Tuesday, October 24, 2017

SIMULIZI, TAMAA MBELE MAUTI NYUMA SEHEMU YA 9

SIMULIZI

TAMAA MBELE, MAUTI NYUMA 9

ILIPOISHIA

Eneo la Lang’ata lilikuwa kando kidogo ya jiji hilo. Lilikuwa eneo linaloishi watu wa vipato vya chini kama Herieth. Lwanzo alimpeleka msichana huyo hadi mlangoni mwa nyumba aliyokuwa anaishi.

Lakini walikuta kitu kilichowashitua.

Kwanza waliona gari la polisi lililokuwa limesimama pembeni mwa mlango. Halafu waliona polisi watatu wakitoka ndani ya nyumba hiyo pamoja na mtu mmoja aliyevaa kiraia ambaye alikuwa akifoka.

“Tutamkamata tu hata ande wapi. Kwao ninakujua ni Kiambu na hana pengine pa kukimbilia!”

“ Haa! Njoroge yule!” Herieth akamaka na kugwaya

“Amefuata nini nyumbani kwako?” Lwanzo akamuuliza.

Msichana akabetua mabega yake.

“Sijui. Tena amekuja na polisi!”

SASA ENDELEA

Lwanzo alilisimamisha gari nyuma ya gari la polisi.

“Hebu tushuke, tuwasikilize” lwanzo akamwambia Herieth huku akifungua mlango wa gari.

“Sijui huyu mwanaume ananitafuta nini mimi” Herieth alilalamika.

“Shuka tu, kama ni kesi yenu, tayari iko mahakamani. Hakuna sababu yoyote ya kuwa na wasiwasi”

Herieth akafungua mlango. Wakati anashuka kwenye gari, mtu aliyekuwa anafoka alimuona.

“Huyo hapo amefika “ akasema huku akimnyooshe kidole Herieth.

“Wewe Njoroge unanitafuta nini lakini…?” Herieth alimuuliza kwa hasira baada ya kushuka kwenye gari.

“Unajua wewe uko huru kwa dhamana, leo ulitakiwa kufika mahakamani lakini hukufika, umekiuka dhamana yako!”

“Wewe inakuhusu nini?”

Lwanzo akaingilia kati.

“Msibishane. Huyu msichana wakati anakuja mahakamani asubuhi alipata ajali ya gari, ametenguka mguu. Mimi ndiye niliyemsaidia kumpeleka hospitali”

“Sasa sisi hatujui. Tunajua kuwa amekiuka dhamana. Polisi wamekuja kumkamata”

“Lakini Njoroge hii ni kazi ya polisi na mahakama, wewe inakuhusu nini?” Herieth akafoka.

“Herieth nyamaza msogombane” Lwanzo alimtuliza.

“Anajifanya hodari sana wa kusema lakini safari hii jeuri yake itakwisha” Njoroge alimwambia Herieth kwa jeuri.

“Wewe unatakiwa kukamatwa kwa sababu mahakama haina taarifa kuwa umepata ajali. Sisi tumekuja kukukamata” Mmoja wa wale polisi akamwambia Herieth.

“Ndio mumkamate mkamuweke ndani hadi kesho atakapofikishwa tena mahakamani chini ya ulinzi wa polisi” Njoroge akasema.

“Hapa tunatoka mahakamani. Ameshatoa taarifa na ametakiwa kufika tena kesho” Lwanzo akawambia.

Polisi mmoja  aliposikia hivyo alimgeukia Njoroge.

“Kama mahakama ina taarifa kuwa alipata ajali hatuwezi kumkamata tena” akamwambia.

“Wewe angalia sana!” Njoroge akamwambia herieh huku akimnyooshea kidole cha onyo.

Herieth hakumjibu kitu, alimtazama tu kisha akapanda kwenye baraza ya nyumba. Njoroge na wale polisi walishuka kwenye baraza wakajipakia kwenye gari na kuondoka.

“Karibu ndani kaka” Herieth akamwambia Lwanzo.

“Asante. Sitaingia ndani. Nitaishia hapa ila kesho asubuhi nitakufuata hapa nikupeleke mahakamani”

“Sawa. Asante kaka”

“Haya kwaheri”

“Karibu sana”

Lwanzo akarudi kwenye gari akaliwasha na kuondoka.

Wakati akiendesha kurudi nyumbani kwake aliwaza kwamba sheria zimeshindwa kuzuia unyanyasaji dhaidi ya wanawake kwa sababu pesa imewekwa juu ya sheria.

Aliendelea kujiambia, kwa sababu ya pesa mtu anaweza kutumia hata vyombo vya dola kumdhalilisha binaadamu mwenzake bila huku akijua fika kuwa hana kosa.

“Udhalilishaji dhidi ya wanawake bado ni tatizo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi na jamii nzima” Lwanzo akajiambia.

Hata hivyo alikuwa amepanga kumsaidia yule msichana hadi dakika ya mwisho ili ahakikishe kuwa haki imetendeka.

Herieth baada ya kuingia chumbani kwake alikaa kwenye kochi na kuanza kuufikiria mguu wake. Alijiambia alipoondoka asubuhi mguu wake ulikuwa mzima kabisa na hakufikiria kuwa angerudi nyumbani akiwa na P.O.P.

“Kweli binaadamu haishi kuumbwa” alijiambia huku akimshukuru Lwanzo, mtu ambaye hakuwa akimfahamu kabla, kwa msaada aliompa kumpeleka hospitali na kisha kumuwekea wakili.

“Kama si yule kaka, sijui ningekuwa katika hali gani leo?” alijiuliza bila kupata jibu.

Taratibu alianza kukumbuka jinsi wazazi wake walivyofariki huko kwao Kiambu na yeye kuamua kwenda jijini Nairobi kutafuta kazi. Alifika Nairobi akiwa na nguo moja tu ya akiba aliyokuwa ameitia kwenye mfuko wa plastiki.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kufika katika jiji hilo na lengo lake lilikuwa kutafuta kazi, kazi yoyote tu ambayo angejaliwa kuipata, iwe kazi ya ndani au ya uchuuzi wa vitu vidogo vidogo.

Ilimchukua karibu saa nzima kuzunguka katika eneo la stendi la Nairobi akiwa hajui aende wapi. Alikuwa akizungumza na kila msichana aliyemuona anafanya biashara ndogondogo.

Hatimaye alikutana na msichana mmoja aliyekuwa akitembeza  vitu vidogo vidogo.

“Naweza kupata kazi kama yako?’ akamuuliza.

“Kwani wewe unatoka wapi?”

“Natoka Kiambu, ndio nimefika sasa hivi”

Msichana huyo aliyeonekana kukomaa lakini mwenye umbo dogo alimtazama Herieth kuanzia kichwani hadi miguuni.

“Unataka kazi?” akamuuliza.

“Unaweza kunipatia?”

“Mimi pia nimeajiriwa kuuza hivi vitu, si kazi yangu”

“Na mimi pia nahitaji”

“Usifikiri ni rahisi, hapa haturuhusiwi kufanya biashara ndogo ndogo tunaibia tu, askari wa jiji wakija tunakimbia. Utaweza?’

“Nitaweza”

“Basi subiri nikiondoka nitakupeleka kwa mama mmoja anayetaka msichana wa kumuuzia biashra yake”

Ndipo Herieth alipopelekwa kwa mama mmoja wa Kijaluo ambaye alimwambia Herieth kuwa alikuwa anataka msichana wa kumsaidia katika kazi yake ya kuuza majungu katika soko moja lililokuwa kando kidogo ya jiji la Nairobi eneo la Kibera.

“Mimi sichagui kazi. Kazi yoyote utakayonipa nitafanya” Herieth alimwambia mwanamke huyo ambaye alimpokea Herieth na kumuajiri kazi ya kuuza majungu.

Herieth hakumaliza hata mwezi mmoja, akajakukutana na msichana mmoja aliyeitwa Sara ambaye alikuwa akiishi jirani na mwanamke huyo wa Kijaluo.

Herieth na Sara wakawa marafiki.

“Kwani mwenzangu unafanya kazi wapi?” Siku hiyo Herieth akamuuliza Sara.

“Nauza baa”

“Huyu mwanamke ninayemfanyia kazi yake ananinyanyasa sana. Nikipata mahali pengine nitamkimbia”

“Utaweza kuuza baa”

“Kwanini nisiweze?”

“Tena una umbo zuri la kuvutia wateja, nikikupeleka kwa tajiri yetu atakupokea mara moja”

“Sasa unajua tatizo ni nini?”

“Ni nini?”

“Ni mahali pa kulala. Hivi sasa nalala kwa yule mwanamke, nikiacha kazi kwake itabidi niondoke kwake”

“Kama ni kulala tu si tatizo, utala na mimi chumbani kwangu”

Siku ya pili yake Herieth akamtoroka yule mwanamke wa Kijaluo. Sara alimpeleka mjini katika baa aliyokuwa anafanya kazi ya ubaamed.

Mmiliki wa baa hiyo ambaye alikuwa ni mtumishi wa serikalini alipomuona Herieth alimpokea mara moja. Harieth akaanza kazi ya ubaamed.

Ni wakati huo ushamba ulipomtoka Herieth na kuonekana kama msichana wa mjini. Kutokana na pesa ndogo ndogo za chenji alizokuwa akiachiwa na bia za ofa ambazo alikuwa akiziuza kwa wateja wengine kwa kisingizio kuwa hawaruhuiwi kulewa wakiwa kazini, mara moja Herieth alibadilika. Aliweza kununua nguo za thamani na kuweza kujiwekea akiba.  Urafiki  wake na sara ukazidi kuwa mkubwa.

Siku moja  Sara akataka kumchuuza mwenzake kwa mwanaume aliyekuwa akimtaka.

“Kuna jamaa atakuja usiku ana visenti vyake mbuzi, nataka ukamchune” Sara alianza kumwambia herieth mara tu walipoingia kazini saa kumi na mbili jioni.

“Ni jamaa gani?”

“Atakuja saa tatu usiku utamuona, ameniambia anakupenda sana”



ITAENDELEA kesho Usikose Uhondo huu hapahapa kumekucha.com

No comments:

Post a Comment