Sunday, September 18, 2016

HADITHI, YAMENIKUTA MIE SALAMA SEHEMU YA 2

HADITHI Inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya Usafirishaji abiria ya Freys Coach ifanyayo safari Tanga, Moshi, Arusha, Babati hadi Singida moja kwa moja kila siku, Ofisi za Freys zipo Tanga barabara ya 12, simu 0622 292990
 
YAMENIKUTA SALAMA MIE 2
 
ILIPOISHIA
 
Wakati nimekaa nje ya chumba cha daktari nikiwaza, daktari alitoka na kuuliza.
 
“Aliyemleta huyu majeruhi aliyegongwa na gari ni nani?”
 
Hapo hapo nilishituka nikajua  kuwa msichana ameshakufa.
 
Nilikuwa nimekaa na watu wengine wanne waliokuwa na shida zao. Nikainuka na kumjibu yule daktari.
 
“Ni mimi”
 
“Majeruhi amepoteza damu nyingi na anahitaji kuwekewa damu ili kuokoa maisha yake. Na hapa tumeishiwa na damu” akaniambia.
 
“Sasa tutafanyaje daktari?”
 
“La kufanya ni kupatikana damu kutoka kwa mtu yeyote, kwani ndugu zake wako wapi?”
 
“Siwatambui. Kama yangu itafaa niko tayari kumsaidia”
 
“Haya twende tukakupime kama unaweza kumtolea”
 
SASA ENDELEA
 
Daktari huyo alinipeleka katika chumba cha maabara. Nilitolewa damu yangu kwa ajili ya kuchukuliwa kipimo.
 
Niliambiwa kwanza ingechunguzwa ili kuonekana kama ilikuwa salama na kama nina damu ya kutosha kumpatia mtu mwingine.
 
Nilisubirishwa kwa karibu saa nzima kabla ya kuambiwa kuwa damu yangu ilikuwa salama na nilikuwa na uwezo wa kumtolea yule msichana.
 
Nilifurahi sana nilipoambiwa hivyo kwani muda wote nilikuwa nikimsikitikia msichana huyo.
 
Kikubwa kilichokuwa kikinisikitisha ni kwamba sikutaka afe. Baada ya damu yangu kutolewa nilipewa kikombe cha chai ya maziwa ili kiniweke sawa.
 
Wakati nakunywa chai, damu niliyotoa ilipelekwa katika chumba alichokuwa  yule msichana. Baadaye kidogo polisi wa usalama barabarani wakafika.
 
Nilikuwa nimeshamaliza kunywa chai na polisi hao walikuwa wameshapewa maelezo na wafanyakazi wa hospitali.
 
Wakanitaka na mimi niwape maelezo, nikawaeleza jinsi ajali ilivyotokea na jinsi nilivyomchukua huyo msichana na kumleta hapo hospitali.
 
“Tumeambiwa kuwa alikuwa anahitaji kuwekewa damu na uliamua kumsaidia?” Polisi mmoja akaniuliza.
 
“Ndiyo nimemtolea damu”
 
“Sijui kama unamfahamu huyu msichana?”
 
Nikatikisa kichwa.
 
“Kwa kweli simfahamu”
 
“Je ile gari iliyomgonga uliiona?”
 
“Ndiyo niliiona”
 
“Unaweza kututajia aina yake na namba yake ya usajili”
 
“Ni Toyota ya rangi nyeupe. Namba yake ya usajili sikuiona yote. Niliona namba za mwanzo tu”
 
“Tutajie hizo hizo”
 
Nikawatajia.
 
“Umetusaidia. Kuna mtu aliona namba zinazofuatia. Mtu mwingine alikariri tarakiu zote. Sasa tutakuwa tumepata namba kamili. Ninaamini tutalikamata hili gari muda usio mrefu”
 
“Mkimpata huyo dereva ni vyema anyang’anywe leseni kabisa. Ni dereva katili sana”
 
“Tukimpata tutamfikisha mahakamani. Mahakama ndio yenye uamuzi”
 
“Sawa”’
 
Baada ya kuzungumza na polisi hao daktari alinifuata na kuniambia kuwa ninaweza kuondoka kwani majeruhi niliyempeleka anaendelea kuwekewa damu.
 
“Ameshazinduka?” nikamuuliza.
 
“Hajazinduka bado lakini tunatarajia kuwa atazinduka muda si mrefu. Tunaendelea kumfanyia uchunguzi kuona kama ameumia kwa ndani”
 
“Sawa. Nitakuja kumuangalia kesho asubbuhi”
 
“Vizuri”
 
Wakati natoka hapo hospitali jua lilikuwa limeshakuchwa. Nilimpigia simu Zacharia nikamuuliza.
 
“Uko wapi?”
 
“Niko ofisini?”
 
“Hamjafunga ofisi bado?”
 
“Ndio tunataka kufunga”
 
“Basi fungeni, mimi sitafika tena huko. Tutakutana nyumbani”
 
“Sawa kaka”
 
Nikajipakia kwenye gari na kurudi nyumbani.
 
Asubuhi ya siku ya pili yake nilipotoka nyumbani nilikwenda hospitali ya Bombo kumjulia hali yule msichana.
 
Nilifurahi kumkuta akizungumza na muuguzi aliyekuwa akimhudumia.
 
“Oh kaka umefika tena?” yule muuguzi aliniuliza akikumbuka kwamba ndiye mimi niliyemleta hospitali yule msichana jana yake.
 
“Ehe nimefika kumjulia hali mgonjwa wangu” nikamjibu huku nikitabasamu.
 
“Mgonjwa wako anaendelea vizuri, Jana tumemuwekea damu na jana hiyo hiyo alizinduka”
 
Wakati nikizungumza na yule muuguzi yule msichana alikuwa akinitazama kwa macho ya shauku na udadisi.
 
“Salma huyu ndiye yule kaka aliyekuleta hospitali” Muuguzi huyo akamwambia.
 
Msichana huyo akashituka.
 
“Ndiye huyu kaka? Nimefurahi kumuona”
 
Msichana akanitazama kwa macho ya bashasha na kuniammbia.
 
“Asante kaka, nnakushukuru sana kwa msaada wako. Mungu atakulipa”
 
“Ni watu wachache sana duniani wenye moyo kama wake, kuacha shughuli yake na kukushughulikia wewe mtu ambaye hakufahamu na zaidi ya hapo akutolee damu iliyoweza kukusaidia hadi leo unajisikia vyema” Yule muuguzi akamwambia.
 
“Ni moyo wa kibinaadamu kweli kweli. Kwa kweli namshukuru sana. Mimi sina cha kumlipa ila Mungu ndiye atakayemlipa”
 
“Asante mdogo wangu kwa shukurani zako. Nimekuja kukujulia hali nijue unaendeleaje kwa sababu jana niliondoka ukiwa bado hujitambui”
 
“Kwa kweli kaka naendelea vizuri, nashukuru Mungu”
 
“Mimi naitwa Ibrahim Amour, ni  mkazi wa Usagara hapa Tanga, sijui wewe mwenzangu unaitwa nani?”
 
“Naitwa Salma Aboud”
 
“Unaishi wapi?”
 
“Ninaishi Chumbageni”
 
“Unaishi na wazazi?”
 
“Ninaishi na mama yangu, Baba yangu alishafariki”
 
“Kwa hiyo mama ayko anayo taarifa kuwa umepata ajali?’
 
“Mama hayuko, amekwenda kijijini tangu juzi”
 
“Basi atakuwa hana habari”
 
“Atakuwa hajui”
 
“Alikwambia angerudi lini?”
 
“Atakuwa huko kwa wiki nzima”
 
“Si kitu, nitakuachia namba yangu ya simu, ukiwa na tatizo unaweza kunipigia”
 
ITAENDELEA kesho usikose uhondo huu hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment