HADITHI hii inaletwa kwa hisani kubwa ya Kampuni ya mabasi ya FREYS COACH ifanyayo safari zake Tanga, Moshi, Arusha, Babati na Singida kila siku, na hufanya safari zake hizo kutoka Singida na Tanga kila siku, kwa mawasiliano 0622 292990
MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA
UKINGONI 6
ILIPOISHIA
Kijana huyo aliyeonekana kuwa
na wasiwasi alikaa kwenye kiti taratibu kama vile aliogopa kukiumiza.
“Unaitwa nani?”
“Naitwa Ramadhani Stambuli”
“Unaishi wapi?”
“Ninaishi Mbezi,
hivi unavyoniona ninatoka Mbezi. Nilikodi teksi”
“Msichana mwenye namba
niliyokupigia ni nani wako?”
“Ni rafiki yangu au niseme ni mpenzi wangu
kwa muda mrefu”
“Sawa. Anaitwa nani?”
“Anaitwa Pili”
“Pili nani?”
“Pili Amrani”
“Anaishi wapi?”
“Anaishi hapa hapa Kinondoni”
SASA ENDELEA
“Mliwahi kukutana kwa siku ya
leo?”
“Tulikutana jana usiku. Leo
hatukuwahi kukutana”
“Kwanini msikutane, si
umesema ni mpenzi wako?”
“Tuwapenzi, sawa lakini kila
mmoja anaishi sehemu yake. Yeye anaishi Kinondoni, mimi ninaishi Mbezi. Mara
nyingi tunakutana usiku kwa sababu mchana tunakuwa makazini. Na kwa usiku wa
leo hatukukutana. Sikujua alikuwa amekwenda wapi na hakujibu sms zangu”
“Yeye anafanya kazi wapi?”
“Ni mpishi wa Waziri Mkuu”
Inspekta Alex akagutuka.
“Ala kumbe yule msichana ni mpishi wa Waziri
Mkuu!”
“Ndiyo”
“Alitoka kazini muda gani?”
“Sijui kwa leo alitoka muda
gani”
“Kwani kwa kawaida anatoka
kazini saa ngapi?”
“Hana muda maalum. Wakati
mwingine anatoka mapema, wakati mwingine anachelewa hadi saa tatu usiku”
“Sasa nikwambie kitu…”
“Ndiyo”
“Kama
masaa mawili hivi yaliyopita tuliarifiwa kuwa kuna msichana ametupwa katika
eneo la shule ya msingi ya Kinondoni…” Alex alimueleza mkasa mzima uliotokea.
Kijana huyo alishituka na
kutikisa kichwa. Kwa sekunde kadhaa akawa ameduwaa akimtazama Inspekta Alex
mdomo wake ukiwa
wazi.
“Sikutaka kukueleza ukweli huo
kwenye simu, nilitaka ufike hapa ndio nikueleze” Alex alimwambia.
“Pili ameuawa?” Kijana huyo
akauliza kama aliyekuwa akiiuliza nafsi yake
mwenyewe.
“Ndiyo ameuawa”
“Moyo wangu hautaki kukubali
mpaka nisadikishe kwa macho yangu. Naomba kama inawezekana nikamuone mwenyewe huko
hospitali” Kijana huyo akasema kwa unyonge.
“Utakwenda kumuona asubuhi.
Unadhani ni kina nani waliofanya kitendo hiki?”
“Kwa kweli siwezi kujua,
sikuwa naye wakati huo” Kijana huyo alijibu kwa kusikitika.
“Unaweza kukisia au kutueleza
watu unaowashuku”
Kijana huyo akatikisa kichwa.
“Kwa kweli sina mtu yeyote
ninayemfikiria kuwa anaweza kufanya kitendo hicho”
“Sawa. Sasa kuna kitu kingine
ambacho wewe ndio utatusaidia, kuipata familia yake”
“Mimi nitawaonesha nyumbani
kwao”
“Basi tunakutaka ufike hapa
kituoni kesho asubuhi ili utupe
ushirikiano wako”
“Sawa. Nitafika hapo kesho
asubuhi”
Siku iliyofuata Ramadhani
Stambuli aliwasili kituoni hapo saa moja na nusu asubuhi. Macho yake yalikuwa
mekundu yaliyovimba, hali iliyoonesha kuwa hakuwa amelala usiku uliopita.
Alipoondoka kituo cha polisi
usiku alirudi nyumbani kwake ambako alikesha akiwaza huku akiomboleza hadi
kunakucha.
Licha ya kufika mapema
kituoni hapo alikutana na Inspekta Alex saa mbili na nusu asubuhi. Alikuwa amesubiri kwa saa nzima
hadi inpekta huyo alipotokea.
Walipokutana, Stambuli
aliambiwa asuburi. Alisubiri hadi saa tatu ambapo Inspekta Alex alimpakia
kwenye gari.
“Sasa tunakwenda hospitali ya
Muhimbili”
“Sawa”
Wakati gari likiwa katika
mwendo Alex alimuuliza Stambuli.
“Mpaka sasa hujaweza
kuwafikiria watu ambao wanaweza kuwa wamemuua Pili?”
“Sidhani kama
watakuwa watu ninaowafahamu. Nadhani
watakuwa ni wahuni tu”
“Ndio sababu polisi
tunahimiza sana
juu ya ulinzi shirikishi jamii katika maeneo yetu. Ulinzi huu unasaidia sana kuzuia uhalifu mdogo
mdogo na hata uhalifu mkubwa”
Stambuli akanyamaza kimya.
Mawazo yake yalikuwa mbali sana.
“Unajua ni kwanini ninasema
hivyo, ni kwa sababu uhalifu kama huu wa mauaji utazuilika kwa vile maeneo yetu yatakuwa na ulinzi
wa wana jamii wenyewe. Na kama kwa bahati mbaya tukio kama
hili linatokea basi ni rahisi wahalifu hao kujulikana au kukamatwa” Alex
aliendelea kumueleza Stambuli.
“Ni kweli” Stambuli
alimkubalia bila kuzingatia alichoambiwa.
Alex alipoona mwenzake
alikuwa amefadhaika akanyamaza hadi alipolisimamisha gari kwenye maegesho ya
hospitali ya Muhimbili.
Walishuka wakaingia ndani ya
majengo ya hospitali hiyo. Dakika chache baadaye Mganga Mkuu alimpa Alex
taarifa ya uchunguzi wa mwili wa maremu Pili iliyokuwa imetiwa kwenye bahasha.
Alex hakuisoma hapo hapo,
aliomba kuuona mwili wa marehemu. Yeye na Stambuli wakapelekwa mochwari.
Walioneshwa mwili wa Pili
ambao mara tu baada ya Stambuli kuuona aliangua kilio hapo hapo.
“Nyamaza bwana, wewe
mwanaume!” Alex alimwambia akimpiga piga mabegani.
Stambuli aliendelea kulia.
“Jikaze rafiki yangu”
Walitoka hapo hospitali huku
Stambuli akiendelea kulia. Lakini alinyamaza baadaye walipoingia kwenye gari.
“Najua inatia uchungu sana kwa sababu marehemu
alikuwa mpenzi wako lakini jikaze kiume uweze kutusaidia” Alex alimwambia
wakati akiliondoa gari.
Stambuli alijifuta machozi
yake kwa kitambaa kabla ya kushukuru.
“Uhalifu umekuwa ni mwingi sana siku hizi katika jiji
hili. Tunazidiwa kwa sababu polisi ni wachache”
Baada ya hapo hawakuzungumza
chochote hadi walipofika kituoni.
Wakiwa ofisini mwa Alex ndipo
inspekta huyo alipoisoma taarifa ya uchunguzi wa mauaji hayo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa
uchunguzi wa madaktari katika mwili wa marehemu umebaini chembe chembe za mate
ya binaadamu katika eneo la shingo mahali ambapo unapita mshipa wa damu. Kuna
kijaraha cha kung’atwa na meno katika mshipa huo ambapo damu ilifyonzwa mwilini
kupitia mshipa huo na kusababisha kifo cha marehemu.
Taarifa hiyo ilikuwa ndefu iliyoandikwa kitaalamu. Alex
alipomaliza kuisoma aliiweka karatasi hiyo kwenye meza. Akamtazama Stambuli.
“Taarifa ya uchunguzi wa
madaktari inaeleza kuwa marehemu aling’atwa katika mshpa wa shingo na kufyonzwa
damu jambo ambalo limesababisha kifo chake” Alex akamwambia Stambuli.
“Alifyonzwa damu na binaadamu
au mnyama?” Stambuli akamuuliza.
“Madaktari wamegundua chembe
chembe za mate ya binaadamu, itakuwa aling’atwa na kufyonzwa damu na binaadamu”
“Ah! Binaadamu anamfyonza
damu binaadamu mwenzake?”
“Ndio uchunguzi ulivyoonesha”
“Hakuuawa?’
“Ameuawa lakini ameuawa kwa
njia hiyo”
Stambuli akatikisa kichwa kisha akawa kama
anajiuliza peke yake.
“Sasa ni nani aliyefanya
unyama huu?”
Alex akamjibu.
itaendelea kesho hapa hapa usikose KUMEKUCHA UPYA
No comments:
Post a Comment