Thursday, October 12, 2017

SIMULIZI, TAMAA MBELE MAUTI NYUMA SEHEMU YA 3

HADITHI hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya Usafirishaji abiria ya Raqeeb Luxury Bus kati ya Tanga na Arusha kila siku kuanzia saa 2 hadi saa 6 mchana kila siku, Raqeeb wako hufanya safari sita kwa siku, kwa mawasiliano piga simu, 0622 292990

TAMAA MBELE, MAUTI NYUMA 3

ILIPOISHIA

Dastan akamueleza alivyojisikia.

“Inawezekana una malaria lakini nenda ukapime kwanza. Tunapimia chumba cha tatu. Baada ya kupima utarudi tena hapa”

“Sawa” Dastan alimjibu na kutoka.

Aliingia chumba cha tatu na kushughulikiwa tatizo lake. Kipimo chake kilionesha kuwa alikuwa na vidudu vine vya malaria. Baada ya kuandikiwa cheti alirudi tena katika chumba cha daktari.

“Hebu nione cheti chako” msichana alimwambia alipomuona akiingia.

Dastan alimpa cheti hicho kisha akaketi..

“Una vidudu vinne” Msichana alimwambia na kuongeza.

“Nitakuandikia dawa ambazo utatumia kwa siku tatu”

Msichana aliandika cheti kingine akamwambia Dastan.

“Jina lako tafadhali”

“Naitwa Dastan Seseko”

SASA ENDELEA

Msichana alishaanza kuandika jina hilo akasita na kumtazama Dastan. Uso wake ulionesha kuwa kulikuwa na jambo lililomshitua.

“Unaitwa Dastan Seseko?” akamuuliza tena Dastan.

“Ndiyo, Dastan Seseko”

“Kuna jina jingine hapo katikati?”

“Ndiyo lipo. Ni Dastan Lwanzo Seseko”

“Wewe ni Mkongo?”

Dastan akatabasamu akiwa hajui ni kwanini mwenzie amemuuliza hivyo.

“Hapana. Mimi ni Mtanzania”

“Ulitokea katika kituo  cha yatima cha Kange”

Dastan alipoulizwa swali hilo na yeye alishituka.

“Umejuaje?”

Msichana hakujibu. Macho yake yaliyokuwa yakimtazama Dastan kwa tashiwishi yalianza kutiririkwa na machozi.

Ilikuwa kama vile hakuelewa kuwa macho yake yalikuwa yakitiririka machozi. Alipohisi matone yakigusa mashavu yake aliyapangusa haraka kisha akaendelea kuandika.

Dastan alikuwa ameduwaa akimtazama. Baada  ya msichana kumaliza kuandika aliinuka akatayarisha sindano.

“Njoo ulale hapa” alimwambia Dastan akimuelekeza kwenye kitanda cha wagonjwa kilichokuwa nyuma  ya meza yake.

Dastan aliinuka akalegeza suruali na kuisega kwenye tako moja kisha akajilaza kifudifudi kwenye kitanda hicho.

Msichana alimpiga sindano. Alipomaliza alimwambia.

“Inuka”

Dastan alinyanyuka akaipandisha suruali yake kisha akarudi kwenye kiti.

Msichana alimtolea vipakiti vya dawa na kumpa maagizo ya jinsi ya kuzitumia kwa siku tatu.

“Itakuwa kiasi gani?” Dastan akamuuliza.

Msichana alimtajia gharama yake. Dastan akalipa.

“Dastan nitapenda kuwa na mazungumzo na wewe baada ya muda wangu wa kutoka kazini” Msichana akamwambia Dastan.

“Kuna maswali najiuliza, kwanini ulishituka nilipokutajia jina langu na kwanini ulitambua kuwa nilitoka katika kituo cha yatima?”

“Nina sababu. Niambie tutakutana wapi ili tuweze kuongea zaidi?”

“Sema wewe.

“Mimi nitatoka kazini saa kumi jioni, nikitoka hapa ninarudi nyumbani”

“Unaishi wapi?” Dastan alimuuliza ili kupata uhakika zaidi wa mahali anapoishi.

“Ninaishi eneo la Bombo?”

Dastan akamkubalia kwa kichwa kabla ya kumuuliza.

“Kama sikosei katika siku za hivi karibuni nimekuwa nikikuona pale Shangwe Hoteli nyakati za usiku, au sio wewe?”

“Ni mimi, huwa ninapenda kwenda kula chakula pale. Basi unaonaje kama tutakutana hapo saa moja usiku?”

“Itakuwa vizuri kwa sababu hata mimi ninakula chakula cha jioni pale Shangwe”

“Basi tukutane hapo. Tafadhali usikose kaka yangu

“Sitakosa”

Dastan akanyanyuka kwenye kiti. Akamuaga msichana huyo na kutoka.

Alirudi nyumbani kwake akameza tembe za dawa kama alivyoagizwa. Alipojiona alikuwa na nafuu kidogo alipanda pikipiki yake akaelekea kazini kwake.

Karibu njia nzima Dastan alikuwa akijiuliza yule msichana aliwezaje kumtambua na alikuwa na kitu gani alichotaka kumueleza.

Pia alijiuliza ni kitu gani kilichofanya atiririkwe na machozi alipomkubalia kuwa alitoka kituo cha yatima?

Upande mmoja wa akili yake ulikosa imani. Alijiambia huenda msichana huyo hutumia mazingaombwe kuwalaghai wanaume na kwenda kuwaua nyumbani kwake.

Hata hivyo alijiammbia ni vizuri akutane naye na ajue atamueleza nini. Kama kutakuwa na suala la kwenda nyumbani kwake, Ddatan alijiambia, hatakwenda.

Sasa aligundua ni kwanini laptop ya msichana huyo ilikuwa ina maelezo ya kidaktari pamoja  na picha za viungo vya binaadamu.

Alipofika kazini kwake Dastan alikutana na fundi mwenzake.

“Hali yako inaendeleaje?” Ali akamuuliza Dastan.

“Kidogo najisikia vizuri, ndio maana nimeweza kuja huku”

“Ulikwenda hospitali”

“Nimekwenda, imegundulika ni malaria”

“kwa hiyo umepata tiba?”

“Ndiyo iliyonisaidia kuweza kuja hapa”

“Siku hizi malaria ni nyingi sana. Inatakiwa tutumie vyandarua vyenye dawa”

“Unaweza kutumia na kuna siku utaumwa tu”

“Unajua si lazima mbu akung’ate kitandani, anaweza kukung’ta ukiwa mahali pengine”

Dastan akaanza kazi zake huku mawazo yake bado yakiwa kwa yule msichana. Alitaka kumueleza mwenzake lakini aliona ilikuwa mapema mno. Habari ya msichana akabaki nayo mwenyewe.

Saa kumi na moja jioni baada ya kufunga ofisi yao alirudi nyumbani. Alipumzika hadi saa kumi na mbili jioni. Akaenda kuoga. Baada ya kuoga alivaa nguo nyingine.

Ilkuwa saa moja kasoro dakika arobaini alipoondoka nyumbani kwake kuelekea Shangwe Hotel.

Wakati anaigesha pikipiki yake mbele ya hoteli hiyo, aliliona gari la yule msichana ambalo alikuwa amelikariri.

Gari hilo lilikuwa katika eneo la kuegesha magari. Akahisi msichana mwenyewe alikuwemo ndani.

Alipoingia ndani ya hoteli alimkuta msichana huyo ameketi katika meza iliyokuwa karibu na eneo la mlango.

Akamfuata.

“Nimekaa hapa karibu na mlango ili uweze kuniona kirahisi utakapofika” msichana akamwambia Dastan kisha akamalizia.

“Karibu ukae”

Dasta alivuta kiti na kukaa.

“Unajisikiaje?” Msichana akamuuliza Dastan.

“Ninajisikia vizuri kidogo, nimeweza hata kwenda kazini”

“Natumaini mpaka kesho utajisikia vizuri sana”

“Nitashukuru sana”

“Utakula nini?”

“Kwani wewe mwenzangu umeagiza nini?”

“Sijaagiza kitu, nimefika sasa hivi tu”

“Huwa mara nyingi nakula nyama choma na ugali au ndizi”

“Basi tuagize nyama choma na ndizi”

“Sawa”

Msichana alimuita mhudumu akamuagiza chakula walichohitaji. Mhudumu alipoondoka msichana alimuuliza Dastan.

“Uliondoka lini katika kituo cha yatima cha Kange?”

“Karibu miaka tisa iliyopita”

“Ulisomea wapi ufundi wa kompyuta?”

“Nilisoma Veta”

“Hivi sasa unaishi wapi?”

“Ninaishi Chumbageni”

“Maisha yanakwendaje?”

“Kwa kweli yanakwenda vizuri”

“Uliwahi kuelezwa historia ni kwanini wewe umekuwa katika kituo kile cha kulelea yatima?”

“Nilielezwa. Kwa kweli ni historia ya kuhuzunisha”

Dastan akamueleza historia yake.  Alimwambia yeye na mdogo wake wa kike walifikishwa katika kituo hicho wakiwa wadogo sana.

Dastan aliambiwa alifikishwa katika kituo hicho akiwa na umri uliokadiriwa kuwa miaka mitano na mdogo wake akiwa na umri wa miaka mitatu.

Aliyewapeleka katika kituo hicho ni afisa ustawi wa jamii ambaye aliwaeleza viongozi wa kituo hicho kuwa mwanamke aliyekuwa na watoto hao alifariki dunia kwa ajali ya gari.

ITAENDELEA kesho Usipitwe na Uhondo huu hapahapa tangakumekuchablog, KUMEKUCHA UPYA

No comments:

Post a Comment