RIWAYA
KAMA UNATAKA FEDHA ZA MAJINI
6
ILIPOISHIA
“Hilo jini linakuwa na mtu anayemiliki hizo
pesa. Kama wewe umezitoa halitakaa kwako tena”
“Mimi nitakuwa huru?”
“Ndiyo. Wewe utakuwa huru”
“Sawa. Sasa hizo pesa ziko
kwenye sanduku la chuma. Kulileta kwako muda huu haitawezekana lakini kama tutasaidiana kulibeba wakati wa usiku, tunaweza
kulileta hapa kwako”
“Una maana kwamba limejaa
pesa hadi juu?”
“Limejaa mpaka pomoni na ni
nyekundu tupu!”
Mganga alitoa ulimi
akaupitisha kwenye mdomo wake wa juu kwa tamaa. Akaniambia.
“Tufuatane sasa hivi hadi
nyumbani kwako, niende nikaziangalie”
“Twende”
Hapo hapo mganga akainuka.
“Nisubiri kidogo”
SASA ENDELEA
Aliingia kwenye chumba
kimojawapo. Baada ya muda kidogo akatoka akiwa amevaa suruali na shati jingine.
“Twenzetu” akaniambia.
Tukatoka. Mganga hakutaka
tupande bodaboda, alitaka twende kwa miguu. Tukaenda kwa miguu hadi kijijini
kwetu.
Tulifika nyumbani kwangu,
nikafungua mlango na kumkaribisha ndani. Nilimuingiza katika chumba changu,
nikamwambia akae kwenye kiti.
Nikainama kwenye mvungu wa
kitanda na kulivuta lile sanduku la chuma. Nikaona amelikodolea macho.
Nilichukua funguo nikafungua ile kufuli.
Nilipolifungua lile sanduku,
mganga alishituka alipoziona zile noti.
“Pesa ni tamu lakini pesa
hizi zina matatizo, zitakusumbua. Zitakusababishia umkose mke wako na mama yako
pamoja na mwanao” akaniambia kwa namna ya kunishawishi nimpe yeye.
“Mimi sizitaki”
Mganga akaendelea kuzitazama
pesa hizo huku macho yake yakimeta.
“Sasa nikwambie kitu”
akaniambia.
“Niambie”
“Mimi naona nilichukue sasa
hivi hili sanduku”
“Hutaliweza, ni zito”
“Hebu ngoja nilijaribu”
Mganga akajaribu kuliinua.
“Mbona ni jepesi sana. Haliwezi kunishinda.
Nataka nikuondolee hili balaa. Hili ni balaa bwana!”
“Sawa. Lifunge ulichukue”
Mganga akalifunga sanduku hilo lililokuwa wazi.
Kisha akalibeba na kuliweka begani.
“Mimi naenda zangu” Mganga
huyo akaniaga mara tu alipoliweka sanduku hilo
begani. Macho yake yalikuwa yakimeta kwa tamaa ya pesa.
“Utaweza kwenda nalo hadi
kule kijijini kwenu?” nikamuuliza.
“Hili litafika bila wasiwasi
wowote”
Hapo hapo nikakumbuka kitu.
Niliukumbuka ule mkoba nilioukuta mvunguni mwa kitanda cha marehemu ambao ndani
yake mlikuwa na vitu vya ajabu ajabu.
“Hili sanduku lilikuwa pamoja
na mkoba fulani, ngoja nikakuletee” nikamwambia na kuongeza.
“Mimi hautanihusu tena”
“Uko wapi?” Mganga
akaniuliza.
“Ngoja nikakuchukulie, uko
chumba kingine’
Nilidhani mganga angelitua
lile sanduku ili asubiri nikamchukulie huo mkoba lakini alibaki na sanduku lake begani,
akaniambia.
“Kaulete. Nakungoja”
Nikatoka katika kile chumba.
Mganga naye alitoka. Nilipoingia katika chumba cha marehemu, mganga huyo
alisimama pale pale ukumbini na sanduku lake.
Niliutoa ule mkoba chini ya
kitanda cha marehemu baba yangu nikaukung’uta vumbi kisha nikatoka nao.
“Huu hapa” nikamwambia yule
mganga huku nikimpa mkoba huo.
Nilidhani mganga huyo
angetaka kuufungua ili aone vilivyokuwa ndani lakini hakuufungua bali nilimuhisi kama anachekelea na macho yake yakimwekamweka hivi, akaniambia.
“Haya naenda zangu”
“Sasa kwa upande wangu
hakutakuwa na matatizo tena?” nikamuuliza.
“Matatizo nitakuwa nayo mimi.
Wewe hutakuwa na matatizo tena”
“Na wale watu wangu kule
kwenye pango itakuwaje?”
“Wale waache kule kule. Kesho
asubuhi tutakwenda sote ili niwashughulikie. Watakuwa wazima”
“Kwa hiyo kesho asubuhi
nikusubiri hapa nyumbani?”
“Ndiyo nisubiri nitakuja na
vifaa vyangu. Wewe endelea tu kuwapelekea chakula”
Mganga aliponiambia hivyo
alikuwa akivuka kizingiti cha mlango wa mbele.
Nilimuona ana haraka.
Nikamwambia.
“Basi tutakutana hapo
asubuhi”
“Sawa”
Mganga akaanza kuchapuka
akiwa na sanduku hilo
begani. Nilisimama barazani nikimtazam alivyokuwa akitembea kwa kasi. Akilini
mwangu nilimsifu. Mganga huyo kiafya alikuwa dhaifu dhaifu lakini alikuwa
amepata nguvu za ghafla kiasi kwamba aliweza kulibeba lile sanduku na kwenda
nalo kwa kasi.
Sikuzijutia zile pesa. Mawazo
yangu yalikuwa kwa mama yangu na mwanangu. Kama
alivyoniambia yule mganga, pesa ni tamu
lakini mashrti yake yalikuwa magumu. Kwa vyovyote vile nisingeyaweza na kama ningeingia tamaa ya kutaka kumiliki pesa hizo,
zingenisumbua.
Ningeweza kupata kichaa au
kufa kabisa.
Baada ya yule mganga kupotea
kwenye macho yangu nilirudi ndani nikaingia chumbani mwangu. Niliketi kitandani
huku kichwa changu kikiwaza hiki na kile.
Nilivyokuwa ninataka mimi,
yule mama yangu na mwanangu walioko kule kwenye pango watolewe haraka na
kushughulikiwa.
Maneno ya yule mganga kwamba
tusubiri hadi kesho asubuhi twende naye pamoja, hayakunifurahisha lakini
sikuweza kumpinga kwa sababu yeye ndiye mtaalamu.
Nilihisi mama yangu na
mwanangu wanapoendelea kukaa katika lile pango, walikuwa wakiendelea kuteseka
na kunikoseha furaha. Kusema kweli sikuwa na furaha hata chembe kila
nilipowakumbuka. Nilikuwa nikipata majonzi yasiyomithilika.
Tena niseme ukweli kifo cha
baba yangu kamwe hakikunihuzunisha hasa vile nilivyogundua kuwa alimfanyia
ukatili mama yangu na mwanangu.
Nikatamani nirudi tena kule
pangoni nikawaone wahanga hao. Nikatoka uani nikatayarisha uji mwingine na
kuutia asali kisha nikautia kwenye chupa.
Ile chupa niliitia kwenye
mfuko nikatia na vikombe viwili kisha nikaanza safari ya kuelekea kule pangoni.
Nilipoingia kwenye lile pango
niliwaona wale watu wamelala fofofo. Walikuwa wanakoroma na kutoa mlio wa
kutisha. Nilijaribu kuwaamsha lakini hawakuamka. Nikaamua kukaa nao hadi
watakapoamka wenyewe.
Yalipita karibu masaa matatu
nikiwa kwenye pango hilo.
Nilikuwa nimeketi kimya nikiwatazama watu hao kwa huruma huku nikimuwaza baba
yangu kuwa alikuwa mtu katili sana.
Sikuwa na shaka yoyote kuwa
muda ule alikuwa akionja adhabu ya Mwenyezi Mungu huko ahera alikokuwa.
Baada ya masaa matatu ndipo
watu hao walipoamka. Nilihisi kama walikuwa na kiu ya maji kwani walikuwa
wamezitoa nje ndimi zao zilizokuwa zinatoka ute.
Laiti ningekuwa na maji
ningewapa lakini sikuwa na maji ya kunywa. Nikaona niwatilie ule uji wanywe.
Nilipowatilia uji huo walikunywa kwa pupa ingawa ulikuwa moto. Kila mmoja
alikunywa vikombe vitatu.
Nilipohisi kuwa walikuwa
wameshiba, moyo wangu uliridhika kidogo.
Nikaondoka hapo pangoni na
kurudi nyumbani nikiwa mnyonge sana.
Nilipofika nilifikia kulala tu. Niliamka saa mbili usiku nikaenda kuoga kisha
nikarudi tena kulala. Siku ile sikula chakula cha jioni.
Ilikuwa kama majira ya saa
sita hivi nilipoamshwa usingizini wakati mlango wa mbele ulipobishwa kwa
kishindo.
Nikatoka ukumbini kisha nikauliza.
“Nani abishaye?”
“Mimi mganga. Tafadhali
nifungulie” Sauti ya yule mganga ikasikika huko nje.
Nikajiuliza mbona mganga huyo
amenifuata usiku huo wakati tulipatana tukutane asubuhi? Na pia nilihisi mganga
huyo hakuwa peke yake hapo nje. Kulikoni?
Nikaenda kufungua mlango huku
nikiwa na alama ya kuuliza usoni kwangu.
Hapo nje nilikuta watu wanne.
Wawili walikuwa wamemshikilia yule mganga. Mmoja alibeba lile sanduku la pesa.
Na mtu wa nne alikuwa ameshika ule mkoba wa ngozi niliokuwa nimempa yule
mganga.
“Karibuni” nikasema huku uso
wangu ukionesha mshangao.
“Tulikubaliana nije asubuhi
lakini nimelazimika kuja usiku huu” Mganga akaniambia. Jinsi sauti yake
ilivyokuwa dhaifu nilitambua kuwa kulikuwa na jambo ambalo halikuwa la kawaida.
Mganga huyo aliendelea
kuniambia.
“Nimekuruishia hilo sanduku lako la pesa
pamoja na mkoba ulionipa. Sivitaki tena. Chukua mwenyewe”
Mganga huyo akamuamuru yule
mtu aliyebeba lile sanduku anipe.
No comments:
Post a Comment