Tuesday, October 10, 2017

HADITHI, MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI SEHEMU YA 11

HADITHI hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya usafirishaji wa abiria FREYS LUXURY COACH ifanyayo safari zake Tanga hadi Singida kila siku kupitia Moshi, Arusha na Babati, na hufanya hivyo kutoka Singida kwenda Tanga kila siku, simu, 0622 292990

MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI 11

ILIPOISHIA


“Na ni kwanini likamatwe gari langu wakati jiji hili lina maelefu ya  magari ya aina ile ya rangi nyeupe?”

“Polisi wanaweza kufanya msako wa kuyakamata”

“Watakamata magari mangapi na watakwenda kuyaweka wapi. Mimi nikisikia kuna msako huo nitawazuia. Nitawambia zoezi hilo litasumbua wananchi”

“Si itaonekana unazuia upelelezi?”

“Hapana. Sasa tujiandae twende huko kwenye msiba tuwape pole na pia tutoe ubani wetu”

“Sawa”

Baada ya kumaliza kula chakula cha mchana Waziri Mkuu na mke wake walikuwa kwenye magari mawili tofauti huku wakiongozwa na gari la polisi lililokuwa na kimulimuli.

Walifika Kinondoni nyumbani kwa wazazi wa Pili ambako tayari watu walikuwa wamejaa na vilio vilikuwa vimetawala.


SASA ENDELEA

Walishuka kwenye gari na kupokelewa na mzee Amrani, baba yake Pili ambaye aliwakaribisha ndani. Wakati Waziri Mkuu alipelekwa upande wa wanaume, mke wake alipelekwa upande wa wanawake.

Baada ya Waziri Mkuu kumpa pole baba wa marehemu na mama wa marehemu pamoja na ndugu wengine, alieleza jinsi alivyoshitushwa na kusikitishwa na mauaji ya mfanyakazi wake huyo.

“Marehemu alikuwa mtumishi mwenye bidii na muaminifu ambaye alikuwa kama sehemu ya familia yangu kutokana na ukaribu wetu. Nasema kwamba tumesikitishwa na kuhuzunishwa kutokana na kifo chake cha ghafla wakati tukiwa bado tunampenda na kumuhitaji. Lakini tuishie tu kusema kwamba bwana ametoa na bwana ametwaa…”  Waziri Mkuu alisema akionesha kusikitika.

Baada ya maelezo yake marefu alitoa shilingi milioni moja ambazo alimwambia baba wa marehemu zilikuwa za ubani wake pamoja na mke wake.

“Tunakushukuru sana mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuungana na sisi katika msiba huu wa binti wetu” Mzee Amrani alimshukuru baada ya kupokea pesa hizo.

Mazishi yatakuwa lini?”

“Tumepanga mazishi yawe kesho saa saba mchana”

“Basi nitafika tumsindikize mwenzetu”

“Tutashukuru sana”

Waziri Mkuu na mke wake hawakukaa sana wakaondoka.

Wakati wanaondoka tu, Thabit Kombo na Inspekt Alex wakawasili kwa gari. Walisimamisha gari mbele ya nyumba ya mzee Amrani kisha wakashuka.

Mzee Amrani alikuwa bado yuko nje akizungumza na watu, Alex akamuona.

“Mtu tunayemtaka yule pale” akamwambia kachero Kombo akimuonesha mzee huyo aliyekuwa amesimama akiwatazama.

“Karibuni” aliwambia huku akimkumbuka Inspekta Alex ambaye ndiye aliyefika kwake mapema na kumpa taarifa ya kifo cha binti yao.

“Tumekuja tena mzee” Alex alimwambia walipomkaribia.

“Ndio. Habari za kazi?”

“Nzuri. Nimekuja na afande wangu kutoka makao ya polisi. Alitaka kukuona na kuzungumza na wewe”

“Nipo tayari kuzungumza naye”

“Tunaweza kwenda nyumba ya pili tukae barazani tuzungumze” Kombo alimwmbia.

“Hakuna shaka, karibuni sana”

Mzee Amrani aliwapeleka nyumba ya pili wakakaa barazani.

“Kwanza nakupa pole sana kutokana na msiba uliotokea’ Kombo alimwambia huku akimpa mkono.

“Asante. Nawashukuru sana vijana wangu”

“Kwa Mungu ndiko tutokeako na ndiko tunakorudi”

“Ni kweli. Kila nafsi itayaonja mauti”

“Sasa mzee wangu nilitaka kukuhoji maswali mawili matatu kuhusiana na marehemu”

“Uliza”

“Mrehemu alikuwa akiishi wapi?”

“Alikuwa akiishi hapa hapa Kinondoni mtaa mwingine. Alikuwa amepanga nyumba”

“Alikuwa anaishi na nani?”

“Katika ile nyumba walipanga watu wawili, yeye na mwanamke mwenzake. Kila mmoja alikuwa na upande wake’

“Nazungumzia kwa yeye, alikuwa anaishi na nani?”

“Alikuwa akiishi peke yake”

“Kwa kadiri unvyofahamu binti yako hakuwa na rafiki wa kiume au wa kike?”

“Marafiki zake siwezi kuwajua isipokuwa binti yangu alikuwa na mchumba’

“Anaitwa nani?”

“Anaitwa Stambuli”

“Mara yako ya mwisho kukutana na binti yako ilikuwa lini?”

“Kila baada ya siku mbili ni lazima aje nyumbani kutujulia hali. Kama sikosei juzi usiku alikuja nyumbani alipotoka kazini kwake”

‘Mara nyingi akitoka kazini anapendelea kutembelea sehemu gani”

Mzee Amrani akatikisa kichwa.

“Kwa kweli siwezi kujua”

“Hilo ndilo swali la msingi lililotuleta hapa kutaka kujua alipotoka kazini jana alikwenda wapi. Tuliambiwa kwamba alikuwa anaumwa na kichwa na aliondoka kazini mapema”

“Jana mpaka saa moja na nusu usiku alikuwa yuko kazini kwake. Nilimtumia meseji kumuuliza kama ametoka kazini, nilikuwa na shida ya kuonana naye, akaniambia bado yuko kazini na hakuniambia kwamba alikuwa anaumwa…”

Kombo alishituka. Waziri Mkuu alimwambia Pili aliondoka kazini saa kumi na moja jioni baada ya kujihisi kuumwa na kichwa.

“Una uhakika na unachokisema mzee wangu?” Kombo akamuuliza Mzee Amrani kwa uso wa mashaka.

“Nina uhakika. Meseji aliyonitumia hii hapa, sijaifuta baado”

Mzee Amrani alitoa simu yake akaingia eneo la meseji na kumuonesha Kombo meseji hiyo aliyotumiwa na mwanawe.

Kombo aliiona.

“Alikutumia meseji hii saa moja na nusu usiku!”

“Ndiyo. Kama ulivyoona mwenyewe, ameniambia hadi muda huo alikuwa bado yuko kazini”

“Na hakukwambia kwamba alikuwa anaumwa?”

“Hapana. Hakuniambia. Kama angekuwa anaumwa angenijulisha”

Kombo akashusha pumzi ndefu. Aliona ulikuwepo utata, tena utata mkubwa.

“Baada ya kutumiana naye meseji, hukuweza kuonana naye tena?”

“Sikukutana naye tena hadi nilipopata taarifa ya kifo chake”

“Kwa hiyo huwezi kujua alirudi saa ngapi nyumbani?”

“Siwezi kujua”

“Sasa ningetaka utupeleke katika hiyo nyumba aliyokuwa anaishi ili huyo mwenzake anayeishi naye upande wa pili atueleze kama alimuona aliporudi”

“Sawa, naweza kuwapeleka”

Dakika chache baadaye makachero hao wakawa wamempakia mzee huyo kwenye gari wakielekea katika nyumba aliyokuwa akiishi Pili.

Nyumba hiyo ilikuwa mtaa wa tatu kutoka mtaa aliokuwa akiishi mzee Amrani.

Walipofika Mzee Amrani aliwaonesha upande aliokuwa akiishi Pili na upande aliokuwa akiishi mwenzake. Kombo akabisha mlango wa upande wa pili. Baada ya muda kidogo akatoka msichana mmoja aliyekuwa amejifunga khanga mabegani na kiunoni.

“Karibuni” akasema kwa sauti ya wasiwasi, uso wake ukionesha huzuni.

Alipomuona mzee Amrani alijaribu kutabasamu.

“Baba tumekutana tena. Naweza kuwasaidia, mna tatizo gani?”

“Sisi ni polisi wa upelelezi, tulikuwa tunachunguza kuhusu mauaji ya Pili” Kombo alimwambia na kuongeza.

“Tumekuja kwako ili uweze kutusaidia lolote unalolijua kuhusu marehemu”

“Marehemu nilikuwa ninaishi naye nyumba moja lakini kila mmoja alikuwa na upande wake. Mimi ninaishi upande huu mwenzangu alikuwa anaishi upande mwingine” Msichana huyo alijibu haraka kama vile alihisi maneno hayo yangewasaidia sana polisi hao.

“Lakini ni watu mliokuwa mko karibu” Kombo alimwambia.

“Ndio. Tulikuwa tuko karibu. Karibuni ndani”

Msichana huyo aliyeonekana kuwa mchangamfu aliwakaribisha sebuleni. Sebule yake ilikuwa ndogo lakini ilipambwa vizuri.

“Karibuni mkae” aliwambia huku naye akiketi.

Baada ya watu wote kukaa kitako Kombo aliendelea na maswali.

“Kwa kifupi tulichotaka kujua, Pili alirudi saa ngapi jana kutoka kazini kwake?”

“Jana nilikutana na Pili asubuhi tu wakati anatoka kwenda kazini kwake. Yeye huwa anawahi kutoka kabla ya mimi. Lakini sikumuona kurudi tena”

“Kwani anaporudi huwa anakutambulisha”

“Anaweza kuja kwangu au mimi nakwenda kwake, tunapiga stori hadi wakati wa kulala. Lakini jana sikumuona na hata taa hazikuwashwa”

“Kama taa hazikuwashwa inamaanisha kuwa hakurudi” Mzee Amrani akasema.

“Tulifikiri labda alirudi kisha akakuaga kuwa anakwenda sehemu fulani” Kombo akamwambia msichana huyo.


ITAENDELEA kesho usikose uhondo huu hapahapa tangakumekluchablog KUMEKUCHA UPYA

No comments:

Post a Comment