HADITHI hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya mabasi ya usafirishaji abiria Tanga hadi Singida kila siku kupitia Arusha, Babati na hufanya hivyo kutoka Singida kwenda Tanga, kwa mawasiliano , 0622 292990
MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA
UKINGONI 10
ILIPOISHIA
“Mimi nimeogopa sana yule polisi
niliyezungumza naye kwenye simu aliponiambia sababu ya kifo cha Pili ni
kufyonzwa damu. Ina maana Sofia
alimfyonza damu nyingi”
“Halafu ile nguvu ya
kumdhibiti yule mwanamke aliipata wapi. Ukiwatazama Pili na Sofia, Pili ana
nguvu zaidi. Alimzidi vipi mpaka akaweza kumfyonza damu na kumuua?”
“Kisha
unajua kuwa mpaka muda huu Sofia
hajui alichotenda. Ina maana kwamba jana usiku alikuwa amerukwa na akili!”
“Inabidi tuendelee kumfanyia
uchunguzi zaidi wa akili yake…”
Waziri Mkuu akakatizwa na
mlio wa simu yake ya mkononi iliyokuwa kwenye mfuko wa koti lake. Hakuwa na
tabia ya kutoa simu kwa haraka inapoita lakini siku ile aliitoa haraka ili
kujua ni nani aliyekuwa akimpigia.
SASA ENDELEA
Akaona jina la waziri wa
Mambo ya Ndani Jackson Maro.
Akapokea simu.
“Hello Maro…!”
“Mheshimiwa nilitaka
kukufahamisha kuwa uchunguzi wa mauaji
ya mpishi wa nyumbani kwako Pili Amrani
unaendelea. Nimearifiwa kuwa polisi wanataka kuja nyumbni kwako kuchukua
maelezo”
Waziri Mkuu alishituka.
“Ni maelezo gani
wanayoyataka?”
“Ni malezo yanayohusiana na
uchunguzi wao”
“Sidhani kama tuna maelezo
yanayoweza kuwasaidia kwa sababu Pili aliondoka hapa nyumbani mapema.
Alituambia alikuwa anajisikia kuumwa. Sasa kilichoendelea huko alikokwenda
hatukijui”
“Sawa. Mtawaeleza hali
halisi. Kuna maswali ambayo watawahoji”
“Watakuja saa ngapi?”
“Watakuja muda huu”
Baada ya kusita kidogo Waziri
Mkuu alisema.
“Sawa waache waje?”
“Nashukuru mheshimiwa”
Waziri Mkuu akaiweka simu juu
ya stuli ndogo ya kioo iliyokuwa mbele yake.
“Ni nani?” Mke wake
akamuuliza akiwa amekunja uso.
“Ni Jackson Maro Waziri
wa Mambo ya Ndani”
“Anataka nini?”
“Ameniambia kuna askari watakuja hapa kwa ajili ya uchunguzi
wa mauaji ya Pili”
“Wanashuku kwamba ameuliwa
hapa?”
“Hapana. Wanakuja kutuhoji tu
kwa sababu inaonekana Pili aliuawa baada ya kuondoka hapa”
‘Sasa tutawaeleza nini hao polisi?”
“Itabidi tupange jinsi ya
kuwaeleza”
Waziri Mkuu akajiweka sawa na
kumuelekea mke wake.
“Sasa sikiliza, hawa jamaa
wakija tuwe na kauli moja. Kwanza
tusiwahusishe wale watoto. Tuwambie hawakuweko. Mimi na wewe ndio tutazungumza.
Umenielewa?”
“Ndio”
“Kwa hiyo tutawambia kuwa
Pili aliondoka saa kumi na moja jioni baada ya kudai kuwa kichwa kinamuuma,
tukamruhusu aende hospitali”
“Labda wanaweza kuuliza
aliondoka kwa usafiri gani kama alikuwa anaumwa?’
“Hatujui. Tutawambia kwamba
hatujui. Hapa nyumbani aliondoka kwa miguu yake. Sasa huko nje hatujui alitumia
usafiri
gani”
“Sawa. Tutawambia hivyo.
Sidhani kama watakuwa na maswali mengine”
“Wanaweza kuwa nayo lakini
tutatumia akili kuyajibu”
Mke wa Waziri Mkuu akabaki
kimya.
Ilikuwa ni baada ya saa moja Waziri Mkuu alipofahamishwa
na mlinzi wa nyumbani kwake kuwa kulikuwa na makachero watatu waliokuwa
wakihitaji kuonana naye.
Waziri Mkuu akatoa ruhusa
makachero hao waingie ndani. Sekunde chache baadaye makachero hao
wakakakaribishwa sebuleni na Waziri Mkuu mwenyewe.
Hawakupoteza muda. Mrakibu wa
polisi kutoka idara ya upelelezi makao ya polisi Thabit Kombo alijitambulisha
na kuwatambulisha wenzake Inspekta Alex na mwenzake Inspekta Temba.
“Mheshimiwa kuna hili tukio
la mauaji ya
Pili Amrani yaliyotokea Kinondoni jana usiku, ndio limetuleta hapa” Thabit
Kombo alianza kumwambia Waziri Mkuu.
“Nimeshaarifiwa kuwa mtakuja. Hili tukio kwa
kweli limenisikitisha sana”
Waziri Mkuu alijidai kusikitika.
“Vile vile ni tukio ambalo
limetushangaza polisi. Mara kwa mara mauaji
yanatokea lakini si ya aina hii ya kuuawa kwa kufyonzwa damu”
“Inawezekana labda ni mnyama
amemfyonza baada ya kuuawa”
“Hapana. Uchunguzi wa
madaktari umebainisha kuwa aliuawa kwa kufyonzwa damu na aliyemfyonza ni
binaadamu”
Waziri Mkuu akajifanya
anatikisa kichwa kusikitika.
“Sijui huu ulimwengu hivi
sasa unaelekea wapi!” alisema.
“Sasa mheshimiwa tumekuja
kukusumbua kidogo. Tunahitaji maelezo kutoka hapa nyumbani kwako ambako yule
msichana alikuwa anafanya kazi”
“Maelezo ya aina gani?”
“Kwanza
tungependa kujua huyu marehemu jana aliondoka hapa saa ngapi?”
Waziri Mkuu akajifanya
anafikiria.
“Kwa kweli jana aliondoka majira
ya saa kumi na moja jioni”
Kombo alikuwa amefungua
jalada alilokuwa ameliweka mapajani. Akaanza kuandika maelezo ya Waziri Mkuu.
“Alikuwa amewahi au ndio muda
wake wa kawaida?”
“Yeye alikuwa ni mpishi wetu.
Sasa kazi ya upishi si kama kazi ya ofisini,
ikifika saa kumi unaondoka. Yeye kuondoka kwake ni mpaka amalize kazi. Wakati
mwingine anaondoka usiku, wakati mwingine anawahi kuondoka”
“Anapotoka kazini anatumia
usafiri gani kurudi nyumbani?’
“Usafiri
unakuwa ni juu yake mwenyewe isipokuwa kuna siku tunamrudisha nyumbani kama ni usiku na kuna siku tunamfuata nyumbani kwake na
gari”
“Kwa hiyo anapoondoka
anatumia usafiri wake?’
“Hapa nyumbani anaondoka kwa
miguu, sasa huko nje anajua yeye mwenyewe atapanda nini. Siku hizi kuna usafiri
mwingi, kuna bodaboda, kuna teksi, kuna daladala”
“Mheshimiwa imeelezwa kuwa
mwili wa marehemu ulitupwa katika eneo la shule usiku wa jana kutoka katika
gari aina ya Toyota
Land Cruisser ya rangi
nyeupe…”
Waziri Mkuu alishituka.
Akanyamaza kimya kumsikiliza
kachero huyo ili ajue angesema nini.
“Katika upelelezi wetu pia
tunataka kulitambua hili gari ili liweze kukamatwa, je hapa nyumbani kwako kuna
gari la aina hiyo?” Thabit Kombo akamuuliza.
Moyo wa Waziri Mkuu ukaanza
kwenda mbio.
Kwanza alishukuru kwamba gari
hilo halikuwepo
pale nyumbani muda ule. Kama lingekuwepo na
makachero hao wangeliona wangelitilia mashaka.
Alitumia kama sekunde tatu
kujiuliza ajibu nini. Akubali kwamba analo gari hilo au akatae. Akajiambia endapo atakubali
anaweza kuingia katika kashifa ya mauaji
itakayopelekea sio tu kujiuzulu cheo chake bali pia kukabiliwa na mashitaka ya mauaji.
Akaona ni bora akatae kwamba
hana gari hilo.
Aliendelea kujiambia kwamba hata kama gari hilo
litaonekana barabarani lisingeweza kushukiwa kwa vile jiji hilo lilikuwa na maelfu ya magari ya aina
hiyo yenye rangi nyeupe.
Waziri Mkuu baada ya kuwaza
alitikisa kichwa.
“Hapa nyumbani hatuna gari hilo” akasema.
Kachero Kombo aliandika
kwenye jalada. Alipomaliza kuandika alimwambia Waziri Mkuu.
“Tunakupa pole kutokana na
msiba huu. Tutaendelea kulitafuta hili gari na waliohusika katika tukio hili,
ili wafikishwe katika vyombo vya sheria”
“Na mimi ninawaomba mjitahidi
kuhakikisha kuwa watu hao wanakamatwa”
“Asante
sana
mheshimiwa. Tutajitahidi kwa kadiri ya uwezo wetu”
Makachero hao walimuaga
Waziri Mkuu na kunyanyuka. Waziri Mkuu aliwasindikiza hadi nje ya nyumba yake.
Makachero hao wakajipakia kwenye gari na kuondoka.
Mara tu Waziri Mkuu aliporudi
ndani mke wake alimuuliza.
“Umesema huna gari hilo, je kama watalikamata barabarani na dereva akasema ni
la kwako, huoni kama umejitia mwenyewe katika
hatia”
“Na ni kwanini likamatwe gari
langu wakati jiji hili lina maelefu ya
magari ya aina ile ya rangi nyeupe?”
“Polisi
wanaweza kufanya msako wa kuyakamata”
“Watakamata magari mangapi na
watakwenda kuyaweka wapi. Mimi nikisikia kuna msako huo nitawazuia. Nitawambia
zoezi hilo
litasumbua wananchi”
“Si itaonekana unazuia
upelelezi?”
“Hapana. Sasa tujiandae
twende huko kwenye msiba tuwape pole na pia tutoe ubani wetu”
“Sawa”
Baada ya kumaliza kula
chakula cha mchana Waziri Mkuu na mke wake walikuwa kwenye magari mawili
tofauti huku wakiongozwa na gari la polisi lililokuwa na kimulimuli.
Walifika Kinondoni nyumbani
kwa wazazi wa Pili ambako tayari watu walikuwa wamejaa na vilio vilikuwa
vimetawala.
ITAENDELEA kesho hapahapan usikose, KUMEKUCHA UPYA
No comments:
Post a Comment