Saturday, October 21, 2017

HADITHI, MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI SEHEMU YA 19

HADITHI

MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI 19

ILIPOISHIA

“Tatizo la binti yenu ni kubwa lakini kwangu mimi ni dogo sana” Mganga huyo alimwambia mke wa Waziri Mkuu.

“Kwa hiyo utaweza kulishghulikia?” Mke wa Waziri Mkuu akamuuliza kwa matumaini.

“Ninaweza kulishughulikia na binti yenu akawa mzima kabisa”

“Tutafurahi kwa sababu ni tatizo lililotusumbua sana. Utahitaji nini na nini?”

“Nitahitaji ng’ombe watatu na shuka nyeusi, yaani kaniki, ziwe vipande vitatu”

“Hivyo vitu vitapatikana. Na wewe mwenyewe utahitaji kiasi gani?”

“Mimi mtanifikiria wenyewe, siwezi kukwambia nataka kima fulani”

“Tuambie tu”

Mganga akatikisa kichwa.

SASA  ENDELEA

“Siwezi kuwatajia kima, nyinyi wenyewe ndio mtanifikiria. Mtakachonipa nitashukuru”

“Sawa. Sasa tunataka uishughulikie hiyo kazi. Binti mwenyewe si umemuona”

“Nimemuona. Atapona tu. Sasa hivyo vitu vitapatikanaje?’

“Nitamtuma shemeji sasa hivi”

“Sasa kama utamtuma shemeji yako, nataka nikwambie kuwa hiyo kazi tutaifanya usiku”

“Usiku saa ngapi?”

“Saa mbili usiku”

“Utaifanya wapi”

“Porini, kwenye mzimu mwingine”

“Kwenye mzimu mwingine itafaa”

“Mzimu ni mzimu, mizimu yote ina asili moja na inasikizana. Kama ule wa kwanza umeondolewa, mzimu mwingine unaweza kufaa. Tofauti ni kuwa utatakiwa ulipe na adhabu, yaani badala ya ng’ombe mmoja wawe watatu kama nilivyokuagiza. Ule mzimu wenyewe utapata ng’ombe wawili na ule mzimu tutakaoutumia utapata ng’ombe mmoja”

“Kumbe wale waganga wa kwanza walishindwa nini?”

“Ujuzi. Ujuzi unatofautiana. Mimi kazi hii ni ya kurithi kwa baba yangu na baba yangu aliirithi kwa babu yangu. Na tangu baba yangu anashirikiana na babu, mimi nilikuwa nao pamoja. Sijisifu lakini nashukuru wazee hao wameniachia ujuzi wa kutosha”

“Sawa. Nimekuelewa. Sasa ngoja nimuite shemeji nimpatie hizo pesa za hao ng’ombe watatu na hizo shuka nyeusi. Wewe utamuagiza pa kuwapeleka ngombe hao”

“Sawa. Muite”

Mke wa Waziri Mkuu alimuita shemeji yake kwa kumpigia simu. Stambuli akafika pale muda ule ule.

“Kumbe hukuwa mbali?”

“Nilikuwa karibu tu”

Akamueleza mazungumzo yake na yule mganga kisha akampa shilingi milioni mbili kwa ajili ya kununua ng’ombe watatu na vipande vitatu vya kaniki.

“Hao ng’ombe nikishawanunua niwapeleke wapi?” Stambuli akauliza.

“Tutatoka pamoja nitakwenda kukuonesha mahali pa kuwapeleka” mganga akamwambia.


“Sawa. Kwa hiyo shemeji atasubiri hapa hapa hadi saa mbili usiku?”

“Itabidi nisubiri hapa hapa, siwezi kurudi Dar kisha nije tena hapa. Lakini nitashauriana na mheshimiwa. Kama kutakuwa na mabadiliko nitawambia”

Stambuli na mganga huyo walipotoka mke wa waziri akampigia mume wake na kumueleza mazungumzo yake na mganga huyo.

“Basi wewe endelea kukaa huko huko. Ikiwezekana unaweza kulala huko huko” Waziri Mkuu akamwambia mke wake.

“Na huyu dereva wangu itakuwaje?’

“Kama utaamua kulala, mwambie aende akatafute chumba kwenye hoteli yoyote Morogoro mjini akufuate kesho hapo kijijini.

“Sawa. Nitaangalia itakavyokuwa”

“Hiyo shughuli ikikamilika utanijulisha”

“Sawa”
                                       ************


Mnamo saa mbili usiku, watu saba walikuwa kwenye msitu chini ya mti mkubwa uliokuwa umezungukwa na kichaka.

Alikuwa Mke wa waziri Mkuu na Sofia. Pia alikuwepo Stambuli na mganga wao pamoja na wasaidizi wake wawili.

Ng’ombe watatu weusi walikuwa wamefungwa kando ya kichaka hicho.

Kaniki moja ilitandikwa ndani ya kichaka. Kaniki nyingine alivalishwa Sofia na kaniki ya tatu aliivaa mganga mwenyewe.

Sofia alikuwa amekalia ile kaniki iliyotandikwa chini. Mganga aliyekuwa ameshika mwengo wa uganga alikuwa akimzunguka huku akitabana maneno ya kiganga.

Wasaidizi wake wawili walikuwa wamesimama karibu yake wakingoja kupewa amri yoyote.

Stambuli na mke wa Waziri Mkuu walikuwa wamesimama pembeni wakitazama.

Baada ya mganga kumzunguka sofia mara saba huku akitabana maneno, aliwaagiza wasaidizi wake wamchinje ng’ombe wa kwanza mbele ya miguu ya Sofia.

Ng’ombe alichinjwa, sofia akarambishwa damu mbichi ya ng’ombe.

“Meza!” Mganga alimwambia Sofia alipomuona ameiweka ile damu mdomoni.

Sofia akaimeza.

Alipakwa damu nyingine kwenye miguu na nyingine kwenye chembe cha moyo kisha akaambiwa ainuke.

Ngombe wa pili akachinjwa na kuachwa. Ngombe wa tatu aliachwa akiwa mzima.

“Mizimu itakuja kumchukua wenyewe usiku” Mganga aliwambia Stambuli na mke wa Waziri Mkuu na kuongeza.

“Kazi imekwisha, sasa tunaweza kwenda zetu”

“Ninataka kukuuliza” Mke wa waziri akamwambia mganga huyo.

“Uliza”

“Huyu binti atakwenda kulala hivyo hivyo pamoja na damu?”

“Ndio. Asioge leo. Ataoga kesho asubuhi”

“Sawa”

Mke wa waziri Mkuu akamtazama Stambuli.

“Hatutarudi Dar leo, tutalala hapa hapa kijijini” akamwambia.

“Mtaondoka kesho asubuhi?’

“Tutaondoka kesho asubuhi”

“Sawa” Stambuli alimwambia mke wa Waziri Mkuu kisha mwanamke huyo akamgeukia mganga aliyemshughulikia mwanawe.

“Ndio kusema kwamba mwanangu ameshapona matatizo yake?” akamuuliza.

“Mwanao ameshapona, hatakuwa na matatizo tena. Mzimu umeshapata ulichokuwa unakitaka” Mganga alimwambia. Kauli ambayo ilimpa matumaini mama yake Sofia.

“Sasa ndio tunaondoka, sijajua nikupe kiasi gani?”

“Utakachotaka wewe”

“Nimetumia pesa nyingi leo” Mke wa Waziri Mkuu alisema huku akifungua pochi yake. Akaongeza.

“Nimebakisha pesa kidogo….”

Alitia mkono kwenye pochi akatoa kitita cha noti.

“Kwa sasa nitakupa laki mbili ili nibakishe pesa za kunirudisha Dar kesho asubuhi ila pesa zingine nitazituma kwa shemeji atakuja kukupa. Sawa?”

“Hakuna tatizo”

Mganga alizipokea laki mbili alizopewa.

“Asante sana”

Wakaagana.

Waliporudi nyumbani mke wa Waziri Mkuu akampigia mume wake.

“Ndio tumerudi kutoka kwenye huo uganga” akamwambia.

“Imekuwaje?’ Waziri Mkuu akamuuliza kwenye simu.

“Ameshafanyiwa”

“Kwa hiyo kazi imekwisha?”

“Imekwisha na tumeamua kulala huku huku”

“Mganga amesemaje, yale matatizo hayatajirudia?”

“Amenihakikishia kwamba Sofia amepona kabisa”

“Kwa hiyo mtarudi asubuhi?”

“Tutarudi asubuhi”

“Nilikwambia umwamie dereva aende akatafute hoteli ya kulala Morogoro”

“Ameshaondoka, hayuko hapa”

“Huyo mganga ametaka kiasi gani?”


itaendelea kesho Usikose kuwa nami kesho nini kitatokea wakati mganga anamlazimisha dereva akalale mjini na kijijini abaki mke wa waziri mkuu.

No comments:

Post a Comment