Tuesday, September 27, 2016

HADITHI, YAMENIKUTA SALAMA MIE SEHEMU YA 8

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
 
YAMENIKUTA SALMA MIE  8 Inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya Usafirishaji abiria Tanga, Moshi, Arusha, Babati hadi Singida kila siku kuanzia saa 12 asubuhi na huanza pia Singida kuja Tanga kila siku, Ofisi kwa Tanga zipo barabara ya 12 simu 0622 292990. Na kwa Singida zipo Stend kuu ya Mabasi0655 591092
 
ILIPOISHIA
 
Nikatingisha kichwa changu kumkubalia.
 
“Asante kwa kunifahamisha, sasa na mimi nataka kumkomoa. Nataka amuache huyo mwanamke anipende mimi  peke yangu, anijali na kunisikiliza, Kila ninachomwambia atii”
 
“Hata kama utataka akununulie gari atakununulia”
 
“Nifanyie hiyo kazi, utahitaji shilingi ngapi?’
 
“Kwa vile umeletwa na mteja wangu wa siku nyingi, nitakufanyia shilingi laki moja”
 
Nikaguna na kumtazama Rita.
 
Sikuwa nimechukua shilingi laki moja. Nilikuwa na shilingi elfu hamsini tu kwenye pochi yangu.
 
“Unajua shoga nilifanya ujinga nilipoondoka nyumbani, nilichukua shilingi elfu hamsini tu”
 
“Sasa mimi nitakutolea elfu hamsini, tukifika nyumbani unirudishie”
 
“Sawa shoga, nitakurudishia”
 
Rita akafungua pochi yake na kutoa shilingi elfu hamsini na mimi nikatoa kiasi kama hicho kutoka kwenye pochi yangu. Tukampa yule mganga.
 
“Anaitwa nani mumeo?” Mganga akaniuliza baada ya kupokea zile pesa.
 
“Anaitwa Ibrahim Amour”
 
SASA ENDELEA
 
Mganga aliuachia mkono wangu akachukua karatasi na kuiandika jina la Ibrahim.
 
“Na wewe unaitwa nani”
 
“Mimi naitwa Salma Aboud”
 
Mganga akaandika jina langu kwenye ile karatasi.
 
Pembeni mwake palikuwa na tunguri kadhaa. Alichukua tunguri mojawapo akakitia kile kiratasi kwenye mdomo wa ile tunguri kisha akaanza kuitikisa huku akitabana maneno kwa kiluga.
 
Kila alipotabana alikuwa akilitaja jina la Ibrahim na jina langu.
 
Baadaye alikitoa kile kiratasi ambacho kilikuwa kimeloa kwa dawa iliyokuwemo ndani ya ile tunguri. Akachukua chetezo kilichokuwa na makaa ya moto akakitia kile kikaratasi, kikaanza kuungua na kutoa moshi.
 
Akachukua tunguri nyingine akaitabania maneno huku akilitaja jina langu na la Ibrahim kisha akachukua karatasi na kumiminia unga fulani kutoka katika ile tunguri, akakiweka kile kikaratasi mbele yangu.
 
Akachukua tunguri nyingine nayo akaitabania kisha akamimina unga kama ule wa kwanza kwenye kikaratasi kingine.
 
Baada ya hapo alikifunga kikaratasi cha kwanza, kikawa kama kipakiti. Halafu alikifunga kikaratasi cha pili.
 
“Sasa sikiliza” Mganga akanimabia.
 
“Ndiyo nakusikiliza”
 
Alichukua kile kipakiti cha kwanza akanipa.
 
“Hiki utamuwekea kwenye maji ya kuoga kwa siku tatu”
 
“Sijakuelewa, nitamuwekea kwenye maji ya kuoga kivipi?”
 
“Yaani katika yale maji anayooga kwenye ndoo, tia hii dawa kidogo bila mwenyewe kukuona”
 
“Sasa sisi hatuogi kwenye ndoo, tunaoga moja kwa moja kwenye bomba”
 
“Mnatumia bomba la mvua?”
 
“Ndiyo”
 
“Sasa itakuwaje, hii dawa ni lazima aioge”
 
“Hakuna njia nyingine?”
 
Mganga akatikisa kichwa.
 
“Ingekuwepo ningekwambia”
 
“Si kitu, nipe”
 
“Utafanyaje?” Rita akaniuliza.
 
“Nitafunga maji kwenye mita kisha nitamtilia maji kwenye ndoo nimwambie maji yamekatika. Atayaoga tu”
 
“Lakini umeambiwa ni kwa siku tatu”
 
“Kwa siku tatu itakuwa vigumu, atagundua kuwa maji yanatoka”
 
Nikamtazama mganga na kumuuliza.
 
“Kwa siku moja haitatosha”
 
“Kama ni kwa siku moja itie mara tatu. Yaani chota kidogo tia, halafu chota mara ya pili tia halafu chota mara ya tatu tia. Itakuwa imemalizika yote.
 
“Ngoja nikwambie nilivyokuelewa. Nikishatia maji kwenye ndoo nichote kidogo hii dawa niitie kwenye maji halafu nichote tena nitie, halafu nichote tena mara ya tatu nitie. Au nimekosea”
 
“Ni sawa”
 
“Kwa hiyo nitaimaliza dawa yote?”
 
“Ndiyo utaimaliza yote”
 
“Haitaonekana kwenye maji?”
 
“Hapana, inayayuka na ni nyeupe tu. Hawezi kuiona”
 
“Sawa”
 
Mganga akachukua  ile pakiti nyingine akanipa.
 
“Na hii utamuwekea kwenye chakula. Unatia kidogo kwenye mchuzi au wali au hata kwenye chai”
 
“Nitie wakati napika au wakati tunakula?”
 
“Wakati wowote, bora uitie tu”
 
“Sasa tatizo ni kwamba tunakula pamoja”
 
“Haina madhara hata kama wewe utakula hicho chakula au mtu mwingine atakula”
 
“Sawa. Nimtilie mara ngapi?”
 
“Mtilie mara moja kwa siku tatu”
 
“Wakati gani?”
 
“Wakati wowote asubuhi au jioni, unaweza kumtilia”
 
“Sawa”
 
“Baada ya siku tatu utaona matokeo yake, utakuja kuniambia”
 
“Atanipenda sana?”
 
“Na atakupa kila kitu unachokitaka”
 
“Nitakushukuru sana babu kwa maana yule mwanaume ananitesa sana”
 
“Mateso yote yatakwisha, utakuwa unamtesa wewe”
 
“Kila itakavyotokea nitakuja kukuambia”
 
“Sawa, sasa kazi yenu imekwisha mnaweza kwenda”
 
Tulipoondoka kwa yule mganga moyo wangu ulikuwa umepata matumaini sana na kufarijika hasa nilivyojua kwamba ninakwenda kumkomesha mume wangu.
 
“Sasa kazi kwako” Rita akaniambia wakati gari ikiwa kwenye mwendo.
 
“Nakwenda kumuwekea leo leo, singoji kesho”
 
“Ndiyo ianze leo”
 
“Nikifika nayafunga maji, atakapotaka kuoga namtilia maji kwenye ndoo”
 
Dakika chache baadaye tukafika nyumbani. Rita alilisimamisha  gari mbele ya geti. Akashuka na  kuniambia  nimsubiri.
 
Alikwenda kufungua mlango akaingia ndani kisha akaja kufungua geti.
 
Geti lilipokuwa wazi aliingia kwenye gari akaiingiza gari ndani. Tukashuka sote. Alikwenda kufunga geti. Alipomaliza tukaingia ndani ya nyumba yake.
 
“Shoga asante, acha niende nikatayarishe mambo” nikamuaga shoga yangu kabla ya kutoka kwenda kwangu.
 
Nilifungua mlango wa nyumba yanngu nikaingia ndani. Wakati nikiwa jikoni nikitafuta mahali pa kuficha vile vipakiti, nikasikia mlango ukigongwa. Nikaviacha vile vipakiti kwenye mkoba wangu, nikaenda kufungua mlango.
 
Nikashituka kuona alikuwa mgeni. Alikuwa mdogo wake Ibrahim aliyekuwa akikaa Dar. Alikuwa anaitwa Mashaka lakini mwenyewe alijiita meshack.
 
Alikuwa ni mdogo wake Ibrahim shangazi kwa mjomba.
 
“Oh shemeji, karibu sana” nikamkaribisha huku nikipokea begi alilokuwa amelipachika kwenye bega lake.
 
“Asante, habari ya hapa?”
 
“Nzuri, za safari”
 
Baada ya kulipokea begi niliingia nalo ndani.
 
“Nashukuru ni nzuri, sijui nyinyi hapa”
 
Meshack aliingia akafunga mlango.
 
Nikamkaribisha sebuleni lakini begi lake nilikwenda kuliweka kwenye chumba cha wageni.
 
Nilipotoka Meshack aliniuliza.
 
“Kaka yuko wapi?”
 
“Yuko kazini kwake, hapa anarudi jioni sana, si ana taarifa kuwa unakuja?”
 
“Anayo taarifa na leo asubuhi wakati najiandaa kuja huku nilimpigia simu kumjulisha kuwa ninakuja”
 
ITAENDELEA kesho hapahapa tangakumekuchablog usikupite uhondo huu nini kitatokea baada ya shemeji yake Salma Meshack kuwa ndani huku kaka yake hayupo?

No comments:

Post a Comment