Thursday, September 15, 2016

HADITHI, YAMENIKUTA SALAMA MIE (1)

SIMULIZI MPYA
 
YAMENIKUTA SALMA MIE 1
 
MTUNZI. FAKI A FAKI 0713 340572
 
Naitwa Ibrahim Amour. Ni mwenyeji wa Morogoro. Nilisoma morogoro hadi kidato cha sita. Nikafanikiwa kuingia chuo kikuu cha Mlimani jijini Dar es Salaam.
 
Nilipohitimu elimu ya chuo kikuu na kupata shahada yangu, nilifanikiwa kupata ajira mamlaka ya mapato TRA, nilifanya kazi kwa miezi michache tu nikahamishiwa Tanga.
 
Baada ya kuishi katika nyumba ya wageni kwa siku chache nilifanikiwa kupata nyumba ya kupangisha maeneo ya Usagara.
 
Wakati huo nilikuwa sijaoa bado na nilikuwa na mdogo wangu aliyemaliza kidato cha nne aliyekuwa amekaa nyumbani huko kwetu Morogoro. Nikamuita ili nikae naye pale nyumbani kwa sababu nilikuwa peke yangu.
 
Zacharia akaja Tanga baada ya kumtumia nauli. Nilikuwa pia na mpango wa kumtafutia kazi sehemu yeyote ambayo ningefanikiwa.
 
Kwa vile bado nilikuwa mgeni katika jiji hilo nikaona nimsubirishe kwanza ili niweze kuzoeana na wenyeji ambapo ingekuwa rahisi kumuombea kazi sehemu yoyote.
 
Nikiondoka asubuhi kwenda kazini ninamuacha Zacharia nyumbani. Kwa kawaida nikiondoka asubuhi hurudi jioni.
 
Mara kwa mara Zacharia alikuwa akiniuliza kuhusu ule mpango wa kumtafutia kazi. Na mimi nilimjibu asubiri kwanza.
 
Baada ya miaka miwili nikafanikiwa kununua gari. Sasa nikawa naenda kazini na kurudi na gari langu. Miezi michache baadaye nikanunua kiwanja jirani tu na pale nilipokuwa naishi.
 
Wakati naanza kujenga msingi tu, nikapata matatizo kazini. Mimi na maafisa wenzangu watatu tulikamatwa na polisi tukidaiwa kujihusisha na wizi wa mapato ya serikali.
 
Tulisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi. Wakati uchunguzi unaendelea tulikuwa nje kwa dhamana. Baada ya uchunguzi huo kukamilika tulifikishwa mahakani.
 
Ilikuwa kesi iliyotuendesha sana. Iliunguruma kwa karibu miezi minane. Katika  kipindi hicho nilikonda kwa hofu na wasiwasi wa kufungwa. Kwa bahati njema shahidi muhimu wa kesi ile ambaye angetoa ushahidi ambao ungeniweka mahali pabaya, alifariki dunia kwa maradhi ya sukari.
 
Hukumu ilipokuja kutolewa mwenzangu mmoja akaenda jela miaka saba. Mwingine alionekana hakuwa na hatia. Mimi nikaachiwa kutokana na kutokuwa na ushahidi wa kutosha.
 
Mwenzangu aliyeonekana hakuwa na hatia alirudishwa kazini. Mimi nikafukuzwa kazi kabisa.
 
Pia nilishukuru. Niliona bora kufukuzwa kazi kuliko kufungwa na ukitoka  huko huna kazi.
 
Hata hivyo mpango wangu wa kuendeleza ujenzi wa nyumba yangu ambao nilikuwa nimeshauanza ukaishia hapo hapo.
 
Nilikuwa na akiba yangu benki nikaamua kuanzisha mradi wa kuchukua tenda za usambazaji vitu mbalimbali katika mashirika, taasisi na idara za serikali.
 
Nikafungua ofisi yangu jirani na maktaba. Baada ya kujitangaza katika maofisi mbalimbali nilifanikiwa kupata tenda ndogo ndogo lakini nikitegemea kuwa baadaye ningeweza kupata tenda kubwa kubwa.
 
Nilikuwa nikisaidiana na Zacharia na nilikuwa nimeajiri msichana mmoja aliyekuwa akibaki ofisini kwa ajili ya  kazi ndogo ndogo kama vile kufungua ofisi asubuhi na kuifunga jioni, kupokea simu na kuhifadhi kumbukumbu zetu za kiofisi.
 
Siku moja nikashuhudia ajali karibu na ofisi yangu.
 
Msichana mmoja ambaye alikuwa akiendesha baskeli aligongwa na gari ndogo ambayo haikusimama.
 
Wakati tukio hilo linatokea mimi nilikuwa nikiondoka na gari langu ofisini kwangu. Nikalisimamisha gari karibu na mahali alipoanguka yule msichana na kuzirai.
 
Kitu kilichonishitua ni kwamba alikuwa akitokwa na damu nyingi iliyokuwa ikisambaa barabarani.
 
Baskeli yake ilikuwa imeanguka kando yake ikiwa imekunjwa kama iliyokanyagwa na treni.
 
Gari lililomgonga lilikimbia mara tu baada ya ajali kutokea.
 
Kutokana na kuona ile damu iliyokuwa ikitoka kwa wingi, nilizima gari nikashuka na kumfuata yule msichana. Sikuwaza hili wala lile, nilimzoa pale chini bila kujali damu iliyokuwa ikimtiririka ambayo ilikuwa ikiingia kwenye nguo zangu.
 
Nilimpakia kwenye siti ya nyuma ya gari langu, nikajipakia na kumuwahisha hospitali ya Bombo ambapo alipokelewa na kushughulikiwa.
 
Sikujua kama angepona kutokana na ile damu iliyokuwa ikimtoka kwa wingi, nikapwatwa na wasiwasi.
 
ITAENDELEA kesho

No comments:

Post a Comment