HADITHI hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya mabasi ya abiria FREYS LUXURY COACH yanayofanya safari zake Tanga hadi Singida kupitia Moshi, Arusha na Babati kila siku, na hufanya hivyo kutoka Singida kwenda Tanga kila siku, kwa mawasiliano, 0622 292990
MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA
UKINGONI 12
ILIPOISHIA
“Angerudi na angeniaga kuwa
anakwenda sehemu, ningewambia”
“Unadhani atakuwa amekwenda
wapi?”
Msichana huyo akabetua mabega
yake.
“Kwa kweli siwezi kujua. Pili
alikuwa mtulivu sana, hakuwa mtu wa kutokatoka sana anaporudi nyumbani.
Mimi mwenyewe nilishangaa kwa kutomuona ile jana usiku.
“Hakuwahi kukueleza kama kulikuwa na mtu ana ugomvi naye?”
“Hakuwahi kunieleza. Pili
mwenyewe alikuwa mpole sana.
Sidhani kama alikuwa na ugomvi na mtu yeyote”
“Hakuwa na tabia ya kwenda
kwa waganga wa kienyeji ambao labda watakuwa ndio waliomfyonza damu”
“Mh!” Msichana aliguna kisha alisema.
“Sijui. Kama
alikuwa anakwenda kwa waganga wa kienyeji basi ilikuwa siri yake. Mimi hakuwahi
kuniambia hata siku moja”
“Kwa hiyo huna tetesi tetesi
zozote ulizozipata zinazohusiana na kuuawa kwake?”
SASA ENDELEA
Msichana akatikisa kichwa.
“Kwa kweli sijapata tetesi
zozote”
“Tunakushukuru sana kwa maelezo yako ambayo ingawa hayakutusadia sana lakini yametupa
mwanga kidogo”
“Na mimi pia nawashukuru,
karibuni tena”
Wakati huo Kombo alikuwa ameshainuka, wenzake nao
wakanyanyuka.
“Haya kwaheri mama” Mzee
Amrani akamuaga.
“Jamanai karibuni sana”
Msichana huyo aliwasindikiza
wageni wake hadi nje. Kombo na wenzake wakajipakia kwenye gari. Walimrudisha
mzee Amrani nyumbani kwake kisha
wakaelekea kituo cha polisi cha Kinondoni.
“Maelezo ya Waziri Mkuu na ya
baba wa marehemu yanapingana sana”
Kombo alimwambia Inspekta Alex.
“Hata mimi nimepata utata
kidogo”
“Waziri Mkuu ametuambia kuwa
marehemu aliondoka kazini kwake saa kumi na moja jioni baada ya kujisikia
kuumwa kichwa na inawezekana kuwa alielekea hospitali. Lakini baba wa marehemu
anasema mwanawe aliendelea kuwa kazini hadi saa moja na nusu usiku”
“Labda urudi tena kwa Waziri
Mkuu akupe ufafanuzi zaidi” Alex alimwambia Kombo.
Kombo akanyamaza kimya.
Aliona kurudi kwa Waziri Mkuu ili ampe ufafanuzi
ilikuwa ni kama kumtuhumu kuwa alisema uongo.
“Hatuwezi kwenda kwa Waziri
Mkuu kama tunaokwenda nyumbani kwa mtu mwingine” Kombo alisema baada ya ukimya.
Akaongeza.
“Suala lenyewe ni muhimu sana kueleweka”
“Ni muhimu kwa sababu
kinachotakiwa ni kujua marehemu alitoka saa ngapi kazini na alipotoka alikwenda
wapi”
Baada ya Alex kusema hivyo
palipita ukimya
mwingine. Kombo alikuwa bado akiendelea kuwaza.
Alimuamini sana
Waziri Mkuu kuwa hawezi kuongopa katika suala kama hilo lakini pia alimuamini yule mzee ambaye
alimuonesha ushahidi wa meseji ambayo marehemu alimtumia saa moja na nusu usiku
kumjulisha kuwa bado alikuwa kazini. Sasa nani atakuwa amesema uongo kati ya Waziri Mkuu na baba wa
marehemu?
“Huu uchunguzi sasa umeanza kuingia
utata!” Kombo alisema na kuutanzua ukimya
uliokuwepo.
“Afande mimi naona suala ni
la kurudi kwa Waziri Mkuu ili atoe ufafanuzi!”
Msisitizo huo wa Alex
ulimkera Thabit Kombo kwa vile mtu aliyemtaja alikuwa mheshimiwa. Lakini mbali
ya kukereka huko Kombo aliona kauli ya Alex ilikuwa ya ukweli na ya maana.
“Nitajadiliana na wakubwa”
Kombo alisema huku macho yake yakitazama mbele ya kioo. Uso wake ulionesha kuwa
alikuwa amezama kwenye mawazo.
“Hilo pia ni wazo zuri, unaweza kwenda kumhoji
mheshimiwa Waziri Mkuu ukajikuta
unalaumiwa”
“Ninajua. Kazi zetu
zinakwenda kwa sheria lakini pia kwa amri”
Kombo alimuacha Alex kituo
cha polisi cha Kinondoni akaelekea makao ya polisi.
Alipofika alikwenda moja kwa
moja kwenye ofisi ya afisa upelelezi wa mkoa.
“Afande nimekwenda nyumbani
kwa Waziri Mkuu kuchukua maelezo yake na pia nimekwenda nyumbani kwa wazazi wa
marehemu, nako pia nimepata maelezo kutoka kwa baba wa marehemu” Kombo
alimwambia afisa upelelezi.
“Je umegundua nini katika
upelelezi wako?”afisa upelelezi akamuuliza.
“Nimegundua kwamba kuna utata
kati ya maelezo ya Waziri Mkuu na maelezo ya baba wa marehemu”
“Umegundua utata gani?”
“Maelezo yamepishana kidogo.
Waziri Mkuu alitueleza kwamba marehemu aiondoka kazini kwake jana saa kumi na moja
jioni. Aliondoka mapema kwa sababu alikuwa anaelekea hospitali baada ya kueleza
kuwa kichwa kilikuwa kinamuuma”
“Ndio”
“Baba wa marehemu ametuambia
kwamba aliwasiliana na mwanawe saa moja usiku akiwa bado yuko kazini.
Alituonesha meseji ambayo marehemu alimtumia baba yake kumjulisha kuwa muda huo
alikuwa bado yuko kazini. Na vile vile baba wa marehemu hakuwa na taarifa
yoyote kuwa mwanawe alikuwa anaumwa”
“Naam. Huo utakuwa ni utata”
“Sasa tufanyeje?”
“Itabidi urudi tena nyumbani
kwa waziri Mkuu ili atuweke sawa. Nitamfahamisha hilo Mkurugenzi wa Upelelezi”
“Sawa”
“Inawezekana alighafilika au
inawezekana baba wa marehemu ndiye aliyeghafilika lakini vizuri umfahamishe ili
atuweke sawa”
“Nimekuelewa afande”
Toyota Land Cruiser la rangi
nyeupe la mheshimiwa Wazirui Mkuu
lilikuwa linatoka Kibaha. Dereva wa gari hilo
alikuwa ametumwa na mheshimiwa kwenda kukagua shughuli zilivyokuwa zikiendelea
katika shamba lake
lililoko nje kidogo ya
mji wa Kibaha.
Shamba hilo lililokuwa na zaidi ya hekta mia moja
lilikuwa na ng’ombe mia tatu wa mheshimiwa Waziri Mkuu na lilikuwa na
wafanyakazi wasiopungua thelathini.
Dereva wa gari hilo Kidas Athumani
alikuwa eneo la Kimara akielekea nyumbani kwa Waziri Mkuu. Aliona lori linataka
kumpita akabana kushoto. Mbele yake kulikuwa na gari jingine dogo alilokuwa
amelikaribia sana.
Kwa vile gari la Waziri Mkuu
lilikuwa kwenye kasi, dereva Kidasi aligusagusa breki ili kuzuia gari
lisiligonge gari la mbele yake kwa nyuma. Moyo wake ulishituka alipogundua kuwa
breki haikutii agizo lake. Gari lilikuwa limefei breki!
Kutahamaki akajikuta
ameligonga kwa nyuma gari la mbele yake!
Kwa sababu gari hilo lilikuwa limefeli breki liliendelea kulibamiza gari hilo hadi liliposimama.
Kidasi alifungua mlango na
kushuka haraka. Alikwenda mbele ya gari hilo
na kulitazama gari aliloligonga. Lilikuwa limebonyea sehemu ya nyuma upande wa
kushoto ambapo taa yake ilikuwa imevunjika.
Mwenye gari hilo
ambalo lilikuwa limesimama, naye alikuwa ameshuka akilitazama gari lake lilivyoharibiwa.
“Unaona!” alimwambia Kidasi kwa
hasira.
“Samahani. Gari langu
lilifeli breki”
Watu wakaanza kumiminika
katika eneo hilo.
Polisi wa usalama barabarani waliokuwa karibu wakajisogeza mahali hapo. Walishaona
kilichokuwa kimetokea.
“Umemgonga mwenzako kwa
nyuma, ni kosa kubwa sana”
Polisi mmoja alimwambia Kidasi.
“Ni kweli gari langu lilikuwa
limefeli breki” Kidasi aliwambia. Uso wake tayari ulishajaa tembe za jasho.
Alitoa kitambaa akajifuta.
Polisi hao walilikagua gari lake kisha
wakamwambia atoe leseni yake waione.
Kidasi aliwapa leseni yake.
Polisi mmoja akaikagua.
“Lete kadi ya gari lako”
Kidasi aliwatolea kadi hiyo
na kuwapa.
Baada ya kuikagua kadi hiyo
polisi huyo alimuuliza Kidasi.
“Gari hii ni ya nani?”
“Ni ya mheshimiwa Waziri
Mkuu”
Polisi hao walishituka.
“Wewe ni dereva wake?” Polisi
mmoja akamuuliza.
“Ndiyo”
Walimrudishia leseni yake na
kadi ya gari.
“Umesema gari ilifeli breki?”
“Ndiyo”
itaendelea kesho hapahapa tangakumekuchablog Usikose KUMEKUCHA UPYA
No comments:
Post a Comment