Friday, October 20, 2017

HADITHI, MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI SEHEMU YA 18

HADITHI

MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI 18

ILIPOISHIA

“Ungeweza kuitimiza nadhiri yako na hilo tatizo lingeondoka lakini sasa kuna tatizo jingine”

“Tatizo gani?”

“Ule mzimu haupo tena, ni afadhali kama ungehamishwa na kupelekwa sehemu nyingine lakini aliondolewa kabisa. Na hivi sasa haupo tena”

Waziri Mkuu akakumbuka amri ya kuuondoa mzimu huo kwenye kijiji hicho aliitoa yeye baada ya kuona kijiji kilikuwa kimepanuka na watu walikuwa wakifanya vitendo vya kishirikina waziwazi na kusababisha fisi waliokuwa wakifuata mizoga ya wanyama kuhatarisha maisha ya watu.

“Ni bora ningeuacha” Waziri Mkuu akajiambia kimoyo moyo.

“Sasa kama huo mzimu haupo haitawezekana kutimiza ile nadhiri?” akauliza huku akiizuia sauti yake isioneshe hofu.

“Haitawezekana. Mzimu wenyewe haupo. Hiyo nadhiri utaitimiza wapi?”

Waziri Mkuu akamkumbuka mwanawe.

“Sasa mwanangu atapona vipi?”

“Hilo swali ni vigumu kukujibu, ungemfuata yule mganga wa kwanza uliyekwenda naye kwenye huo mzimu”

SASA ENDELEA

“Nimeambiwa huyo mganga amekwishakufa”

Mganga akatikisa kichwa kusikitika.

“Hilo suala litakuwa gumu sana”

“Una maana gani, una maana kwamba mwanangu hatapona”

Mganga aliendelea kutikisa kichwa.

“Kupona itakuwa vigumu sana”

Waziri mkuu alitoa macho ya taharuki.

“Unasemaje?”

“Mheshimiwa kwa upande wangu, sina uwezo wa kukusaidia” Mganga akasema huku uso wake ameuinamisha chini akiyakwepa macho ya mheshimiwa.

“Unadhani nani anaweza kunisaidia?”

“Sijui lakini unaweza kujaribu kwa waganga mbalimbali”

“Loh! Itakuwa ni kazi!”

“Hakuna njia nyingine ya kufanya isipokuwa kuhangaika tu, kujaribu huku na huku”

“Namsikitikia sana mwanangu na ninajuta kuweka ile nadhiri”

“Na ni kwanini uliweka nadhiri halafu ulishindwa kuitimiza katika muda wake?

“Kusema kweli sikudhani kama yangekuwa makubwa kiasi hiki”

“Umedharau kitu ambacho hukijui. Ni bora usingekwenda kuweka nadhiri ile”

“Yaani ninajuta..!”

Palipita kimya cha karibu nusu dakika kabla ya mganga huyo kuinuka na kumuaga Waziri Mkuu aliyekuwa amechanganyikiwa

“Mheshimiwa naona nikuage…ninakwenda zangu”

“Ehe! Ndio unakwenda?” Waziri Mkuu akamuuliza baada kuzinduka kwenye mawazo.

“Naona niende, kuna kazi zinaningoja”

Waziri Mkuu naye akasimama. Hisia za uheshimiwa zilikuwa zimeshamtoka.

“Sasa utanisaidiaje?”

“Labda nijaribu kukuulizia kwa wataalamu wengine.

“Basi jaribu kufanya hivyo, nitakupa zawadi yako. Utakuwa unawasiliana na huyu ndugu yangu anayeishi hapa”

“Sawa. Kama nikifanikiwa kupata mtu anayeweza kulitatua hilo tatizo nitamfahamisha”

“Asante sana”

Wakapeana mikono kuagana.

Mganga akatoka. Waziri Mkuu alirudi kwenye kochi akaketi na kukiinamisha kichwa chake.

Ndugu yake akaingia na kuketi kando yake. Waziri Mkuu akamtazama.

“Nina matatizo makubwa ndugu yangu, inabidi nikueleze lakini hii iwe ni siri yako” akamwambia.

“Itakuwa ni siri yangu, ni matatizo yapi kaka?”

Waziri Mkuu akamueleza tatizo la mwanawe na jinsi waganga walivyomueleza kuwa lilitokana na mizimu.

“Niliwahi kuweka nadhiri kwenye ule mzimu ulioondolewa halafu sikutimiza nadhiri ile” alimwambia.

“kwa hiyo huo mzimu ndio umemuingia binti yetu?”

“Ndivyo ninavyoambiwa na wataalamu na inaweza kuwa ni kweli kwa sababu vipimo vyote vya hospitali vimeonesha kuwa Sofia hana matatizo”

“Sasa huwezi kuitimiza hiyo nadhiri kwa sasa?”

“Haiwezekani kwa sababu ule mzimu haupo tena”

“Huyu mganga niliyemleta amekushauri nini?”

“Ameshindwa”

“Tutatafuta waganga wengine, wapo wengi”

“Basi nitafutie, itabidi nirudi Dar muda huu lakini ukimpata nipigie simu nitakuja mimi au mke wangu”

“Hakuna tatizo kaka, nitafanya kazi hiyo”

Waziri Mkuu akarudi Dar. Asubuhi ya siku iliyofuata kabla ya kutoka kwenda ofisini kwake ndugu yake akampigia simu.

“Asubuhi njema kaka” Sauti kutoka simu ya upande wa pili ikasikika.

“Na kwako pia. Mmeamka salama huko?”

“Sisi tumeamka salama, sijui nyinyi huko?”

“Huku pia tumeamka salama. Umeshughulikia lile suala langu?”

“Nimelishughulikia jana ile ile na nimepta mtu ambaue ataweza kutusaidia”

Waziri Mkuu alijisikia kupata nguvu ndani ya kiwiliwili chake.

“Kweli eh!” akauliza.

“Sasa sijui utakuja lini huku?”

“Umemueleza hali halisi ilivyo?”

“Nimemueleza kila kitu na nimemueleza kuwa ule mzimu kwa sasa haupo tena. Ameniambia uje”

“Atakuja mke wangu pamoja na huyo binti”

“Atakuja lini?”

“Atakuja leo hii”

“Saa ngapi?”

“Sijaua saa lakini watakapokuja nitakufahamisha”

“Sawa, basi nawasubiri”

Wakati ule mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa chumbani kwake akatoka haraka na kwenda sebuleni ambako mke wake alikuwa akizungumza na Sofia.

“Hebu njoo chumbani” akamwambia.

Mke wake alimuacha Sofia akamfuata mume wake chumbani.

“Kuna nini?”

“Stambuli amenipigia simu ameniambia yule mtaalamu atakayeweza kuyashughulikia haya matatizo amepatikana, sasa nataka uende Morogoro na Sofia baada ya kumaliza kazi zako”

“Naweza kuacha kazi zote ili niende naye”

“Basi fanya hivyo, mimi naenda ofisini”

“Wewe nenda, tukitoka nitakupigia simu”

“Sawa”

Dakika chache baadaye akiwa ofisini kwake Waziri Mkuu akapigiwa simu na mke wake.

“Ndio tunatoka”

“Sawa. Nataka huyo dereva wako asijue kitu”

“Hatajua”

“Unijulishe kitakachoendelea”

“Nitakujulisha”

Mke wa waziri Mkuu alifika Morogoro katika kijiji alichotoka mume wake.

Shemeji yake Stambuli baada ya kumkaribisha nyumbani alimwambia asubiri ili aende akamchukue huyo mganga aliyezungumza naye.

Aliondoka kwa gari lake kuelekea alikokuwa akiishi mganga huyo ambako kulikuwa kijiji cha pili

Alipofika alimkuta mganga huyo akihudumia mtu. Akamsubiri hadi alipomaliza, alimfuata na kumwambia kuwa mke wa Waziri Mkuu pamoja na binti yao mwenye matatizo walikuwa tayari wamefika nyumbani kwake.

Mganga huyo kwa heshima ya kumhudumia binti wa Waziri Mkuu alijiandaa haraka haraka akajipakia kwenye gari ya Stambuli wakaondoka.

Walipofika kwa mke wa Waziri Mkuu, Stambuli aliwapisha. Sofia pia hakutakiwa kusikiliza yale mazungumzo.

ITAENDELEA kesho Usikose kuwa nami hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment