Sunday, October 15, 2017

SIMULIZI, TAMAA MBELE MAUTI NYUMA SEHEMU YA 5

TAMAA MBELE, MAUTI NYUMA 5

ILIPOISHIA

Gari la Hilda ndilo lililotangulia. Walikwenda hadi eneo la bombo. Msichana akasimamamisha gari katika nyumba ile ile ambayo Dastan alikuwa akiifahamu.

Dastan naye alisimamisha pikipiki nyuma ya gari hilo. Alitreremka kwenye pikipiki. Wakati huo Hilda alikuwa ameshashuka akifungua mlango.

“karibu kaka. Hapa ndio nyumbani kwangu” alimwambia Dastan na kufungua mlango.

Dastan alitangulia kuingia kisha akaingia Hilda na kufunga mlango.

Walitokea katika sebule pana ya kupendeza.

“Karibu ukae” Hilda alimwambia Dastan ambaye alichagua kochi  mojawapo akaketi.

“Nikupatie kinywaji gani?”

SASA ENDELEA

“Dakika chache tu zilizopita tumekula na tumekunywa. Kwa kweli sihitaji kinywaji kwa sasa” Dastan alimwambia Hilda.

“Basi nisubiri kidogo”

Hilda alitoka katika mlango wa sebule akaingia katika chumba kimoja wapo. Baada ya muda kidogo alitoka na kwenda kuketi sebuleni.

“Unaishi na nani humu ndani?” Dastan akamuuliza.

“Ninaishi na mlinzi wangu. Mlinzi wangu pia anaishi hapa hapa, nimempa nyumba ya uani anakaa na mke wake”

“Hii ndio nyumba ambayo uliishi ulipochukuliwa na walezi wako?”

“Ndiyo, niliishi hapa. Nikasoma nikiwa hapa mpaka walezi wangu wakafariki, wakaniachia nyumba. Sasa imekuwa ni yangu”

“Umepata bahati sana Hilda. Inakupasa uwashukuru sana hao watu. Wana moyo wa ubinaadamu kweli”

“Kwa kweli nawashukuru sana. Hivi kaka yangu sijakuuliza, umeshaoa?”

“Bado”

“Unangoja nini?”

“Ndio niko kwenye mipango ya kutafuta mchumba”

“Mbona wasichana wako wengi sana, sema hujapata uliyempenda”

“Ni sawa. Sijapata yule ambaye analingana na mimi”

“Sasa kaka, nashukuru kuwa tumekutana na kujuana. Mimi nilikuwa na wazo moja”

“Wazo gani?”

“Wazo la kwenda Nairobi kuitafuta asili yetu. Inavyoonekana yule mama aliyekuja na sisi, alikuja kutulea. Alivyofariki ndio ikabidi tupelekwe katika kituo cha yatima. Kutokana na maelezo ya yule mtu niliyemuua inaonekana kuna kitu kimejificha nyuma ya pazia”

“Ni wazo zuri. Kitu ambacho ninakiwaza sana ni huyo mtu aliyetumwa aniue ili nisiende Nairobi kurithi mali kwa Omondi”

“Sasa hayo yote tutayajua huko huko”

“Ninakubaliana na wazo lako. Tujiandae kwa safari ya Nairobi”

                                    *************


Yapata miaka ishirini na minane iliyopita Lwanzo Seseko aliwasili katika  jiji la Nairobi akitokea Congo DRC. Aliondoka kwao baada ya kijiji chao kuvamiwa na waasi wa serikali ya Congo. Nyumba zao zilichomwa moto na watu wengi waliuawa kwa kupigwa  risasi.

Lwanzo aliyekuwa amelala chumbani mwake alisikia vurugu na milio ya risasi, alipotoka nje alimshuhudia baba yake na mama yake wakipigwa risasi na kufa hapo hapo.

Kijiji kizima kilikuwa kimeenea vurugu huku nyumba zikiungua moto. Lwanzo alirudi ndani akavunja ua na kupata nafasi ya kukimbia.

Katika safari yake ya kwenda Nairobi alikuwa  na wenzake watatu ambao wote walikufa njiani, akabaki peke yake.

Mtu wa kwanza aliyekutana naye katika jiji la Nairobi alikuwa mkamba mmoja aliyeitwa Omondi.

Omondi alikuwa akifanya kazi katika duka la mfanya biashara mmoja mwenye asili ya Asia. Kazi yake ilikuwa ni kutoa vitu vilivyonunuliwa kutoka stoo.

Omondi alimwammbia Lwanzo kwamba tajiri yake alikuwa anataka kuongeza mfanyakazi mmoja wa  duka.

Lwanzo akakubali kupelekwa kwa mfanyabiashara huyo kuanza kazi hiyo ya duka.

Alipokubaliwa akaanza kazi hiyo akiwa na wafanyakazi wenzake wasiopungua watatu.

Lilikuwa duka kubwa la vifaa vya ujenzi na umeme lililokuwa katikati ya jiji la Nairobi.

Lwanzo alikuwa akilala kwenye vibanda vya masikini nje kidogo ya jiji la Nairobi eneo wa Kibera ambako kunasadika kuwa na vurugu mara kwa mara. Alikuwa akitembea kwa miguu mwendo wa karibu kilometa saba kila siku kwenda na kurudi kazini kwake.

Ili kuwahi kazini, Lwanzo alikuwa akiamka saa kumi na moja alfajiri na kuanza safari ya miguu kuelekea Nairobi. Riziki aliyokuwa anaitia tumboni mwake asubuhi ni kikombe cha kahawa na kashata.

Mchana hula kipande cha muhogo wa kuchoma na masala na jioni huenda kupika mwenyewe ugali na kauzu wa kuchemsha.

Alifanya kazi katika duka hilo kwa miaka miwili. Lwanzo hakuwa akijua kuwa Muhindi waliyekuwa wakimuuzia duka  alikuwa ni mfanya magendo mkubwa. Alikuwa akisafirisha meno ya tembo nje ya nchi na biashara hiyo ndiyo iliyompa utajiri mkubwa.

Fedha alizokuwa akipata kutokana na biashara hizo ni dola za Kimarekani ambazo kwa sababu ya kuhofia kugundulika kutakatisha pesa hakuwa akiziweka benki.

Alikuwa akizitunza  kwenye boksi lililokuwa ofisini kwake.

Kulikuwa na siku moja shehena yake ya meno ya tembo ilikamatwa nchini China. Polisi wa INTERPOL wakafahamishwa kuwa mwenye mzigo huo ni wa mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia aliyeko Nairobi.

Wapambe wa Muhindi huyo walioko China walimpigia simu kumjulisha juu ya kukamatwa kwa mzigo wake na wakamwambia kuwa huenda saa chache zijazo akakamatwa huko huko.

Baada ya polisi wa INTERPOL kupata jina na anuani yake waliwasiliana na wenzao walioko Nairobi. Saa chache tu baada ya taarifa hiyo kuwasili Nairobi, makacherro sita wa Kenya walivamia duka lake.

Wakati makachero hao wanawasili, mfanyabiashara huyo ndio alikuwa anamaliza kuongea na mpambe wake aliyekuwa China. Alipowaona makachero hao akajua kuwa amefuatwa kukamatwa.

Katika vitu vilivyokuwa vikimpa mashaka ni boksi lenye dola lililokuwa ofisini kwake. Alijua kama dola hizo zitaonekana atashindwa kuzitolea maelezo na hivyo kumuweka mahali pabaya.

Kitu cha kwanza alichofanya ni kumtuma Lwanzo ofisini kwake atoe lile boksi na kwenda kulitia kwenye pipa la takataka.

Wakati lwanzo analitoa boksi hilo hakujua lilikuwa na nini. Alipishana na makachero hao kwenye mlango wa duka akatoka nje na kwenda kulitia kwenye pipa la takataka.

Lakini wakati analitia kwenye pipa  la takataka, boksi hilo lilifunguka. Aliona kulikuwa na mfuko wa nailoni kwa ndani.  Akataka kujua kilichokuwamo.

Alipoushikashika mfuko huo aligundua kulikuwa na kitu kama vibunda vya noti.

Mara moja aliutoboa na akaona vitita vya dola za Kimarekani. Alitazama kila upande wa barabara. Hakukuwa na watu waliokuwa wakimtazama. lakini hakuweza kuzichukua pesa hizo hapo hapo.

Alishuku kwamba tajiri yake alimwambia alitie hilo boksi ndani ya pipa la takataka kwa kuwahofia wale makachero walioingia dukani hapo.

Lwanzo alichungulia dukani akaona tajiri yake alikuwa anahojiwa, wakati huo huo gari la taka lilikuwa linapita  Alikwenda kulifungafunga vizuri lile boksi kabla ya wafanyakazi wa gari la taka kulichukua pipa  hilo na kumiminia taka ndani ya gari.

Gari likaoondoka. Lwanzo alifikiria zile pesa, akaona bora afe nazo. Akaanza kulifuata lile gari. Aliendelea kulifuata katika mtaa mmoja hadi mwingine. Gari liliposimama na yeye alisimama kulisubiri, lilipoondoka aliendelea kulifuata.

Gari hilo lilipojaza mzigo wa taka likaanza safari ya kuelekea mahali ambako taka hizo zilikuwa zinatupwa. Alikuwa akipafahamu  kwani ndiko huko huko alikokuwa naishi.

Akapanda matatu (daladala za Kenya) kulifuatilia gari hilo. Wakati anafika katika eneo hilo alikuta gari hilo likimimina taka hizo. Kulikuwa na watu ambao walikuwa wakisubiri taka zimwagwe ili waanze kuchakua  kutafuta vitu vya kwenda kuuza.

Maboksi yalikuwa mengi. lwanzo akawa makini na lile boksi lililokuwa na pesa. Alindelea kuchakua kulitafuta hadi alipoliona. Akalichukua na kuondoka nalo.

Kibanda alichokuwa anaishi hakikuwa mbali na mahali hapo. Alikwenda katika kibandani kwake akajifungia chumbani na kuutoa mfuko wenye dola za Kimarekani uliokuwa ndani ya boksi hilo.

Ule msemo wa kulala masikini na kuamka tajiri ukatimia kwa Lwanzo.


Siku ile alikutana na Omondi usiku. Omondi akamuuliza.

“Kwanini uliondoka kazini mchana?”

“Nilikimbia nilipoona polisi wameingia”

“Kumbe wewe muoga sana?”

“Niambie mlisalimika?”


Itaendelea kesho Usikose Uhondo huu nini kitatokea, Ungana nami kesho

No comments:

Post a Comment