RIWAYA
KAMA UNATAKA FEDHA ZA MAJINI
3
ILIPOISHIA
Baada ya kukaa na kuwaza
nikiwa pembeni mwa kitanda nilichoulaza mwili wa baba, nikayakumbuka yale
maneno ya baba aliyoniambia.
“Cha kwanza ninachotaka
kukwambia ni kuwa endapo nitafumba macho siku yoyote, urithi wako uko chini ya
mvungu wa kitanda nilicholala”
Nikajiambia baba yangu
alishajua kuwa atakufa leo ndio maana aliniita na kunieleza maneno hayo.
Lakini shauku ya kutaka kujua
kile alichoniambia ni urithi wangu kilichoko chini ya mvungu ikanipata.
Nikachutama na kumulika taa chini ya mvungu wa kitanda chake.
Nikaona mfuko wa ngozi kisha
nikaona sanduku la chuma. Shauku yangu ikawa kwenye lile sanduku la chuma.
Nikatia mkono mvunguni na
kulivuta. Lilikuwa zito. Ikabidi nitumie mikono miwili, nikalitoa kwenye
mvungu.
Lilikuwa llimefungwa kwa
kufuli kubwa ya shaba.
Nikafikiria niivunje ile kufuli ili nitazame kilichomo ndani lakini nikakumbuka
baba yangu alikuwa na tabia ya kutembea na funguo nyingi anazozifunga kiunoni.
SASA ENDELEA
Nikajua lazima kutakuwa na
funguo ya kufuli ile.
Nikainuka na kumtazama
kiunoni. Nikaziona zile funguo alizozifunga kwenye mkanda wake. Nikazitoa.
Zilikuwa karibu funguo tano.
Nikawa natafuta ufunguo unaokubaliana na ile kufuli. Nikagundua funguo mbili.
Kwa vile sikujua ni funguo ipi itakayofungua ile kufuli, nilizijaribu zote.
Moja ilikataa hata kuingia kwenye tundu ya kufuli. Nyingine ikakubali na ndiyo
iliyofungua kufuli hiyo.
Kufuli ilipofunguka
niliichomoa nikaufungua mlango wa sanduku hilo.
Nilipotupa macho ndani nilishituka nikajiuliza kama
kweli baba yangu alikuwa na utajiri wa kiasi kile!
Noti nyekundu za elfu kumi
kumi zilikuwa zimejaa ndani sanduku hilo
hadi juu! Wakati ninazitazama niliona kama
ninachanganyikiwa kwa sababu sikuwahi kuona fedha nyingi kiasi hicho.
“Baba yangu alizipata wapi
pesa hizi?” nikajiuliza kwa mshangao lakini sikupata jibu akilini mwangu.
Nikaona nizitoe zile pesa na
kuzihesabu. Nilifanya ile kazi usiku kucha! Mpaka kunaanza kupambazuka sikuwa
nimemaliza kuzihesabu noti zote.
Nikaona nizirudishe kwenye
lile sanduku. Nikalifunga na kutia ile kufuli kisha nikalibeba na kwenda nalo
katika chumba nilichokuwa ninalala mimi. Nikalitia mvunguni.
Nikarudi tena katika chumba
cha baba. Nikaufunika mwili wake kwa shuka yake aliyokuwa akijifinika. Nikaamua
nikae kwenye kiti nisubiri kuche ili nitoe taarifa kwa majirani kuwa mzazi
wangu amefariki usiku.
Ilipofika saa kumi na mbili
asubuhi nikampigia simu mke wangu na kumjulisha kuwa babamkwe wake amefariki
usiku.
Mke wangu alishituka sana akaniambia
angefanyaje wakati baba yake naye alikuwa katika hali mbaya.
“Wewe mshughulikie mzazi wako
kwanza, huku tutazika tu” nikamwambia.
Akanipa pole nyingi na
kuniambia kuwa alikuwa ananisikitikia hasa vile ambavyo nilikuwa peke yangu.
Baada ya mazungumzo yetu nikakata simu na kuwapigia ndugu na jamaa waliokuwa
pale Korogwe.
Baada ya hapo nikatoka nje. Muda
huo baadhi ya watu walikuwa wanakwenda mashamba na wanawake walikuwa wakifanya
usafi nje ya nyumba zao.
Watu wa kwanza kuwaarifu
walikuwa ni wale majirani zetu wa karibu. Baada ya kuwapa taarifa na wakafika
nyumbani kwangu. Kuna waliojitolea kusambaza habari zile kwa majirani wa mbali
zaidi.
Ndugu wa upande wa baba walipofika
tulikubaliana kuwa marehemu tumzike mchana wa siku ile ile kwa vile hakukuwa na
cha kungoja.
Tuliita walimu waliokuja kuuandaa
mwili wa marehemu kwa ajili ya mazishi ikiwa ni pamoja na kufanya visomo vilivyohitajika. Hadi
inafika saa sita mchana, kila kitu
kikawa tayari. Mwili wa marehemu ulitiwa kwenye jeneza na kutolewa kwa ajili ya
kupelekwa msikitini kuswaliwa.
Baada ya marehemu kuswaliwa
alitolewa kupelekwa makaburini tayari kwa ajili ya mazishi.
Tulipomaliza kuzika tulirudi
ntumbani ambako baada ya kufanyika dua ya mwisho ya kumuombea marehemu, nilitoa
hutuba fupi kuwashukuru ndugu jamaa na majirani walioshirikiana na mimi katika
msiba huo.
Kama ilivyo kawaida katika
mazishi yoyote yale, niliuliza kama marehemu alikuwa akimdai mtu yeyote au kama alikuwa anadaiwa na mtu yeyote yule.
Sikupata jibu. Nikataoa
angalizo kama kutatokea mtu yeyote ambaye anadaiwa na marehemu au anamdai
marehemu anifuate mimi na kunifahamisha anachodai ili niweze kumlipa na kama anadaiwa yeye anilipe mimi.
Baada ya hapo niliwashukuru
tena watu wote na kuwapa ruhusa ya kuondoka. Watu wakatawanyika na kurudi
katika shughuli zao.
Tulibaki ndugu watupu
tukaweka vikao vyetu. Baada ya vikao hivyo ndugu hao nao wakatawanyika.
Nyumbani kulibaki wanawake wachache ambao walikaa kwa siku tatu kukamilisha
mila zetu. Siku ile ya tatu walioga maji na kuondoka.
Nikabaki peke yangu kwenye
nyumba ile. Mara tu baada ya watu kuondoka nilijifungia chumbani mwangu
nikalitoa lile sanduku la pesa. Nililifungua nikatoa zile pesa na kuzimwaga
kwenye godoro. Zilienea godoro lote.
Nikaanza tena kuzihesabu ili
nijue zilikuwa ni kiasi gani. Siku ile ya kwanza nilipozihesabu niliziacha
nusu. Sasa nikaamua kuzihesabu zote.
Kwa vile pesa zenyewe
ziliwekwa katika vitita vya shilingi milioni moja moja. Ilinirahisishia kazi ya
kuzihesabu.
Zile pesa nilizozihesabu
nilikuwa ninazirudisha mle mle kwenye sanduku.
Nilianza kuhesabu kutoka saa
tatu asubuhi, hadi inafika saa sita mchana sikuwa nimezimaliza pesa zote.
Kulikuwa na kiasi kikubwa ambacho kilikuwa kimebaki.
Nikaendelea kuhesabu ili
nikimalize kiasi hicho lakini kila nilivyoendelea niliona kama
vile zile pesa zilikuwa haziishi. Nikaanza kupata wasiwasi.
Sanduku lilikuwa linakaribia
kujaa lakini pesa zilizobaki zilikuwa nyingi kuliko zile nilizozihisabu na
kuzitia kwenye sanduku hilo.
“Pesa zote hizi si zilitoka
kwenye sanduku hili hili?” nikawa najiuliza.
“Mbona sasa zinaonekana ni
nyingi?” nikaendelea kujiuliza.
Ile kazi ya kuhesabu ikaanza
kunitia uvivu. Sasa nikataka nizirudishe zile pesa zote kwenye sanduku nione kama zitajaa na kubaki.
Baada ya kufanya hivyo
nikaona maajabu. Pesa hizo ambazo sikuwa nimezihesabu ambazo niliona zilikuwa
nyingi kuliko zile nilizozitia kwenye sanduku, nilipozirudisha kwenye sanduku hilo ziliingia zote bila
kubaki.
Kwa kweli nilipata wasiwasi.
Nikazitazama pesa hizo kisha nikalifunga lile sanduku na kulirudisha mvunguni.
Nikakaa kitandani na
kujiuliza, baba yangu alipata wapi pesa zile wakati mwenyewe alikuwa masikini.
Lakini kulikuwa na matukio ya
wakati wa nyuma ambayo yalinifikirisha. Ile nyumba tuliyokuwa tunakaa pale
kijijini ilikuwa ni ya gharama kubwa na aliijenga marehemu baba yangu. Hakukuwa
na mtu yeyote ambaye alijua baba yangu alipata wapi pesa za kujengea nyumba ile
wakati raslimali yake ilikuwa ni shamba dogo tu.
Pia nilikumbuka kuwa aliwahi
kufungua duka kubwa halafu akalifunga. Hakukuwa na aliyejua alipata wapi pesa
za kufungulia duka lile. Pia alinunua gari la thamani akaliendesha kwa siku
chache tu kisha akaliuliza.
Wakati ule sikupata akili ya
kumuuliza baba alipata wapi pesa za kufungua duka au kununua gari, nilipata
akili ya kumuuliza kwanini alilifunga lile duka na kwanini aliuza lile gari.
Jibu lake
lilikuwa alilifunga lile duka kwa
sababu wachawi wakiona ana mali
watamuandama sana.
Na kuhusu gari aliniambia
ameliuza kwa kuogopa fitina za watu.
Sasa niligundua kuwa baba
yangu alikuwa na pesa lakini hakutaka kutambulika. Alihofia kwamba endapo
angejulikana kuwa ni tajiri angeuawa kwa mujibu wa mtazamo wake.
Kwa vile hakutaka ajulikane
kuwa alikuwa na pesa aliishi kama masikini. Na
hata mimi mwanawe nilijua kuwa baba yangu alikuwa masikini. Lakini kumbe hakuwa masikini.
Lakini kitu ambacho kiliumiza
akili yangu kukifikiria ni jinsi baba yangu alivyopata pesa zile. Baba yangu
hakuwa na raslimali yoyote zaidi ya shamba, alipata wapi pesa hizo?
Wakati ninajiuliza swali hilo likanijia swali jingine, kwanini pesa hizo
zinaonekana kama zina miujiza fulani. Wakati
wa kuzihesabu zinaonekana kuwa ni nyingi na huwezi kuzimaliza?
Labda swali hilo ndilo ambalo lilinipa utata zaidi kwa
sababu lilikuwa halina jibu.
Baada ya kutopata jibu
nilitoka mle chumbani nikaingia katika chumba cha marehemu baba yangu.
Nilichutama chini ya kitanda nikatia mkono na kutoa ule mkoba ambao niliuona
mvunguni.
Niliutoa na kuona ulikuwa
umejaa vumbi. Nikaukung’uta kisha nikaketi kitandani na kuufungua.
Ndani ya mkoba huo, niliona
kitabu kidogo kilichokuwa na maandishi ya kiarabu. Nilikuta pete ya fedha
ambayo baba yangu alikuwa akipenda kuivaa. Ilikuwa na kito cha rangi ya bahari
kilichowekwa alama ya nyota na mwezi.
Pia nilikuta chupa ambayo
ndani yake mlikuwa na yai zima lililoandikwa maandishi ya kiarabu kwa wino
mwekundu. Pia mlikuwa na talasimu iliyokuwa na picha ya mtu. Sikuweza kujua
lile yai liliingia vipi ndani ya ile chupa wakati mdomo wa chupa ulikuwa na
uwazi mdogo sana.
Mbali ya ile chupa kulikuwa
na kipande cha ubao mweusi uliokuwa na maandishi ambayo sikuweza kutambua
yalikuwa ya lugha gani, Kigiriki si Kigiriki, Kichina si Kichina! Pia kulikuwa
na vikorokoro vingine ambavyo sikuweza kuvielewa. Vitu hivyo kwa kweli
vilinishangaza.
Baada ya kuviangalia kwa
dakika kadhaa nilivirudisha ndani ule mkoba.
Nilichukulia kwamba
wazee wa zamani walikuwa na vikorokoro
vingi vya kiasili walivyokuwa wanavihifadhi kwa imani mbalimbali. Na kwa kweli
nisingeweza kujua baba yangu alikuwa amehifadhi vitu vile kwa sababu gani.
Nikaamua kuurudisha ule mkoba
mvunguni nilikoutoa. Mkoba huo haukushughulisha sana akili yangu. Akili yangu ilikuwa
imeshughulishwa zaidi na zile pesa. Nilipotoka pale chumbani nilitaka kurudi
tena chumbani mwangu nizitazame tena zile pesa kwenye lile sanduku la chuma
lakini nikajizuia. Niliona kama nilikuwa ninafanya jambo la kitoto.
No comments:
Post a Comment