Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kitaaluma zikiwemo za Umeme na Ufundi wa Komputer. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 7727246
Hatimaye ameingia Chadema. Ilianza kama uvumi lakini jana ilikuwa dhahiri baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutangaza rasmi kukihama chama tawala, CCM na kujiunga na Ukawa kupitia Chadema, huku akisisitiza; “Sasa basi, imetosha.”
Baada ya kukabidhiwa kadi ya Chadema na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe,
Lowassa alisema amejiunga na chama hicho kikuu cha upinzani ili
kutekeleza azma yake ya kuwakomboa Watanzania na kuendeleza safari ya
matumaini kupitia Ukawa.
“CCM kimepotoka, kimepoteza mwelekeo na sifa za kuendelea kuiongoza Tanzania,” alisema Lowassa katika mkutano wa kumkaribisha Chadema uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Ledger Bahari Beach na kurushwa moja kwa moja na vituo kadhaa vya televisheni na redio.
Dakika chache baada ya mkutano huo, CCM
kupitia mitandao yake ya kijamii ilitangaza kuitisha mkutano wa
wanahabari leo mchana kutoa taarifa muhimu, ikiaminika kuwa utakuwa wa
kumjibu kiongozi huyo.
Katika mkutano huo, Lowassa alitumia
dakika 13 kueleza sababu za kujiunga Chadema, mbele ya wenyeviti wenza
wa vyama vinavyounda Ukawa; Mbowe, Dk Emmanuel Makaidi (NLD), James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Prof. Ibrahim Lipumba (CUF).
Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, Naibu wake (Bara), John Mnyika, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu hawakuonekana na hawakupatikana kuzungumzia sababu za kutokuwapo katika tukio hilo muhimu.
Lowassa ambaye aliingia katika ukumbi huo saa 10.20 jioni akiwa ameambatana na mkewe, Regina,
watoto wake, ndugu na jamaa, pia aligusia sakata la kampuni ya kufua
umeme ya Richmond lililosababisha ajiuzulu wadhifa wa waziri mkuu mwaka
2008, kwamba alifanya hivyo kwa manufaa ya nchi na alishindwa kuvunja
mkataba huo kutokana na amri kutoka mamlaka ya juu.
Wakati Lowassa akizungumza, wanachama wa Chadema walikuwa wakiitikia ‘peoples power’, na alipomaliza hotuba yake wanachama wao waliimba wimbo maalumu kuwa wana imani naye, “Tuna imani na Lowaasaa, oya oya oyaa.”
Katika hotuba yake, Lowassa aligusia jinsi mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM ulivyogubikwa na mizengwe na kusisitiza: “Nimetumia
muda huu kutafakari kwa kina yaliyotokea Dodoma na hatima yangu katika
siasa nchini. Pamoja na yaliyotokea Dodoma azma yangu iko palepale ya
kuanza mchakamchaka wa maendeleo ya kuiondoa nchi katika umaskini.
“Najua
sote tumevunjika moyo kwa yaliyotokea Dodoma na mazingira yaliyopelekea
matokeo yale. Mchakato uligubikwa na mizengwe, ukiukwaji wa maadili,
uvunjaji wa katiba na taratibu za uchaguzi za CCM.”
“Sikutendewa
haki. Kwa mantiki hii nitakuwa mnafiki kama nitaendelea kujidanganya
mimi mwenyewe na umma wa Watanzania kwa kusema kuwa bado nina imani na
CCM…,
MWANANCHI
Siku moja baada ya tovuti ya Mwananchi kunukuu habari zilizoripotiwa
na Mtandao wa African Review, kuhusu mishahara ya marais wa Afrika na
kwingineko duniani, Ikulu imekanusha habari hizo ikisema si za kweli.
Bila kutaja mshahara wa rais ni kiasi gani, taarifa ya Ikulu
iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu juzi, ilisema
habari hizi siyo za kweli. Ni uongo na uzandiki. Ni uzushi mtupu na ni
uzushi wa hatari.
Taarifa ya Ikulu imeikariri ripoti hiyo ya Mtandao wa African Review
ikisema: “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete
anashikilia nafasi ya tano miongoni mwa viongozi 38 wa Afrika wanaolipwa
mshahara mnono zaidi.
“… Kuwa Rais Kikwete analipwa Dola za Marekani 192,000 kwa mwaka,
ikiwa ni malipo ya Dola za Marekani 16,000 kwa mwezi… Mshahara wa Rais
kwa mwezi ama kwa mwaka haufikii na hata wala kukaribia kabisa kiwango
kinachotajwa na Gazeti la Mwananchi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo
bila kutaja kiwango anacholipwa.
Taarifa hiyo iliendelea kusema: “Tangu Uhuru, mwaka 1961, Rais wa
Tanganyika na baadaye tangu mwaka 1964 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania amekuwa miongoni mwa viongozi wanaolipwa mishahara ya chini
kabisa duniani. Mshahara wa Rais wa Tanzania kwa mwezi ni wa chini kiasi
cha kwamba mshahara wake unazidiwa, tena kwa mbali na mishahara
wanayolipwa baadhi ya watendaji wakuu wa baadhi ya taasisi za umma
nchini.
“Ni jambo la kushangaza kwamba Gazeti la Mwananchi, linalochapishwa
hapa nchini, linaweza kupata kiasi cha uongo anacholipwa Rais wa
Tanzania katika mitandao ya nje badala ya kuuliza rasmi na kupewa majibu
sahihi kwa kujiingiza katika uzushi wa kupindua kiasi hiki.
“Gazeti la Mwananchi haliwezi kuwa na nia nyingine yoyote isipokuwa
nia ya kuwachochea wananchi na kuwajengea chuki dhidi ya Serikali yao na
kiongozi wao mkuu,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu.
Ilimaliza taarifa hiyo kwa kusema: “Ni matarajio yetu, kuwa Gazeti la
Mwananchi litafanya jitihada za makusudi, kama taaluma ya uandishi wa
habari inavyoelekeza, kutafuta usahihi wa jambo hili na kuwaambia
Watanzania ukweli.”
HABARILEO
Taasis ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Singida inamhoji Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba kuhusiana na tuhuma za kukiuka Sheria ya gharama za Uchaguzi na Sheria za Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini.
Hatua hiyo imekuja siku chache tu baada
ya wagombea ubunge watatu kati ya wanne wanaogombea jimbo la Iramba,
mkoani hapa kugomea mchakato wa kampeni kuelekea kura za maoni wakidai
baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Siasa walikuwa wakimbeba mgombea mwenzao,
Mwigulu Nchemba.
Wagombea waliogomea zoezi hilo ni Juma
Killimbah, David Jairo na Amon Gyunda ambao walisema waliamua kuchukua
hatua hiyo kutokana na msimamizi wa uchaguzi kura za maoni CCM katika
jimbo hilo, Mathias Shidagisha na msaidizi wake, Mwita Raphael, kubariki
wao kuchezewa rafu na Nchemba.
Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Singida Joshua Msuya
alisema kuwa Nchemba anahojiwa kutokana na madai ya kukiuka makatazo
mbalimbali yaliyoainishwa kwenye Sheria za Kuzuia na Kupambana na Rushwa
namba 11 ya mwaka 2007.
Alisema kuwa makatazo hayo yanajumuisha
vitendo vyote vinavyokiuka sheria hiyo kabla ya kampeni, wakati wa
kampeni na baada ya kampeni ambapo baada ya uchunguzi wa kutosha
kukamilika jalada husika hupelekwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kwa
uamuzi wa mwisho.
Kutokana na malalamiko mbalimbali
kuifikia ofisi ya TAKUKURU, Msuya ametoa tahadhari kwa wagombea wote wa
udiwani na ubunge mkoani hapa kutojihusisha na vitendo vyovyote
vinavyoashiria kushawishi wanachama kuwachagua vinginevyo wakigundulika
hatua kali dhidi yao zitachukuliwa.
Wakati kampeni zinaendelea kwenye
majimbo mbalimbali mkoani hapa, vitendo vya ukiukwaji wa Sheria ya
gharama za Uchaguzi vimekuwa vikiripotiwa kwa wingi kuliko wakati
mwingine wowote wa kipindi cha uchaguzi.
Aidha, inaripotiwa kuwa hali si shwari
katika jimbo la Mkalama kutokana na baadhi ya wagombea wenye uwezo
kifedha kudaiwa kumwaga fedha na zawadi mbalimbali kwa wanachama na
wananchi wa kawaida ili wagombea hao waweze kuwachagua siku ya kura za
maoni itakapofika.
MWANANCHI
Hayawi hayawi sasa yamekuwa. Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa
ameweka rekodi ya kuwa kada wa kwanza aliyewahi kushika nafasi ya
waziri mkuu kukihama chama tawala, CCM na kujiunga na upinzani.
Katika orodha ya mawaziri wakuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
tangu uhuru, Lowassa ni waziri mkuu wa tisa kushika madaraka hayo.
Alishika wadhifa huo kuanzia Desemba 30, 2005 hadi Februari 7, 2008.
Makada wengine wa CCM waliowahi kushika wadhifa wa waziri mkuu ni, Julius
Nyerere, Rashidi Kawawa, Edward Sokoine, Cleopa Msuya, Dk Salim Ahmed
Salim, Joseph Warioba, John Malecela, Frederick Sumaye na Mizengo Pinda.
Lowassa ni kati ya mawaziri watatu waliowahi kuwania urais mara mbili
na kushindwa. Wengine ni Malecela (1995 na 2005), Sumaye (2005 na
2015). Mbunge huyo wa Monduli aliyejitokeza 1995 na 2015 na ambaye
amekuwa akisononeka namna mchakato wa kupata mgombea ulivyoendeshwa,
ameamua kuhamia upinzani ili kuweka haki ndoto ya safari yake ya
matumaini.
Katika kipindi cha wiki tatu sasa, kumekuwapo minong’ono ndani na nje
ya CCM na kwenye mitandao ya kijamii, kwamba nchi itatikisika kutokana
na fununu za Lowassa kuhamia upinzani.
Kulikuwapo kila aina ya propaganda za kubeza hatua hiyo na nyingine
zikipongeza na kutahadharisha kuwa, kama angehamia upinzani, ungekuwa
mwisho wa CCM.
Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, mawaziri wakuu sita
wamewahi kuomba kuteuliwa na CCM kupeperusha bendera ya urais na
kushindwa, lakini hakuna aliyethubutu kuhama chama hicho tawala.
Mwaka huu, Lowassa alijitosa kwa mara ya pili kuwania urais,
akiungana na makada wengine 37 wa CCM waliorudisha fomu wakiwamo Sumaye
na Pinda.
Majina ya Lowassa na mawaziri wakuu wenzake hayakupenya hata Tano
Bora, yaliishia katika Kamati ya Maadili. Wajumbe watatu wa Kamati Kuu
walifichua kile walichodai ukiukwaji mkubwa wa kanuni kwani kamati
iliyopaswa kuchuja majina ni Kamati Kuu na siyo Kamati ya Maadili.
Dk Emanuel Nchimbi ambaye amekuwa mjumbe wa CC kwa miaka 17, Sophia
Simba na Adam Kimbisa, walitangaza rasmi kujiweka kando na maamuzi hayo
ya Kamati Kuu.
HABARILEO
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala,
imewataka wafanyabiashara waliojenga vibanda vyao katika eneo la
Jangwani, kuvibomoa vibanda hivyo mara moja kabla ya kesho kwa kuwa
wamekiuka utaratibu kwa kujenga eneo hatarishi.
Aidha Manispaa hiyo imesema endapo muda
waliotoa ukifika agizo hilo likiwa halijatekelezwa watapitisha
tingatinga eneo hilo kwa ajili ya kubomoa vibanda hivyo na kisha
kuwachukulia hatua wahusika kwa kufanya uvamizi.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi
alisema lengo lao lilikuwa ni kuwasaidia wafanyabiashara wanaopanga
bidhaa zao barabarani lakini sasa wapo watu waliovamia eneo hilo na
kujenga vibanda.
“Tunatangazia
wavamizi hao wabomoe mara moja na baada ya hapo kama agizo
halitatekelezwa tutabomoa na tutawashitaki kwa uvamizi… Naomba muelewe
kwamba Manispaa ya Ilala haijatoa eneo la kujengwa.”
“Ardhi
yote iliyopo Manispaa inasimamiwa na Manispaa lakini hakuna mtu
aliyejenga katika eneo la Jangwani aliyepewa kibali na Manispaa… Nia
ilikuwa kuwasaidia wafanyabiashara wanaotandika bidhaa zao chini ila kwa
sasa waliopo pale si wahusika bali ni wavamizi kwa kuwa wanaotandika
bidhaa hadi leo wapo mitaani.”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Isaya Mngurumi
alisema walishatamka kwamba eneo hilo haliruhusiwi kujengwa kibanda na
waligawa kwa wale wanaotembeza vitu mkononi ili wafanye kama gulio kwa
kupanga bidhaa zao chini.
“Lile
ni eneo hatarishi kwa ajili ya ujenzi wa kudumu, hivyo likitumika kama
gulio kwa kumwaga bidhaa chini, kipindi cha mvua watasitisha biashara
lakini waliojenga hawakufuata utaratibu na tunawataka wabomoe mara
moja,” alisema.
HABARILEO
Ikiwa zimebakia siku mbili kwa wakazi wa
jiji la Dar es Salaam kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la
Wapigakura kwa mfumo wa kieletroniki (BVR) kuisha, wengi wameiomba
Serikali kuongeza muda wa kujiandikisha ili watu wengi wasiachwe bila
kuandikishwa.
Imebainika pia kuwa idadi ya watu inazidi kuongezeka katika vituo vya BVR, tofauti na ilivyokuwa awali.
Katika vituo kadhaa katika manispaa za
Ilala, Temeke na Kinondoni, kulikuwa na idadi kubwa ya watu katika vituo
vya kujiandikisha, licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC) kuongeza mashine katika maeneo ambayo yana wakazi
wengi.
Kutokana na siku za kuandikisha kufika
ukingoni, wananchi wengi wameonekana kujitokeza na kuwa kwenye misururu
mirefu. Wengine wameweka kambi katika vituo ili kuhakikisha wanapata
fursa hiyo muhimu, huku wengi wakilalamikia kutoandikishwa licha ya
kufika vituoni kwa takribani kati ya siku mbili au tatu bila
kuandikishwa.
Katika Kituo cha Chuo cha Taifa cha
Usafirishaji (NIT) kilichopo eneo la Mabibo, kulikuwa na umati wa
wananchi wakiwa wameketi chini huku wengine wakionekana kukata tamaa,
hasa kutokana na wengine hata kutopewa namba au kuandikishwa majina yao.
Awali zilikuwepo mashine nne, lakini
sasa zimeongezwa na kufikia 12. Pamoja na Tume kuongeza mashine, bado
idadi ya watu wanaojitokeza imezidi kuongezeka. Katika kituo cha Shule
ya Msingi Msewe, idadi kubwa ya wananchi walionekana kupiga kambi bila
kukata tamaa.
Aidha, Ofisa kutoka Tume, Gudluck
Msomigulu anayesimamia vituo vilivyopo eneo la Shule ya Msingi ya
Mlimani, alisema pamoja na kuongezewa mashine na kufika nne, bado
wameelemewa na idadi ya watu wanaojitokeza kila siku.
Katika kituo kilichopo eneo la Utawala
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam( UDSM) ukumbi wa Nkurumah, kulikuwepo
msururu mkubwa wa watu waliokuwa wakisubiri kuandikishwa, ilhali kukiwa
na mashine moja.
HABARILEO
Waziri Mkuu wa Australia, Tony Abbot amempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuamua kukabidhi madaraka kwa kiongozi mwingine kwa mujibu wa Katiba nchini Tanzania.
Baada ya kuitumikia nchi kwa miaka 10
kuanzia mwaka 2005, Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kukabidhi madaraka
kwa Rais wa Awamu ya Tano mara baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25,
mwaka huu.
Kutokana na kuheshima Katiba na
kuendesha kwa ufanisi mchakato wa kumpata mrithi wake kuanzia ngazi ya
chama tawala, CCM, Abbot amesema; “Nakupongeza
sana kwa uamuzi wako wa kukabidhi madaraka kwa amani nchini kwako , ni
jambo la nadra sana Barani Afrika, kuwa na utaratibu mzuri na wa Amani
namna hii.’’
Aidha, Abbot alimtaka Rais Kikwete awe na uhakika kuwa “ Australia itaendelea kuisaidia Tanzania katika juhudi zake za kuleta maendeleo na kukuza uchumi.”
Rais Kikwete na Waziri Mkuu Abbot pia
wamezungumzia jinsi nchi zao zinaweza kuendelea kushirikiana katika
kulinda usalama baharini, kukuza zaidi ushirikiano wa kidiplomasia,
kiuchumi na kijamii.
Rais Kikwete yuko nchini Australia kwa mwaliko rasmi wa Kiserikali kutoka kwa Gavana Mkuu wa Australia, Peter Cosgrove.
Alipokelewa jana katika makao Makuu ya
kiongozi wa Australia kwa heshima zote kwa kupigiwa mizinga 21 na
kuandaliwa chakula rasmi cha mchana na baadaye kupanda mti kuashiria
kuimarisha mashirikiano baina ya nchi hizi mbili kwa kipindi kirefu
kijacho.
Tanzania na Australia zimedumu katika
ushirikiano baina ya nchi zao tangu miaka ya 1960 na sasa nchi mbili
hizi zimeazimia kuimarisha mahusiano haya zaidi katika sekta mbalimbali
zikiwemo za uwekezaji na biashara kati yao.
Baadaye jana, Rais Kikwete alitarajiwa
kukutana na wawekezaji wakubwa wa Australia ambao tayari wanawekeza
nchini Tanzania kwa ajili ya mazungumzo ya namna ya kuendeleza sekta
mpya ya gesi nchini na jinsi Tanzania inaweza kunufaika kutokana na
kupata gesi.
Tayari Serikali ya Australia na kampuni
binafsi za gesi na mafuta, zinaisaidia Tanzania hasa katika Vyuo vya
Ufundi Stadi (VETA) na tafiti mbalimbali katika Kilimo.
Leo, Kikwete anatarajiwa kutunukiwa digrii ya udaktari wa heshima ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Newcastle,
kwa mchango wake mkubwa alioutoa katika uongozi kwa kipindi cha miaka
10 aliyokaa madarakani nchini Tanzania na Dunia kwa ujumla. Mara baada
ya kupokea shahada yake, Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nyumbani
Tanzania.
NIPASHE
Kampeni za ubunge ndani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) jimbo la Mtera, Dodoma zimeingia dosari, baada ya kuzuka
vurugu za vijana wanaodaiwa kuwa wapambe wa Mbunge anayemaliza muda
wake, Livingstone Lusinde, kufanya fujo wakati wa kunadi wagombea.
Tukio hilo lilitokea juzi wakati
wagombea ubunge kupitia chama hicho wakiwa katika kampeni za kujinadi
kwa wapigakura wa kwenye kijiji cha Manzase, wilayani Chamwino.
Inadaiwa kuwa vijana hao wanaodaiwa kuwa
sio wakazi wa kijiji hicho walipelekwa kwa magari matatu aina ya Fuso
na kuanzisha vurugu baada Lusinde kumaliza kujinadi kwa wapigakura na
kuwataka vijana hao kuanza kuzomea mgombea atakayepanda jukwaani
kujinadi.
Baada ya kushuka mbunge huyo ndipo
vijana hao walipoanzisha vurugu zilizovuruga mkutano huo na baadhi ya
wagombea kukosa nafasi ya kujinadi.
Kutokana na vurugu hizo, wagombea tisa
waligoma kuendelea na kampeni hadi kiitishwe kikao kitakacho jumuisha
wagombea wote ili kujadiliana na viongozi wa chama na kutoka na
maazimio.
Kikao hicho kilifanyika jana asubuhi chini ya Katibu wa mkoa, Alberth Mgumba, na kuelekeza kusogeza muda wa kuanza kampeni hizo.
Wagombea wakitakiwa kuondoka saa mbili asubuhi, lakini walianza kuondoka kuelekea vijijini saa tano.
Katika kikao hicho wagombea wote tisa
kati ya kumi walimlalamikia Lusinde kwa Mbungu kwamba aliwatumia
kuwatumia vijana kufanya fujo ili kuharibu mikutano mara anapomaliza
kuwahutubia wananchi.
“Nani
asiye jua kuna vijana kama wale wa jana (juzi) sio wakazi wa eneo lile,
lakini walikuwapo kwenye mkutano ule na ndio walikuwa mstari wa mbele
kuharibu mkutano huo kwa kufanya fujo na kuzomea wagombea wengine,” alisema mmoja wa washindani wakubwa wa Lusinde.
Wagombea wote waliazimia kuwa katika
mikutano iliyobaki katika vijiji mbalimbali wakikutwa watu ambao si
wakazi wa eneo husika inabidi waondolewe na polisi kudhibiti uwezekano
wa kuvuruga mikutano ya kampeni.
Mgumba alisema kuwepo kwa changamoto
katika mikutano kampeni ni jambo la kawaida kwa kuwa kila mgombea ana
tabia zake, hivyo hawawezi kufanana na kwamba changamoto hizo
zitatatuliwa ndani chama.
NIPASHE
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeongeza saa za kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR) mkoani Dar es Salaam kutoka saa moja asubuhi badala ya saa mbili ya sasa hadi saa 12 jioni.
Tume imesema hatua hiyo imefuatia
malalamiko ya wakazi wa mkoa huo kuwa baadhi ya vituo vinachelewa
kufunguliwa na kufungwa mapema.
Kadhalika NEC imesema idadi ya
waliokwishaandikishwa kwenye daftari hilo hadi juzi jijini humo, imefika
1,172, 855 kwa Kinondoni watu 490,228, Temeke 389,558 na Ilala 302,
871.
Pia jumla ya mashine za BVR ambazo hadi
sasa zitatumika katika uandikishaji katika jiji hilo ambalo ni mkoa wa
mwisho katika kazi hiyo ni 3,717 kwa Ilala yenye vituo 395, ina BVR 927
sawa na asilimia 117, Kinondoni yenye vituo 702, BVR 1462 sawa na
asilimia 104 huku Temeke yenye vituo 572 ikiwa na BVR 1,328 sawa na
asilimia 116.
Hata hivyo, NEC imesema mashine hizo zinatarajiwa kuongezwa kadri ya uhitaji wake kwenye vituo vya kujiandikisha.
Baada ya kukutana na uongozi mzima wa Mkoa wa Dar es Salaam kujadili uandikishaji huo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, alisema vituo vya kujiandikisha vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa mbili hadi saa 12 jioni.
Alisema kwa sasa tume hiyo haiwezi kuzungumza iwapo imeongeza muda, lakini itahakikisha watu wote waneandikishwa mkoani humo.
Jaji Lubuva aliongeza kuwa maofisa
uandikishaji wote wasio na uzoefu wa kutosha kwenye vituo wataondolewa
na kutaka makundi maalumu wakiwamo wazee, wajawazito wapewe kipaumbele.
JAMBOLEO
Mapadri watatu na mtawa mmoja wa Kanisa
Katoliki Jimbo la Rulenge wilayani Ngara walifariki dunia jana papo hapo
huku watu 13 wakijeruhiwa katika ajali ya barabarani wakiwahi Karagwe
kwenye misa ya shukrani ya mwenzao aliyepata daraja hilo hivi karibuni.
Tukio lingine ni la juzi ambapo watu
saba walikufa na wengine 44 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi na
treni ya mizigo mkoani Tabora. Ajali hiyo ya juzi watu wanne walikufa
papo hapo huku wengine wakifia njiani wakipelekwa Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Tabora, Kitete.
Katika tukio la kwanza la Ngara, kwa
mujibu wa mmoja wa mapadri waliokuwa katika msafara huo, Erasto Nakule,
ajali hiyo ilitokea jana saa 2:00 asubuhi katika barabara iendayo nchi
jirani ya Uganda katika eneo la Bugorora wilayani Missenyi mkoani
Kagera.
Alisema gari aina ya Land Cruser lenye namba ya usajili T.650 BY1 la Jimbo Katoliki la Rulenge lililokuwa likiendeshwa na Padri Florian Tuombe
ambaye pia amefia katika Hospitali ya Mkoa Kagera liligongana uso kwa
uso na basi la Kampuni ya Sabuni lenye namna ya usajili T.166 AGU.
Alisema basi la Sabuni lilikuwa likitoka
wilayani Karagwe kwenda mkoani Mwanza, ambapo Land Cruser ilikuwa
ikitoka Biharamulo kwenda Karagwe.
Padri Nakule aliwataja mapadre waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni pamoja na Michael Mwelinde (70), Onesmo Buberwa (40) na Florian Tuombe aliyekuwa dereva na Mtawa Magreth Kadebe (60).
Hata hivyo, habari zaidi zinaeleza kuwa
mapadri hao walikuwa ni walimu wa Seminari ya Rutabo wilayani Muleba na
kwamba walikuwa wakienda kwenye misa ya shukrani ya Padre Evisius
Shumbusho inayofanyika nyumbani kwao Karagwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kagera, Augustine Ollomi
alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa taarifa za awali
zinaonesha kuwa chanzo chake ni dereva wa Land Cruser kuendesha bila
kuchukua tahadhari hivyo kugongana uso kwa uso na basi la Sabuni.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment