hadithi
NILIJUA NIMEUA 8
ILIPOISHIA
“Nzuri Zacharia. Kumbe
unaishi Zanzibar?”
“Nilienda kwa muda, niko Dar”
“Kikazi uko wapi?”
“Baada ya kuchukua shahada
yangu ya sheria niliajiriwa na Wizara ya mambo ya nje”
“Nimefurahi kukuona, karibu
tena Tanga”
“Asante. Nahitaji teksi ya
kunipeleka mjini”
“Mimi pia ni dereva wa teksi.
Hapa nimefuata abiria”
“Kumbe unaendesha teksi!
Vizuri sana.
Basi twenzetu”
Nikatoka naye. Mara tu baada
ya kujipakia kwenye teksi mazungumzo yakaanza.
“Ajira zimekuwa ngumu sana. Nimeangukia kwenye
udereva” nilimwambia Zacharia wakati nikiiwasha teksi.
SASA ENDELEA
“Kwa sasa hivi sekta binafsi
ndio kimbilio la watu wengi. Hata mimi kuna uwezekano mkubwa nikaacha kazi na
kujiajiri mwenyewe”
“Wewe mwenzetu una shahada yako
ya sheria, unaweza kujiajiri mwenyewe. Taabu ni kwetu sisi tulioishia
sekondari”
“Hapana. Ajira ni ajira tu.
Hata kuendesha teksi ni ajira, ilimradi tu unapata riziki yako na maisha
yanakwenda. Kwani teksi ni ya kwako mwenyewe?”
“Hapana si yangu”
“Lakini masilahi yapo”
“Nashukuru, si sawa na kukosa
kabisa”
“Mimi nataka kuwa wakili wa
kujitegemea. Nitakuja kufanya kazi zangu hapa Tanga”
“Itakuwa vizuri sana. Huduma ya uwakili
inahitajika sana na katika mkoa wetu tuna mawakili wachache sana”
“Pengine mwakani nitakuwa
nimeshapata leseni”
“Nakuombea mafanikio.
Unakwenda wapi?”
“Mtendele Hotel”
“Pale Chuda?”
“Ndiyo Chuda. Nitakuwa pale
kwa wiki moja hivi”
“Zanzibar ulifuata nini?”
“Nilienda kikazi”
‘Tulifika Mtendele Hotel.
Wakati anashuka alinikaribisha. Na mimi nikashuka na kumfuata.
“Hatuwezi kuachana haraka.
Hatujakutana miaka mingi” aliniambia wakati tunapenya katika lango la hoteli
hiyo mpya.
Wakati anaandikisha chumba
aliniambia nikae kwenye kiti, akaniagizia bia.
Alipopatiwa chumba alirudi
tukaakaa sote. Na yeye akaagiza bia. Tulikunywa huku tunazungumza hadi nikakata
chupa nne. Baada ya kulipia bia tulizokunywa alinipa shilingi laki mbili.
“Chukua hizo rafiki yangu”
akaniambia. Nikamshukuru sana.
“Nipatie namba yako ya simu
ili kama nitahitaji teksi nikuite” akaniambia.
“Sawa”
Nikampa namba yangu na yeye
akanipa yake. Tukaagana na nikamuacha hapo hoteli.
Nilirudi nyumbani kwangu
kwenye saa mbili usiku. Kwa vile nilipewa laki mbili na Zacharia, sikutaka
kuendelea na kazi usiku. Niliona nirudi nyumbani nilale.
Lakini nilipofika nyumbani
mke wangu aligundua kuwa nilikuwa nimelewa.
“Unatoka wapi?” akaniuliza.
Nikamueleza kuwa ukweli.
“Na mimi nataka. Nenda
kanunue zingine tuje tunywe” akaniambia.
Sikubishana naye. Nikatoka na
kujipakia kwenye teksi yangu. Dakika chache tu baadaye nikarudi nikiwa na
makopo sita ya bia.
Kwanza tulikula chakula cha jioni. Baada ya kula tukaanza
kunywa. Tuliendelea kunywa hadi saa sita usiku.
Kabla hatujamaliza bia zetu
tulisikia kishindo kilichotokeaa uani. Baadaye tulisikia kama
kulikuwa na mtu anatembea.
“Hebu nenda uko uani,
isijekuwa mwizi ameingia” Halima akaniambia.
Nikanyanyuka. Nilikuwa
nimelewa sana
kwa vile sikuwa na uzoevu wa kunywa bia mara kwa mara.
“Chukua panga usiende mikono
mitupu”
“Panga liko wapi?”
Halima akanipatia panga hilo. Nikalishika na
kutoka nalo uani. Kwa vile taa ilikuwa inawaka nliweza kuona bila matatizo. Kwanza sikuona kitu. Nikawa natafuta tafuta kwenye
vipembe.
Ghafla taa ya uani ikazimika.
Nikashituka na kujiuliza nani amezima taa? Ikabidi nirudi ndani haraka
kwani kama kulikuwa na mtu mbaya amejificha sehemu angeweza
kunishambulia.
Kwa vile kulikuwa na giza sikuweza kuona mbele,
nikajigonga na pipa la maji lililokuwa mbele yangu. Kwa vile nilikuwa nimelewa
ilibaki kidogo tu nianguke chini. Wakati nasepetuka nikahisi kitu kikinivamia
nyuma yangu. Nikashituka na kudhani ni mwizi alikuwa anataka kunishambulia.
ITAENDELEA KESHO na usikose nini kitajiri katika sehemu ya 9 ya hadithi hii hapa hapa tangakumekuchabliog
No comments:
Post a Comment