HADITHI
MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA
UKINGONI 17
ILIPOISHIA
Kwa sababu ya kiherehere,
aliamua kwenda kijijini kwao kuwaona wazee. Kulikuwa na bibi mmoja ambaye
alikuwa mganga maarufu kijijini kwao akampeleka kwenye mzimu wa kwao na
kumfanyia maombi ya kishirikina
kwenye mzimu huo.
Akamuombea kupata uwaziri
mkuu.
Baada ya maombi kukamilika,
bibi huyo alimtaka Dastan Lazaro wakati huo akiwa si waziri mkuu, kuweka
nadhiri kwenye mzimu huo kuwa endapo atateuliwa kuwa waziri mkuu atapeleka
ng’ombe kwenye mzimu huo.
“Hilo ni sharti. Ukiteuliwa kuwa waziri mkuu kama unavyotaka, uje uchinje ng’ombe hapa” Bibi huyo
alimsisitizia Lazaro.
“Hilo
jambo dogo sana”
“Sawa. Kazi yetu imekwisha,
turudi”
Waziri Mkuu alikumbuka kwamba
alipoteuliwa kushika wadhifa huo alisahau kutimiza nadhiri aliyoiweka.
Kuna siku mke wake
alimkumbusha. “Mume wangu unakumbuka kwamba uliniambia uliweka nadhiri kwenye
mzimu kwamba utapaleka ng’ombe.?”
“Mke wangu huo ni ushirikina”
SASA ENDELEA
“Lakini si ulikwenda mwenyewe
ukakubali
kuweka nadhiri wewe mwenyewe”
“Nilimfuatisha tu yule bibi
lakini sikuwa nikiamini”
“Kwa hiyo umeamua uache?”
“Unadhani naweza kufanya
upuuzi ule? Si nitaharibu hata heshima yangu”
Dastan Lazaro akapuuza sharti
alilopewa na mganga. Mzimu aliopelekwa ulikuwa maarufu na watu mbalimbali
walikuwa wakifika kwenye mzimu huo kwa dharura zao za kishirikina.
Eneo hilo lilikuwa likikaribisha fisi waliokuwa
wakifuata mizoga ya wanyama waliokuwa wakitolewa makafara kwenye mzimu huo.
Kijiji kilipopanuka mzimu huo ukawa
upo karibu na makazi ya watu, ndipo Waziri Mkuu alipoamuru uondolewe.
Magreda ya halmashauri
yalipelekwa kwenda kuung’oa mzimu huo, ukawa haupo tena. Eneo hilo lilisafishwa likawa jeupe. Ziara za
kuzuru mzimu huo zikawa hazipo tena. Baadaye mahali hapo palikuja kujengwa
shule ya kijiji.
Baada ya Waziri Mkuu kuvuta
kumbukumbu hiyo alimtazama mke wake.
“Mganga alikwambia uje
uniulize kama nilitimiza ile nadhiri?”
akamuuliza
“Ndio aliniambia nije
nikuulize kisha
niende nikamjibu”
“yeye alijuaje kama nilikwenda kuweka nadhiri kwenye mzimu ule?”
“Alijua baada ya kupiga
ramli”
“Sio kwamba wewe ndio
ulimueleza?”
“Hapana. Sikumueleza. Yeye
ndiye alinieleza mimi”
“Alikuwa na maana kwamba
kutotimiza ile nadhiri ndio kumemsababishia mtoto wetu matatizo aliyonayo?”
“Ndivyo alivyonieleza”
“Kivipi?”
“Alitaka kwanza nikampe jibu
ndio atanieleza”
“Nenda kamwambie kwamba
sikutimiza ile nadhiri. Sasa mtoto amedhurika kivipi?”
“Kesho nitakwenda kumueleza”
Asubuhi yake, mke wa Waziri
Mkuu pamoja na Sofia
wakaenda Morogoro. Wakiwa kijijini kwao Vicky, yaani mke wa Waziri Mkuu
alimuacha Sofia
nyumbani kwao, akaenda peke yake kwa yule mganga.
Alipofika alimueleza kuwa
baada ya mume wake kuupata uwaziri mkuu hakutimiza ile nadhiri aliyoweka kwenye
mzimu.
“Hilo ndilo lililoleta tatizo kwa binti yenu”
Mganga akamwambia.
“Limeleta tatizo kivipi?”
“Ule mzimu uliahidiwa damu,
yaani yule ng’ombe angechinjwa kwenye ule mzimu na mzimu ungepata damu. Sasa
baada ya mume wako kutotimiza ahadi yake mzimu ule ulimuingia binti yenu, sasa
unafyonza damu za watu”
Mke wa Waziri Mkuu
alishituka.
“Kumbe ule uliompata mwanangu
ni mzimu?” akauliza kwa mshangao.
“Ni mzimu”
“Kwani ulitaka ng’ombe wangapi?”
“Ng’ombe mmoja tu alioahidi
mume wako”
“Sasa mbona ameshafyonza damu watu wawili?”
“Na utaendelea kufyonza watu
zaidi”
“Kwanini sasa?”
“Ni kwa sababu mmeufanyia
dharau. Mmeuahidi kitu halafu hamkutimiza”
“Si mimi, ni baba yake”
“Ndio unawakomoa nyote”
Vicky akatikisa kichwa
kusikitika.
“Sasa hauna tiba?”
“Hauna tiba nyingine”
“Isipokuwa?”
“Mume wako atimize ile
nadhiri yake?”
“Akitimiza ndio itakuwa tiba
yake?”
“Ndio”
Vicky akarudisha jibu kwa
mume wake.
“Mume wangu ulikosea sana kwenda kuweka nadhiri
kwenye mzimu kisha ukapuuza”
“Mganaga amekwambiaje?”
“Ameniambia baada ya kuacha
kupeleka yule ng’ombe, ule mzimu umemuingia mtoto wetu, sasa unafyonza damu za
watu ukiwa mwilini mwake”
Waziri Mkuu akashituka.
“Mpaka lini?”
“Mpaka utimize ile nadhiri
yako”
“Ngoja kesho nitakwenda kwa
yule bibi niliyekwenda naye wakati ule. Tutakwenda kuyamaliza huko huko”
Siku iliyofuata Waziri Mkuu
akaenda Morogoro. Alikwenda kijijini kwao na kufika nyumbani kwa yule bibi
aliyekwenda naye kwenye ule mzimu.
“Yule bibi alikufa tangu
mwaka jana?” Mwanamke mmoja alimwambia Waziri Mkuu alipomuuliza mwanamke huyo.
Waziri Mkuu akashusha pumzi
ndefu.
“Kumbe yule bibi alikufa?”
“Alikufa, hatuko naye tena”
“Hivi hakuna mtu mwingine
aliyechukua kazi zake?”
“Yule bibi hakuwa na mtoto
wala mjukuu”
“Na wale wasaidizi wake wako
wapi?”
“Msaidizi wake alikuwa mmoja
tu na ndiye aliyetangulia kufa”
Waziri
Mkuu hakuwa na jingine
isipokuwa kuaga na kuondoka. Aliporudi nyumbani kwao alimuuliza ndugu
yake kama alikuwa anamfahamu mganga yeyote wa kienyeji aliye
hodari.
“Namfahamu”
“Kama
namuhitaji unaeza kumleta hapa muda huu?”
“Naweza”
“Hebu nenda kamlete, nina
shida naye”
Ndugu huyo wa Waziri Mkuu
aliondoka na gari lake. Baada ya nusu
saa tu alirudi akiwa na mtu mwingine ambaye alimpeleka kwa Wazi Mkuu.
“Mganga mwenyewe ndiye huyu”
akamwambia
“Karibu sana” Waziri Mkuu alimwambia mganga huyo.
“Asante”
Ndugu wa Waziri Mkuu
aliondoka na kuwaacha. Waziri Mkuu akamueleza mganga huyo tatizo la binti yake
na jinsi walivyoambiwa na mganga wa awali kwamba tatizo hilo linatokana na nadhiri aliyoweka kwenye
mzimu.
“Ni kweli kwamba uliweka
nadhiri hiyo?” mganga akamuuliza Waziri Mkuu.
“Ni kweli niliiweka lakini
sikuwahi kuitimiza kwa sababu ya shughuli kuwa nyingi”
itaendelea kesh hapao usikose Uhondo huu hapa
No comments:
Post a Comment