Watoto kupimwa moyo tumboni
KUTOKANA na idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa na magonjwa ya
moyo, wajawazito sasa watapimwa kuangalia mtoto aliye tumboni kama
ameathirika na magonjwa hayo.
Uchunguzi wa magonjwa hayo ambao utaendeshwa na Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kikwete (JKCI), utahusisha ujawazito wa kuanzia wiki 18 na
kuendelea.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa JKCI,
Maulid Kikondo alisema uchunguzi huo utafanyika bure hospitalini hapo
kwa siku tatu kuanzia Oktoba 12 hadi 14, mwaka huu.
“Tumegundua watoto wengi wanazaliwa na magonjwa ya moyo lakini upo
utaalamu ambao wenzetu wamekuwa wakiutumia wa kupima ujauzito ukiwa na
wiki 18 na kuendelea huweza kubaini mapema iwapo mtoto aliyeko tumboni
ana matatizo au la.
“Mwenzetu Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto, Naiz Majani
alikwenda nje ya nchi na akapata mafunzo, amerudi hivyo tutaanza
kuwachunguza wajawazito,” alisema.
Alisema uchunguzi huo utafanywa kwa kutumia kifaa maalumu kiitwacho Fetal Echo-cardiology .
Kikondo alisema hawajaweka idadi maalumu ya wajawazito wanaotarajia
kuwapima kwa kutumia kifaa hicho na amewataka wafike kwa muda
uliopangwa.
“Kila atakayekuja atahudumiwa, mtoto anapogundulika kuwa na tatizo ni
rahisi kutibiwa punde tu anapozaliwa na kuwa na afya njema akafurahia
maisha kuliko akizaliwa na baadaye kugundulika kwa vile matibabu yake
yanachukua muda ikizingatiwa wengi huletwa wakiwa wamechelewa,” alisema.
Kikondo alisema pamoja na hilo, Oktoba 9 hadi 16, mwaka huu wataendesha
kambi nyingine ya upasuaji kwa watoto 30 wenye magonjwa hayo.
“Madaktari wa JKCI watafanya upasuaji huo kwa kushirikiana na madaktari
wenzao kutoka Addis Ababa wa hospitali ya Al muntada,” alisema.
MGBLOG