagizwa. Nikageuka na kutoka mbio.
Nilirudi nyumbani nikawatayarishia
uji wa mapumba ya mahindi kama nilivyoagizwa kisha nikautia uji huo asali ya nyuki.
Sikuona vibaya kuwapelekea uji wa mapumba ya mahindi kwa sababu ni mzuri na
mimi mwenyewe niliwahi kuunywa mara nyingi.
Uji ulipoiva niliutia kwenye
chupa ya chai nikachukua vikombe viwili na kutoka mbio kurudi kule pangoni.
Niliingia kwenye lile pango
nikawamiminia uji kwenye vile vikombe na kuwapa. Walikuwa hawawezi kunywa
wenyewe. Walikuwa kama watu waliopooza. Ilibidi niwanyweshe. Uji ulikuwa moto
lakini walikunywa hivyo hivyo kwa sababu ya njaa.
SASA ENDELEA
Kila mmoja alikunywa vikombe
vinne. Sasa nikahisi kuwa walikuwa wakijsikia vyema. Hata hivyo hawakuwa watu
wa kuzungumza chochote. Walikuwa wameduwaa tu huku wakitoka ute.
Wakati nawatazama, machozi
yalianza kunitoka. Nikajiuliza ni kwanini baba yangu alikuwa katili kiasi kile.
Hivi watu wanaodaiwa kumiliki pesa za majini wanakuwa katili kiasi hiki?
Nikaendelea kujiuliza kama kulikuwa na umuhimu wa kuendelea kuzifurahia zile
pesa za marehemu baba yangu wakati zimekatisha uhai wa mama yangu na mwanangu
wa pekee ambao sasa wamekuwa mazezeta wasiojielewa?.
Sasa fikira zangu zikawa
katika kuwaokoa viumbe hao waliokuwa katika mateso mazito. Sikuhitaji tena zile
pesa ambazo kwa wakati ule niliziona kama sumu
iliyokuwa inanyemelea kunimaliza mimi mwenyewe.
Nikawa nafikiria jinsi ya
kuwaokoa viumbe hao ili warudi katika uhai wa kawaida na mimi mwenyewe niweze
kuyanusuru maisha yangu.
Nikajiuliza nifanye nini
wakati yule jini alishaniambia kuwa ni lazima nitii na nifuatishe maagizo yake
kwa vile ndio makubaliano yake na marehemu baba yangu.
Upande mmoja wa akili yangu
uliniambia kuwa hatua yoyote nitakayochukua kwenda kinyume na maagizo
niliyopewa, inaweza kuyagharimu maisha yangu.
Nikaondoka katika lile pango
nikiwa na chupa yangu niliyokuwa nimeitilia uji. Wakati natoka nilimuona mama
yangu na mwanangu wakinitazama. Walikuwa wakinitazama bila kujielewa lakini
nilihisi kama vile walikuwa wakiniambia
nisiwaache pale lakini hawakuwa na uwezo wa kutamka maneno.
Nikatembea taratibu kurudi
nyumbani huku nikiwaza. Picha ile mama yangu na mtoto wangu ilikuwa imekaa
katika akili yangu wakati wote. Ilikuwa picha ambayo sikuipenda hata kidogo.
Nilipofika nyumbani niliketi
kwenye kigoda huku nikiendelea kuwaza.
Wazo la kutolewa kafara kwa
mke wangu nalo liknijia akilini. Nikaona kama sitaharakisha kuchukua hatua stahiki, nitamkosa mke wangu
ingawa sikujua ingekuwa ni lini.
Hapo nikapata wazo jingine la
kwenda kwa mganga. Nikajiambia kwenda kwa mganga lilikuwa ndilo suala sahihi
kwa matatizo yaliyokuwa yananikabili.
Sasa nikawa nafikiria niende
kwa mganga gani. Kulikuwa na waganga kadhaa pale kijijini kwetu. Nikagundua
kulikuwa na mganga mmoja aliyekuwa maarufu zaidi ambaye alikuwa akiishi kijiji
cha pili. Nikaamua kwenda kwa mganga huyo nikiamini kwamba angeweza kulipatia
ufumbuzi tatizo langu.
Nilipopata wazo hilo sikutaka kukaa tena,
nikaondoka kwenye kigoda nikatoka na kufunga mlango. Nilikwenda kwenye kituo
cha bodaboda. Nikapakiwa kwenye pikipiki na kuelekea katika hicho kijiji
kilichokuwa na huyo mganga.
Kijana wa bodaboda
alinishusha mbele ya nyumba ya mganga huyo. Uzuri wa waganga wa vijijini ni
kwamba hata kama ni hodari kiasi gani huwezi
kukuta msururu mrefu wa watu nyumbani kweke. Muda ule niliofika nilikuta watu
watatu tu waliokuwa wakisubiri kuingia kwa mganga huyo.
Niliposhuka kwenye bodaboda
nilikwenda barazani mwa nyumba hiyo nikawasalimia watu hao niliowakuta kisha
nikakaa kwenye foleni.
Yalipita karibu masaa mawili
hadi ilipofika zamu yangu. Niliingia kwenye ukumbi wa mganga huyo uliokuwa
umetandikwa jamvi. Mganga mwenyewe alikuwa ameketi karibu na ukuta akiwa amevaa
kaniki na shati jeupe.
Kando yake kulikuwa na
chetezo kilichokuwa kinafuka moshi uliokuwa unanukia harufi ya udi.
Mbele yake kulikuwa na na
rundo la vitabu vilivyokuwa vimewekwa chini. Juu ya ukuta aliokuwa ameegemea
kulikuwa na tunguri kadhaa zilizokuwa zimepachikwa.
“Karibu, kaa hapo” Mganga
aliniambia huku akinionesha mahali pa kukaa. Nikakaa chini mbele yake.
“Naweza kukusaidia”
akaniambia.
“Nina shida. Naomba msaada
wako”
“Shida gani?”
Nikamueleza tatizo lililokuwa
limenipeleka pale. Mganga akashituka aliposikia kuwa ninamiliki sanduku la pesa
za majini.
“Pesa za majini zina
matatizo” Mganga akaniambia na kuongeza.
“Matatizo yake ni kama hayo. Mimi namfahamu baba yako lakini sikuwa nikijua
kama alikuwa akimili pesa za majini. Kumbe
alimtoa mhanga mke wake na mjukuu wake. Mwenyewe amekufa na siri imefichuka!”
“Sasa naomba msaada wako”
“Ulitaka nikusaidieje?”
“Kwanza
uwaokoe mama yangu na mwanangu ambao wanateseka kule mapangoni. Na pili
ninataka kuepukana na zile pesa. Mimi sizitaki tena”
Mganga akacheka.
“Kwanini huzitaki?”
“Masharti yake ni magumu
kwangu. Yule jini aliniambia niende nikamzini makaburini. Sitaweza”
“Lakini baba yako aliyaweza
yote hayo”
“Kosa alilofanya ni
kunifanya mimi kuwa mrithi wake wa pesa
zile na kwa hivyo ninatakiwa nimrithi na yule jini wake jambo ambalo
siitaliweza. Baya zaidi ni kuwa ninatakiwa nimtoe kafara mke wangu ili mama
yangu akifa pawepo na mtu mwingine”
“Kwa kweli ni tatizo. Lakini
kuna watu wengine wanazitaka hizo pesa za majini na wako tayari kuwatoa kafara
ndugu zao au wazazi wao pamoja na watoto wao”
“Ni kweli watu hao wapo na
mmojawapo ni huyo marehemu baba yangu. Hakujali kumtoa kafara mke wake na
mjukuu wake ili apate pesa”
“Nikwambie kweli kuwakomboa
mama yako na mwanano litakuwa ni tatizo kwa sababu yule jini anayehusika hivi
sasa unaye wewe”
Aliponiambia hivyo
nilishituka.
“Mimi siko naye” nikamwambia
na kuongeza.
“Sijakubaliana naye”
“Makubaliano ni yale ya jini
huyo na baba yako kwamba atakapokufa yeye mrihi utakuwa ni wewe. Kwa hiyo baada
ya baba yako kufa, wewe ndio umemrithi huyo jini!”
Nikajishika kichwa na
kukitikisa kusikitika.
“Huu ni upuuzi. Ushirikina
wao utanihusu nini mimi? Huyu baba alikuwa mtu wa aina gani!” nikajisemea kisha
nikamuuliza yule mganga.
“Yaani haitawezekana
kuwakomboa mama yangu na mwanangu?”
“Haitawezekana”
“Haitawezekana hata kama sizitaki zile pesa zao, wachukue wenyewe?”
Niliporudia kutaja pesa yule
mganga alitulia kimya. Nikamuona kama alikuwa akiwaza kitu.
“Una uhakika kwamba hizo pesa
huzihitaji?” akaniuliza baada ya ukimya mfupi.
“Sizihitaji. Namuhitaji mama
yangu na mwanangu!?” nilimwambia kwa sauti kali ili aweze kunielewa vizuri..
“Na una uhakika kwamba
hujazitumia hata kidogo?”
“Sijazitumia na sitazitumia”
“Sasa sikiliza, niletee mimi
hizo pesa kama huzihitaji. Mimi nitajua jinsi
ya kuzifanya”
“Lakini nakuomba uzingatie tatizo la msingi!”
“Tatizo la msingi ni lipi?’
“Ni kuwapata mama yangu na
mwanangu”
“Mama yako na mwanano utawapata
kwa sababu hizo pesa utakuwa umezitoa kwa mtu mwingine. Mimi ndiye nitakaye
beba jukumu hilo”
“Na lile jini litakuja kwako?”
“Hilo jini linakuwa na mtu anayemiliki hizo
pesa. Kama wewe umezitoa halitakaa kwako tena”
“Mimi nitakuwa huru?”
“Ndiyo. Wewe utakuwa huru”
“Sawa. Sasa hizo pesa ziko
kwenye sanduku la chuma. Kulileta kwako muda huu haitawezekana lakini kama tutasaidiana kulibeba wakati wa usiku, tunaweza
kulileta hapa kwako”
“Una maana kwamba limejaa
pesa hadi juu?”
“Limejaa mpaka pomoni na ni
nyekundu tupu!”
Mganga alitoa ulimi
akaupitisha kwenye mdomo wake wa juu kwa tamaa. Akaniambia.
“Tufuatane sasa hivi hadi
nyumbani kwako, niende nikaziangalie”
“Twende”
Hapo hapo mganga akainuka.
“Nisubiri kidogo”
Je nini kitatokea? Usikose kuwa nami kesho hapahapa
No comments:
Post a Comment