RIWAYA
KAMA UNATAKA FEDHA ZA MAJINI
8
ILIPOISHIA
Bado kulikuwa na lile suala
la kufanya mapenzi na yule mwanamke wa kijini juu ya kaburi saa nane za usiku.
Jambo hilo nalo
kwa upande wangu lilikuwa haliwezekani kabisa.
Baada ya kuwaza sana, niliona ufumbuzi ni
kuacha zile pesa kisha nifunge nyumba na kumfuata mke wangu turudi Dar.
Nilijiambia kama nitaondoka
pale Korogwe na kutoshughulika na zile pesa, huenda matatizo yataniepuka.
Lilikuwa wazo zuri lakini hapo
hapo niligundua kuwa lilikuwa wazo la kutapatapa kwa mfamaji. Nilijiuliza endapo
nitandoka pale Korogwe, nitamuachia nani mama yangu na mwanangu wanaoteseka
kule pangoni?
Pango lenyewe liko Magoma na ni kipande cha kuchapuka--- Nani atawapa chakula au nani atakuja kuwaokoa?
Nikaona nisingeweza kuondoka hapo
Korogwe kabla ya kupata ufumbuzi yakinifu
kuhusu mama yangu na mwanangu.
Niliendelea kuwaza hadi
asubuhi. Ulionikurupusha kitandani ulikuwa ni mlio wa simu yangu ya mkononi.
Niliketi kitandani nikaichukua simu yangu na kutazama namba ya aliyekuwa akinipigia.
Nikaona alikuwa mke wangu. Nikaipokea
simu.
SASA ENDELEA
Baada ya kuulizana hali na
mke wangu nilitaka kumueleza kuhusu lile tatizo lililotokea.
Lakini nikajizuia baada ya kuona
ningemtia hofu mke wangu.
“Umesema Baba anaendelea
vizuri kwa sasa?” nikamuuliza.”
“Anaendelea vizuri.
Namtazamia kwa siku mbili, tatu. Kama hali
yake haitabadilika naweza kumuacha nikaja huko”
Mke wangu aliponiambia hivyo
nilishituka kidogo. Mimi nilikuwa sitaki afike tena pale Korogwe. Nilihisi kama
atakafika ungekuwa ndio mwisho wake.
“Usiharakishe. Huku hakuna
lolote. Muuguze kwanza mzee. Likizo bado ndefu”
“Nimesema nitakuja kama ataendelea kupata nafuu”
Nilitaka kumwambia asije kabisa.
Nikaona kama nitamng’ang’aniza sana kwenye suala
hilo, aingeweza
kupata wasiwasi. Angeweza kushuku kuwa nimepata msichana mwingine.
“Basi sawa. Ukijiona unataka
kuja tuwasiliane kwanza. Umenielewa?”
“Nimekuelewa mume wangu”
Baada ya hapo tuliagana
nikaiweka ile simu kwenye kitanda. Ingawa tulikuwa tumemaliza kuzungumza lakini
moyo wangu bado ulikuwa na wasiwasi. Lile suala la yeye kuja pale Korogwe
sikulipendelea.
Nilihisi kwamba ningemkosa
mke wangu kama atakuja hapo Korogwe kwani majini
wa zile pesa za marhemu baba yangu walishaniambia kuwa wanataka kumtoa kafara
mke wangu pindi mama yangu atakapokufa.
Kutokana na hali ya mama nilivyoiona wakati ule,
anaweza kufa wakati wowote.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida nilijikuta
nikimuombea baba mkwe wangu aendelee kuumwa ili mke wangu abaki Dodoma hadi nitakapoondoka
pale Korogwe.
Ilikuwa dua mbaya lakini
sikuwa na jinsi. Ilibidi nimuombee hivyo kutokana na usalama wa binti yake.
Nikawaza kwamba kuna wazee
waliowaachia watoto wao urithi wa majumba, magari, mashamba na pesa za halali. Na
kuna wazee wengine huwaachia watoto wao urithi wa hatari. Kuna wanaorithi
mikoba ya uganga wa mashetani. Kuna wanaorithi uchawi na kuna wanaorithi pesa
lakini ni pesa za majini zenye masharti mabaya kama
pesa zile za baba yangu.
Urithi kama ule wa kuangamiza
roho za watu tena watu wanaokuhusu haukuwa urithi unaofaa asilani! Nikajiambia.
Niseme ukweli hizi pesa za
majini ziliniendesha puta kweli kweli. Ziliniendesha puta kwa sababu
nilizikataa lakini niliamini kuwa zingeniendesha puta hata kama
ningezikubali.
Kwa upande wangu nilipania
kufa na kupona kuhakikisha kuwa urithi wa pesa zile unanitoka ingawa mpaka muda
ule nilikuwa sijui ningefanya nini.
Baada ya siku ile zilipita
siku tatu. Nilikuwa nikifikiria nifanye nini. Katika siku zote hizo tatu
nilikuwa nikiwapelekea chakula wale wahanga waliokuwa kule pangoni.
Siku ya nne yake ndipo
nilipokutana na mtu mmoja ambaye alinipa matumaini kidogo. Nilikutana naye
kwenye mkahawa ambako huenda kula chakula kila siku.
Ilikuwa subuhi, nilikwenda
kwenye mkahawa huo kunywa chai. Wakati nakunywa chai kulikuwa na watu wawili
ambao pia walikuwa wanakunywa chai kibakuli cha maharege na kipande cha mkate wa ajemi huku pembeni wakiwa na kikombe cha chai ya rangi, walikuwa wakizungumza kuhusu mwenzao mmoja
aliyeponeshwa kichaa na mganga wa majini.
“Alikuwa amepigwa jini, yule
jini alitolewa mbele yetu. Hivi sasa huyo bwana ni mzima kabisa” Mtu mmoja akamwambia
mwenzake.
“Kumbe kile kichaa
kilikuwa ni cha jini?” Mwenzake
akamuuliza.
“Tena jini mwenyewe alitumiwa
na ndugu yake”
“Walikuwa wanagombania nini?”
“Wanagombania nyumba ya
urithi”
“Umtie mwenzako kichaa kwa
sababu ya nyumba tu!”
Wakati watu hao wakizungumza,
mimi nilikuwa nikiwasikiliza. Yule mtu aliyekuwa akielezewa mkasa ule
alitangulia kuondoka akabaki yule aliyekuwa akieleza.
Nilipoona yupo peke yake
nikamwambia.
“Samahani, nilikusikia
ukizungumza kuhusu mganga aliyemtoa mtu jini”
“Ndiyo nilikuwa ninamueleza
yule rafiki yangu kuhusu mwenzetu mmoja aliyekuwa na kichaa” Yule mtu
akanijibu.
“Hivi sasa amepona kabisa?”
“Amepona, ni mzima anaendelea
na shughuli zake”
“Nilikusikia ukisema alikuwa ametupiwa jini?” nikamuuliza
yule mtu.
“Ndiyo, alitupiwa jini na
ndugu yake lakini ametolewa na huyo mganga”
“Inaonekana huyo mganga ni
hodari sana?”
“Kwa kweli ni hodari, sisi
hatukutarajia kama angeweza kumponesha yule
mtu. Alidumu na kichaa kwa miaka miwili”
“Sasa ningekuomba unielekeze
kwa huyo mganga, na mimi nina matatizo yangu kuhusiana na majini”
“Naweza kukupeleka hadi
nyumbani kwake, ni mtu ambaye tunafahamiana”
“Kwa kweli nitakushukuru sana”
Tulipomaliza kunywa chai,
yule mtu alinipeleka hadi kwa huyo mganga.
Alikuwa ni ustaadhi moja
aliyekuwa amevaa kanzu nyeupe na kofia iliyodariziwa.
“Karibuni” akatukaribisha.
Yule mtu niliyekwenda naye
alimueleza kuwa alikuwa amenipeleka mimi ili aweze kunisaidia.
“Naomba umsikilize, ana
matatizo yake”
“Sawa. Nitamsikiliza”
Baada ya hapo yule mtu
aliyenipeleka akaondoka na kuniacha. Nikamueleza yule ustaadhi matatizo
yaliyokuwa yananikabili kuhusiana na zile pesa za majini.
Wakati namueleza Ustaadhi
huyo alikuwa ametulia kimya akinisikiliza kwa makini. Ule utulivu wake peke
yake ulinipa matumaini.
Nilimuelezea kila kitu
kuhusiana na zile pesa pamoja na wale watu waliotolewa muhanga kule pangoni
ambao nilikuwa ninawapelekea chakula kila siku.
Sikutaka kumueleza kuhusu
yale yaliyomkuta yule mganga wa kwanza kwa kuogopa ningemtia hofu.
Ustaadhi baada ya kunisikiliza aliniambia.
“Fedha za majini zipo. Kuna
feha ambazo majini wanakupa kwa kukuchunuka wao wenyewe lakini pia kuna fedha
ambazo watu wanaozitaka hupewa masharti na majini na wakikubaliana nao hupewa
pesa hizo”
Ustaadhi alinyamza kidogo lakini
nilijua kuwa kulikuwa na kitu ambacho alitaka kunieleza.
“Sasa kama alivyokueleza huyo
jini aliyekuwa na baba yako kuwa baba yako alikwenda Zanzibar mahali panapoitwa Kisima cha Giningi
na kuomba kupata pesa hizo kwa masharti
ya kumtoa kafara mke wake na kumiliki mke wa kijini” akaendelea kunaimbia baada
ya kimya kifupi.
“Ndiyo hivyo” nikamjibu.
“Hapo Kisima cha Giningi,
mimi niliwahi kufika. Ni sehemu ambayo hufanyika matambiko na mambo ya kiasili.
Ni sehemu ambayo huaminika kuwa ni ya uchawi na majini”
“Kumbe wewe umeshawahi kufika
mahali hapo?’ nikamuulliza.
“Nimeshawahi. Nilikwenda
kumuagua mtu. Huyo mtu niliondoka naye hapa hapa. Uganga wake ulitakiwa
kufanyika mahali hapo. Nikaenda naye”
“Kwanini uganga wake ulitakiwa
kufanyika mahali hapo?’
“Ni kwa sababu jini aliyekuwa
ametumiwa alinunuliwa mahali hapo. Na jini huyo alitoa sharti kwamba aende
akatolewe mahali hapo hapo alipotoka”
“Na ni kweli alitoka?”
“Ndiyo alitoka”
“Sasa utanisaidiaje hili tatizo langu?”
“Nikwambie ukweli tatizo lako
ni gumu. Kama nitajidai kuwa naweza kukusaidia
ninaweza kupata matatizo kwani hao majini wanaokalia hizo pesa ni majini
hatari. Ni majini wa jamii ya Subiani. Sisi huwaita Subiani Damisi au jini
maiti. Wanaweza kukukata mara moja”
Ustaadhi huyo aliponiambia
hivyo alinitisha. Uso wangu ulifadhaika hapo hapo.
Hapo nikaona nimuhadithie
kile kisa cha yule mganga aliyetandikwa bakora.
Utaadhi huyo alipokisikia
kisa hicho aliangua kicheko.
“Huyo mganga alipata tamaa.
Alitaka kuzichukua pesa hizo akiamini kuwa alikuwa na majini wanaoweza kumlinda.
Lakini huyo jini wa baba yako alipomfuata, majini wa huyo mganga
walisambaratika. Ni bahati yake alitandikwa bakora. Angeweza kumuua kabisa”
“Kwa hiyo utanisaidiaje”
nikamuuliza tena mganga huyo huku sauti yangu ikiwa imenywea.
“Sikufichi, hakuna mganga
yeyote atakayeweza kukusaidia kwa tatizo hilo
labda akudanganye tu”
No comments:
Post a Comment