Saturday, October 7, 2017

HADITHI, MBIO ZA SAKAFUNI KUISHIA UKINGONI SEHEMU YA ( 7 )

HADITHI inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya mabasi ya FREYS LUXURY COACH zifanyazo safari zake Tanga, hadi Singida kupitia Moshi, Arusha, Babati hadi Singida kila siku, simu 0622 292990

MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI 7

ILIPOISHIA

“Ni kazi yetu sisi polisi kuchunguza na kujua ni nani aliyefanya unyama huo. Kwa vile tumeshapata taarifa hii tutaifanyia kazi”

“Mtaweza kuwakamata hao watu?”

“Kama tutafanikiwa kuwagundua tutawakamata tu”

“Ninawaomba mjitahidi kufanya hivyo ili watu hao wafikishwe mahakamani wapate adhabu inayostahili kwa kosa lao”

“Nimekuelewa. Sasa ninakuomba unifikishe kwa ndugu na jamaa wa marehemu”

                                             ***************

Kwa upande wa Waziri Mkuu, saa tatu  kamili asubuhi Waziri Mkuu alikuwa ofisini kwake. Kabla ya kuondoka nyumbani kwake alimwambia mke wake ikifika saa nne aijaribu namba ya marehemu Pili aone kama inaita. Kama inaita na kama itapokelewa aulize ni kwanini Pili hajafika kazini hadi muda huu.

Wakati Waziri Mkuu yuko ofisini kwake, mke wake akampigia simu kwa kutumia namba za simu za mikononi.

“Kuna taarifa yoyote uliyoipata huko?’ akamuuliza.

“Sijapata taarifa yoyote, je wewe umesikia lolote?”

“Sijasikia kitu ndio maana nimekuuliza wewe”

“Mimi pia sijapata taarifa yoyote”

“Umefanya vile nilivyokwambia?”

“Ndiyo nataka nipige ile namba”

“Piga sasa hivi”

“Sawa”

SASA ENDELEA

Vicky akakata simu na kuipiga namba ya Pili. Simu ya Pili ikawa inaita. Vicky alishituka. Wakati ule Inspekta Alex ndio alikuwa anataka kutoka ofisini na Stambuli.

Simu ya Pili ilikuwa mezani kwa Inspekta Alex. Alex alipoona simu hiyo inaita akaishika na kutazama namba iliyokuwa inapiga.

Namba ilikuwa imehifadhiwa kwa jina la “Mama Lazaro”. Wakati anaipokea Alex hakutambua kuwa jina hilo lilimaanisha mke wa Waziri Mkuu Dastan Lazaro.

“Halloh!” Akasema baada ya kuipokea simu hiyo.

Mke wa Waziri Mkuu aliposikia sauti ya kiume akauliza.

“Wewe nani?”

“Ungejitambulisha wewe kwanza”

“Mimi ni mke wa Waziri Mkuu, hii namba ni ya mpishi wa nyumbani ambaye hajafika kazini hadi sasa”

Inspekta Alex akagwaya.

“Samahani mama Lazaro, sikukufahamu. Kuna tatizo limetokea?”

“Tatizo gani?”

“Hapa unaongea na Inpekta Alex wa kituo cha polisi cha Kinondoni….” Alex akamueleza tukio zima lililokuwa limetokea.

Mke wa Waziri Mkuu akajifanya anashituka.

“Pili ameuawa? Ameuawa wakati gani?”

“Ndio tunaendelea na uchunguzi ili tujue aliuawa na kina nani na aliuawa wakati gani?”

“Madaktari wameshaufanyia uchunguzi mwili wa marehemu?”

“Wameufanyia uchunguzi na wameshatupa taarifa ya uchunguzi wao”

“Wamegundua marehemu ameuawa kwa kitu gani?”

“Taarifa yao inatatiza kidogo. Wanasema alifyonzwa damu kupitia mshipa wake wa shingo”

Mke wa Waziri Mkuu aligutuka akaikumbuka ile damu waliyoikuta midomoni mwa mwanawe.

“Yaani kufyonzwa damu ndio kumesababisha kifo chake?”

“Ndiyo uchunguzi wa madaktari ulivyoonesha”

“Sasa hiyo damu alifyonzwa na mnyama au binaadamu?”

“Taarifa imesema alifyonzwa na binaadamu”

“Wana uhakika gani?”

“Wamegundua chembechembe za mate ya binaadamu kwenye shingo yake”

“Sasa nyinyi polisi mtafanya nini?”

“Ndio tunawatafuta waliohusika na tukio hilo”

“Kweli mtaweza kumgundua mtu aliyefanya hivyo”

“Anaweza kugundulika”

“Kwa namna gani?’

“Mtu ambaye tutamshuku tutampeleka hospitali ili mate yake yafanyiwe uchunguzi, kama zitapatikana chembechembe za mate aliyokutwa nayo marehemu, atakuwa ndiye huyo huyo”

Mke wa Waziri Mkuu akashusha pumzi.

“Sasa ngoja nimfahamishe mheshimiwa kwa sababu hadi sasa hana taarifa yoyote”

“Sawa mama Lazaro”

Mke wa Waziri Mkuu akakata simu.

Alipokata akampigia mheshimiwa wake Dastan Lazaro.

Akamueleza kila kitu alichoelezwa na Inspekta Alex. Kilichomshitua mheshimiwa Waziri Mkuu ni maneno ya mke wake alipomwambia ameelezwa kuwa muuaji anaweza kugunduliwa kutokana na chembechembe za mate yake endapo yatafanyiwa uchunguzi.

Waziri Mkuu akajiambia kama polisi watataka kuja kufanya uchunguzi nyumbani kwake na kumtilia shaka mwanawe Sofia, itakuwa kazi ndogo kugundua kuwa ndiye yeye aliyemfyonza damu marehemu. Ni kiasi cha kumpeleka hospitali ya Muhimbili tu!

“Nitakuja nyumbani mchana tuongee vizuri” Waziri Mkuu akamwambia mke wake kwa sauti iliyofadhaika.

Alipoiweka simu juu ya meza aliinamisha kichwa chake na kuanza kujiwazia. Alikuwa na muda mfupi tu toka ashike wadhifa huo wa Waziri Mkuu.

Chama cha Rais Isaac Mosha kilipotwaa madaraka mwaka mmoja uliopita kufuatia uchaguzi wa vyama vingi, Rais Mosha alimteua yeye kushika wadhifa huo wa Waziri Mkuu. Alikuwa mmoja kati ya wabunge watatu wa chama chake waliofikiriwa kuwa wangeweza kutwaa wadhifa huo.

Alijiambia endapo itajulikana kuwa ni mwanawe aliyemuua mpishi wao, tukio hilo linaweza kuwa kashfa kubwa kwa upande wake na atalazimika kuwajibika.

Atapoteza kazi, atapoteza heshima na atapoteza madaraka yake ambayo mwenyewe alijua hakuyapata kirahisi kama watu wengi walivyokuwa wakidhani.

Hivyo alikuwa na kila sababu ya kufadhaika na kupata hofu.

                                           **********

Mara baada ya kuzungumza na mke wa Waziri Mkuu, Inspekta Alex alitoa taarifa ya kuzungumza na mama Lazaro kwa mkuu wake kisha akamtaka Stambuli ampeleke kwa wazazi wa marehemu Pili.

Stambuli ambaye katika muda wote alikuwa akihuzunika kutokana na kuuawa mpenzi wake, alimpeleka mpelelezi huyo katika mtaa mmoja walikokuwa wakiishi wazazi wa marehemu Pili.

Alex alikutana na baba yake Pili, mzee Amrani na mama Amrani na kuwauliza kama wana binti anayeitwa Pili Amrani ambaye ni mpishi wa Wairi Mkuu.

Wazee hao walikubali kuwa wana binti huyo.

“Je mna taarifa zake zozote?”

“Taarifa kama zipi?” mzee Amrani alimuuliza akiwa ameshituka.

“Inaonekana kama hamna taarifa ya tukio lililotokea”

“Labda hatuna, hebu tufahamishe”

“Nasikitika kuwambia kuwa binti yenu ameuawa”

Inspekta Alex alishuhudia uso wa mzee Amrani na wa mke wake ukitepeta.

“Unasemaje. Binti yetu ameuawa?” mzee Amrani akamuuliza Alex kwa taharuki.

Alex akawaeleza mkasa mzima uliotokea.

“Upelelezi bado unaendelea na mwili wa marehemu upo hospitali ya Muhimbili”

Tayari machozi yalikuwa yakimtoka mama Amrani.

“Ni nani aliyemfanyia mwanangu unyama huo jamani?” alihoji kwa uchungu.

“Kama nilivyowambia tupo kwenye uchunguzi, ni imani yetu kuwa mtu huyo au watu hao watapatikana” Alex aliwambia.

                                      *************

Alex alirudi kituoni akiwa ameshamuacha Stambuli. Aliporudi tu alikutana na mlinzi wa shule ya msingi ya Kinondoni akimsubiri.

“Nilikuwa nimetoka kidogo” alimwambia baada ya kushuka kwenye gari.

“Niliambiwa kuwa umetoka nikaona nikusubiri” Mlinzi huyo aliyefika akiwa na mavazi yake ya kiulinzi alisema.

“Sawa. Tuingie ofisini”

Waliingia ofisini mwa Inspekta Alex.

“Kaa kwenye kiti”

Mlinzi huyo alikaa kuielekea meza iliyokuwemo ofisini humo.

Baada ya Alex kuketi alifungua faili lililokuwa juu ya meza yake kisha akamtazama mlinzi huyo.

“Madaktari wametuambia yule msichana alifyonzwa damu pale shingoni kisha maiti yake ikaja kutupwa kule shuleni” akamueleza.

“Alifyonzwa damu?” Mlinzi alishituka.

“Ndio uchunguzi wa madaktari umeonesha kuwa alifyonzwa damu”

“Alifyonzwa damu kwa wapi?”

Itaendelea kesho usikose uhondo huu, KUMEKUCHA UPYA

No comments:

Post a Comment