Saturday, October 15, 2016

HADITHI, YAMENIKUTA SALMA MIE SEHEMU YA 20

HADITHI
 
YAMENIKUTA SALMA MIE 20
 
ILIPOISHIA
 
Ushauri wa Rita haukunifurahisha. Ulikuwa kinyume na mawazo yangu. Mawazo yangu yalikuwa ni kupanga jinsi ya kuachana na Ibrahim ili niolewe na Chinga. Hata hivyo sikutaka kumfichulia Rita undani wangu. Nikamwaambia 
 
“Naenda kumla tu. Si amejileta mwenyewe?”
 
“Huyo mumeo umemwambia unakwenda wapi?”
 
“Nimemwambia ninaenda Makorora kwa shangazi amaumwa”
 
Wakati tunazungumza na mimi nilijisogeza karibu na kioo cha kabati na kuweka sawa nywele zangu pamoja na kuukwatua uso wangu kwa kutumia vipodozi vya Rita.
 
Ilinichukua karibu nusu saa kujiweka sawa. Nilipohakikisha kuwa nilikuwa nimependeza nikavaa baibui langu kisha nikatoa simu yangu na kumpigia Chinga.
 
Simu ilipopokelewa nikamuuliza. 
 
“Uko wapi Chinga?”
 
“Nipo hotelini” Chinga akanijibu kwenye simu kabla ya kuniuliza. 
 
“Utakuja muda gani?”
 
“Ndio ninakuja”
 
“Unakuja sasa hivi?”
 
“Ndiyo ninatoka. Nitakwenda kukodi teksi”
 
“Sawa, basi ninakusubiri”
 
“Okey” nikakata simu na kumwambia Rita. 
 
“Natoka. Jamaa ananisubiri hotelini”
 
Rita akanisindikiza hadi mlango wa mbele, nikatoka. Nilitembea kwa miguu hadi kwenye kituo cha daladala ambako nilisubiri teksi itakayopita niisimamishe. Katika eneo hilo hakukuwa na kituo cha teksi cha karibu.
 
Nilipoona teksi haitokei na muda unazidi kwenda nikaamua kupanda bodaboda.
 
SASA ENDELEA
 
“Nipeleke Chuda” nikamwaambia kijana mwenye pikipiki.
 
“Chuda sehemu gani?” akaniuliza
 
“Karibu na hoteli ya Mtendele”
 
Sikutaka kumwambia anipeleke moja kwa moja katika hoteli hiyo kwani angenishuku vibaya.
 
“Kaa twende” akaniambia.
 
Nikajipakia nyuma yake. Pikipiki ikaondoka. Ingawa giza lilikuwa linaingia na isingekuwa rahisi kwa mtu anayenifahamu kunitambua, niliuziba uso wangu kwenye mgongo wa dereva wa bodaboda ili nisijulikane.
 
Mwendo wa nusu saa ukatufikisha Chuda.
 
“Simama hapa hapa” nikamwaambia kijana wa bodaboda tulipokuwa tunaikaribia hoteli ya Mtendele.
 
Kijana akasimamisha pikipiki. Nikashuka na kumlipa pesa zake kisha nikatembea kwa miguu kuelekea upande ilikokuwa hoteli ya Mtendele.
 
Nilipofika nilijipenyeza kwenye geti bila kusita. Kwenye ukumbi kulikuwa na wateja wachache wakipata vinywaji. Sikuwajali, nikaenda mapokezi na kumkuta msichana mwenzangu niliyemuulizia  Chinga.
 
“Aliacha agizo kwamba akitokea mgeni wake aende chumbani kwake. Yuko chumba namba 15, kipo ghorofa ya kwanza” msichana huyo akaniambia.
 
Nikapanda ngazi hadi ghorofa ya kwanza, nikakitafuta chumba namba 15 nikakiona.Nikaenda kubisha mlango. Nilibisha mara moja tu kasha nikasubiri. Baada ya sekunde chache mlango ulifunguliwa. Chinga akatoa kichwa ukumbini.
 
“Oh!  Salma karibu ndani” akaniambia aliponiona.
 
Alinipisha kwenye mlango, nikaoingia. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza  tangu niolewe na Ibrahim kuingia katika chumba cha hoteli na mwanaume.
 
Kusema kweli baada ya kuingia humo chumbani niligwaya nikajihisi kuwa ni mwenye hatia. Lakini nikajikaza ili nitimize lile nililokuwa ninalitaka. Niliamini kabisa kwamba wakati ule sikuwa mimi kama mimi, kulikuwa na nguvu ya shetani iliyokuwa ikinisukuma ndani ya moyo wangu.
 
Humo ndani kulikuwa na kitanda kipana cha sita kwa sita. Upande mwingine kulikuwa na kabati la kioo. Katikati ya chumba  kulikuwa na meza iliyokuwa na chupa nne za bia, moja ikiwa tupu. Kulikuwa na pakiti la sigara na kibiriti. Kando ya meza palikuwa na sofa moja.
 
Nikajua kuwa Chinga alikuwa ameketi kwenye sofa hilo akinywa bia. Nikataka kwenda kuketi kitandani lakini nilibadili mawazo nikaenda kuketi kwenye lile sofa. Chinga akafunga mlango. Alipoona nimeketi kwenye sofa yeye akakaa kitandani.
 
“Habari za nyumbani?” akaniuliza huku akitabasamu.
 
“Nzuri, za hapa?”
 
“Hapa kwema. Leo umependeza” akaniambia
 
Aliponiambia hivyo  niliona aibu kwa sababu nilijua alishuku kuwa nilijikwatua kwa ajili yake
 
“Kawaida tu” nikamwaambia kwa kuvunga kisha nikabadili mazungumzo haraka. 
 
“Ulikuwa unakunywa bia?” nikamuuliza
 
“Si unajua tena….” akanijibu bila kumaliza sentensi yake. Akanyoosha mkono na kuichukua bilauli iliyokuwa imejaa kilevi akaipiga funda kisha akairudisha juu ya meza
 
“Nikuagizie bilauli yako unywe kidogo kidogo?” akaniambia.
 
“Situmii na sina muda. Nimekuja mara moja tu tuzungumze ile habari yetu kisha nirudi”
 
“Tunahitaji muda wa kutosha Salma. Mbona unaonekana kuwa na haraka hivyo?”
 
“Si unajua bado niko mikononi kwa mtu. Kuondoka kwenyewe ni kwa kuiba”
 
“Kwani umemwaambia unakwenda wapi?”
 
“Kwa shangazi Makorora. Nilidanganya kuwa shangazi anaumwa ili nije huku”
 
“Hakushituka kuona unaondoka usiku?”
 
“Ni kwa sababu mchana nilikuwa na kazi ya kufua nguo”
 
“Sasa Salma tutafanya nini?. Unadhani suala lake litakuwa kikwazo tusiwe pamoja?”
 
“Litakuwa kikwazo. Wewe si unataka kunioa?”
 
“Na umesema hataweza kukupa talaka hata kama utaidai?”
 
“Hataweza kunipa”
 
“Je ukiifuatilia Bakwata?”
 
“Bakwata nikawaambie nini?”
 
“Kwamba huyo mwanaume hana uwezo wa kuishi na wewe, kwa hiyo unataka muachane”
 
“Bakwata hawatakubali, wataona ninamkataa kwa sababu amepofuka. Wataninasihi niendelee kuwa naye hivyo hivyo”
 
Chinga akapiga funda jingine la bia. Alipoirudisha birauli aliniambia. 
 
“Hatutakosa njia nyingine. Nakupa muda uendelee kufikiri lakini jaribu kumshinikiza akupe taraka”
 
“Wewe utakuwa hapa Tanga mpaka lini?”
 
“Sina muda mrefu. Naweza kuondoka siku yoyote nitakayoamua”
 
“Basi tuendelee kufikiria njia nyingine. Kwa vile sina nia ya kuendelea kuishi naye, kama hataniacha yeye nitamuacha mimi!”
 
“Lakini umenipenda?” Chinga akaniuliza ghafla. Macho yake yalionesha kuwa ulevi ulikuwa umeanza kumchukua. Iliwezekana alianza kunywa muda mrefu.
 
ITAENDELEA kesho hapahapa usikose uhondo huu nini kitatokea

No comments:

Post a Comment