Monday, September 26, 2016

HADITHI, YAMENIKUTA SALAMA MIE SEHEMU YA 7

HADITHI inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya Usafirishaji abiria ya Freys inafanyayo safari zake Tanga, Moshi, Arusha , Babati hadi Singida kila siku, Freys hufanya safari zake kama hivyo Singida kila siku. Tanga ofisi zake zipo Tanga barabara ya 12, simu 0622 292990
 
YAMENIKUTA SALMA MIE 7
 
ILIPOISHIA
 
Alipoondoka na mdogo wake nikaenda bafuni kuoga. Nilipomaliza nilivaa. Nikaenda kuketi sebuleni kwangu kusubiri Rita anipigie simu.
 
Nilipoona kimya na muda unakwenda nikampigia mimi.
 
“Shoga habari ya asubuhi?” nikamuuliza alipopokea sim.
 
“Nzuri shoga, mume wangu ndio ameondoka sasa hivi. Nilikuwa nataka kukupigia kukwambia jitayarishe”
 
“Nimeshajitayarisha shoga”
 
“Basi njoo, mimi najiandaa”
 
Nikarudi chumbani kwangu kuchukua baibui langu nikalivaa na kupachika mkoba wangu begani, nikatoka.
 
SASA ENDELEA
 
Nilifunga mlango wangu wa mbele kwa funguo nikaenda nyumbani kwa jirani yangu.
 
Aliniacha sebuleni kwa karibu nusu saa kisha naye akatoka na kuniambia.
 
“Twenzetu”
 
Tulikwenda nyuma ya nyumba yake akafungua geti na kulitoa gari.
 
“Wewe jipakie kabisa, mimi nafunga geti” akaniambia na kurudi kwenye geti.
 
Aliingia ndani akalifunga geti hilo kisha akazunguka kwa mlango wa mbele.
 
Alifunga mlango na kuja kwenye gari. Wakati huo nilikuwa nimeshajipakia nikiwa kando ya siti ya dereva.
 
Akafungua mlango na kujipakia.
 
“Sasa twenzetu” akaniambia huku akiliwasha gari.
 
Alilirudisha gari kinyume nyume hadi barabarani. Akaligeuza na tukaanza safari yetu.
 
“Kinachonikera kwa yule mganga ni foleni ya watu, yaani ukifika unakuta msururu wa watu wanaomsubiri” Shoga yangu aliniambia wakati gari likiwa katika mwendo.
 
“Yeye mwenyewe anakuwa wapi” nikamuuliza.
 
“Anakuwepo ila wale watu wanafika kabla mwenyewe hajaamka. Wanamsubiri hapo nje mpaka aamke, aoge, anywe chai, unakuta foleni inakuwa ndefu”
 
“Sasa tutafanyaje shoga, tutawahi kurudi mapema kweli?”
 
“Tujaribu kubahatisha, tunaweza tusikute foleni ndefu. Kuna siku niliwahi kuja sikukuta mtu yeyote lakini kuna siku nilikuta foleni iliyonikatisha tamaa”
 
“Ukafanyaje?”
 
“Ilinibidi nisubiri hivyi hivyo. Mpaka nashughulikiwa ilikuwa imeshafika saa sita’mchana. Lakini nashukuru mambo yangu yalikwenda vizuri”
 
“Kama tutakuta foleni ndefu utaniacha niendelee kusubiri, hata kama nitaondoka jioni si kitu”
 
Dakika chache baadaye tukawa tumefika katika eneo hilo la Kisosora. Nyumba ya mganga huyo ilikuwa kibanda kidogo kilichojengwa kwa miti na udongo. Mbele ya kibanda hicho kulikuwa na nyumba kubwa ya matofali iliyokuwa haijakalmilika.
 
Tuliacha gari mbele ya ile nyumba tukaingia uani. Tulikuta watu ambao hawakuzidi kumi waliokuwa wameketi kwenye baraza ya kibanda hicho.
 
“Leo hakuna watu wengi, ni wale wachache tu” Rita akaniambia.
 
“Mbona hawajapanga foleni’ nikamuuliza.
 
“kila mtu anajijua ni wa ngapi kuingia. Sisi ndio tutakuwa watu wa mwisho. Labda waje wengine nyuma yetu”
 
Na sisi tukaenda kwnye ile baraza. Tuliwasalimia watu tuliowakuta kisha tukakaa.
 
Wakati tunakaa, mtu mmoja akatoka ndani ya kile kibanda. Alikuwa ni mteja aliyekwishahudumiwa. Mtu mwingine akaingia.
 
Baada ya nusu saa mtu huyo naye akatoka akaingia mwingine. Yule aliyeingia hakukaa sana, akatoka na kuingia mwingine.
 
Kitu kilichonipa moyo ni kuwa foleni ilikuwa ikienda kwa haraka.
 
Ilikuwa inakaribia kuwa saa nne na nusu, mimi na Rita tulipoingia.
 
Mganga mwenyewe alikuwa mzee aliyekuwa amejifunga kaniki. Chumba chake hakikuwa na mwanaga wa kutosha kutokana na kuwa na dirisha dogo. Tulipoingia tu nilianza kusikia joto.
 
“Karibuni” Mganga huyo akatuambia.
 
Alikuwa amekaa kwenye jamvi lililoenea chumba kizima.
 
Tukakaa kwenye jamvi mbele yake.
 
“Shikamoo” Rita akamwamkia na mimi nikamwammkia.
 
“Marahaba hamjambo”
 
“Hatujambo. Naona kama umenisahau” Rita akamwambia.
 
Mganga akamtazama vizuri.
 
“Kama nakukumbuka”
 
“Mimi ni Rita. Niliwahi kuja ukanishughulikia matatizo ya mume wangu”
 
“Ahaa! Nimekukumbuka. Uliniambia unaishi Usagara”
 
“Haswaa! Ni kweli umenikumbuka”
 
“Muda mrefu umepita sijakuona ndio maana nimekusahahu kidogo. Habari za siku?’
 
“Nzuri. Nimekuletea huyu mteja, ni rafiki yangu”
 
“Ana matatizo gani”
 
“Atakueleza”
 
Nikataka kumpima yule mganga kujua uwezo wake.
 
“Shida yangu nataka unitazamie ramli?” nikamwambia.
 
“Hapa ramli ndio nyumbani kwake, nipe mkono wako” Mganga akaniambia huku akininyooshea mkono wake.
 
Nikanyoosha mkono wangu na kumpa. Akaushika na kutazama kiganja changu.
 
“Huu mstari wa maisha unaonesha kuwa una tatizo na mume wako. Maisha yako hayaendi vizuri’ Mgaga akaniambia kisha akanitazama na kuniuliza.
 
“Kweli au uongo?”
 
“Ni kweli” nikamjibu.
 
“Enhe. Matatizo ya mume wako hayatofautiani sana na matatizo aliyokuwa nayo mume wa mwenzako. Kweli au uongo?”
 
“Ni kweli”
 
“Enhe. Mwanamme pesa anapata lakini hazionekani. Ugomvi hawishi nyumbani. Kweli au uongo”
 
“Ni kweli”
 
“Yaani ni sawa na kusema kuwa mapenzi hayapo nyumbani. Si kama ilivyokuwa wakati mnaanza sasa maisha. Kweli, uongo”
 
“Ni kweli”
 
Sasa mama una wasiwasi, unahisi kama mko wengi. Kweli, uongo’
 
“Ni kweli”
 
“Alama za kiganja chako zinanionesha kuwa mumeo ana nyumba ndogo iliyoharibu akili yake”
 
Hapo  hapo nikamtazama Rita kwa mshangao.
 
“Unasikia maneno hayo. Mimi nilikwambia utaambiwa kila kitu” Rita akaniambia.
 
“Yaani mume wangu ana mwanamke wa nje?” nikamuuliza mganga huyo kwa taharuki.
 
“Wewe unadhani ni kitu gani kimeharibu tabia yake?’
 
“Huyo msichana ndio amemuharibu?”
 
“Yaani ndio anampenda kuliko wewe”
 
Nikatingisha kichwa changu kumkubalia.
 
“Asante kwa kunifahamisha, sasa na mimi nataka kumkomoa. Nataka amuache huyo mwanamke anipende mimi  peke yangu, anijali na kunisikiliza, Kila ninachomwambia atii”
 
“Hata kama utataka akununulie gari atakununulia”
 
“Nifanyie hiyo kazi, utahitaji shilingi ngapi?’
 
“Kwa vile umeletwa na mteja wangu wa siku nyingi, nitakufanyia shilingi laki moja”
 
Nikaguna na kumtazama Rita.
 
Sikuwa nimechukua shilingi laki moja. Nilikuwa na shilingi elfu hamsini tu kwenye pochi yangu.
 
“Unajua shoga nilifanya ujinga nilipoondoka nyumbani, nilichukua shilingi elfu hamsini tu”
 
“Sasa mimi nitakutolee elfu hamsini, tukifika nyumbani unirudishie”
 
“Sawa shoga, nitakurudishia”
 
Rita akafungua pochi yake na kutoa shilingi elfu hamsini na mimi nikatoa kiasi kama hicho kutoka kwenye pochi yangu. Tukampa yule mganga.
 
“Anaitwa nani mumeo?” Mganga akaniuliza baada ya kupokea zile pesa.
 
“Anaitwa Ibrahim Amour”
 
ITAENDELEA kesho usikupite uhondo huu nini kitatokea pale kwa mganga kabla hawajaondoka na baada ya kuondoka huko mbele

No comments:

Post a Comment