Thursday, October 13, 2016

HADITHI, YAMENIKUTA SALMA MIE SEHEMU YA 18

HADITHI
 
YAMENIKUTA SALMA MIE
 
ILIPOISHIA
 
Nikafungua mlango wa gari na kushuka. Nikiwa nje ya gari nilimpungia mkono wa kumuaga na yeye akanipungia.
 
Nikaondoka zangu. Na yeye akaondka na gari. Nilipitia kwenye bucha ya nyama nikanunua kilo moja ya nyama kisha nikaenda kwenye duka ninalonunulia vitu. Nikanunua kilo mbili za mchele na mahitaji mengine kisha nikarudi nyumbani.
 
Sebuleni nilimkuta shemeji Zacharia akiangalia Tv. Ibrahim hakuwepo. Nikajua alikuwa chumbani amelala. Sikuingia chumbani kwa kuwa nilijua angeniuliza ninakotoka kwa vile nilichelewa sana.
 
Nikaingia katika chumba kingine ambacho huweka nguo zangu za kufanyia kazi za nyumbani. Nikabadili nguo nilizokuwa nimevaa kisha nikaingia jikoni na kutayarisha ile nyama. Nyama ilipokuwa jikoni nilichambua mchele. Nilikuwa nimekusudia kupika pilau.
 
Baada ya masaa mawili pilau ikawa tayari. Nikatenga chakula juu ya meza. Nikamwaambia shemeji akamchukue kaka yake waende wakale. Mimi nilijipakulia kwenye sahani yangu nikaenda kuketi uani peke yangu.
 
Wakati ninakula kile chakula nilikuwa nikimuwaza Chinga na jinsi nitakavyoweza kuwa naye. Nilijiambia itakuwa ni uzembe kuacha aoe mke mwingine wakati alikuwa ameshanipenda na amekuwa akinipa pesa nyingi.
 
“Nitaendelea kuishi na hili zezeta hadi lini? Mwisho nitakosa hata nguo ya kuvaa” nikajisemea peke yangu.
 
SASA ENDELEA
 
Baada ya kumaliza kula chakula nilirudi ndani. Nilimkuta Ibrahima na mdogo wake na wao wamemaliza kula.
Zacharia aliondoa vile vyombo akaviingiza jikoni kisha akatoka kusafisha meza. Nilijua kuwa alifanya hivyo kwa kuniogopa mimi kwani tayari alikwishaiona hali ilivyo pale nyumbani.
 
Tangu kaka yake apofuke macho nilikuwa mkali kama simba na sikuwa na adabu kwa kaka mtu wala kwa mdogo mtu.
 
“Ukimaliza kusafisha meza uje uoshe vyombo” nikamwambia Zacharia.
 
“Nioshe vyombo?” akaniuliza kwa mshangao. Ilikuwa ndiyo mara yangu ya kwanza kumwambia hivyo.
 
“Sasa kumbe ulitaka aoshe nani? Kama hutaki mwaambie kaka yako aje aoshe yeye!” nikamwaambia kwa jeuri na kuongeza.
 
 “Mmenifanya mimi ni kama mtumishi wenu.Chakula nitafute mimi, kupika nipike mimi na vyombo pia nioshe mimi!. Haitawezekana”
 
Zacharia akanyamaza kimya.
 
“Zacharia nenda kaoshe” Ibrahim akamwaambia mdogo wake.
 
Zacharia alipomaliza kusafisha meza aliingia jikoni kuosha vyombo.Mimi nilikwenda kuoga kisha nikabaki chumbani nikijua kuwa Ibrahim asingeingia tena muda ule.
 
Mchana ukapita. Ilipofika usiku wakati Ibrahim ameingia chumbani kulala, mimi niliketi sebuleni kuangalia Tv peke yangu. Zacharia pia alikuwa ameshaenda kulala.
 
Lakini lengo langu halikuwa kuangalia Tv. Lengo langu lilikuwa kumpigia simu Chinga tuzungumze. Nikambipu na muda uleule akanipigia.
 
“Vipi Chinga umeshalala?” nikamuuliza baada ya kupokea simu.
“Hapana, nilikuwa namalizia bia yangu ya pili ndipo nikalale” akaniambia.
 
“Kumbe unakunywa?”
 
“Bia zangu hazizidi mbili. Ni za kupatia usingizi tu. Uko wapi?”
 
“Niko nyumbani”
 
“Mbona umenipigia, jamaa yuko wapi?”
 
“Yuko chumbani ameshalala, mimi nipo sebuleni.Nilitaka tuzungumze kidogo”
 
“kuhusu nini?”
 
“Kuhusu yale mazungumzo yetu. Ni kwamba mimi nimeshakubali lakini sasa huyu mwanaume nitamuachaje?”
 
“Si umdai talaka tu”
 
“Hawezi kuitoa.Mimi ndio tegemeo lake kwa sasa”
 
“ Hilo si tatizo.Tukutane hapo kesho tuzungumze hilo suala”
 
“Tukutane wapi?
 
“Sema wewe”
 
“Au nikufuate hapo hoteli?”
 
“Saa ngapi?”
 
“Usiku itakuwa vizuri”
 
“Utaweza kutoka usiku?”
 
“Nitatoka hivyo hivyo. Mchana sitaweza kuja hapo. Kuna macho ya watu wengi”
 
“Sasa nikufuate na gari au….?”
 
“Nitakuja na teksi. Wewe niambie upo chumba namba ngapi”
 
“Nipo chumba namba 15, kipo ghorofa ya kwanza”
 
“Mimi nitakuja humo chumbani moja kwa moja”
 
“Sawa lakini utaniambia saa utakayo kuja”
 
“Nitakuambia kesho”
 
“Haina tatizo. Sasa utanipigia saa ngapi hapo kesho?”
 
“Siwezi kukuambia kwa sasa lakini nitakupigia wakati wa mchana kukujulisha. Na huo usiku nitakapo ondoka pia nitakujulisha”
“Sawa nitakusubiri”
“Okey.Usiku mwema”
 
“Na kwako pia’
 
Chinga akakata simu.  Moyo wangu ukawa umefarijika kwa kuzungumza naye. Nikainuka na kuingia chumbani. Wakati ninapanda kitandani kulala nilidhani kuwa Ibrahim alikuwa usingizini. Niligeuka upande wangu nikajilaza. Mara nikasikia sauti yake akiniita.
 
Kwanza nilinyamaza. Aliponiita mara ya pili nikamuuliza.
 
“Unasemaje?”
 
“Unajua mke wangu hivi sasa tabia yako imebadilika sana …..” akaniambia.
 
Hapo hapo nikajua alikokuwa anaelekea. Nikamkata kauli.
 
“Unaanza…unaanza…unaanza! Sitaki maneno. Kama huna maneno ya maana ya kuniambia nitatoka humu chumbani nikuachie chumba chako nikatafute pa kulala”
 
Ibrahim akanyamaza. Uwanja wa kusema ukawa ni wangu.
 
“Mwanaume una gubu kama nini. Kila unalofanyiwa huridhiki. Unataka roho yangu au unataka nini?.Hebu niambie!”
 
“Salma mimi sina gubu isipokuwa tabia yako unayoionesha tangu mimi nipate matatizo ya macho…..”
 
Sikumngoja amalize maneno yake, nikainuka kwa jazba na kuketi kitandani.
 
“Sitaki maneno mengi. Kama mimi nimekuwa sina tabia nzuri kukuletea chakula wewe na ndugu yako ule, basi nipe talaka yangu niondoke. Halafu utafute huyo mke mwenye tabia nzuri” nikamwaambia kwa ukali huku nikimnyooshea mkono wa kudai talaka.
 
“Salma wewe hutaki kuambiwa ukweli. Ukiambiwa ukweli unakuja juu. Mbona juzi na jana wakati nikiwa mzima hukudai talaka?”
 
“Hukuwa na gubu kama ulivyo hivi sasa. Maneno yamekuwa hayaishi. Balaa gani hili jamani!.Ule muda wa kulala na kupunzisha mwili, ndiyo unaanza maneno. Sasa mimi nitaondoka hapa kwako hata kama hutanipa talaka!”
 
Nikashuka kwenye kitanda huku nikiendelea kugomba. 
 
“Sitalala tena humu ndani. Nimechoka na kelele zako”
 
“Sasa unakwenda wapi?” Ibrahim akaniuliza aliposikia ninafungua mlango.
 
Sikumjibu kitu nikatoka na kwenda sebuleni. Nikajilaza kwenye kochi. Baada ya muda kidogo nilimuona akitoka chumbani huku akiniita.
 
“Salma! Salma!”
 
Alikuwa akipapasa kwenye kuta akielekea sebuleni.
 
Nikamnyamazia kimya. Alipoona kimya akadhani labda nilikuwa nimetoka nje na kwenda zangu. Akapapasa ukuta hadi kwenye chumba anacholala Zacharia. Akamgongea.
 
“Zacharia! Hebu fungua mlango!” sauti yake ilikuwa imefadhaika.
 
Zacharia alipofungua mlango nilisikia akimwaambia. 
 
“Shemeji yako ametoka, sijui amekwenda wapi. Hebu toka umuangalie”
 
“Kwani amekuambia anakwenda wapi?” Zacharia akamuuliza.
 
“Hakuniambia. Tulisemeshana kidogo akatoka kwa hasira, sijui amekwenda wapi”
 
Zacharia akatoka na kuja sebuleni, akawasha taa na kuniona nimelala kwenye kochi.
 
“Shemeji si huyu hapa” akasema.
 
“Yuko wapi?” Ibrahim akamuuliza kwa pupa.
 
“Amelala kwenye kochi ”
 
Ibrahim akapapasa kuta na kuja pale sebuleni.
 
“Yuko wapi?” akauliza tena.
 
Wakati wote huo nilikuwa nimenyamaza kimya.
 
“Shemeji kaka anakuuliza” Zacharia akaniambia.
 
Mimi nikaendelea kunyamaza.
 
“Salma!” Ibrahim akaniita.
 
Sikumjibu.
 
ITAENDELEA kesho usikose

No comments:

Post a Comment