Sunday, September 25, 2016

SHULE YA MSINGI KILULU KATIKA MUONEKANO WAKE

 Tangakumekuchablog

Muheza, VYUMBA vitatu vya madarasa shule ya msingi Kilulu Wilayani Muheza Mkoani Tanga vimefungwa kufuatia uchakavu wa majengo yake  na mabati kutoboka na kuwa kero wakati wa mvua na jua.
Shule hiyo ambayo imejengwa toka mwaka 1950 kwa nguvu za wananchi pia choo kimebomoka hali inayohatarisha afya za wananchi na usalama wao baada ya shimo hilo refu kutoa harufu kali.
Akizungumza na waandishi wa habari ,  Afisa mtendaji kata ya Kilulu, Jonathan Siafu, alisema kufuatia hali hiyo wanaiomba Serikali na wadau wa elimu kuisaidia ili kuwawezesha watoto kusoma kwa utulivu na kuepuka kujazana darasa moja.
Alisema hali ya uchakavu wa majengo umekuwa wa muda mrefu na wananfunzi kuwa katika wakati mgumu hasa wa mvua ambapo hunyeshewa hali ambayo inalazimika kuwahamisha vyumba vyengine na  ufundishaji wake huwa wa mashaka.
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo, Hashim Kiango (CCM), alisema kwa sasa shule imefikia hali mbaya ambapo baadhi ya wakati wanafunzi hudondokewa na vipande vya mabati na miti ambayo imeliwa na wadudu.
Alisema inawalazimu kuitisha mkutano wa wananchi ambapo watafanya harambee lengo likiwa ni kuinusuru ili isianguke na kuwa kero kwa wanafunzi  kwa kukosa masomo na kupatiwa uhamisho kusoma shule nyengine.
“Shule hii iko barabarani ni mbele ya macho kwa kila apitae hapa na  sijui kwa nini  kwa muda mrefu hakuna hatua yoyote ya kuinusuru, hii ni aibu kwetu kwani bado elimu hatuipi kipaumbele” alisema Kiango na kuongeza
“Kila mgeni anaepita hapa huishangaa na kupiga picha kama kwamba shule imefungwa au inasubiriwa kukarabatiwa, na kila siku hali inazidikuwa mbaya na hakuna hatua yoyote ya kuinusuru” alisema
Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Enzi, Haruni Mussa, alisema shule hiyo imesahauliwa hadi kufikia milango na madirisha kudondoka jambo ambalo ni aibu kwa mustakabali wa elimu.
Alisema milango na madirisha yameng’oka hivyo kutokuwa na udhibiti wa wanafunzi na usalama wakati wa usiku kwa vifaa vya shule na vyawanafunzi hivyo kutaka wadau wa elimu kuiangalia kwa jicho la pili.
“Shule haina milango wala madirisha na nyakazi zausiku kutokuwa na usalama wa vifaa vya shule na vya wanafunzi na kuwa hatari” alisema Mussa
Ameitaka jamii kuiangalia shule hiyo kwa jicho la pili na kuinusuru elimu kwa watoto wao na kwa taifa kwa jumla kuwa msaada kwa maisha ya vijana wao baadae.
                                                    Mwisho


 Diwani kata ya Kilulu Wilayani Muheza Mkoani Tanga, Hashim Kiango pamoja na viongozi wengine wa kijiji wakiangalia moja ya vyumba vya madarasa matatu yaliyochakaa na kulazimika wanafunzi kuhamishwa kwa usalama wao.


 Diwani wa kata ya Kilulu Wilayani Muheza Mkoani Tanga, Hashim Kiango na mwenyekiti wa kitongoni cha Kilulu, Omary Jumanne, wakiangalia shimo la choo cha shule ya msingi ya Kilulu kilichobomoka na kuwa hatari kwa usalama na afya za wananfunzi shuleni hapo.

Kwa habari matukio na michezo ni hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment