Tuesday, September 20, 2016

HADITHI, YAMENIKUTA SALAMA MIE SEHEMU YA 4

HADITHI inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya Usafirishaji abiria Freys Coach inayofanya safari kati ya Tanga, Moshi, Arusha, Babati hadi Singida kila siku na hufanya hivyo kutoka Singida kila siku saa 12 asubuhi 0622 292990
 
YAMENIKUTA SALMA MIE 4
 
ILIPOISHIA
 
Mama huyo alicheka niliposema ‘mgonjwa wangu’
 
“Haya nawaacha kidogo”
 
Akaondoka.
 
“Nikupatie kinywaji gani kaka?” salama akaniuliza.
 
“Hapana, sihitaji kinywaji chochote”
 
“Kwanini, tunayo juisi ya parachichi”
 
“Nitakuja kunywa siku nyingine, usijali”
 
Tukaendelea kuzungumza kwa karibu nusu saa. Wakati nataka kuondoka nilimuachia Salma shilingi elfu hamsini.
 
“Hizi zitakusaidia kununua vitu vidogo vidogo” nikamwambia.
 
“Asante kaka, nashukuru”
 
Salma alikwenda kumuita mama yake ili niagane naye. Mama huyo alipokuja akanishukuru kwa mara nyingine kwa msaada nilioutoa kwa mwanawe siku alipopata ajali.
 
SASA ENDELEA
 
Jina langu ni Salama Aboud, nilikuwa mtoto wa tatu wa mzee Aboud ambaye alifariki dunia wakati mimi nikiwa darasa la saba.
 
Katika kipindi chote hicho nilikuwa nikiishi na mama yangu ambaye alikuwa akinipenda na kunidekeza sana.
 
Kutokana na utoro wangu wa shule nilishindwa kuendelea na masomo ya sekondari. Niliacha masomo nikiwa kidato cha tatu. Vile mama yangu alikuwa anashindwa kunikemea na kwa vile hakukuwa na mtu mwingine wa kunisema kitu, basi nilifanya vile nilivyotaka mimi.
 
Kaka zangu walionitangulia mmoja alikuwa amefariki, wawili walikuwa wakikaa Dodoma kwa baba mdogo.
 
Siku ile niliyopata ajali walikuja Tanga kunijulia hali kisha waliondoka kurudi Dodoma.
 
Sikujua ni kitu gani kilichofanya nimzowee sana Ibrahim. Pengine ni kutoka na wema alionifanyia siku ile nilipopata ajali. Kwanza nilimchukulia kama msamaria mwema lakini mazoea yetu yalipozidi nilianza kumpenda na nikawa na hisia ya kuishi na mtu kama Ibrahim.
 
Nilivutiwa sna na staili yake ya maisha na tabia yake. Lakini Ibrahim hakuwa akionesha kutambua mawazo yangu. Jambo hilo lilikuwa likinikera sana. Kusema kweli nilikuwa ninatamani tuwe wapenzi.
 
Usishangae kwamba nilikuwa nikiwaringia sana wanaume. Walitokea wanaume wawili waliotaka kunioa nikawakataa bila sababu yoyote.
 
Mama yangu kwa kufuatisha mawazo yangu, naye aliwatolea nje.
 
Mara kwa mara mama alikuwa akiniuliza.
 
“Utaolewa lini mwanangu, wenzako wote wameolewa?”
 
“Hao walioolewa waache waolewe, mimi niache tu”
 
“Sasa utakaa hivi hivi mpaka lini?”
 
“Kwani kuna mume aliyekwambia ananitaka nikamkataa?”
 
“Si walikuja vijana wawili ukawakataa mwanangu”
 
“Bado unawakumbuka tu”
 
“Nawakumbuka kwa sababu sioni dalili ya kutokea mume mwingine, naona kama umejitia nuksi”
 
“Muda wangu wa kuolewa ukifika nitaolewa tu mama”
 
Haukupita muda mrefu ndipo alipojitokeza Ibrahim.
 
Ibrahim nilimuonesha dalili zote za mapenzi kwani haikuwa rahisi kwangu mimi mwanamke kumueleza wazi kuwa nimempenda.
 
Siku moja nikaukata mzizi wa fitina. Nilimtumia meseji nikamwambia.
 
“Natamani ningekuwa mke wako Ibrahim”
 
Akarudisha jibu na kuniuliza.
 
“Kwanini?”
 
Nikamtumia meseji nyingine ya kumwambia.
 
“Nimependa tabia zako”
 
Akanijibu tena kwa kuniambia.
 
“Kama ungependa tuoane subiri nijiandae”
 
Kwa sababu nilikuwa nampenda, jibu lake hilo likanifurahisha.
 
Siku ya pili yake tulikutana katika hoteli moja tukazunguza sana kuhusu mapenzi.
 
Akaniambia yeye ni muangalifu sana katika kutafuta mchumba lakini katika siku chache tulizokuwa pamoja amegundua kuwa ninafaa kuwa mchumba wake. Ibrahim hakujua alikuwa amenifurahishaje kutokana na kauli yake hiyo.
 
Dhamiri yetu ikatimia. Baada ya kuzungumzia uchumba kwa wiki kadhaa, hatimaye Ibrahim akaleta barua ya uchumba kwa mama yangu.
 
Mama yangu aliipokea kwa mikono miwili kwa sababu nilishamueleza jinsi nilivyokuwa ninampenda Ibrahim.
 
Mama alimfahamisha baba mdogo aliyekuwa Dodoma kuwa kumeletwa barua ya uchumba ya Salma.
 
Baba mdogo akanipigia simu kuniuliza kama nimempenda huyo mchumba.
 
“Nimempenda ndio maana nilimuelekeza aje kwetu” nikamjibu.
 
“Nimesikia kuwa ndiye yule aliyekusaidia ulipopata ajali?”
 
“Ndiye yeye”
 
“Imekuwa heri. Huyo ni mchumba mwema. Mimi pia nimemkubali”
 
Baada ya baba mdogo kuzungumza na mimi alimpigia mama akamwambia kuwa na yeye amekubaliana na huo uchumba.
 
Mbali ya kumjulisha baba mdogo, mama pia aliwajulisha wajomba, yaani ndugu zake. Wote wakaukubali uchumba huo na jibu likapelekwa kwa Ibrahim kuwa uchumba wake umekuwa makubuli, yaani umekubaliwa.
 
Sasa ikawa ni mipango ya harusi. Mipango ya harusi yetu ilichukua karibu miezi mitatu. Nataka niseme ukweli kuwa tangu nijuane na Ibrahim mpaka tunakuwa wachumba sikuwahi kutembea naye hata siku moja.
 
Mimi sikutaka jambo hilo kwa sababu baadhi ya wanaume ukishatemmbea nao hubadili mawazo na kutafuta wachumba wengine.
 
Ibrahim pia hakuonesha kuwa na uchu wa wasichana. Alipoona dhamiri yangu ilikuwa ni kuoana, hakuwahi hata siku moja kunishawishi tufanye kitu.
 
 Kwa hilo peke yake nilimsifu na kuona alikuwa mwanaume madhubuti aliyeweza kuuzuia moyo wake. Ni wanaume wachache sana wenye tabia kama ya Ibrahim.
 
Ndoa yetu ilifungwa siku ya ijumaaa saa saba na nusu. Ilifungwa katika msikiti wa Chumbageni baada ya mshuko wa swala ya ijumaa.
 
Mimi nilikuwa niko nyumbani nikimsubiri mume atoke msikitini. Tangu asubuhi nilikuwa saluni nikipambwa na kuchorwa piko. Nilirudishshwa nyumbani saa sita.
 
Nilipelekwa saluni nikitokea kwa kungwi ambako nilikaa kwa wiki maja nikifundwa jinsi ya kuishi na mume.
 
Nakumbuka somo moja muhimu nililolipata kwa kungwi ni kuwa nisimnyime mume wangu anapotaka penzi hata kama niko jikoni napika.
 
“Acha kazi zako ukamridhishe mumeo” kungwi wangu aliniambia.
 
Ibrahim aliporudi nyumbani kutoka msikitini alifuatana na watu watatu mmojawapo akiwa sheikh aliyetuozesha.
 
Ibahim alinipa mkono mke wake. Na hii ni kawaida. Mume akishakuoa akiingia chumbani hukupa mkono.
 
Sheikh akatuombea dua na kututaka tuishi maisha marefu, tupate watoto wema, tuishi kwa upendo na kuaminiana. Lakini akaongeza sentesi moja mabayo sikuipenda. Alisema.
 
“Mvumiliane, msameheane, muaminiane lakini kama itatokea mnaachana muachane kwa wema”
 
Kichwa changu kilikuwa kimefunikwa kwa mtandio unaoonya. Sheikh aliposema hivyo, niliinua uso wangu niliokuwa nimeuinamisha chini. Nikamtupia jicho Ibrahim huku yale maneno, “Kama itatokea mnaachana muachane kwa wema…” yakipita akilini mwangu.
 
Wakati namtupia jicho Ibrahim nilikuwa kama namuuliza. “Hivi tutakuja kuachana mimi na wewe?”
 
Moyoni mwangu sikutarajia kwamba hilo lingeweza kutokea kwa vile sheikh alishatuambia tuvumiliane, tusameheane na tuaminiane.
 
Niliamini kwa falsafa ya kuvumiliana, kusameheana na kuaminiana, suala la kuachana lingekuwa mbali sana na ndoa yetu.
 
ITAENDELEA kesho hapahapa tangakumekucha blog usikose uhondo huu nini kitatokea baada ya wawili hao kufunga ndoa na ile kauli ya Sheikh kusema mukiokosana muachane kwa wema
 
 
 
 
 
 

No comments:

Post a Comment