HADITHI
MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA
UKINGONI 16
ILIPOISHIA
Baada ya hapo ndipo mke wa
Waziri Mkuu alipomsafisha Monica ile damu na kuliweka vizuri lile jaraha ili
lisioneshe athari ya meno.
“Mimi naona tuweke plasta
hapa watakaomuosha wataiondoa watajua alijiumiza mwenyewe” Mke wa Waziri Mkuu
alishauriana na mume wake ambaye limkubalia.
Baada ya kuushughulikia mwili
wa Monica ndipo Waziri Mkuu alipotoa taarifa ya kifo cha mwanawe usiku ule ule.
Viongozi wa serikali wakaanza
kumiminika nyumbani kwa Waziri Mkuu. Raisi mwenyewe pia alifika usiku huo huo
baada ya kupata habari ya kifo hicho.
Waziri Mkuu alikuwa akitoa
maelezo ya uongo aliyokuwa ameyapanga na mke wake juu ya kifo cha binti yao.
Kwa vile kifo hicho kilikuwa
kimetokea ghafla, watu wengi walipatwa na mshangao waliposikia taarifa ya
Waziri Mkuu.
SASA ENDELEA
Asubuhi kulipokucha
maombolezo yakaanza nyumbani kwa Waziri Mkuu. Wakati wote mke wa waziri Mkuu na
Vero, binti yao
wa kwanza, walikuwa sambamba na Sofia. hawakumpa nafasi ya kuwa peke yake kwa
sababu yakutomuamini.
Hatimaye mwili wa Monica
uliagwa kwa heshima za viongozi wa Serikali na wananchi waliofurika mchana kabla ya kusafirishwa kijijini kwao Morogoro kwa ajili ya
mazishi.
Baada ya mazishi ya Monica
ndipo Waziri Mkuu na mke wake walipokaa chini kulizungumzia suala la Sofia.
“Sasa itabidi uende naye Nairobi kama ambavyo
tulipanga” Waziri Mkuu alimwambia mke wake.
“Niende naye lini?”
“Hatuna muda wa kupoteza,
yasije yakatokea mengine. Utakwenda naye kesho kwa ndege”
“Umeshatayarisha mipango
yote?”
“Mipango iko tayari.
Kinachohitajika ni safari tu”
“Sawa”
Siku
iliyofuata Sofia na mama yake wakapanda ndege kuelekea Nairobi nchini
Kenya. Walitua katika uwanja wa Jommo Kenyatta wakapanda teksi iliyowapeleka
katika
hospitali ya magonjwa ya akili iliyokuwa nje kidogo ya jiji la Nairobi.
Siku ile ile vipimo vya akili
ya Sofia
vilichukuliwa na siku ile ile matokeo yake yalipatikana. Sofia aligunduliwa alikuwa mzima kabisa wa
akili. Matokeo hayo yalimshangaza mama yake.
Akaona ampigie mume wake
kumjulisha.
Waziri Mkuu alipoambiwa hivyo
na mke wake naye alishangaa.
“Hawakugundua tatizo lolote?”
akamuuliza.
“Ripoti yake inaonesha kuwa
hana tatizo lolote la akili”
“Umewaeleza kuhusu vitendo
ambavyo amevifanya”
“Siwezi kuthubutu kufanya
hivyo”
“Ni kweli. Sasa jaribu
kuchukua vipimo vya malaria”
“Itabidi twende katika
hospitali nyingine. Hii ni ya magonjwa ya akili peke yake”
“Mnaweza kwenda”
Sofia na mama yake wakapanda tena teksi iliyowapeleka
katika hospitali nyingine iliyokuwa katikati ya jiji.
Sofia alifanyiwa uchunguzi wa damu yake kuangalia vimelea
vya malaria lakini jibu lililotoka ni kuwa Sofia hakuwa akiugua malaria.
Mama yake alimpigia tena simu
mume wake akamjulisha kuhusu matokeo hayo.
“Mh! Ni mambo ya ajabu!”
Waziri Mkuu akasema.
“Lingekuwepo moja kati ya
malaria au ugonjwa wa akili tungeelewa”
“Sasa tuseme ana tatizo
gani?”
“Tatizo lake halijulikani”
“Halijulikani lakini lipo.
Lazima tatizo liwepo”
“Sisi tunalala leo tunarudi
kesho”
Waziri Mkuu akanyamaza kimya.
“Mbona umenyamaza?”
“Ninafikiria. Tegemeo langu
kubwa lilikuwa huyo mtoto atakutwa na matatizo kichwani mwake…”
“Hayakukutwa. Sasa
unashaurije?”
“Basi mnaweza kurudi hapo
kesho”
Usiku wa siku ile walilala
katika hoteli moja jijini humo asubuhi yake wakapanda ndege kurudi Dar.
Waziri Mkuu alituma gari
kwenda kuwapokea kiwanja cha ndege. Gari hilo
liliwapeleka nyumbani. Siku iliyofuata Sofia
na mama yake walikwenda kwao Morogoro.
Mke wa waziri Mkuu akaenda
kwa mganga mmoja kijijini kwao na kumuelezea kuhusu matatizo ya mwanawe.
“Inawezekana ana matatizo
lakini hatuwezi kuyajua mpaka nipige ramli” Mganga akamwambia.
“Tunataka tuyajue na uyatibu,
piga ramli”
Mganga akapiga ramli yake ya
kuchungulia tunguri. Alikuwa akichungulia kwenye tundu ya tunguri kisha anaeleza alichokuwa
anakiona.
“Ramli yangu inanionesha
mbali sana”
Mganga akasema.
“Mbali, wapi?”
“Ramli inakwenda kwa baba
yake”
“Amefanya nini?”
“Huyu ndiye amemdhuru mtoto…”
“Eti nini, baba yake ndio
amemdhuru binti yetu? Amemdhuru kivipi?”
“Hebu nieleze wewe mke wake,
kabla ya mumeo kuwa Waziri Mkuu alifanya nini?”
Mke wa Waziri Mkuu akabetua
mabega.
“Sijui”
“Hakuna sehemu ambayo
alikwenda kutambika au kufanya maombi?”
“Ndiyo nakumbuka. Alikwenda
kwa bibi mmoja kijijini kwao wakaenda kwenye mzimu”
“Walikwenda kwenye huo mzimu
kwa madhumuni gani?”
“Mh! Ni kwa mambo yao haya ya kisiasa”
“Yapi,
hebu nieleze”
“Mimi aliniambia alikwenda
kutambikiwa na kuweka nadhiri kwenye mzimu wa kwao kuwa endapo atateuliwa kuwa
Waziri Mkuu atapeleka ng’ombe kwenye ule mzimu”
“Je alipoteuliwa kuwa Waziri
Mkuu alitimiza nadhiri aliyoweka?”
“Mh! Sijui sasa…”
“Nenda kamuulize alipeleka
yule ng’ombe?”
“Kwa hiyo kama
hakupeleka linaweza kuwa ndio tatizo?”
“Ndio”
“Sasa ngoja nirudi Dar,
niende nikamuulize Jibu atakalonipa nitakuja kukuambia”
“Utakuja lini tena?”
“Nitakuja kesho”
“Utanikuta”
Mke wa Waziri Mkuu akarudi
Dar pamoja na Sofia. Wakati wa usiku akamueleza mumewe kuwa alikwenda kwa
mganga wa kienyeji na kuelezwa aliyoelezwa.
Waziri Mkuu alipoyasikia
maelezo ya huyo mganga akashituka.
Mawazo yake yakarudi nyuma miaka kadhaa iliyopita, wakati huo akiwa Waziri wa
Nchi ofisi ya Makamu wa Rais.
Chama chake kilikuwa
kimeshinda uchaguzi. Rais alikuwa anasubiri kuapishwa ili aunde serikali yake. Kulikuwa na watu watatu waliokuwa
wakitajika kupewa wadhifa huo, mmojawapo akiwa yeye.
ITAENDELEA kesho kesho Usikose Uhondo huu nini kitafuatia
No comments:
Post a Comment