Saturday, October 21, 2017

SIMULIZI, TAMAA MBELE MAUTI NYUMA SEHEMU YA 8

SIMULIZI,

TAMAA MBELE, MAUTI NYUMA 8

ILIPOISHIA

Lwanzo akanyamaza kimya. Dakika chache tu baadaye akalisimamisha gari mbele ya jengo lililokuwa na ofisi ya wakili wake.

“Tushuke, tumeshafika” Alimwambia Herieth huku akifungua mlango.

Herieth naye alishuka. Ilibidi Lwanzo amshike mkono ili aweze kutembea vizuri.

“Itabidi nikununulie magwato ya kutembelea”

“Nitashukuru”

Waliingia katika ofisi ya mwanasheria huyo ambaye aliwakaribisha kwenye viti.

“Oh bwana Lwanzo. Karibuni mkae”

Lwanzo na msichana huyo waliketi kwenye viti.

“Habari za mtokako?” Mwanasheria huyo akawauliza.

“Si nzuri sana. Nina tatizo. Ninahitaji msaaada wako” Lwanzo alimwambia.

“Una tatizo gani?”

SASA  ENDELEA

Lwanzo alimueleza kuhusu tatizo la Herieth la kesi iliyokuwa inamkabili.

“Lakini mwenyewe atakueleza kwa undani zaidi. Herieth hebu eleza hilo tatizo likoje” Lwanzo akamwambia Herieth.

Herieth akaeleza kuhusu uhusiano wake na mwanaume aliyemtaja kwa jina la Njoroge. Akaeleza jinsi rafiki yake wa karibu alivyomsaliti na kumchukua mwanaume wake jambo lililosababisha avunje uchumba wake na mwanaume huyo.

“Yule mwanaume alitaka niendelee kuwa naye huku akiendelea kutembea na rafiki yangu. Hilo sikulikubali. Nikaamua tuvunje uchumba, lakini yule bwana aliendelea kuning’ang’ania”

Herieth aliendelea kueleza jinsi mwanaume huyo alivyombambikia kesi ya wizi wa shilingi laki tano ili amkomoe.

“Ninaamini polisi waliipokea ile kesi kwa misingi ya rushwa tu” akasema kwa hasira.

“Ana ushahidi gani kwamba ulimuibia hizo pesa?” wakili akamuuliza.

“Mmoja wa mashahidi wake ni yule mwanamke wake ambaye anasema aliniona nikichukua hizo pesa”

“Lakini wewe hukuchukua?”

“Sikuchukua. Ningepata pesa hizo ningekuwa katika hali hii jamani?”

“Umeshafikishwa mahakamani?”

“Nilifikishwa kwa mara  ya kwanza wiki mbili zilizopita. Kesi ilitajwa kisha ikaahirishwa hadi leo lakini leo nako likatokea tatizo.
Wakati naenda mahakamani niligongwa na pikipiki, mguu wangu ukatenguka. Huyu kaka alisimamisha gari lake akanipeleka hospitali nikafungwa hili P.O.P. Kwa hiyo sikuweza kuhudhuria kesi”

“lakini ulifikisha taarifa kuwa ulipata ajali?”

“Sikuweza. Lakini baada ya kufungwa P.O.P, huyu kaka alinipeleka mahakamani nikajieleza kwa makarani wa mahakama wakaniambia kesi yangu imehirishwa hadi kesho”

“Hebu nieleza nini kilitokea siku hiyo ambayo unadaiwa kuiba hizo pesa?”

“Mimi nilikwenda kwa huyo mwanaume kuchukua nguo zangu zilizokuwa kwake kwa sababu uchumba wetu ulishavunjika. Nilipofika, mwenyewe sikumkuta lakini nilimkuta huyo hawara yake ambaye ni rafiki yangu. Kwa kweli tulijibishana maneno mabaya mpaka ikafikia kutaka kugombana”

“Nani alianzisha ugomvi huo?’

“Ni yeye. Aliniambia  kuwa nilikuwa nimemfuata mwanaume ambaye hanitaki. Nikamwambia sikufuata mwanaume, nimefuata nguo zangu. Hapo ndipo ugomvi ulipoanza”

“Ulichukua hizo nguo zako?”

“Nilivyokuta mwenyewe hayuko sikuzichukua”

“Hizo pesa zinazodaiwa kuibiwa ziliibiwa mahali gani?”

“Chumbani kwa Njoroge”

“Njoroge ndio nani?”

“Ndiye huyo mwanaume”

“Wewe ulifika humo chumbani?”

“Ndio nilifika na ndiko nilikogombana na huyo msichana”

“Amedai hizo pesa uliziiba mahali gani?”

“Eti kwenye kabati la nguo?”

“Wewe ulilifungua hilo kabati?”

“Ndio nililifungua”

“Ulilifungua kwa madhumuni gani wakati ulisema hukuweza kuchukua nguo zako kwa sababu mwenyewe hakuwepo”

“Ni baada ya yule msichana kuniletea ujeuri lakini watu walinisihi kuwa nimsubiri mwenyewe. Nikaondoka”

“Hao watu walitokea wapi?”

“Ni wapangaji wengine wanaoishi katika ile nyumba”

“Kwa hiyo hao waliona kama hukulifungua hilo kabati?”

“Ndio waliona”

“Na waliushuhudia ugomvi wenu mwanzo hadi mwisho?”

“Waliingia mle chumbani waliposikia kelele lakini mpaka ninaondoka walikuwepo”

“Kumbe unao mashahidi waliiona kuwa hukuchukua kitu”

“Mimi ninajua hao hawawezi kwenda kunitolea ushahidi mimi. Wao na Njoroge lao moja”

“Kwanini?”

“Kwa sababu wanaishi pamoja. Atawafundisha uongo kama alivyomfundisha mwanamke wake”

“Kama watakwenda kutoa ushahidi wa uongo tutawahoji maswali watajikangaja tu”

Wakili akamtazama Lwanzo.

“Nitaishughulikia hii kesi. Kesho nitakuwepo mahakamani asubuhi”

“Umemuelewa vizuri huyu msichana?” Lwanzo akamuuliza.

“Nimemuelewa lakini kwa upande wa kesi yake itabidi nisome shitaka lake nione linasema nini”

“Ni shitaka la wizi” Herieth akadakia.

“Wizi uko wa aina nyingi. Itabidi nione shitaka lilivyoandikwa”

“Sawa. Kwa hiyo umesema utaishughulikia hii kesi” Lwanzo akamuuliza tena.

“Nitaishughulikia”

“Kutokana na maelezo machache uliyoyasikia hapa unaonaje, unaweza kumsaidia asipatikane na hatia?”

“Nitajitahidi”

“Utahitaji kiasi gani?’

“Nitakujibu kesho nitakapotoka mahakamani. Si utakuja?”

“Itabidi nije”

“Basi tutakutana hapo”

“Sawa. Kwa hiyo tunaweza kwenda?”

“Ndiyo. Mnaweza”

Lwanzo na herieth wakatoka ofisini. Walipojipakia kwenye gari Lwanzo alimuuliza msichana.

Unaishi wapi?”

“Naishi Langata”

Lwanzo akaliwasha gari.

“Umepangisha chumba au unakaa kwa mtu?”

“Nina chumba changu”

“Ngoja twende nikupeleke”

Lwanzo akatia gea na kuliondoa gari.

“Sisi wanaume tuna tabia tofauti. Kuna wanaume wana tabia za kike kabisa” Lwanzo alimwambia Herieth wakati gari ikiwa kwenye mwendo.

“Ni kweli. Wa kwanza ni Njoroge”

“Kama alimuona rafiki yako ni wa maana zaidi hapakuwa na haja ya kukubambikia kesi wewe”

“Tena yule msichana ndiye mshenga aliyetumwa na Njoroge alipokuwa ananitaka mimi”

“Halafu baadaye wakatakana wenyewe?’

“Kwanini wasitakane hapo mwanzo!”

“Huo ndio upuuzi wa baadhi ya wanaume. Mtu unapoongozwa na tamaa ya ngono unaweza kutembea hata na shemeji yako”

“Na yule rafiki yangu pia siye. Yeye ndiye chanzo cha yote. Aliona nikiolewa na Njoroge nitafaidi, nitapumzika nyumbani. Akaona aniharibie. Lakini mimi sijali na aolewe yeye afaidi yeye. Mungu ni mwema nitapata mwanaume mwingine wa maana zaidi”

ITAENDELEA kesho Usikose kuwa nami hapahapa

No comments:

Post a Comment