Friday, July 31, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO, JULY 31TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Euducation Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kitaaluma na kielimu. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746

HOOOT
MWANANCHI
Wabunge wawili waliohama CCM hivi karibuni, James Lembeli na Ester Bulaya wamepitishwa katika kura za maoni kuwania ubunge kupitia chama chao kipya.
Wakati Lembeli akipitishwa kwa kura za kishindo kuwania ubunge katika Jimbo la Kahama Mjini, Bulaya alishinda katika nafasi ya viti maalumu baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro cha Jimbo la Bunda Mjini.
Wanasiasa hao sasa wanasubiri uteuzi wa Kamati Kuu ya Chadema utakaofanyika Agosti 5 na 6.
Katika uchaguzi huo wa juzi, mbunge huyo wa zamani wa Kahama aliwabwaga wenzake 13 aliogombea nao akipata kura 168 kati ya 262 zilizopigwa, akifuatiwa na John Katibu aliyepata kura 45, Peter Shita (17) na Emmanuel Madoshi aliyepata kura 10.
Wengine ni Muta Nyerere (4), Felician Maige (4), Zacharia Obadia (3), Tadeo Mwati (2), Arnold Mtajwaka (2), Prosper Denga (2), Deusdedit Madinda (1), Reuben Macheyeki (1). Victor Mbwana na Richard Makingi waliambulia patupu. Katika uchaguzi wa viti maalumu, Winfrida Mwinula alishinda kwa kura 34 akifuatiwa na Salome Makamba aliyepata kura 30.
Kama isingekuwa ni kura za maoni za viti maalumu zilizomfuta machozi, Bulaya alikuwa tayari ametupwa nje baada ya kuanguka katika Jimbo la Bunda Mjini.
Bulaya aliyekuwa miongoni mwa makada saba wa chama hicho waliokuwa wanawania kuliwakilisha jimbo hilo, alipata kura 37 kati ya 182 zilizopigwa akiwa nyuma ya Pius Masururi aliyeibuka mshindi kwa kura 65 na  Magembe Makoye aliyepata kura 40.
Baadaye katika mkutano wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), uliofanyika baadaye usiku, Bulaya alipata kura 71 kati ya 110 zilizopigwa na kuwabwaga Godliver Masamaki aliyepata kura 31, Joyce Sokombi (4), Minza Shani (3), Dk Jane Nyamsenda (1) na Alice Wandya aliyeambulia patupu.
Awali, Bulaya alikwaa kisiki baada ya jina lake kuwa miongoni mwa waliokatwa na kamati ya utendaji inayosimamia majimbo hayo wakidaiwa ni wageni katika chama; wapenda fujo na matabaka, akiwa pamoja na Chacha Nyamhanga, Sulemani Daudi lakini walirudishwa kundini baada ya kikao cha viongozi na watiania.
Katika Jimbo la Bunda Vijijini, Sulemani Daudi aliibuka mshindi kwa kura 84 kati ya 127 zilizopigwana kuwashinda John Masenza aliyepata kura 14, Dk Lucas Webiro (11), Frank Mongateko (8), Edgar Chibura (5) na Mathias Bandio aliyepata kura mo
MWANANCHI
Tume ya Uchaguzi (NEC) leo imetangaza kuongeza siku nne zaidi za uandikishaji wa wapigakura kwa kutumia teknolojia ya BVR baada ya idadi kubwa ya wakazi wa Dar es Salaam kuitikia wito wa zoezi hilo.
Awali zoezi hilo lilikuwa likamilike kesho, Julai 31, lakini sasa litaendelea hadi Agosti 4, mwaka huu ili kukabiliana na idadi kubwa ya watu waliojitokeza kujiandikisha.
Kwa mujibu wa chombo hicho chenye mamlaka ya kusimamia shughuli zote za uchaguzi nchini, hadi jana, zaidi ya wakazi 1,000,000 walikuwa wamekwishaandikishwa jijini Dar es Salaam.
Ikizingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Nec inatarajia kuandikisha jumla ya wakazi zaidi ya 2.8 milioni wa jiji hilo lenye idadi kubwa ya watu nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, hadi sasa jumla ya zaidi ya watu 18 milioni wamekwishajiandikisha wakati tume ilitarajia kuandikisha watu kati ya 22 milioni na 23 milioni.
NIPASHE
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), inatarajia kuanza kuwasaka viongozi wa umma waliotumia nafasi zao vibaya ikiwamo kuiba na kujilimbikizia mali ndani na nje ya nchi.
Viongozi hao watasakwa na Takukuru kupitia kitengo maalum kilichoanzishwa mwaka jana ambacho kimeanza kupewa mafunzo nchini Uingereza.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward  Hoseah (pichani), aliyasema hayo jijini Dar es Salaam juzi alipokuwa akijibu baadhi ya maswali ya waandishi wa habari.
Dk. Hoseah aliyasema hayo muda mfupi baada ya kufungua mafunzo ya watumishi wa Takukuru ambao wapo katika kitengo hicho ili kuwajengea mbinu na uwezo wa kufanya uchunguzi dhidi ya viongozi walioiba na kujilimbikizia mali.
Alisema kitengo hicho cha Takukuru pia kitakuwa na kazi ya kupambana na masuala ya utakatishaji wa fedha haramu kwa kuwa tatizo hilo linazidi kukua hapa nchini.
Aliongeza kuwa kitengo hicho kilianzishwa rasmi mwaka jana, lakini hakikuanza kazi yake kutokana na kuchelewa kupatikana mtalaam wa kutoa mafunzo kwa watumishi hao.
”Tumejizatiti kukabiliana na viongozi wa umma waliojilimbikizia mali kwa kutumia watalaam wetu ambao wanapatiwa mafunzo,” alisema.
Dk. Hoseah alisema huu ni mwanzo na kwamba watahakikisha wanafanya kazi vizuri ili kuwabaini watu walioiba na kujilimbilikizia mali huku akisema kwamba sheria ni msemeno
Kuhusu wanasiasa wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, Dk. Hoseah alisema mtu yeyote asithubutu kufanya hivyo kwa kuwa Takukuru imesambaa kila wilaya na kwamba watakamatwa.
”Hawa wagombea wasifanye mchezo mchafu, ninawaonya kwa kuwa tutawakamata popote walipo,” alisisitiza.
Aliwaonya wanasiasa wanapita maeneo mbalimbali na kuanza kuchonga barabara na kutoa zawadi nyingine kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa na Takukuru itawashughulikia.
Aliongeza kuwa mtu yeyote atakayepindisha sheria kwamba Takukuru ipo macho muda wote na itawamulika wanasiasa ama wapambe wao ambao watataka kuwahonga wananchi kuwashawishi wawapigie kura.
Hata hivyo, kauli ya Dk. Hoseah imekuwa ya kawaida kutolewa kwa kuwa aliwahi kutangaza vita na wala rushwa wakubwa hapa nchini huku akiahidi kuwaburuza mahakamani, lakini mpaka leo hakufanya hivyo.
NIPASHE
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, amekanusha kumshushia kipigo Dk. Joseph Chilongani, ambaye ni mgombea mwenzake katika mchakato wa Chama Cha mapinduzi (CCM), kupata mgombea ubunge Jimbo la Kongwa.
Awali ilidaiwa kuwa Jumatatu jioni Ndugai, alitumia fimbo kumpiga Dk. Chilongani, ambaye alipoteza fahamu kabla ya kupelekwa hospitali ya wilaya hiyo, ambako aliendelea na matibabu mpaka jana aliporuhusiwa.
Mganga Mkuu wa Wilaya, Festo Mapunda, alilieleza NIPASHE jana kuwa walimruhusu kutokana na hali yake kiafya kuwa nzuri.
Naye Naibu Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, hakuwa tayari kueleza ikiwa mpaka jana alikuwa amepokea taarifa rasmi ya tukio hilo kutoka kwa walalamikaji badala yake alisema Dk. Chilongani, jana aliendelea na kufanya kampeni kama kawaida.
Madai dhidi ya Ndugai yalielezwa na Dk. Chilongani, kuwa sababu ya mtafaruku huo ilikuwa mzozo uliyoibuka kati ya Ndugai na mgombea mwingine, Simon Ngatunga, na baadaye Ndugai kumtuhumu Dk.
Chilongani kuwa alikuwa akitumia simu yake ya kiganjani, kumrekodi video ili kusambaza mitandaoni. Hata hivyo Ndugai alisema jana kuwa miongoni mwa wagombea tisa wanaowania nafasi hiyo, baadhi wamepandikizwa kwa lengo la kufanyia fujo.
“Tangu tuanze kampeni, wagombea mapandikizi wanafanya kazi ya kunitukana na kunidhalilisha kila tunakokwenda, mmoja ananiporomoshea matuzi ikitokea nikajibu, wanakuwa wameshapanga mmoja wao wa kunirekodi ili wazidi kunidhalilisha mitandaoni,” alieleza Ndugai
Alisema tukio la Jumatatu, wakiwa kwenye mkutano wa hadhara Ngatunga, alimtukana matusi ya nguoni na kusababisha mzozo kati yao, wakati watu wakiendelea kumsihi ampuuze yule kijana huyo akagundua Dk. Chilongani akitumia simu yake kumrekodi.
“Nilishamuonya mara kadhaa aache kujifanya mwandishi wa habari, kwa kuachukua video tena akinilenga mimi tu, lakini hakusikia nilichofanya niliigonga ile simu aliyokuwa akiitumia kuchukua video,” Ndugai alisema.
“Nikaigonga nikimwambia hebu usiendelee kunichukua video na kikamera chako hicho simu ikaanguka chini, nikashangaa kuona na yeye akijiangusha chini kama wachezaji wa mpira wa miguu,  ambao hujiangusha kwa lengo la kusingizia wamefanyiwa fujo ili wenzao wapewe kadi nyekundu.”
Kwa mujibu wa Ndugai, hakumpiga Dk. Chilongani wala hakujaribu kumpiga Ngatunga.
NIPASHE
Hofu imetanda ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wananchi kwa ujumla kutokana na kutoonekana kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, katika matukio mawili makubwa ya kisiasa yanayohusu mustakabali wa chama hicho.
Dk. Slaa hakuonekana siku ya kihistoria Jumanne wiki hii, iliyokuwa maalum kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kutangaza kujivua uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga Chadema.
Kadhalika, Dk. Slaa hakuonekana jana makao makuu ya chama wakati Lowassa alipofika kuchukua fomu ya kuwania urais kupitia chama hicho akitarajiwa kuwakilisha Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa), katika hafla iliyotikisa jiji la Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa juu wa Chadema.
Hata hivyo, Dk. Slaa alihudhuria kikao cha dharura cha kamati kuu ya Chadema Jumapili iliyopita ambacho kiliendelea hadi usiku wa manene na hoja kuu ikiwa ni kujadiliana na Lowassa na kumpokea katika chama hicho.
Dk. Slaa alionekana katika baadhi ya picha zilizovuja kutoka katika kikao hicho akiwa na viongozi waandamizi wa Chadema huku akijadili jambo na Lowassa, ambaye katika siku za hivi karibuni ambekuwa gumzo kubwa baada ya kubadili upepo wa siasa za Tanzania.
Tangu juzi kumekuwa na mijadala mirefu ndani ya mitandao ya kijamii, juu ya aliko Dk. Slaa, wengine wakibashiri kuwa ameamua kuacha siasa.
Hata hivyo, Dk. Slaa mwenyewe hajawa radhi ama kupokea simu yake au kujitokeza hadharani kujibu maswali ya umma juu ya kinachomsibu.
Mbali na kutokuonekana Chadema, Dk. Slaa pia hakuonekana kwenye mkutano wa Ukawa, uliofanyika Jumatatu wiki hii makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), ambao wenyeviti wenza wa umoja huo walimkaribisha Lowassa kujiunga nao.
Wakati wa Dk. Slaa akiadimika kwenye hadhara, viongozi waandamizi wa Chadema kwa nyakati tofauti wameithibitishia NIPASHE kuwa kila kitu “kimedhibitiwa” kuhusu tetesi kwamba kiongozi huyo amesusa.
“Sikiliza brother Dokta yuko freshi. Kila kitu kinakwenda kama tulivyopanga. Hakuna ukweli wa lolote juu ya madai eti Dokta anakwenda CCM,” kilisema chanzo chetu kilichoomba kutotajwa kwa sasa.
Wakati hali ikiwa hivyo, kuna taarifa kwamba Dk. Slaa anashinikizwa sana na watu wa ndani ya familia yake ambao wanadaiwa kusumbuliwa zaidi na ubinafsi, hasa baada ya mabadiliko ya kisiasa ambayo yamekikumba chama hicho kufuatia kujiunga kwa Lowassa.
Watu hao wa ndani wa familia ya Dk. Slaa wanadaiwa kuwa walikuwa wamejiandaa kuwa sehemu ya harakati za katibu mkuu huyo kuwania tena urais mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka 2010.
“Sisi tunawaza jinsi ya kuivunjavunja CCM, lakini wapo watu wanawaza jinsi ya kuwa sijui nini sijui nani?
Hapa tunatafuta njia ya kuing’oa CCM hata kama ni kwa kutumia nguvu ya shetani,” alisema kiongozi mmoja wa Chadema.
Lowassa aliamua kujiunga Chadema baada ya kuchoshwa na siasa zilizojaa chuki za kumzuia kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kusaka tiketi ya kuwania urais kupitia CCM.
Katika hatua nyingine, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, aliliambia NIPASHE kwamba, Dk. Slaa alishiriki vikao vyote muhimu vilivyoafiki, Lowassa kujiunga na chama hicho.
“Jana (juzi) usiku nilikuwa naye na wiki hii alishirika kikao cha kamati kuu ambacho mliona picha kwenye mitandao,” alisema.
Alipoulizwa alipo, Dk. Slaa, Lissu hakutoa majibu ya moja kwa moja zaidi ya kusema kwamba akiwapo mwenyekiti kwenye kikao chochote inatosha na siyo lazima, viongozi wote wa kitaifa wawepo.
Kuhusu Naibu Katibu wa Chadema, Tanzania Bara, John Mnyika na yeye kutoonekana katika mikutano hiyo, alijibu kwa kifupi kwamba anaumwa.
Licha ya kutafutwa mara kadhaa kupitia simu yake ya mkononi juzi na jana, Dk. Slaa hakupatikana badala yake mtu mmoja mwanamke alipokea na kusema mpigaji amekosea namba.
Alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno ili aeleze kilichomsibu kushindwa kuhudhuria matukio muhimu ya kumkaribisha Lowassa pia hakujibu.
NIPASHE
Mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli (pichani),  ameiomba serikali kuendelea kujenga barabara ya lami awamu ya pili hadi makao makuu ya Wilaya ya Simanjiro toka KIA, huku akiwataka Watanzania kukataa watu wanaowatenganisha kwa misingi ya ukabili, dini na vyama vya siasa.
Alitoa wito huo jana wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami ya kilomita 26 toka KIA hadi Mererani, Manyara iliyohudhuriwa na  Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Bilal.
Alisema ni vizuri Watanzania wakaendeleza na kuwaogopa baadhi ya watu wanaotaka kuwatenganisha kwa misingi ya vyama, ukabila na udini, kwani hakuna tija kwa Taifa.
“Haya maendeleo hayachagui ukabila, dini wala vyama vya siasa, ndio sababu serikali inajenga barabara kila mahali bila kujali chama gani kipo mahali hapo, hiyo ndiyo misingi tulionayo,” alisema.
Alimuomba Makamu wa Rais kuendeleza barabara hiyo hadi makao makuu ya Simanjiro, katika awamu ya pili baada ya kumalizika awamu ya kwanza.
Dk. Magufuli alisema ujenzi  wa barabara ya KIA hadi Mererani amekabidhiwa mkandarasi China Hennan International Cooperation Group Co. Ltd , ambaye alimtaka kuikamilisha kwa wakati.
Alisema ujenzi wa barabara hiyo utagharimu Sh. bilioni 32.2 na kumtaka mkandarasi huyo kuajiri vijana wa eneo hilo ili nao wanufaike na matunda ya miradi ya eneo lao.
Alisema hadi sasa serikali inaendelea na ujenzi wa barabara za lami kilomita. zaidi ya 17,000 kati ya hizo 5,500 zimekamilika kwa kiwango cha lami, jambo ambalo ni la kupongezwa na kila mpenda maendeleo.
Alisema barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kutokana na kuwapo kwa machimbo ya madini ya Tanzanite ambayo yanaingizia mapato makubwa serikalini.
Dk. Bilal alimsifia Dk. Magufuli kuwa ni jembe na anastahili kupeperusha bendera ya urais ya CCM, kutokana na kazi alizofanya bila kutetereka.
Aliwaomba wananchi kuacha kuhujumu mradi huo kwa kuiba vifaa, badala yake wavilinde ili kumpa moyo mkandarasi.
“Lakini nimepokea ombi la Dk. Magufuli la kutaka barabara iendelee awamu ya pili hadi makao makuu ya wilaya na itakuwa hivyo, pia tutafikiria kuyaleta maji eneo hili haraka iwezekanavyo,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick  Mfugale, alisema barabara hiyo itakuwa na vituo vya mabasi vitano na madaraja matano na inakadiriwa kudumu kwa miaka 20.’
MTANZANIA
Idara ya uhamiaji nchini imesema inawashikilia wahamiaji haramu 2,048 kutoka nchi mbalimbali kwa tuhuma za kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Naibu kamishna wa uhamiaji na msemaji mkuu wa idara hiyo, Abbas Mussa alisema jana kuwa wahamiaji hao wanatoka nchi za Kenya, Burundi na Uganda.
Alisema walikamatwa katika mikoa 14 wakijifanya ni Watanzania, lakini ilibainika kuwa siyo raia baada ya idara hiyo kufanya uchunguzi kwenye vituo vya uandikishaji.
“Baadhi yao tumewafikisha mahakamani, lakini wengine bado uchunguzi unaendelea na wakibainika nao watachukuliwa hatua,” alisema Mussa.
Aliongeza kuwa wengi ya wahamiaji hao walifika mikoa ya Kagera, Mara, Tanga, Kigoma, Rukwa, Kilimanjaro, Ruvuma, Geita, Shinyanga, Mtwara, Pwani, Mbeya, Morogoro na Dar es Salaam.
“Inasikitisha sana, kwani baadhi ya waliokamatwa walishajiandikisha na kupewa vitambulisho kama raia wa Tanzania,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, Idara imeamua kuongeza maofisa katika vituo ili kuendelea kuwabaini wahamiaji hao.
Mussa aliwataka wananchi kutoa taarifa mara wanapobaini watu ambao siyo raia wanajiandikisha.
Aliongeza kuwa maombi ya hati za kusafiria yameongezeka maradufu kutoka hati 4,938 Julai 2014 hadi 8,703 Julai 2015 kwa upande wa Bara na kutoka hati 588 Julai 2014 hadi hati 1,028 Juni 2015 kwa upande wa Zanzibar.
Alisema idara inawataarifu wananchi kuwa siyo lazima kubadilisha hati inapokwisha muda wake, badala yake mmiliki anaweza kubadili na kupatiwa nyingine wakati wowote atakapokuwa akisafiri.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment