HADITHI hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya mabasi isafirishayo abiria kati ya Tanga hadi Singida kila siku na kutoka Singida kwenda Tanga kupitia, Babati, Arusha hadi Moshi, ofisi kwa Tanga zipo barabara ya 12 Ngamiani, kwa mawasiliano, 0622 292990
MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA
UKINGONI 15
ILIPOISHIA
Hakupata jibu. Akasogea
kwenye kitanda ambako Sofia
alikuwa amelala akamtazanma kwa makini. Maswali matatu yakamjia tena akilini.
Kwanini Sofia ana damu
midomoni?
Damu ile imetoka wapi?
Na kwanini tumbo take
limejaa?
Moyo wake ukiwa umeshituka,
mke wa Waziri Mkuu alitoka haraka akashuka ngazi na kumfuata mume wake
aliyekuwa chumbani.
“Hebu twende ukawaone wale
watoto” alimwambia kwa sauti ya kutaharuki.
Waziri Mkuu naye alishituka.
“Wana nini?” akamuuliza.
“Hebu twende ukawaone
mwenyewe”
Mke wa Waziri Mkuu alikuwa
ameshatangulia kutoka. Waziri Mkuu akamfuata nyuma.
SASA ENDELEA
Walipanda ngazi na kuingia
katika chumba walichokuwemo Sofia
na Monica.
“Hebu watazame”
Waziri mkuu akawatumbulia
macho mabinti zake wawili, mmoja akiwa kitandani na mwingine akiwa chini.
“Uliwakuta wakiwa hivi hivi?”
“Niliwakuta hivyo hivyo,
Monica yuko chini ana michirizi ya damu shingoni na Sofia
yuko kitandani, mdomoni ana damu na tumbo lake limejaa…!”
Waziri Mkuu akiwa ameshituka
alichutama akamtazama Monica.
“Monica! Monica! Monica!”
alimuita mara tatu.
Monica hakuitika wala
kugeuka. Mke wake alijaribu kumshika na kumuinua. Monica alikuwa baridi na
alikuwa amelegea kama mnyoo. Akamrudisha chini
na kuweka mkono kifuani kwake kusikiiza mapigo ya moyo wake.
Wakati akifanya hivyo Waziri
Mkuu alikuwa akimtazama.
“Moyo unapiga?” akamuuiza.
Mke wake akatikisa kichwa.
“Sina hakika kama mwanangu yuko hai” akasema.
“Isije kuwa lile tukio la
mpishi wetu limejirudia kwetu?”
Waziri mkuu naye aliuweka
mkono wake kwenye pua ya Monica kuona kama
alikuwa anapumua, hakuhisi dalili yoyote kuwa Monica alikuwa anahema.
Hapo hapo akaguna. Uso wake
ukasawijika. Alikuwa kama mtu ambaye alitaka kulia.
Akanyanyuka na kusogea kunako
kitanda, akamtazama Sofia.
Kwa kumtazama kwa macho tu aligundua kuwa Sofia
alikuwa akipumua tena alikuwa akipumua kwa nguvu kama
alikuwa anakabwa pumzi.
Tumbo lake lililokuwa
limejaa kuliko kawaida lilikuwa likienda juu na kurudi chini. Tembe za jasho
zilikuwa zikiendelea kutanda kwenye paji la uso wake.
Midomo yake alikuwa
ameichanua. Damu nyeusi ya mtu mwenye afya njema ilionekana kwenye papi za
midomo hiyo. Meno yake yalionekana. Yalikuwa mekundu kwa damu.
“Sofia!” Waziri Mkuu alimuita.
Sofia aliendelea kupumua tu kama
mtu aliyekuwa kwenye usingizi mzito.
Mke wa Waziri Mkuu alisogea
karibu na kitanda akamshika mkono Sofia
na kumuita.
“Sofia!”
Sofia akashituka, akafumbua macho na kuwatazama mama yake
na baba yake kwa macho makali. Macho yenyewe yalikuwa mekundu yakionesha kuwa
alikuwa katika usingizi mzito.
Sofia alipozinduka aliduwaa kwa sekunde kadhaa kabla ya
kuinuka na kujifuta midomo yake. Aliifuta ile damu kisha akaitazama damu hiyo
kwenye mikono yake.
“Hii ni damu!” akasema peke
yake na kuuliza.
“Imetoka wapi?”
Alijipangusa tena kisha
akaitazama damu hiyo.
“Ninatoka damu midomoni”
alisema kisha akateuka.
Wakati huo wote baba yake na
mama yake walikuwa wakimtazama.
“Inatoka wapi hiyo damu?”
Baba yake akamuuliza.
Sofia akabetua mabega.
“Sijui baba, kinywa chote
kimejaa harufu ya damu. Hapa nilipoteuka nimeteuka damu halafu naona tumbo
langu limejaa”
Wakati Sofia akisema hivyo
Baba yake na mama yake walikuwa wakitazamana kwa mshangao.
“Monica yuko wapi?” baba yake
akajaribu kumuuliza.
“Nilikuwa naye hapa kitandani
tunazungumza halafu usingizi ulinipitia. Labda ameondoka”
Waziri Mkuu akamtazama mke
wake.
“lazima kuna tatizo” akasema.
“Kwani mwanangu
unajisikiaje?” Mke wa Waziri Mkuu akamuuliza Sofia.
“Najisikia kichwa kinaniuma” Sofia alisema.
“Hebu toka naye” Waziri Mkuu
akamwambia mke wake.
Mwanamke huyo alimshika mkono
Sofia
akamwambia ashuke kwenye kitanda.
“Monica si huyu hapa amelala
chini!” Sofia
alisema alipomuona Monica, lakini hakukuwa na yeyote aliyemjibu.
Alitoka na mama yake.
Waziri Mkuu alisali kisha
akaubeba mwili wa Monica na kuuingiza katika chumba cha wageni, akaulaza kwenye
kitanda.
Hapo ndipo alipomchunguza
Monica kwa makini. Mbali ya kuthibitisha kuwa Monica alikuwa ameshakufa
aligundua pia jaraha la meno kwenye shingo ya Monica, pale pale palipokuwa na
michirizi ya damu.
Akashusha pumzi ndefu.
Aliketi pembeni mwa kile kitanda akawa anajiuliza, mwanawe Sofia alikuwa amepatwa na nini?
Alishagundua kuwa Sofia alikuwa amemfyonza
damu mwenzake hadi kumuua. Alifahamu pia kuwa wakati Sofia
akifanya hivyo hakuwa akijitambua na baada ya hapo akapitiwa na usingizi mzito kama ilivyotokea siku ile kwa Pili.
Baada ya muda kidogo mke wake
aliingia mle chumbani. Alisimama mbele ya kitanda kilicholazwa mwili wa Monica
na kuangua kilio.
“Hapana, usilie mke wangu.
Tatizo limeshatokea tunatakiwa tupange tutafanya nini. Kwanza Sofia yuko wapi?”
Mke wake alijifuta machozi.
“Sofia nimemuacha sebuleni anaangalia tv”
“Sasa hebu keti hapa tupange”
Mke wake akaketi kwenye pembe
ya kitanda karibu na mume wake.
“Monica ameshakufa na ameuawa
na Sofia, amemfyonza damu kama alivyomfyonza
yule mpishi wetu” Waziri Mkuu alimwambia mke wake ambaye aliposikia maneno ya
mume wake alianza tena kulia.
“Nimekwambia usilie, jikaze
kwanza. Sofia
atakuwa na matatizo ya akili. na matatizo yake ni makubwa kuliko ya
mwendawazimu anayevua nguo”
“Si ndio tulipanga tumpeleke Nairobi kesho kutwa
akafanyiwe uchunguzi, sasa leo tatizo limejitokeza tena”
“Tulichelewa. Lakini si kitu.
Sasa huyu binti yetu aliyekufa tutasema ameuawa na nini?”
“Tutasema alikufa mwenyewe”
“Ana jeraha kwenye shingo
yake!”
“Tumfute ile damu tumuweke
sawa, tusimpeleke hospitali kuchunguzwa. Mtu anapokufa si lazima apelekwe
hospitali”
“Ni sawa. Labda tuseme kuwa
aliumwa ghafla”
“Ndio. Tunaweza kusema alidai
kuwa alikuwa anajisikia vibaya baya. Wakati tunamuandaa kumpeleka hospitali
akafariki ghafla”
“Itatosha”
“Hakuna atakayetuhoji
chochote. Kifo ni kitu cha kawaida”
“Tukishamzika ndio
tutashughulikia suala la Sofia”
ITAENDELEA kesho Usikose uhondo huu nini kitatokea na kufuatia.
No comments:
Post a Comment