RIWAYA
KAMA UNATAKA FEDHA ZA
MAJINI 10
ILIPOISHIA
Mke wangu akakata simu.
Badala ya kuwa na furaha ya kuzungumza na mke wangu, moyo wangu ukajaa
machungu.
Kile nilichokuwa nikikihofia
sasa kilikuwa kinakaribia kutokea.
Mke wangu umeng’ang’ania kuja
huku lakini huku kuna matatizo ambayo siwezi kukuambia kwa sasa, nikajikuta
nikisema peke yangu.
Nikajiambia kama mke wangu
atakuja hapo kesho huenda huo ukawa ndio mwisho wake.
Licha ya kutambua bayana madhara ambayo yangeweza kumkuta mke wangu
nilishindwa kumzuia asije. Mwenyewe ameshaanza shutuma zisizo na msingi, hajui
jinsi dakika zake zilivyokuwa zinakaribia.
Wakati nikiwaza hivyo kichwa
changu kilikuwa kipo kwenye mchakato wa haraka haraka kutafuta ufumbuzi wa
suala hilo.
Nikakumbuka ile ndoto niliyoiota kwamba nilikwenda Pemba
mahali panapoitwa Giningi na kukutana na
yule mwanamke wa kijini.
SASA ENDELEA
Nilikuwa nikifahamu kuwa jini huyo alichukuliwa na baba yangu
kutoka mahali hapo ambapo ndipo
alipopatia utajiri wake. Nikakumbuka kuwa yule jini alinieleza kuwa hapo
Giningi kuna mzee mmoja anayeitwa Habib Sultani ambaye ndiye anayewauzia watu
majini wanaozalisha pesa.
Hao majini wanamuita mzee
huyo “baba.”, yaani wanamfanya kama baba yao
na ndiye huyo ambaye katika ile ndoto niliambiwa amekwenda shamba.
Nikapata wazo moja. Wazo hilo lilikuwa ni kwenda Pemba
kumtafuta mzee huyo na kumueleza hali halisi kuhusu matatizo yaliyokuwa
yananikabili. Ikiwezekana nimrudishie pesa zake na yeye achukue majini wake.
Wazo hilo likanipa nguvu, nikaona ndio wazo pekee
ambalo litanipatia ufumbuzi wa matatizo yangu.
Sasa kama nataka kusafiri
kwenda Pemba, nikajimbia, muda ulikuwa ndio
ule. Sikuwa na muda tena wa kupoteza
kwani mke wangu angefika kesho yake.
Nikiianuka kwenye kitanda
nikaenda bafuni kuoga. Nilipomaliza nilirudi ndani nikavaa nguo nyingine za
safari. Nilichukua begi langu nikatia nguo mbili za akiba nikatoka na kufunga
mlango wa nyumba.
Sikumuaga mtu yeyote nikaanza
safari ya miguu kuelekea stendi ya mabasi. Nilipofika nilipanda basi la kwenda
Tanga.
Wakati nimo safarini kuelekea
tanga likanijia wazo jingine kuwa endapo sitampata huyo mzee nitafanya nini.
Kwa kweli hapo sikuwa na jibu lakini waswahili wanasema “Mfa maji hushika maji”
Na mimi kwa vile nilikuwa mfa maji nikaamua kushika maji.
Nilipofika Tanga nilikwenda
kwenye duka la mkazi mmoja wa Pemba ambaye nilikuwa nikimfahamu, nikamuulizia
kuhusu usafiri wa kwenda Pemba. Akaniambia
maneno ya kunikatisha tamaa.
“Usafiri wa kwenda Pemba
unafanyika kwa wiki mara moja, inabidi ukae hadi jumamosi ndio utapata usafiri
wa Pemba” Mtu huyo akaniambia.
Siku ile ilikuwa ni jumatano.
Kwa maneno yake ni kwamba nilipaswa kukaa hadi siku ya jumamosi ndipo niondoke
kwenda Pemba wakati nilihitaji kufika Pemba
siku ile ile.
Hapo nikagwaya. Jasho
lilikuwa linanitoka kwenye uso wangu.
“Kwani wewe ulihitaji kwenda
lini?” mtu huyo akaniuliza.
“Nilihitaji kufika leo”
“Labda uende Pangani. Kule
kuna usafiri wa kila siku wa kwenda Pemba na
Unguja”
“Si kitu, naweza kwenda
Pangani”
“Lakini usafiri wa huko ni wa
majahazi. Utaweza kusafiri kwenye jahazi?”
“Nitaweza. Acha jahazi hata
kwa dau nitakwenda”
Mpemba huyo akacheka.
“Kwani una dharura kubwa sana?” akaniuliza.
“Nina dharura kubwa, ni
muhimu nifike leo”
“Basi wewe nenda Pangani.
Mabasi ya Pangani yapo wakati wote”
Kutokana na muongozo wa
rafiki yangu huyo sikuhangaika tena kwenda bandarini kuulizia usafiri wa Pemba,
nikaenda katika kituo cha mabasi nikapanda basi la Pangani. Nililikuta basi hilo limejaa na lilikuwa
tayari kuazna safari. Ikanibidi nisimame baada ya kutopata siti.
Mpaka nafika Pangani ilikuwa
saa tisa alasiri. Nilikuwa na matumaini madogo sana ya kufika Pemba kwa siku
ile.
Ile ilikuwa ndio mara yangu
ya kwanza kukanyaga katika mji huo wa kihistoria niliokuwa nikiusikia na
kuusoma kwenye ramani. Nilikuwa na shauku ya kwenda kupaona mahali palipokuwa
na soko la watumwa ambapo pamekuwa ni kivutio kikubwa cha watalii lakini muda
haukuniruhusu.
Nilishuka pwani nikakuta
kulikuwa na majahazi kibao.
Ili nijue taratibu za usafiri
wa hapo nilimfuata mtu mmoja nikamuulizia kuhusu usafiri wa Pemba.
“Muulize mtu yule pale”
Mtu huyo naye akanielekeza
kwa mtu mwingine aliyekuwa amekaa pembeni chini ya mti akivuta sigara.
Jinsi alivyokuwa amevaa
alionesha alikuwa mmoja wa manahodha wa zile jahazi. Nikamfuata.
Wakati namkaribia nilianza
kusikia kupuo la harufu ya bangi. Yule mtu alikuwa akizidi kupuliza moshi.
Nilipofika karibu yake nikagundua kuwa sigara aliyokuwa akivuta ilikuwa bangi.
Alikuwa akivuta kwa uhuru
bila kujali kuwa alichokuwa akivuta kilikuwa haramu. Mpaka ninamfikia
hakuonekana kushituka. Alikuwa akiendelea kuvuta.
“Habari ya saa hizi?”
nikamsalimia mtu huyo aliyekuwa na mwili mfupi uliokakamaa.
Alikuwa na macho madogo
yaliyoiva kwa bangi.
Mtu huyo akanitazama kisha
akanijibu.
“Nzuri”
“Nilikuwa naulizia usafiri wa
kwenda Pemba”
“Wewe ndiye unayetaka kwenda
Pemba?” akaniuliza.
“Ndiyo.
“Jahazi ile pale, tutaondoka
sasa hivi”
Alinionesha jahazi moja iliyokuwa
baharini ambayo tayari ilikuwa imejaa
watu.
“Kwa hiyo niende nikajipakie”
“Lipa nauli kwanza”
“Ni kiasi gani?”
“Elfu saba”
Niliona kilikuwa kiasi kidogo
sana. Nikatoa kiasi hicho na kumpa.
Nilimpompa pesa hizo alizima
bangi yake. Kipisi kilichobaki alikitia mfukoni kisha akainuka.
“Haya twende” akaniambia.
Nikafuatana naye kuelekea
baharini.
“Sega suruali yako isiingie
maji” akaniambia.
Nikasega suruali yangu.
Tukaenda kupanda jahazi pamoja. Kumbe alikuwa akisubiriwa yeye avute bangi
kwanza ndipo jahazi liondoke.
Nilitafuta mahali nikakaa na
kuanza kuitafakari safari hiyo ambayo ilishaanza kunitia mashaka.
Nahodha mwenyewe ameshavuta
bangi, jahazi limejaa abiria na mizigo na bahari ilionekana haikuwa shwari.
Lakini kutokana na umuhimu wa
safari yenyewe ilibidi niende tu. Ingawa mimi nilipata hofu kidogo lakini
usafiri huo ndio unaotumiwa siku zote na baadhi ya abiria kwa vile unapatikana
kila siku na nauli yake ni nafuu.
Yule mtu alikuwa ndiye
nahodha. Akiwa kwenye ile jahazi alikuwa na lugha chafu na alikuwa mkali kama
pilipili.
Dakika chache tu baada ya kujipakia sisi safari ikaanza.
Jahazi iliondoka polepole, tukaanza kuiacha pwani ya Pangani. Baada ya masaa
mawili mji wa Pangani hatukuuona tena.
Ghafla upepo mkali ukaanza
kuvuma tukawa tunakutana na mawimbi makubwa makubwa. Nikaona baadhi ya abiria wanawake wakianza kupiga kelele. Huku
baadhi wakitapika hasa watoto.
Chombo chetu kilikuwa
kikiinuliwa na mawimbi na kisha kurudishwa chini kwa kishindo. Abiria mmoja
ambaye nilikuwa nimekaa naye akaanza kutapika.
Nahodha alikuwa amesimama
ameshikilia kamba. Kazi yake ilikuwa ni kulielekeza jahazi kulielekea wimbi
linapotokea. Sikujua ilikuwa ni kwanini alifanya vile. Mimi niliona ilikuwa vyema kulikwepa wimbi na sio kulifuata.
Wakati anapolielekea wimbi
ndipo jahazi linapoinuliwa na kisha kurudishwa chini na hapo ndipo watu
wanapotapika na kupiga kelele.
Hali ilizidi kuwa mbaya mpaka
mimi mwenyewe nikaona matumbo yamenichafuka. Nikasikia baadhi ya abiria wakipiga
kelele kumwammbia nahodha.
“Rudisha chombo
bandarini! Rudisha chombo bandarini!
Hali si shwari”
Wengine walikuwa wakisema.
“Nahodha utatuua wewe, kuna
watoto humu!”
“Alikuwa akivuta bangi, huyo
hana akili!” Mwanamke mmoja alisema kwa hasira.
Pamoja na kelele zote hizo nahodha
huyo hakumsikiliza mtu yeyote, aliendelea kukielekeza chombo hicho kwenye
mawimbi. Ile dharuba iliyokuwa ikitupiga haikumtia hofu hata chembe.
Pale ndipo nilipogundua
sababu ya baadhi ya manahodha kuvuta bangi, ni kutaka kupata uwezo wa kiakili
wa kukabiliana na ile hali endapo itatokea.
Yule mtu alionekana kama
mwehu. Wimbi linapokuja linatutosa. Na yeye alitota chapa chapa lakini
hakuonesha kupata hofu wala kujali. Siku ile niliapa kuwa sitasafiri tena na
jahazi na sikujua kama tungefika salama Pemba.
Yale mawazo ya kufa
yakanifanya nimkumbuke mke wangu. Nikakumbuka kwamba nilimuahidi kumtumia nauli
na nikahisi kwamba angenipigia simu kuniulizia tena.
Nikatoa simu yangu na kuizima
ili akipiga simu asinipate.
No comments:
Post a Comment