Thursday, September 29, 2016

HADITHI, YAMENIKUTA SALAMA MIE SEHEMU YA 10

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
 
YAMENIKUTA SALMA MIE 10 inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya Freys Coach ifanyayo safari zake Tanga, Moshi, Arusha, Babati hadi Singida kila siku, kwa mawasiliano 0622 292990
 
ILIPOISHIA
 
Baada ya kusalimiana naye aliniuliza “Vipi?”
 
“Mpango wangu umekwama” nikamwambia huku nikiketi kwenye kochi.
 
“Kwa sababu ya huyo mgeni?”
 
“Na sijui ataondoka lini!”
 
Rita alipoona nimechukia akanicheka na mimi nikajidai kucheka.
 
“Huyo mgeni siku zote haji, anangoja nina mipango yangu ndio anakuja. Si balaa hili!”
 
“Pengine hatakaa sana, ni wasiwasi wako tu”
 
“Kama hatakaa sana ndivyo ninavyotaka”
 
Mgeni huyo alikaa kwetu kwa siku nne. Usiku wa siku hiyo ya nne akaniambia kuwa kesho yake ataondoka kurudi Dar kwani alikuja kutujulia hali tu. Nilifurahi sana aliponiambia hivyo.
 
Asubuhi ya siku iliyofuata Mashaka akaondoka kurudi Dar. Nikaona sasa nitumie ile nafasi kufanya ile dawa yangu. Ilipofika jioni nilijaza maji kwenye ndoo zote na kwenye mabeseni kisha nikaenda kufunga mita ya maji.
 
Mume wangu alipokuja nikatangulia kumwambia kuwa maji yalikuwa yamekatika.
 
“Yamekatika saa ngapi?” akaniuliza.
 
“Hivi jioni”
 
“Sasa tutaoga nini?”
 
“Niliwahi kuchota. Nimejaza ndoo zote”
 
“Oh! Umefanya vizuri sana”
 
Ilipofika usiku yeye alikuwa wa kwanza kwenda kuoga. Aliponiambia nimtayarishie maji, nikaenda kukichukua kipakiti kimoja kati ya vile viwili nilivyopewa na mganga, nikachota ile dawa na kuitia mara tatu kwenye ndoo kama alivyoniagiza yule mganga.
 
SASA ENDELEA
 
Nilipoona bado ilikuwa ikielea juu ya maji, nilitia mkono wangu nikatibuatibu yale maji, ile dawa ikapotea.
 
Wakati mume wangu anaoga nilikuwa nikitayarisha chakula mezani, ile dawa nyingine nikaitia kwenye wali upande ule ambao nitamtilia yeye kwenye sahani.
 
Baada ya kuoga mume wangu alikuja mezani. Mara tu alipoketi kwenye kiti nilimsikia akisema.
 
“Mbona kichwa kinaniuma halafu macho yanniwasha?”
 
Akawa anayafikicha fikicha macho yake.
 
“Hicho kichwa kimekuanza saa ngapi?” nikamuuliza.
 
“Kimenianza wakati huu huu”
 
“Basi kula chakula halafu ule dawa”
 
Hapo hapo nikamuona akitikisa kichwa na kutazama kila upande kwa haraka haraka kabla ya kuniambia.
 
“Haa! Mke wangu macho yangu yamefunga kiza, sioni kitu!”
 
“Huoni kitu kwa sababu gani?” nikamuuliza.
 
“Sijui” akaniambia huku akijitahidi kuyafumba macho yake na kuyafumbua.
 
“Au ni kwa sababu ya hicho kichwa ulichosema kinakuuma?”
 
“Kichwa hakiwezi kusababisha macho yasione kabisa. Mimi sioni kabisa”
 
Wakati akisema Ibrahim alikuwa akiyaangaza macho yake kila upande kutafuta mwanga.
 
“Mke wangu nimepofuka macho!” akaniambia kwa sauti iliyotia huruma.
 
Nikaguna. Maelezo hayo yalikuwa yamenishangaza.
 
“Hebu nitazame nione macho yako” nikamwambia.
 
Mume wangu akageuza uso wake upande wangu. Macho yake yalikuwa ni mazima lakini yalionesha wazi kuwa hayakuwa yakiona kitu.
 
“Huoni kabisa?” nikamuuliza.
 
“Sioni”
 
“Mbona macho yako ni mazima na yako kama kawaida?”
 
“Sasa sijui kilichonitokea. Hii hali nimeiona baada ya kumaliza kuoga”
 
Isijekuwa ni ile dawa niliyomtilia kwenye maji aliyooga ndiyo iliyompofua macho mume wangu? Nikajiuliza kimoyomoyo.
 
Wakati nikijiuliza hivyo Ibrahim alikuwa akijitahidi kuyafikicha macho yake huku akijaribu kutazama bila mafanikio.
 
“Sijui ni kitu gani kimenitokea jamani?”  akajisemea peke yake.
 
“Hebu nisubiri hapo hapo” nikamwambia na kuinuka.
 
Niliingia chumbani nikiwa nimekishika kile kipakiti cha dawa  niliyomtilia kwenye chakula. Nikakitazama vizuri. Hapo hapo niligundua kuwa nilikuwa nimechanganya zile dawa. Ile dawa niliyoambiwa nimtilie kwenye chakula ndiyo niliyomtilia kwenye maji ya kuoga na ile niliyoambiwa nimtilie kwenye maji ya  kuoga  nilimtilia kwenye chakula.
 
Sasa nikajiuliza ile dawa ndiyo iliyompofua macho Ibrahim kwa sababau niliitumia kinyume na nilivyoagizwa?
 
Nikamsikia Ibrahim akiniita.
 
Nikatoka mle chumbani na kumfuata pale kwenye  meza.
 
Ibrahim alinigundua kuwa nimefika kwa kunipapasa.
 
“Bado huoni kabisa” nikamuuliza.
 
“Sioni, naona kiza kitupu. Yuko wapi Zacharia?”
 
“Nafikiri yuko nje”
 
“Hebu muite”
 
Nikatoka nje na kumuita Zacharia mdogo wake. Zacharia alinifuata mezani akijua nimemuitia chakula.
 
“Huyu hapa” nikamwambia ibrahim.
 
“Zacharia!” Ibrahim akamuita.
 
Zacharia mwenyewe alishituka kuitwa na kaka yake kwa sauti kubwa akiwa yuko karibu naye kabisa.
 
“Ndiyo kaka”
 
“Nilikuwa nimekwenda kuoga, sasa natoka bafuni nije hapa nikaona kichwa kinaniuma. Mpaka nafika hapa  macho yangu yakazima kabisa. Hivi tunavyozungumza sioni kabisa”
 
“Alah! Huoni kabisa” Zacharia akamuuliza kwa mshangao.
 
“Sioni. Tangu muda huo nilikuwa namueleza shemeji yako kuwa sioni”
 
“Ina maana ni macho yenyewe tu hayaoni au kuna sababu?”
 
“Sijui”
 
Zacharia akaguna.
 
“Isije kuwa nina presha, kwa maana kichwa kilianza kuniuma?’
 
“Labda ni presha” nikaitilia nguvu hoja ya presha.
 
“Basi twende tukapime. Kama ni presha upate tiba yake”
 
“Subiri nikavae twende” Ibrahim alisema huku akijitahidi kuinuka kwenye kiti.
 
Nilimshika mkono nikamuongoza kuelekea chumbani. Tulipokuwa chumbani nilimvua saruni aliyokuwa amejifunga nikampa suruali na shati. Alipovaa nilimwambia achukue pesa za hospitali.
 
Akafungua kabati na kupapasa kabla ya kuukamata mkoba wake ambao huweka pesa.
 
“Hebu nitolee shilingi laki moja” akaniambia huku akinipa ule mkoba.
 
Niliuchukua nikaufungua. Ndani ya mkoba huo mlikuwa na vitita vya noti ambavyo hesabu yake alikuwa akiijua mwenyewe. Pesa hizo ndizo alizokuwa akizizungusha kwenye baishara yake.
 
Nilihesabu shilingi laki moja nikampa. Hakugundua kuwa ninampa pesa hizo mpaka nilipozigusisha kwenye mkono wake. Akazipokea na kuzitia mfukoni.
 
Niliurudisha ule mkoba kwenye kabati kisha nikatoka naye.
 
“Zacharia uko wapi?” akauliza mara tu tulipotoka chumbani.
 
“Niko hapa” Zacharia aliyekuwa amekaa kwenye meza alimjibu.
 
“Njoo unishike mkono twende, nafikiri hii itakuwa ni presha” Ibrahim akamwambia kisha akakumbuka kitu.
 
“Hebu tutolee ufunguo wa gari, nimeusahau” akaniambia.
 
Nikarudi chumabni na kuchukua funguo ya gari nikampa Zacharia.
 
“Gari utaendesha wewe” nikamwambia.
 
“Itabidi”
 
Zacharia akamshika kaka yake mkono wakatoka.
 
Nilipobaki peke yangu mle ndani nilikwenda ikata ile sehemu ya chakula niliyoitia ile dawa kwa ajili ya Ibrahim, nikaenda kuimwaga kwenye pipa.
 
Nilihofia kwamba huenda Ibrahim akirudi kutoka hospitali atataka kula. Nilikuwa sitaki ale ile dawa ambayo ilikuwa ni ya kuoga.
 
Yasije yakatokea mengine, nikajiambia.
 
Nikataka nimpigie simu Rita nimwambie, lakini niliogopa kutoa ile siri kwamba mume wangu amepofuka macho kwa sababu ya ushirikina wangu.
 
Lakini nilipanga kwamba kila itakavyokuwa kesho yake niende kwa yule mganga nimueleze hali iliyotokea, pengine angeweza kuwa na ufumbuzi.
 
Kwa upande mwingine nilijipa moyo kwamba huenda dawa ile aliyooga siyo iliyomfanya mume wangu asione bali ni presha kama mwenyewe alivyokuwa anahisi.
 
Niliomba Mungu iwe ni presha kweli. Kama itakuwa si presha itakuwa ni ile dawa, nilijiambia.
 
Ilipita karibu saa nzima, nikampigia simu Zacharia. Zacharia alipopokea simu nikamuuliza.
 
“Enhe mmefika hospitali?”
 
ITAENDELEA Kesho usikose hapahapa tangakumekuchablob

No comments:

Post a Comment