Thursday, September 22, 2016

MASIKINI SALAMA MIE SEHEMU YA 5

HADITHI SEHEMU YA 5
Hadithi hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya Usafirishaji abiria Freys Coach ifanya safari zake kuanzia Tanga, Moshi, Arusha, Babati hadi Singida kila siku, Ofisi za Freys Tanga zipo barabara ya 12 Ngamiani Stend ya zamani ya Mikoani, simu 0622 292990

 
 
HADITHI
 
YAMENIKUTA SALMMA  MIE 5
 
ILIPOISHIA
 
Baada ya sheikh kutuombea dua hiyo, sherehe za ndoa yetu zikaendelea hadi usiku wa manane. Lakini mimi na Ibrahim tuliondoka mapema kwenda nyumbani kwake Usagara.
 
Usiku wa siku ile ndio kwa mara ya kwanza, mimi nilimjua Ibrahim na yeye alinijua mimi kwa maana kwamba ndio tulikutana kwenye sita kwa sita.
 
Baada ya kitendo hicho cha siku ya kwanza, ndio nilimpenda zaidi Ibrahim na naamini hata yeye alinipenda zaidi.
 
Ibrahim na mimi tukawa tumefungua ukurasa mpya wa maisha.
 
Maisha ya siku za mwanzo mwanzo yalikuwa ya upendo sana. Ibrahim akitoka katika shughuli zake hurudi nyumbani. Kadhalika na mimi sikuwa mtu wa kutoka toka wala wa kwenda kwa majirani.
 
Na hilo ni funzo nililolipata kwa kungwi wangu kuwa nikiwa kwa mume wangu niachane na safari zisizokuwa na msingi na pia niepukane na mashoga na majirani wasio wazuri.
 
SASA ENDELEA
 
Jirani yangu mmoja wa nyumba tuliyopakana nayo upande wa kushoto alihama nyumba, akaja mpangaji mwingine, mtu mmoja na mke wake.
 
Huyo mwanaume alikuwa mtu mzima kidogo, alifikia umri wa miaka hamsini wakati mke wake alikuwa bado msichana ila alikuwa amenizidi mimi kidogo kwa umri.
 
Baada ya kuishi na majirani hao kwa mwezi mmoja nikajikuta nimependa staili yao ya maisha. Kila mmoja wao alikuwa na gari. Mume mtu alikuwa na gari lake na mke naye alikuwa na gari lake.
 
Aliyekuwa akifanya kazi ni mume, mke alikuwa yuko nyumbani tu wakati wote. Lile gari alikuwa akilitumia kwenda sokoni au kwenda safari zake nyingine.
 
Mwanaume huyo anapoondoka nyumbani asubuhi hurudi jioni na anaporudi huwa hatoki tena. Vicheko vyao wakati wa usiku vilikuwa vikisikika hadi ndani kwetu.
 
Taratibu nilijikuta nikizooeana na mke wa huyo jamaa.
 
Kulikuwa na siku kulikuwa na tatizo la kukatika  maji. Msichana huyo akaja nyumbani kwangu asubuhi na kubisha mlango.
 
Niliposikia mlango unabishwa nilikwenda kuufungua nikamkuta amesimama mbele ya mlango.
 
“Mmeamkaje jamani?” akanisalimia.
 
“Hatujambo, sijui wewe” nikamjibu.
 
“Samahani jirani yangu, nataka kukuuliza huku kwenu maji yanotoka?”
 
“Hayatoki” nikamjibu na kuongeza.
 
“Yalikatika tangu jana usiku”
 
“Basi mwenzako sina habari kuwa maji yamekatika, nafungua bomba nakuta tupu. Mume wangu anataka ajimwagie aende kazini. Hukuweka akiba kidogo ukanigaia”
 
“Nina tenki la juu, huwa naweka akiba ya maji. Maji yanapokatika sipati taabu”
 
“Mh mwenzangu umenizindua. Nitamwambia mume wangu naye anunue”
 
“Sasa lete ndoo uje umchotee”
 
“Asante jirani, ngoja nikachukue ndoo”
 
Msichana huyo aliondoka. Nilifunga mlango nikaenda kufungua mlango wa uani na kumsubiri.
 
Alipotokea nikamuita.
 
“Njoo kwenye mlango huu”
 
Msichana huyo akaingia katika mlango huo wa uani. Nilikwenda naye kwenye bomba nikamwambia aweke ndoo yake. Nikamfungulia maji.
 
Ndoo yake ilipojaa akaniambia.
 
“Unanipa ndoo hii moja au nije unipe ya pili, kwa maana hii ataoga mume wangu, bado mimi sasa…”
 
“Na ya kupikia je…?” nikamuuliza.
 
“Hapo sasa!”
 
Tukacheka.
 
“Nakwambia hawa watu wa idara ya maji nao watatupa shida!” akaniambia.
 
“Njoo uchote shoga yangu usijali, leo kwangu kesho kwako”
 
“Ngoja nipeleke hii kwanza…”
 
Msichana huyo alibeba ile ndoo akatoka. Niliingia ndani nikaendelea na shughuli zangu. Punde tu nikamsikia akiniita.
 
“Jirani nimerudi!”
 
“Chota tu, nina kazi kidogo” nikamwambia.
 
“Asante jirani”
 
Niliendelea na kazi zangu. Baadaye nikamsikia tena.
 
“Nachota hii ya tatu”
 
“Chota tu” nikamwambia.
 
Alipomaliza kuchota aliniambia.
 
“Haya jirani asante, nakwenza zangu”
 
“Haya jirani”
 
Kutoka siku ile ndipo nilipoanza urafiki na jirani yangu huyo. Alikuwa akija nyumbani kwangu kuzungumza na wakati mwingine mimi nilikuwa nakwenda nyumbani kwake. Nikalifahamu jina lake. Alikuwa anaitwa Rita..
 
Rita akawa rafiki yangu mkubwa, tukafikia hadi kuazimana nguo na vitu vingine na pia tulipeana siri zetu za ndani.
 
Kutokana na urafiki wetu huo niliweza kugundua kuwa maisha aliyokuwa akiishi Rita na mume wake hayakuwa kama maisha niliyokuwa ninaishi mimi na mume wangu.
 
Wenzetu walikuwa wanaishi maisha ya hali ya juu na ya kifahari. Rita alikuwa akiniambia kila kitu alichohitaji, mume wake alikuwa akimtimizia. Alihitaji gari akamnunulia. Na wakati ule tunaanza kufahamiana alikuwa akimjengea nyumba maeneo ya Kange.
 
“Mume wangu si mgumu, ananisililiza na kunijali” Rita aliniambia na kuongeza.
 
“Kila ninachohitaji ananipatia”
 
“Basi una raha shoga yangu. Umepata mume mzuri. Wangu mimi ukitaka kitu mpaka kwa mbinde”
 
“Lakini hata huyu wangu aliponioa alikuwa hivyohivyo, nilifanya kumtengeneza”
 
Nikashituka.
 
“Ulimtengenezaje shoga?”
 
“Nilimuendea kwa mganga nikamlisha madawa mpaka yakamkolea”
 
“Wacha shoga!. Kumbe kuna madawa yanayoweza kubadili tabia ya mwanaume?”
 
“Yapo. Si unamuona mume wangu alivyo. Sasa nakwambia hakuwa hivi! Kuninunulia nguo ilikuwa ni mpaka tugombane”
 
“Wangu mimi hatugombani, ni mgumu tu. Kila siku yeye hana pesa lakini biashara anafanya. Sijui pesa zake zinakwenda wapi!”
 
“Basi ana mwanamke nje, ndiye anayemla. Mwenzangu wala chuya, mchele waliwa na mwenzio!”
 
Rita aliponiambia hivyo alinicheka na mimi nikajidai kucheka lakini moyo wangu ulipata fadhaa sana nilipohisi kuwa inaweza kuwa ni kweli mume wangu akawa na msichana  wa nje anayekula pesa zake.
 
Siku ile niliwaza sana yale maneno aliyoniambia shoga yangu.
 
Mume wangu aliporudi jioni nilijaribu kumwambia.
 
“Mume wangu huninunulii hata pikipiki na mimi”
 
“Unataka pikipiki ya nini mke wangu?”
 
“Pikipiki ya nini? Watu wananunuliwa magari, wewe unasema pikipiki ya nini?”
 
“Kama ni gari si hili tunalo”
 
“Hilo ni la kwako. Mimi nataka pikipiki”
 
“Tuombe Mungu, kazi zangu zikienda vizuri nitakununulia”
 
“Utaninunulia lini?”
 
ITAENDELEA kesho na usikose uhondo huu ini kitatokea

No comments:

Post a Comment