Sunday, October 16, 2016

HADITHI, YAMENIKUTA SALMA MIE SEHEMU YA 21

HADITHI
 
YAMENIKUTA SALMA MIE 21
 
ILIPOISHIA
 
“Ni kwa sababu mchana nilikuwa na kazi ya kufua nguo”
 
“Sasa Salma tutafanya nini?. Unadhani suala lake litakuwa kikwazo tusiwe pamoja?”
 
“Litakuwa kikwazo. Wewe si unataka kunioa?”
 
“Na umesema hataweza kukupa talaka hata kama utaidai?”
 
“Hataweza kunipa”
 
“Je ukiifuatilia Bakwata?”
 
“Bakwata nikawaambie nini?”
 
“Kwamba huyo mwanaume hana uwezo wa kuishi na wewe, kwa hiyo unataka muachane”
 
“Bakwata hawatakubali, wataona ninamkataa kwa sababu amepofuka. Wataninasihi niendelee kuwa naye hivyo hivyo”
 
Chinga akapiga funda jingine la bia. Alipoirudisha birauli aliniambia. 
 
“Hatutakosa njia nyingine. Nakupa muda uendelee kufikiri lakini jaribu kumshinikiza akupe taraka”
 
“Wewe utakuwa hapa Tanga mpaka lini?”
 
“Sina muda mrefu. Naweza kuondoka siku yoyote nitakayoamua”
 
“Basi tuendelee kufikiria njia nyingine. Kwa vile sina nia ya kuendelea kuishi naye, kama hataniacha yeye nitamuacha mimi!”
 
“Lakini umenipenda?” Chinga akaniuliza ghafla. Macho yake yalionesha kuwa ulevi ulikuwa umeanza kumchukua. Iliwezekana alianza kunywa muda mrefu.
 
SASA ENDELEA
 
“Kama nisingekupenda nisingekuja huku” nikamjibu.
 
“Kama ni kweli kunywa bia kidogo”
 
“Nimekuambia situmii”
 
“Onja kidogo”
 
“Nitaonya siku nyingine”
 
“Basi njoo uketi hapa”
 
Alimaanisha nikaketi naye kitandani.
 
“Hapa nilipokaa panatosha”
 
Chinga akainuka na kunifuata akanishika mkono na kuniinua. 
 
‘Mbona uko hivyo Salma? Hebu twende tukakae pale”
 
“Chinga utasababisha nichelewe nyumbani” nikajidai kulalamika huku nikimfuata kwenye kitanda. Nikaketi na yeye akaketi.
 
“Wewe umeshaamua kuwa na mimi, unajali nini kuchelewa? Wewe ni wangu tu au si kweli?”
 
Nikanyamaza kimya na kubaki kumtazama machoni. Akatabasamu na kunipitishia mkono kiunoni. 
 
 “Una macho ya kimahaba kweli!” akaniambia kisha akanibusu midomoni. Kilichofuatia baada ya hapo sitakisema. Ni aibu.
 
Ilikuwa saa nne ikikaribia kuwa na nusu Chinga aliponirudisha nyumbani. Nilimwaambia asimamishe gari nyumbni kwa jirani yangu Rita ili Ibrahim na mdogo wake wasijue kuwa nimeletwa na gari.
 
Chinga akanipa shilingi laki moja kabla sijashuka kwenye gari.
 
“Ahsante” nikamwaambia kabla ya kuagana naye.
 
Nikashuka kutoka kwenye gari na kutembea kuelekea nyumbani.
Nilikuta mlango wa mbele ukiwa umefungwa. Nikabisha. Zacharia akaja kunifungulia, nikaingia.
 
“Habari ya saa hizi?” akanisalimia.
 
“Nzuri” nikamjibu huku nikizuga kwa kuangalia kwenye runinga.
 
“Unatazama kanda?” nikamuuliza.
 
Niliona deki imewashwa na kuonesha filamu za kina Kanumba.
 
“Ndiyo shemeji” Zacharia akanijibu huku akifunga mlango kisha akaniuliza.
 
“Vipi hali ya shangazi?”
 
“Bado anaumwa” nikamjibu huku nikiketi kwenye sofa.
 
Nikajifanya nataka kuangalia ile kanda. Zacharia aliondoka kwenye mlango naye akaja kuketi.
 
“Kwani ana tatizo gani?” akaniuliza.
 
“Ni uzee tu. Kila mahali panamuuma. Na presha yake pia iko juu” nikadanganya. Kwa kuwa sikutaka tuendelee na mazungumzo yale nikamuuliza. 
 
“Kaka yako ameshalala?” nikamuuliza Zacharia.
 
“Ameingia chumbani muda mrefu”
 
“Mmekula nini?”
 
“Tumekunywa chai. Nilikwenda kununua mkate”
 
Nikajidai kumuuliza  “Mmenibakishia na mimi?”
 
“Tumekuachia silesi zako”
 
“Mmefanya vizuri, njaa inaniuma”
 
Baada ya hapo tukabaki kimywa tukiangalia ile kanda. Kukaa kwangu pale na kuangalia ile kanda ilikuwa ni kuvunga tu kwani nilijua nilikuwa nimechelewa kurudi na nilikuwa na ile hisi ya kutenda dhambi.
 
Ghafla Ibrahim akatoka mle chumbani na kumuuliza mdogo wake.
 
“Shemeji yako hajarudi hadi muda huu?”
 
ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment