Sunday, October 30, 2016

HADITHI, YAMENIKUTA SALMA MIE SEHEMU YA 24



HADITHI
 
YAMENIKUTA SALMA MIE ( 24)
 
ILIPOISHIA
 
Katika maongezi yetu tulipanga kukutana kesho yake usiku pale pale hoteli. Baada ya hapo nikamwaambia kuwa nilikuwa nyumbani kwa shoga yangu Rita na kumtaka asalimiane naye.
 
Nikampa simu Rita, wakasalimiana. Baada ya hapo Rita akanirudishia simu.
 
Nilikaa kwa Rita hadi saa mbili usiku nikarudi nyumbani kwangu.
Kulikuwa na wali uliobaki mchana, Nikaona tule huo huo. Nikachemsha chai na kuitia kwenye chupa kisha nikaandaa chakula hicho mezani. Kama kawaida yangu nilijitengea chakula changu na kwenda kuketi uani peke yangu.
 
Nilipomaliza kula na kurudi ndani nilikuta chakula kimebaki kingi. Kumbe Ibrahim hakula, alikunywa chai tupu. Na mimi kwa jeuri yangu sikutaka kumuuliza kwanini hakula chakula kwani nilishagudua tangu niliporudi kutoka kwa Rita, Ibrahim alikuwa amekasirika.
 
SASA ENDELEA
 
Alionekana kuwa mnyonge sana.Nilihisi labda alinifikilia nilikuwa natoka kwa mwanaume. Kama alinidhania hivyo alikuwa amejikangaja.
 
Licha ya kwamba nilitaka kumfanya mpumbavu lakini Ibrahim alikuwa mtu mwenye subira na busara pia, kwani alisubiri hadi usiku wakati tunajiandaa kulala chumbani ndipo aliponitolea undani wake.
 
Akanieleza kwamba amegundua kuwa nilikuwa na mwanaume mwingine wa nje.
 
Kwanza nilidhani alikisia kwa vile nilivyokwenda kwa Rita, nikamwaambia atoke aende akamuulize Rita kama nilikuwa kwake ama nilikuwa kwa mwanaume.
 
Lakini Ibrahim alikuwa timamu, akaniambia. 
 
 “Achilia mbali habari ya Rita. Mimi sizungumzii juu ya kwenda kwako kwa Rita. Unaye mwanaume na jana ulikwenda kwake uliponiambia unakwenda kwa shangazi yako.”
 
Ingawa ukweli wake usingekuwa tishio kwangu kwa sababu tayari nia yangu ilikuwa kuachana naye lakini aliponiambia vile nilishituka na kidogo nilinywea. Hata hivyo nikajihazahaza kwa kutoa kicheko cha uongo nikijifanya namshangaa.
 
“Wewe sasa huo upofu wako utakutia kichaa, uliniona wapi na huyo mwanaume?” nikamuuliza ili nijue alijuaje kuwa nilikwenda kwa mwanaume.
 
“Ni kweli nimekuwa kipofu lakini sina kichaa, nipo timamu. Ninachokuambia nina hakika nacho. Wewe una mwanaume ambaye una mpango naye uondoke kwangu, lakini ninakwambia binaadamu haishi kuumbwa na utu ni bora kuliko kitu.
 
“Yaliyonikuta mimi, na wewe yanaweza kukukuta. Na ni utu wako pekee utakaokupa thamani ya ubinaadamu na siyo kitu. Nilitaka kukuambia hivyo tu.Maneno yangu yameisha”
 
“Lakini nataka uniambie nani amekuambia kuwa nina mwanaume na nina mipango ya kuondoka kwako.Au unahisi hisi tu?” nikamuuliza. Kusema kweli sauti yangu ilikuwa imenywea kidogo.
 
“Asubuhi ulikuwa unazungumza na nani kwenye simu pale uani?” Ibrahim akaniuliza.
 
Moyo ukanipasuka. Sasa nikagundua kuwa Ibrahim aliyasikia mazungumzo yetu na Chinga tulipokuwa tunazungumza kwenye simu wakati wa asubuhi.
 
Ukweli ni kwamba nilitahayari kwa sababu sikutaka Ibrahim ajue jambo hilo lakini kwa vile alikuwa ameshalijua sikuwa na jinsi.
Nikamjibu kwa kumropokea 
 
“ Kama kazi yako ni kusikiliza watu wanaoongea kwenye simu utasikiliza mengi sana”
 
Baada ya hapo sikumsema tena. Nikapanda kitandani upande wangu nikalala.
 
“Mimi nakuonya kama mume wako lakini kama unanidharau endelea na mwenendo wako” Ibrahim akaniambia.
 
Hapo ndipo aliponipandisha madudu yangu.
 
“Babu wee usiniletee kelele! Mimi nataka kulala, unanionya kitu gani nisichokijua?” nikamwambia kwa sauti ya dharau.
 
“Kuelezana kupo. Mimi ni mume wako hata kama umenidharau. Siwezi kuona una mahusiano na mwanaume wa nje nisikuambie” Ibrahim akaniamia kwa sauti tulivu.
 
“Huyo mwanaume umenifumania naye au ni umbea wako wa kusikiliza simu za watu? Kwani wewe unanipa pesa yako au ninajihudumia mwenyewe? Mume ni pesa siyo maneno matupu. Mimi sijioni kama nina mume, nisingehangaika mchana kutwa kwenda kuombaomba kwa watu. Wenye waume zao huwaoni nini?”
 
“Sawa bibi, kama leo umefikia kuniambia hivyo ili kunionesha kuwa umepata mwanaume mwenye pesa nakuombea heri. Ibrahim leo ni kipofu lakini narudia kukuambia kuwa binaadamu haishi kuumbwa na utu wa mtu si pesa”
 
Maneno yake yakazidi kunipandisha.
 
“Usiniapize mwana wa mwenzio. Binaadamu haishi kuumbwa maana yake nini?” nikamuuliza kwa ukali.
 
Ibrahim hakujibu kitu. Nikaendelea kumwaambia.
 
“Sasa kama mimi nimeshakuwa Malaya, nina wanaume je wewe unachukua uamuzi gani?”
 
“Uamuzi unao wewe mwenyewe” Ibrahim akaniambia kwa sauti iliyonyeea.
 
“Basi nipe talaka yangu niondoke. Huo ndiyo uamuzi wangu. Kwanza nimeshachoka na maisha ya kuhangaika!”
 
Ibrahim akanyamaza kwa vile nilikuwa nimemfikisha mahali asipopataka.
 
“Usijitie kunyamaza, umeyataka mwenyewe. Nipe talaka yangu!” nikaendelea kumwaambia.
 
Lakini Ibrahim aliendelea kubaki kimya, nikawa ninasema peke yangu. Mwishowe na mimi mikanyamaza.
 
Asubuhi kulipokucha nikajitia kufura. Sikusafisha nyumba wala sikuchemsha chai. Nilitoka bila kumuaga mtu nikaenda kwa Rita..Nilikunywa chai huko huko kisha nikaingia chumbani mwake nikalala mpaka saa sita. Nilipoamka nikarudi nyumbani.
 
ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment