RIWAYA
KAMA UNATAKA FEDHA ZA MAJINI
2
ILIPOISHIA
Baada ya sekunde chache
nikisikia sauti ya mke wangu kwenye simu. Alikuwa bado analia.
“Hebu nyamaza kwanza
tushauriane. Shemeji ameniuliza kuhusu mazishi lakini sikuwa na jibu”
“Mimi nitakuja kesho asubuhi.
Msizike mpaka nifike” Mke wangu alijikaza akaniambia.
“Kama
utaondoka asubuhi, kila ilivyo utafika huku usiku. Kwa hiyo tutazika usiku
utakapofika”
“Nadhani nitakuja peke yangu.
Huku baba amezidiwa tena. Kaka atabaki”
“Sawa”
“Basi ni hivyo”
“Vizuri, nakutakia safari
njema”
SASA ENDELEA
Baada ya kuzungumza na mke
wangu nilimueleza baba kuwa tutazika usiku wa kesho yake baada ya mke wangu
kuwasili kutoka Dodoma.
“Amekwambia atawasili saa
ngapi” akaniuliza.
“Atafika usiku huo huo”
“Watu wengi wananiuliza
kuhusu mazishi lakini nimekuwa sina jibu, sasa nitawaeleza kuwa mazishi
yamepangwa kufanyika kesho usiku”
“Waeleze hivyo. Na tumeyapanga
muda huo kwa sababu ya kumsubirisha mama yake, vinginevyo tungeweza hata kuzika
kesho mchana”
Ilipofika saa tano usiku, mke
wangu alinipigia simu tena akaniuliza kilichokuwa kinaendelea nikamueleza.
Akaendelea kunisisitiza kuwa tusizike
mpaka atakapowasili.
“Tumeshapanga kuwa mazishi
yatafanyika baada ya wewe kufika”
“Sawa. Mimi nimeshajiandaa,
kesho asubuhi naondoka” mke wangu akaniambia.
Usiku wa siku ile hatukulala.
Mimi na baba tulikuwa tukitafakari kuhusu msiba ule uliotutokea ghafla.
Asubuhi kulipokucha
tuliendelea kupokea wageni waliokuja kuomboleza kwenye msiba huo. Baadhi ya
watu walitoka katika vijiji vingine vya karibu.
Matayarisho ya mazishi
yaliendelea hapo nyumbani hadi jioni. Mke wangu alifika na basi lililowasili
saa moja usiku. Alinipigia simu kunijulisha kuwa alikuwa ameshawasili.
Nikawaagiza wifi zake waende wakampokee.
Wakaenda kumpokea na kuja
naye lakini walipofika tu hapo nyumbani kilio kikaanza upya. Mke wangu alianza
kulia na wifi zake nao wakalia pamoja naye..
“Mwanangu umepatwa na
nini…mwanangu umepatwa na nini…mbona mwanangu umenitoka ghafla…” Ndiyo maneno
aliyokuwa akimtamka mke wangu.
Ndugu na jamaa walijaribu
kumnyamazisha. Akanyamaza na kuingia katika chumba kilichokuwa na mwili wa
marehemu lakini alipouona mwili wa mwanawe akaanza tena kulia.
Kwa vile tulipanga
atakapofika mke wangu, mwili wa marehemu utolewe kwa ajili ya kwenda kuzikwa,
shughuli hiyo ikafanyika.
Mpaka inafika saa tatu usiku,
jeneza lilikuwa limeshafikishwa makaburini. Baada ya mazishi tukarudi nyumbani.
Mke wangu aliendelea kubaki
hapo Korogwe kwa wiki nzima kabla ya kurudi tena Dodoma.
Hazikupita hata wiki mbili
baba yangu naye akapatwa na homa ghafla. Nilimpeleka hospitali nikidhnani
alikuwa na malaria lakini baada ya kuchukuliwa vipimo aligundulika hakuwa na
malaria. Hata hivyo alipewa tembe za kwenda kumeza nyumbani.
Baada ya kutumia tembe hizo
alipata nafuu kidogo lakini zilipita karibu wiki mbili baba alikuwa ndani
akijiuguza.
Usiku mmoja akaniita na
kuniambia.
“Mwanangu naona kiza mbele
yangu. Kuna kitu nataka kukwambia”
Aliponiambia hivyo nilishituka
nikamkazia macho na kumuuliza.
“Unataka kuniambia nini
baba?”.
“Cha kwanza ninachotaka
kukwambia ni kuwa endapo nitafumba macho siku yoyote, urithi wako uko chini ya
mvungu wa kitanda nilicholala” akaendelea kuniambia huku akielekeza mkono wake
chini ya mvungu wa kitanda.
Mimi nilikuwa nimenyamaza
nikimsikiliza kwa makini.
“Sasa kuna majukumu ambayo
nataka nikukabidhi lakini si hapa. Itabidi tutoke usiku huu twende mahali fulani”
Hapo nikamuuliza.
“Ni majukumu gani hayo baba
na hapo mahali unapotaka twende usiku huu ni wapi?”
“Nifuate tu”
Baba alikuwa ameshainuka
kwenye kitanda. Kitu ambacho kilinishangaza ni kuwa alipoinuka alikuwa na nguvu
mpka nikahisi kuwa alikuwa amepona.
Nikapata matumaini. Na mimi
nikanyanyuka na kumwambia.
“Haya twende”
Nikatoka naye pale nyumbani.
Nakumbuka ilikuwa saa saba usiku.
“Ni usiku huu, chukua silaha”
akaniambia.
“Kwani ni mbali sana baba?”
“Ni mbali kidogo”
“Kwanini tusiende kesho”
“Mimi nataka twende leo”
Nikarudi ndani na kuchukua
sime. Nilipotoka, nikamwambia.
“Haya twende”
Tukaanza safari.
“Acha mimi niwe mbele yako”
Baba akaniambia wakati tunakwenda.
Nikamuacha atangulie mbele
yangu. Njia tuliyokwenda ilikuwa ikielekea lilikokuwa shamba lake. Nikahisi
tulikuwa tunakwenda shambani kwake. Lakini tulipolikaribia shamba hilo tuliliacha shamba
upande wa kushoto tukashika njia ya upande wa kulia.
Kimoyomoyo nilikuwa
nikijiuliza, baba alikuwa ananipeleka wapi usiku ule. Kwa mbali tulikuwa
tukisikia milio ya fisi pamoja na ya wanayama wengine.
Kile kitendo ch baba kuwa
mbele yangu kilinizuia nisimuulize maswali mengi yaliyokuwa yakipita akilini
mwangu.
Baada ya muda kidogo tukawa
tumeingia kwenye njia iliyoelekea kwenye pori.
Ilikuwa njia nyembamba ya kupita kwa miguu.
Sehemu yenyewe ilikuwa
inatisha lakini baba alikuwa akitembea bila kuonesha wasiwasi wa aina yoyote.
Mimi niliyekuwa nyuma yake nikiwa nimeshika sime mkononi ndiye niliyekuwa
nikitazama kila upande kwa wasiwasi.
Wakati tunazidi kutokomea
katika pori hilo, ghafla nilimuona baba akianza kusita
sita. Kasi yake ya kutembea ilipungua. Mwisho akawa aamesimama akielekeza mkono
upande wangu kama aliyekuwa akihitaji msaada.
Nikaushika mkono wake na
kumuuliza.
“Nini baba?”
Nikamuona kama aliyekuwa
anataka kuanguka, nikamshika vizuri.
Niliuona uso wake. Alikuwa
kama aliyekuwa akisikia maumivu.
Hakuweza kusema kitu hadi
nilipomlaza chini kichali chali.
Kwanza alinyoosha kidole chake kuelekea ule upande tuliokuwa
tunakwenda.
“Kule mbele kuna mti wa
mkuyu. Utakuta katika moja ya matawi yake nimening’iniza kitambaa chekundu na
cheusi...utakata kushoto utakuta kichaka kikubwa. Ukiingia ndani ya kichaka
hicho utakuta pango…” akaniambia lakini huo ulikuwa ndio mwisho wa maelezo
yake.
“Ni pango gani baba?”
nikamuuliza haraka.
“Safari yangu itaishia
hapa…wewe nenda tu…” akaniambia.
“Sijakuelewa baba. Unasema….?”
Kabla hata sijamaliza kumuuliza
nilichotaka kumuuliza alivuta pumzi ndefu kisha akazishusha. Akawa kimya. Hapo hapo nikajua kuwa baba yangu alikuwa
ameshakufa.
Alikuwa ameniacha njia panda.
Sikujua baba alikuwa ananipeleka wapi huko alikoniambia kuna pango. Na pia
sikujua alikuwa anakwenda kunionesha nini usiku ule.
Nilichofanya hapo ni kumbeba
begani na kurudi naye nyumbani. Kwa vile nilitembea naye mwendo mrefu, hadi
tunafika nyumbani nilikuwa nimechoka.
Nilimuingiza chumbani kwake
nikamlaza kitandani kisha nikammulika taa kumtazama usoni kwake. Kwa kweli mzee
alikuwa ameshakufa!
Likizo yangu ile ilikuwa ya
balaa. Nilipofika tu hapo Korogwe alikufa mwanangu, siku ile tena mzee wangu naye
ananiaga katika mazingira ya kutatanisha.
Baada ya kukaa na kuwaza
nikiwa pembeni mwa kitanda nilichoulaza mwili wa baba, nikayakumbuka yale
maneno ya baba aliyoniambia.
“Cha kwanza ninachotaka
kukwambia ni kuwa endapo nitafumba macho siku yoyote, urithi wako uko chini ya
mvungu wa kitanda nilicholala”
Nikajiambia baba yangu
alishajua kuwa atakufa leo ndio maana aliniita na kunieleza maneno hayo.
Lakini shauku ya kutaka kujua
kile alichoniambia ni urithi wangu kilichoko chini ya mvungu ikanipata.
Nikachutama na kumulika taa chini ya mvungu wa kitanda chake.
Nikaona mfuko wa ngozi kisha
nikaona sanduku la chuma. Shauku yangu ikawa kwenye lile sanduku la chuma.
Nikatia mkono mvunguni na
kulivuta. Lilikuwa zito. Ikabidi nitumie mikono miwili, nikalitoa kwenye
mvungu.
Lilikuwa llimefungwa kwa
kufuli kubwa ya shaba.
Nikafikiria niivunje ile kufuli ili nitazame kilichomo ndani lakini nikakumbuka
baba yangu alikuwa na tabia ya kutembea na funguo nyingi anazozifunga kiunoni.
Je nini kitatokea? Usikose kuwa nami hapo kesho hapahapa
No comments:
Post a Comment