Sunday, October 9, 2016

HADITHI, YAMENIKUTA SALMA MIE SEHEMU YA 16

HADITHI inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya Usafirishaji abiria FREYS COACH, Tanga hadi Singida kila siku saa 12 na 12;30. Gari mbili Luxury Coach na Ordinary. kwa mawasiliano 0622 292990
 
YAMENIKUTA SALMA MIE 16
 
ILIPOISHIA
 
Ibrahim akanyoosha mkono. Msangi akamuwekea kwenye kiganja.
 
“Ahsante ndugu yangu” Ibrahim akamshukuru na kumwambia.
 
“Usiache kunikumbuka. Ukikaa siku mbili tatu uwe unakuja kutujulia hali. Siku nyingine tunashinda bila kuijua riziki”
 
“Sawa kaka. Kuja kuwajulia hali ni lazima nije. Wewe ni kaka yangu, siku ambazo hunioni ni kwamba na mimi pia hali siyo nzuri”
 
“Ninajua. Nakushukuru sana ”
 
Baada ya hapo Msangi akatuaga na kuondoka.
 
Kwa vile nilishaziona zile pesa zilizotolewa na Msangi nikaenda kuketi na Ibrahim ili nimsomeshe ziingie mikononi mwangu.
 
“Mume wangu unajua kuwa nilimkopa jirani pesa tuliyotumia juzi. Sasa kama umepata nipe nimrudishie” nikamwaambia
 
“Mbona hukuniambia tangu hiyo juzi?” akaniuliza.
 
“Ningekuambia ungekuwa nazo hizo pesa za kumlipa?” nikamng’akia.
 
SASA ENDELEA
 
 “Nisingekuwa nazo lakini ulipaswa uniambie tu nijue kuwa tunadaiwa”
 
“Mume wangu nitakuambia madeni mangapi tunayo daiwa? Kila siku ninakwenda kukopa”
 
“Hizo pesa unazokwenda kukopa mbona sizioni?”
 
Hapo nikamjia juu
 
“Huzioni kwani hiki chakula tunachokula humu ndani unafiri nina hawara anayenihonga? Au wewe unanipa pesa yako?”
 
“Basi mke wangu, haina haja uje juu. Niambie hizo hela unazodaiwa ni shilingi ngapi nikupe”
 
“Nipe hizo hela zote ulizopewa, mimi mwenyewe ndiyo nitajua nadaiwa kiasi gani na kiasi gani nitabakisha kwa matumizi yetu”
 
Ibrahim hakutaka makubwa, alitoa zile pesa na kunipa.Nilijua wazi kuwa hakuridhika lakini hakuwa na la kufanya. Nikazichukua zile pesa na kuondoka.
 
Siku ya pili yake baada ya kunywa chai niliondoka hapo nyumbani bila kumwambia  Ibrahim ninakwenda wapi. Nilikwishaamua kutomuaga ninapokwenda mahali kwani sikuona umuhimu wa kufanya hivyo kwa mwanaume ambaye sasa amekuwa kama mzigo kwangu.
 
Saa nne nikawa kwenye kituo cha daladala nikimsubiri yule kijana niliyeahidiana naye. Na yeye alikuwa na ahadi ya kizungu. Alipitisha dakika moja tu kabla ya kuwasili katika kituo hicho cha daladala. Nikajipakia kwenye gari yake tukaondoka.
 
“Habari za nyumbani?” akaniuliza
 
“Nzuri. Sijui zako”
 
“Nashukuru kumekucha salama”
 
Baada ya hapo ukapita ukimwa wa muda kabla ya kijana huyo kuniuliza. 
 
“Hivi kama mume wako asipopona utafanyaje?”
 
Lilikuwa swali gumu ambalo sikuwahi kufikiria jibu lake.
 
“Sijui” nikamjibu.
 
Nilipomjibu hivyo akanyamaza. Lakini dukuduku likawa limenipata. Nilipomuona yupo kimya nikamuuliza 
 
“Kwanini umeniuliza hivyo? Umehisi kwamba hataweza kuona tena?”
 
“Nimekuuliza tu kujua mawazo yako lakini usikate tamaa. Endelea kumsilikiza mzee atakavyokuambia” akaniambia.
 
Tulipofika Kisosora tulikuta wateja kadhaa waliokuwa wakisubiri kuingia kwa mganga. Yule kijana akaniambia 
 
“Tuingie tu wewe umeshakuwa mwenyeji”
 
Tukaingia. Aliniingia kwenye chumba kingine akaniambia nikae kwenye kiti. Nikakaa,  yeye akatoka. Baada ya muda kidogo akarudi akiwa na baba yake.
 
“Shikamoo” nikamwamkia.
 
“Marahaba. Habari za kwako?” mganga huyo akaniuliza huku akikaa kwenye kitanda kwani hakukuwa na kiti kingine. Yule kijana alibaki akiwa amesimama.
 
“Mume wako anaendeleje?” mganga akaniuliza.
 
“Bado hali yake ni ile ile”
 
“Basi mngeendelea kuwaona madaktari”
 
“Tumehangaika sana kwa madaktari bila mafanikio. Inawezekana ameshapofuka”
 
“Kwani mboni zake za macho zimekuwa nyeupe kabisa?”
 
“Ni nyeusi lakini inawezekana ameshapofuka. Wako watu wenye mboni zao kama kawaida lakini ni kipofu”
 
“Kwani huyo mwanaume umezaa naye?”
 
“Hatujapata mtoto”
 
“Ni miaka mingapi sasa tangu muoane?”
 
“Inafika miaka mitatu lakini nimeharibu mimba mara mbili”
“Subiani wako ndiye asiyetaka watoto”
 
“Mimi nina subiani?”
 
“Ndiyo, ni jini dume. Nilishaliona tangu siku yako ya kwanza ulipokuja kwangu”
 
“Mimi sijui kama nina jini”
 
“Si unaota ndoto za kufanya mapenzi na wanaume?”
 
“Ndiyo, ninaota mara kwa mara”
 
“Basi ni hilo jini”
 
“Wakati mwingine ninaota nimezaa kitoto”
 
“Ndiyo hilo hilo . Usipojishughulikia unaweza usipate mtoto”
 
“Mume mwenyewe ndiyo yule, huyo mtoto hata nikimpata si atakuja kuteseka bure?”
 
“Kwani mwanaume ni yeye peke yake?’
 
“Kwanini?”
 
“Unaweza kupata mume mwingine mwenye pesa zake”
 
“Una maana yule niachane naye?”
 
“Sasa ni akili yako mwenyewe. Kama umeona kuna mwanaume mwenye uwezo wake kipesa anakuhitaji, unaweza kuamua tu lakini inategemea na akili yako mwenyewe. Kama unaona uendelee na mume huyo huyo, mwenye uamuzi ni wewe”
 
Nikashusha punzi ndefu.  
 
“Babu naona umeniweka njia panda” nikamwaambia yule mzee.
 
“ Hilo ni suala la kufikiri wewe mwenyewe, mimi ninakushauri tu kwa sababu yupo mtu anatafuta mke wa kuoa na ana pesa. Nimeona anaweza kukufaa”
 
“Yuko wapi huyo mtu?”
 
“Yupo. Nenda kafikilie kwanza. Ukiamua kuachana na huyo bwana njoo nitakuonyesha.Yeye yupo tayari kukuoa”
 
“Atakuwaje tayari kunioa wakati hajaniona?” nikamuuliza.
 
Mganga akacheka. 
 
“Ameshakuona na amekupenda lakini tatizo ni hilo kwamba una mume”
 
Hapo nikashangaa kidogo.
 
“Ameniona wapi?” nikamuuliza yule mganga.
 
Badala ya kunijibu alicheka kisha akanyanyuka ili atoke mle chumbani.
 
“Babu mbona huniambii, unatoka?”
 
Mzee alikuwa ameshafika kwenye mlango akageuka na kuniambia. 
 
 “Zungumza na mwenzako, yeye atakuambia”
 
Aliponiambia hivyo akatoka mle chumbani. Yule kijana akakaa pale alipotoka baba yake.
 
“Naona baba amekupenda, anataka uwe mkwe wake” kijana huyo akaniambia.
 
“Anataka niwe mkwe wake kwa nani?” nikamuuliza.
 
“Mimi nilikuja hapa Tanga kutafuta mke. Kwa kweli siku ile ya kwanza nilipokuona nilikupenda na nikamueleza baba. Akaniambia kuwa una mume wako. Lakini kama nyumbani kwako kuna matatizo twende zetu Dar”
 
Nikainamisha kichwa changu chini, nusu ilikuwa kwa aibu na nusu kufikilia yale maneno aliyoniambia. Nikawa namtazama kwa kumuiba. Nilimtazama kichwani mpaka miguuni. Kwa kweli alikuwa amevaa nguo za thamani na alionekana mtanashati na mwenye pesa lakini…...
 
“Mbona uko kimya?” akaniuliza alipoona nimenyamaza.
 
“Nafikilia hayo maneno uliyoniambia”
 
“Umeyaonaje?”
 
“Si wezi kukujibu kwa sasa, acha nikafikirie kwanza”
 
“Kitakachoendelea kuniweka hapa Tanga kwa sasa itakuwa ni jibu lako”
 
“Kwani wewe unafanyakazi gani?” nikamuuliza.
 
“Mimi ni mfanyabiashara”
 
“Una duka?”
 
“Sina duka isipokuwa huchukua oda kwa wenye maduka halafu ninakwenda nchi za nje kama vile Dubai au China kununua bidhaa na kuwaletea”
 
Aliponiambia hivyo niligutuka, nikajiambia kimoyomoyo.  “Kumbe huyu kijana ana pesa za maana”
 
 
ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment