Tuesday, July 21, 2015

SOMA HABARI KUBZWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO, JULY 21 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kitaaluma zikiwemo za Umeme, ufundi na Computer na Kiingereza. Kituo kipo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746

todayNIPASHE
Uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR), jijini Dar es Salaam, unaanza kesho huku takriban mashine 8,000 zikitarajiwa kutumika kwa kazi hiyo.
Pia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, ametoa onyo kali kwa maofisa waandikishaji watakaochelewa kufika na kuondoka kabla ya muda katika vituo vya uandikishaji.
Sadiki  alisema uandikishwaji jijini humu utaanza kesho na kuhitimishwa Julai 31, mwaka huu.
Alisema takribani wakazi milioni mbili wanatarajiwa kuandikishwa katika BVR na kwa wakazi wenye sifa takribani milioni mbili wa Jiji la Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Sadiki, vituo 1,684 vitatumika katika uandikishaji kwa Manispaa za Ilala (396), Temeke (572) na Kinondoni (706).
Alisema Manispaa ya Kinondoni itakuwa na maofisa uandikishaji 1,412 na wa akiba 136, waandishi wasaidizi 706 na wa akiba 136.
Aidha, alisema Manispaa ya Temeke nayo itakuwa na maofisa uandikishaji 1,144, wa akiba 128, waandishi wasaidizi 572 na wa akiba 128.
Alisema Ilala itakuwa na maofisa uandikishaji 792 na wa akiba 144, waandishi wasaidizi 136 na wa akiba 144.
Katika manispaa hizo pia kutakuwapo na ofisa mwandikishaji wa halmashauri, ofisa uchaguzi, maofisa wasaidizi wa majimbo na kata na wataalam wa Tehama.
Sadiki alitoa wito kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi na mapema kujiandikisha kwani kinyume chake watapoteza haki yao ya kupiga kura.
Alisisitiza kuwa wasio raia wa Tanzania hawaruhusiwi katika uandikishwaji huo na atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.
Aliwataka maofisa uandikishaji kufika vituoni kwa wakati na kuondoka kwa muda uliowekwa na  Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ili kuwaondolea usumbufu wananchi.
Sadik alisema maandalizi yakiwamo mafunzo kwa wahudumu, yalishafanyika kwa manispaa zote.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema vituo vutafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni kila siku.
NIPASHE
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, jana alikana kutoa lugha ya matusi dhidi ya  Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kwamba mtoto, hana akili na mpuuzi.
Askofu Gwajima alikanusha tuhuma hizo wakati akisomewa maelezo ya awali mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilfred Dyansobera anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Joseph Maugo, alidai kuwa kati ya Machi 16 na 25, mwaka huu katika viwanja vya Tanganyika Packers, vilivyopo Kawe jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alitoa lugha ya matusi kwamba ‘mimi Askofu Gwajima nasema askofu Pengo ni mpuuzi mmoja yule, mjinga mmoja, amekula nini yule, sijui amekula nini yule mtoto hana akili yule’ alinukuu maneno hayo.
Alidai kuwa Askofu Gwajima alitoa maneno hayo yakufadhaisha dhidi ya Askofu Pengo na kwamba yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Upande huo wa Jamhuri ulidai kuwa Machi 27, mwaka huu mshtakiwa alifikishwa Kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa.
Ilidaiwa kuwa alifunguliwa mashitaka na kufikishwa mahakamani dhidi ya tuhuma hizo.
Hata hivyo, Askofu Gwajima alikana mashitaka hayo lakini alikiri majina yake, wadhifa wake, kuhojiwa Kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kweli kanisa lake liko Kawe na kushitakiwa mahakamani hapo.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa unatarajia kuita mashahidi saba na watawasilisha vielelezo vitano.
Wakati huo huo, mahakama hiyo imepiga kalenda kusoma maelezo ya awali ya kesi inayomkabili askofu huyo na wenzake watatu, baada ya mshtakiwa wa nne kuwa mgonjwa.
Kesi hiyo itasikilizwa mbele ya Hakimu Dyansobela Agosti 10, mwaka huu.
NIPASHE
Baadhi ya barabara zilizokuwa zinajengwa jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupunguza msongamano, ujenzi wake umekwama baada ya wakandarasi kuzitelekeza na kuondoa vifaa vyao.
Barabara hizo zilianza kujengwa mwanzoni mwa mwaka jana katika maeneo mbalimbali.
Waziri wa ujenzi, Dk. John Magufuli mwanzoni mwa mwaka huu alizitembelea barabara hizo na kuweka mawe ya msingi, lakini kwa sasa hakuna shughuli yoyote inayoendelea eneo la ujenzi.
Uchunguzi uliofanywa katika barabara ya Tangibovu hadi Goba katika Wilaya ya Kinondoni umbali wa kilomita tisa umebaini kwa sasa hakuna magari wala tingatinga eneo la ujenzi.
Aidha, kuanzia Goba hadi Mbezi Luis ujenzi umesimama kwa muda huku wananchi wakishindwa kujua sababu ya kazi hiyo kukwama.
Baadhi ya wananchi katika maeneo hayo wameshangazwa kuona magari na vifaa vingine vilivyokuwa vikitumika katika ujenzi huo kuondolewa wakati kipindi ambacho ujenzi ungefanyika vizuri kuliko kipindi cha mvua.
Barabara nyingine ambayo ujenzi umesimama ni ya Ubungo External kupitia Maji chumvi hadi Bonyokwa.
Pia inayotokea Tabata dampo hadi Kigogo na Wazo kupitia Tegeta A hadi Goba ambazo ujenzi wake ulipangwa kukamilika ndani ya miezi 12.
Mkataba wa ujenzi huo ulisainiwa Machi mwaka jana na wakandarasi waliambiwa wahakikishe wanakamilisha kazi hiyo katika kipindi walichokubaliana na serikali.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Patrick Mfugale, akizungumza siku ya kusaini maktaba huo na Wakandarasi aliahidi kwamba kazi hiyo itakamilika kama mkataba unavyosema.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi kanda Maalum ya Dar es salaam inawashikilia watu wawili akiwemo mtoto wa miaka 15 kwa kujihusisha na matukio mbalimbali ya ujambazi likiwemo tukio la uvamizi na mauaji kituo cha Polisi Stakishari.
Mbali na hilo jeshi hilo limefanikiwa kukamata bunduki 16 kati ya hizo 14 ziliibiwa katika tukio la stakishari, ambazo zilikuwa chini ya handaki Wilaya ya Mkuranga pamoja na milioni 170.
Suleiman Kova alisema watuhumiwa hao pamoja vitu hivyo vilikamatwa kutokana na msako wa unaoendelea wa kupambana na makosa mbalimbali ya uhalifu kwa kutumia silaha za moto.
“Julai 17 zilipatikana taarifa za eneo la Taungoma kulikua na majambazi waliohusika kwenye tukio la stakishari, wakijiandaa kufanya tikio la uhalifu, kikosi kilikwenda haraka eneo la tukio na kuweka mtego na kufanikiwa kuwanasa washukiwa watano…walainza kupambana  baada ya kukataa kusimama na majambazi watatu walifariki dunia”Kova.
Alisema silaha 14 zilizopatikana  ziliporwa katika kituo cha stakishari bado hazijakamilisha idadi ya zilizopotea na jeshi hilo bado linaendelea na msako.
Kova alisema ndani ya shimo pia wlaikuta silaha ya kichina aina ya Norinko ambayo haitumiwi na majeshi ya Tanzania, risasi 25 pamoja na fedha taslimu milioni 170 ambazo zilifungwa katika sanduku maalum la kabati.
MWANANCHI
Baadhi ya wabunge wa Chadema wamezungumzia taarifa zinazosambaa zikieleza kuwapo mkakati wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhamia katika chama hicho, wengi wao wakimkaribisha.
Wakati wabunge hao wakikubali kumpokea, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa amesema wananchi wasubiri mambo yatakapokuwa tayari badala ya kutegemea mitandao ya kijamii.
Nitazungumza pale mambo yatakapokuwa sawa, siwezi kuzungumza sasa, subirini… sasa hivi mambo mengi yanazungumzwa kwenye mitandao,” alisema Dk Slaa ambaye pia anatajwa kuwa mgombea wa chama hicho ndani ya Ukawa.
Msemaji wa Lowassa, Aboubakary Liongo alipoulizwa kuhusu kuwapo kwa mpango huo alisema hawezi kulizungumzia hilo kwa kuwa ni suala la mtu binafsi. Hata hivyo, jitihada za kumpata Lowassa jana hazikufanikiwa kwani simu yake iliita pasi na kupokewa.
Hivi karibuni, idadi kubwa ya madiwani wa CCM walirudisha kadi zao na kujiunga na Chadema wakisema sababu ni kutoridhishwa na kukatwa kwa jina Lowassa kati ya wagombea urais wa CCM.
Kadhalika, mtandao wa kijamii uliokuwa ukimuunga mkono mbunge huyo wa Monduli unajulikana kwa jina la 4U Movement ulitangaza kuhamia Chadema hali inayoashiria kuwa kuna dalili ya Lowassa pia kujiunga nao.
Wakiandika katika akaunti ya Twitter ya 4U Movement, wafuasi hao walisema: “Ukimya ni hekima na ukimya ni busara. Ukimya wa Edward Lowassa ni kutafakari Safari ya Matumaini… Tuungane kuyapata mabadiliko nje CCM.”
MWANANCHI
Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya nchi, Lawrence Masha amemkwepa hasimu wake kisiasa, Ezekia Wenje katika Jimbo la Nyamagana, Mwanza na kwenda kugombea ubunge Sengerema ambako atavaana na mbunge anayemaliza muda wake, William Ngeleja.
Aidha, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Said Arfi ambaye hivi karibuni alitangaza kujivua uanachama wa chama hicho, amejiunga na CCM na amechukua fomu za kuwania ubunge katika Jimbo la Nsimbo, Katavi.
Katika uchaguzi uliopita mwaka 2010, Masha aligombea kipindi cha pili katika Jimbo la Nyamagana (CCM), katika mpambano uliokuwa na ushindani mkali na kuangushwa na Wenje wa Chadema.
Awali, kabla ya uchaguzi huo, Masha akiwa waziri mwenye dhamana na mambo ya ndani, alimwekea pingamizi Wenje akidai hakuwa raia, lakini hoja hiyo haikumzuia mshindani wake, badala yake ilimwongezea kura za huruma hadi akaibuka mshindi.
Safari hii Masha amepima maji na kuamua kumvaa waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Ngeleja ambaye hivi karibuni alikuwa miongoni mwa wanaCCM 38 walioomba kuwania urais, lakini akaondolewa katika hatua za awali.
Alipoulizwa jana, Masha alisema amechukua fomu Sengerema kwa sababu ni nyumbani kwao, ndipo alikozaliwa na kukulia, hivyo ameamua kushirikiana nao kusukuma gurudumu la maendeleo.
Nyamagana pia ni nyumbani, hivyo tutaendelea kushirikiana ili kuleta maendeleo kwa kila jimbo. Sijafanya maridhiano yoyote ya kuachiana jimbo, lakini natumia haki yangu ya kugombea popote,” alisema.
Hata hivyo, hata katika jimbo la Sengerema alikoomba kugombea hayuko salama kutokana na nguvu ya upinzani iliyopo kupitia Chadema ambacho nguvu yake ilidhihirika katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Desemba mwaka jana pale ilipochukua viti vyote katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Sengerema na maeneo mengine ya vijijini.
Mbali na Masha na Ngeleja, wengine waliojitokeza katika jimbo hilo kupitia CCM ni Anna Shija, George Rweyemamu, Philemon Tano, Dk Omari Sukari, Dk Angelina Samike, Jumanne Mabawa, Mussa Malima, Baraka Malebele, Joshua Shimiyu na Zablon Bugingo.
HABARILEO
Mbunge wa jimbo la Mpanda Mjini kwa miongo miwili, Said Amour Alfi (CHADEMA) amejiunga rasmi na CCM. Amekuwa miongoni mwa makada 23 wa chama hicho, waliochukua na kurejesha fomu za kuomba kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Arfi amechukua fomu kuwania ubunge katika jimbo jipya la Nsimbo, wilayani Mlele. Mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, chini ya uongozi wa Freeman Mbowe, alitangaza kujivua uanachama wake Chadema hivi karibuni katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Msingi Kashaulili mjini Mpanda, huku akisisitiza kuwa alikotoka alichoshwa na siasa za kinafiki.
Katibu wa CCM wa Mkoa wa Katavi, Averin Mushi amethibitisha kuwa Arfi alichukua na kurejesha fomu za maombi ya kugombea ubunge katika jimbo jipya la uchaguzi la Nsimbo kwa tiketi ya CCM .
Hivi karibuni , Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza majimbo mapya ya uchaguzi, ambapo Jimbo la Katavi limegawanywa na kuanzishwa kwa majimbo mawili ya Uchaguzi ya Nsimbo na Kavuu.
Akitangaza idadi ya makada wa CCM waliorejesha fomu za kuomba kugombea ubunge katika majimbo manne ya uchaguzi mkoani humo, Mushi alieleza kuwa hadi pazia lilipokuwa likifungwa Jumapili, makada 23 wa chama hicho, akiwemo Arfi, walikuwa wamerejesha fomu zao .
Alisema kuwa katika Jimbo la Nsimbo makada waliorejesha fomu ni pamoja na Arfi, Shaaban Hassanali “Dallah”, Richard Mbogo, Manamba Emmanuel na Mapesa Frank.
Alitaja makada waliorejesha fomu jimbo la Katavi kuwa ni Isaack Kamwele, Meneja wa Tanroads mkoa wa Katavi na Shafi Mpenda ambaye ni Mhasibu wa kampuni ya magazeti ya Serikali (TSN).
Wengine ni Maganga Kampala na Oscar Albano. Alisema katika jimbo jipya la Kavuu, waliorejesha fomu ni Zumba Emmanuel Mselem, Abdallah Saida ambaye ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Katavi na Prudencia Kikwembe, Mbunge Viti Maalumu.
Arfi aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa, kabla ya kujiuzulu wadhifa huo na baadaye kujivua uanachama hivi karibuni aliwahi kutuhumiwa na Chadema kumsaidia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kupita bila kupingwa katika Jimbo la Katavi (CCM) kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010 kwa kuwashawishi baadhi ya wagombea kuondoa majina yao.
Hata hivyo, Arfi amekuwa akikanusha tuhuma hizo na kusababisha kutokuelewana na baadhi ya viongozi wenzake ambapo alifikia uamuzi wa kujiuzulu nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa Novemba 22, mwaka 2013 kwa kile alichosema amechoshwa na siasa za kinafiki ndani ya chama hicho.
Aidha, katika waraka wake wa kujiuzulu Umakamu Mwenyekiti, alisema hakuwa tayari kubanwa na hata kuchaguliwa aina ya marafiki. Sehemu ya waraka huo inasomeka.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment