Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha elimu cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kielimu na kitaaluma. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
NIPASHE
Madudu ya zoezi la uandikishaji wapiga
kura kwa kutumia mfumo wa kielektroniki (BVR), yameendelea kuwakumba
wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na kulazimisha baadhi ya wanaume
kujitanda khanga, wengine kubeba watoto wasio wa kwao, kutumia vyeti vya
ugonjwa na kutoa rushwa ili waweze kuandikishwa haraka.
Mbinu hizo zimetokana na Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC) kuruhusu wanawake wajawazito, wenye watoto, wazee na
wagonjwa kupewa kipaumbele kwenye zoezi hilo.
Katika tukio lililoripotiwa jana la mashine ya BVR kukutwa kwenye nyumba ya mtu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, ameagiza akamatwe mara moja na kuchukuliwa hatua.
Mashine hiyo ilidaiwa kufichwa nyumbani
kwa mtu mmoja aliyetajwa kwa jina moja la Baba Furaha kwa mkakati wa
kuandikisha watu nyakati za usiku.
Sadiki alisema kuwa mtu huyo aliyekutwa
na mashine hiyo nyumbani kwake ni kinyume cha utaratibu uliowekwa na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na kuagiza akamatwe.
Alisema mtu huyo anatakiwa kuchukuliwa hatua mara moja ili iwe fundisho kwa wengine.
“Sijapata
taarifa rasmi, lakini kama tukio hili lipo na mtu huyu akakutwa na
mashine nyumbani kwake, kwanza anatuvurugia utaratibu uliowekwa na
anatakiwa kukamatwa mara moja,” alisema.
Kuhusu taarifa za baadhi ya maeneo
watendaji wa mitaa kudaiwa kuorodhesha majina ya wana-CCM usiku
kinyemela mtaani kisha kuyapeleka vituoni ili wapewe kipaumbele kwenye
uandikishaji, Sadiki alisema nao wachukuliwe hatua.
Sadiki alisema inawezekana matukio hayo
yapo na kuwataka wananchi na viongozi ngazi za chini, wanapowabaini
wahusika wafikishwe polisi.
“Hatuwezi
kuvumilia watu wanaovuruga utaratibu kwa sababu haya sio maelekezo ya
Nec, kuandikisha ni asubuhi hadi saa 12:00 jioni zaidi ya hapo ni
kuvunja sheria,” alisema.
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Julius Mallaba, alipoulizwa kama Tume ina taarifa ya matukio hayo alisema bado hayajafika Nec.
Baadhi ya wanaume walilazimika kutumia
mbinu ya kujitanda khanga ili waonekane wanawake wakati vituo vingine
wapo waliojitengenezea cheti ili waonekane wagonjwa.
Wananchi hao walikuwapo vituoni
wakilalamikia kufika kituoni hapo siku tatu bila ya kupata vitambulisho
huku wengine wakipata bila ya kukaa foleni. Kitendo hicho kilichowafanya
baadhi yao kutumia njia mbadala ikiwamo kutoa rushwa ili wapitishwe
haraka kujiandikisha.
NIPASHE
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amepita bila kupingwa katika mchakato wa kura ya maoni ya ubunge wa jimbo la Hai, mkoani Kilimanjaro, baada ya kuvuna kura 269.
Licha ya kupita kwa kishindo, wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi huo, walimpigia Mbowe kura tano za kumkataa.Akitangaza matokeo, Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kaskazini na Mbunge wa Karatu, Mchungaji, Israel Natse alisema: ” Mbowe aliyekuwa mgombea pekee wa nafasi ya ubunge, alipigiwa kura za ndiyo 269 sawa na asilimia 98.2, lakini pia alipigiwa kura tano za hapana na wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Kura ya Maoni.”
Akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa mkutano huo, kuhusu haki ya kikatiba ya wajumbe wa mkutano huo kupiga kura ya hapana; Mchungaji Natse alisema kuwa kura za kumkataa zilitokana na kukua kwa demokrasia ndani ya chama hicho kinachojiandaa kushika dola baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Katika uchaguzi huo uliofanyika katika mji mdogo wa Bomang’ombe, wajumbe halali waliopaswa kushiriki zoezi hilo walikuwa 274 kutoka Kata zote za Wilaya hiyo.
Hata hivyo; akizungumza muda mfupi baada ya kutangazwa matokeo hayo, Mbowe alisema,”Nawashukuru sana wajumbe kwa kuniamini na kunipa heshima ya kuendelea kutetea ubunge wa Hai na pia kuendeleza mapambano dhidi ya utawala wa CCM. Nawahakikishia kwamba nitashinda tena kwa kishindo na moto watauona mwaka huu.”
Mbowe alisema sababu ya yeye kuendelea kupigania ukombozi wa nchi kutoka mikononi mwa CCM ambayo imewagawa Watanzania katika makundi ya walionacho na wasionacho, hakuwezi kumfanya asiwaze juu ya ukombozi wa fikra na maendeleo ya kweli dhidi ya umma wa Watanzania.
MTANZANIA
Kikosi maalum cha wapiganaji na majeshi ya ulinzi na usalama kinachopambana na watu wanaojihusisha na ugaidi, wanaosadikiwa kujificha katika mapori ya Mkuranga na Kisarawe Mkoani Pwani, kimebaini uwepo wa kambi kubwa tatu za magenge ya kigaidi katika ukanda wa Pwani ya Tanzania.
Kubaini kwa kambi hizo kumekuja baada ya msako mkali na mapambano ya siku kadhaa yaliyofanywa na wapiganaji hao katika maeneo ya Pwani ambapo wiki iliyopita walifanikiwa kuwatia nguvuni magaidi watano.
Kwa mujibu wa taarifa hizi magenge matatu ya kigaidi yapo katika Mikoa ya Lindi, Morogoro na Pwani katika maeneo ya Kisarawe na Mkuranga ambapo pia kuna idadi kubwa ya wanachama wa magenge hayo.
Taarifa zinazema ni katika ngome hizo ambapo fedha na silaha zinazoporwa na magaidi zinahifadhiwa.
Magenge hayo yana baadhi ya watu ambao ni wazoezi katika medani ya vita na uchunguzi uliofanywa na Taasisi za usalama zimebaini kuwepo na watu zaidi ya 300 waliyojiunga nayo wakiwemo askari wa zamani na kiongozi wao mkuu aliwahi kupata mafunzo ya kikomandoo
MWANANCHI
Mbunge wa Kahama, James Lembeli,
ambaye hivi karibuni alitangaza kuihama CCM na kujiunga na Chadema, kwa
mara ya kwanza amepokewa na umati mkubwa mjini Kahama hali iliyomfanya
aangue kilio akiwa jukwaani.
Lembeli alisindikizwa na wabunge wa majimbo ya Mwanza waliomaliza muda wao, Haines Kiwia, Ezekiel Wenje na Mbunge wa Biharamulo, Anthony Mbasa katika na msafara wa magari, bodaboda na bajaji aliingia mjini hapa saa 9:30 mchana.
Lembeli na msafara wake walilakiwa na
watu mbalimbali wakiwamo wafanyabiashara waliosimamisha shughuli zao kwa
muda huku wakionyesha alama ya vidole viwili ambavyo hutumiwa kama
alama ya utambulisho ya Chadema
Katika msafara huo, wananchi hao
walifunga barabara zote za mjini hapa hali iliyosababisha foleni ndefu
hadi walipofika kwenye Viwanja vya CDT ambako mkutano huo ulifanyika.
Wakiwa katika mkutano huo Katibu wa
Chadema Mkoa wa Shinyanga, Zacharia Thomas alimwelezea Lembeli kama
mwanasiasa aliyekomaa ambaye nyota yake aliifukia jalalani lakini kwa
kuhamia Chadema itang’ara zaidi.
Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Kiwia
aliwataka wananchi wa Kahama pamoja na kumuunga mkono Lembeli wanapaswa
kuwa na nguvu ya pamoja kuhakikisha kama atateuliwa na Chadema kuwania
ubunge, wahakikishe wanalinda kwa nguvu kura.
Alisema Lembeli anaweza kushinda kwa
nguvu kubwa Jimbo la Kahama lakini anaweza kuhujumiwa na wasimamizi wa
uchaguzi ambao ni wakurugenzi wa halmashauri.
Kwa upande wake Lembeli aliyekuwa
ameambatana na mama yake mzazi, Maria Kasembo alisema, uamuzi alioufanya
ni mgumu lakini wizi na rushwa iliyokuwa ikifanyika katika ofisi za CCM
ilimlazimu kuamua kuhama na kujiunga na Chadema.
Lembeli ambaye alikuwa akihutubia umati
wa wananchi kwa kutumia kitabu cha Biblia alisema, uamuzi wake huo ni
sawa na mwana aliyekuwa amepotea na sasa amerudi kuwakomboa wana wa
Israel.
Alisema kuhama kwake kwenda Chadema
atafanya kazi kubwa ya kutetea wanyonge kuliko alivyokuwa ndani ya CCM
sehemu iliyojaa wizi na rushwa.
Hata hivyo, alipofikia kueleza
kilichomtoa CCM, Lembeli aliangua kilio akisema pamoja na kufanya kazi
kubwa hakupewa shukrani badala yake akawa mtu wa kuletewa wala rushwa na
watoa rushwa ili wagombee ubunge kwenye jimbo lake la Kahama.
Pia, alisema pamoja na kugombea ubunge
Kahama Mjini kama atashinda na kuwa mbunge atasaidia wananchi wa majimbo
ya Kahama na Ushetu.
jimbo ambalo limezaliwa kutoka Kahama ambayo kwa pamoja ameyatumikia kwa miaka tisa na nusu na anajua matatizo yao.
Naye Mbunge wa Nyamagana aliyemaliza
muda wake, Wenje alisema anamtambua Lembeli hata alipokuwa mbungeni
misimamo yake ilionyesha kama mpinzani hivyo kuhama CCM ndipo
atakavyofanya kazi vyema.
Wenje alisema Chadema hakuna mgeni
mwanachama, yeyote akiingia leo anaanza kazi papo hapo hivyo Lembeli
tangu siku aliyoingia alianza kazi ndiyo maana alikwenda Bunda kufanya
kazi za chama hivyo Kahama wamuunge mkono.
Kwa kutumia mkutano huo, Lembeli
alitangaza rasmi kuwania ubunge Jimbo la Kahama Mjini na kuwatoa
wasiwasi wagombea wengine kwa madai demokrasia itazingatiwa wakati wa
mchakato wa kura za maoni ndani ya chama.
MWANANCHI
Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira amesema hakuwahi kuwa na mvutano wowote na Mbunge wa Viti Maalum, Ester Bulaya, kwa kile alichodai kuwa siyo ‘saizi’ yake kwenye uwanja wa siasa.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana,
Wasira alisema hakuwahi kuvutana na Bulaya na kwamba, kitendo chake cha
kuhamia Chadema, kimempotezea mashabiki wengi hususan vijana wa Jimbo la
Bunda mkoani Mara.
Hata hivyo, Bulaya alipoulizwa kuhusu
hilo alisema kuhama kwake CCM kumemrahisishia kupata wafuasi wengi
wakiwamo vijana na wazee huku, akidai kupigiwa simu mara kwa mara za
kupongezwa kwa uamuzi wake wa kujiunga Chadema.
“Tangu
nilipokuwa CCM, nilikuwa mwakilishi wa vijana na huku Chadema ndiyo
kwenyewe, nimeendelea kuiteka Bunda tofauti na awali,” alisema Bulaya.
Alisema hakuwahi kufikiria uamuzi wa
kukodi wananchi ili wahudhurie kwenye mikutano yake, bali uhusiano bora
kati yake na wakazi wa Bunda ndio uliosababisha umati wa watu kufurika
katika mkutano uliofanyika juzi.
Wasira ambaye pia ni Mbunge wa Bunda
(CCM), alisema vijana wengi wa jimbo hilo walikuwa wanampenda Bulaya kwa
sababu alikuwa CCM ambayo ndiyo chama kilichomlea kisiasa hadi hapo
alipofikia hivi sasa.
“Mfano
mzuri ni juzi katika mkutano wake uliovunja rekodi ya kuhudhuriwa na
watu wengi, wananchi waliletwa kwa malori kutoka sehemu mbalimbali
zikiwamo Mwanza na Serengeti,” alisema Wasira ambaye ameomba kuteuliwa kugombea jimbo hilo kwa mara nyingine.
Alidai kuwa Chadema imekuwa ikijinasibu
kuwa haiwezi kukodisha wananchi kuhudhuria katika mikutano yao, lakini
juzi ilikuwa hivyo.
Akizungumzia hali ya ushindani iliopo
kwa wagombea waliojitokeza na kuchukua fomu ya kugombea jimbo la Bunda,
Wasira alisema upo kiasi na endapo CCM itampitisha tena, yupo tayari
kupambana na yeyote kutoka upinzani hata Bulaya ambaye si saizi yake.
“Kizuri
kinajiuza bwana, sikuwa na sababu ya kukodi watu waje kushiriki kwenye
mkutano wangu, yeye na chama chake ndio wenye tabia hiyo. Hata hivyo,
wataambulia patupu safari hii,”Bulaya.
Bulaya alipouulizwa endapo Chadema
ikimpitisha kuwania Bunda ataweza kupambana na mgombea kutoka chama
chake za zamani akiwamo Wasira, alijibu:
“Sioni
‘saizi’ yangu kati ya wote waliojitokeza kuchukua fomu ya Bunda, ni
bora Wasira akapumzika kwani kizazi chake kwa sasa hakipo.”
Katika hatua nyingine; Wasira amekanusha taarifa kuwa amempiga Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mara, Chistopher Sanya.
Wasira alikiri kutokea kwa ubishi wa
kawaida kati yake na Sanya, lakini siyo wa kufikia hatua ya kupigana na
kwamba, wanaosambaza taarifa hizo wana lengo la kumchafua kisiasa.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete
ametunikiwa Tuzo ya Utawala Bora Afrika kwa mwaka 2015 kutokana na
jitihada zake za kudumisha na kuimarisha utawala bora nchini.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilieleza kuwa Rais Kikwete ametunikiwa tuzo hiyo na Taasisi ya African Archievers Awards yenye makao makuu nchini Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Kikwete anaungana na Askofu Desmond Tutu
wa Afrika Kusini aliyekuwa wa kwanza kupewa tuzo hiyo mwaka 2011
kutokana na mchango wake wa kutetea haki za binadamu, usawa na amani.
“Rais
Kikwete ameteuliwa kutoka miongoni mwa watu 1,202 ambao majina yao
yaliwasilishwa kwenye jopo la kimataifa, linalojitegemea na lenye
wajumbe kutoka Uingereza na Afrika Kusini kwa ajili ya uteuzi,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, kutokana na
tuzo hiyo, Rais Kikwete amealikwa kwenda kuipokea nchini Afrika Kusini
kesho mjini Johannesburg.
Hata hivyo, Rais Kikwete hataweza kwenda
kutokana na kukabiliwa na majukumu mengi, hivyo badala yake atakwenda
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha Rose Migiro.
Katika barua ya kumjulisha Rais Kikwete kuhusu uteuzi wake, Mtendaji wa African Achievers Awards, Rex Indaminabo alisema: “Uongozi
wa African Achievers Awards unayo furaha kukujulisha juu ya uteuzi wako
wa kupokea Tuzo katika kundi la Utawala Bora Afrika.”
Mtendaji huyo aliongeza: “Ni
kwa furaha na heshima kubwa kuwa wajumbe wa Bodi ya Ushauri na Taasisi
ya Uongozi na Menejimenti wanakupongeza kwa mafanikio haya.”
MWANANCHI
Ni wiki ya mtikisiko. Hivi ndiyo
unavyoweza kuelezea hali itakavyokuwa nchini kutokana na matukio makubwa
ya kisiasa yanayotazamiwa kutokea ndani ya wiki inayoanza leo ambayo
yanaweza kubadili mwelekeo wa siasa za Tanzania.
Hali hiyo inatokana na vuguvugu la
kisiasa linalohusisha viongozi wenye ushawishi kuhama vyama vyao vya
siasa na kutimkia kwenye vyama vingine, ikiwa ni siku chache kabla ya
kufanyika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
Ni wiki ambayo itapambwa na matokeo ya
kikao cha Baraza Kuu la Uongozi wa CUF kilichofanyika jana mjini
Zanzibar kuhusu mustakabali wake ndani ya Ukawa, ikizingatiwa kuwa hivi
karibuni chama hicho kiliamua kujiweka kando ya vikao vya umoja huo hadi
vikao vya juu viamue.
Hata hivyo, habari ambazo gazeti hili
limezipata zinasema kuwa uwezekano wa chama hicho kujitoa ndani ya Ukawa
ulikuwa mdogo kutokana na kuogopa hasira za wananchi wenye matumaini na
umoja huo.
Aidha, kulikuwa na taarifa kuwa kikao
cha jana kilikuwa kinaangalia jinsi watakavyoshiriki katika umoja huo na
kwamba kulikuwa na matumaini makubwa.
Vile vile, hii ni wiki ambayo kura za
maoni zinazoendelea katika vyama vikubwa vya siasa, kuonyesha baadhi ya
vigogo wakiangushwa na kujaribu kutafuta upenyo wa madaraka katika vyama
vingine.
Pia, ni wiki ambayo chama kikuu cha
upinzani, Chadema kimeamua kusogeza mbele tarehe za kuchukua na
kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa kugombea urais kutoka jana hadi
Ijumaa, katika kile kinachotazamwa kama kusubiri mchakato wa kumpata
mgombea urais.
Kana kwamba hiyo haitoshi, hii ni wiki
ambayo minong’ono ya waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa ambaye jina
lake limekatwa katika orodha ya wasaka urais wa CCM anaweza kuhamia
Chadema.
Tayari baadhi ya viashiria vya hali hiyo
vimeanza kuonekana ambapo wiki iliyopita wabunge wawili wa chama tawala
cha CCM, James Lembeli na Ester Bulaya waliachana na chama hicho na
kujiunga na Chadema huku chama hicho cha upinzani kikitamba kujiandaa
kuwapokea vigogo wengine zaidi.
Kiashiria kingine cha mtikisiko ni hatua
ya madiwani 18 wa CCM wilayani Monduli na wengine 10 wa UDP na CCM
Bariadi kuhamia Chadema.
Lakini pia wapo wabunge na madiwani wanaohama Chadema kwenda chama cha ACT-Wazalendo.
Vuguvugu hilo la kisiasa limekolezwa na
kauli za wanasiasa wawili vijana kwa nyakati tofauti, Godbless Lema na
Zitto Kabwe kuwa wiki hii itakuwa ya mshikemshike kutokana na mambo
yaliyopangwa kufanyika.
MWANANCHI
Wanachama wa Chadema wamedai kufichua mpango unaofanywa na baadhi ya
viongozi wa CCM wa kumwekea pingamizi Mbunge wa Jimbo la Hai, Freeman Mbowe ili asiwanie ubunge.
Kiini cha mipango hiyo ni hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Hai
iliyomtia hatiani kwa kosa la kumshambulia mwangalizi wa ndani katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Nassir Yamin.
Katika hukumu hiyo, iliyotolewa Juni 17 na Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Hai, Dennis Mpelembwa alimhukumu Mbowe kulipa faini ya Sh1 milioni au kwenda jela mwaka mmoja.
Hata hivyo, Mbowe ambaye ni mgombea pekee na kushinda kura za maoni
kwa kupata 269 za ndiyo na tano za hapana, alilipa faini hiyo na
kuachiwa huru baada ya wafuasi wake kuchanga fedha hizo.
Mipango hiyo inayodaiwa kuwa ni ya CCM kutaka kutumia hukumu hiyo
kumzuia Mbowe kuwania ubunge, ilielezwa jana katika Mkutano Mkuu maalumu
wa kura za maoni za ubunge Jimbo la Hai.
Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo, James Swai alimuuliza Mbowe
amejiandaaje, kwa sababu kuna madai kuwa CCM wana mpango wa kutumia kesi
hiyo ili kumwengua kugombea nafasi hiyo.
Hata hivyo, wakati akijibu swali hilo, Mbowe hakueleza wazi kama
anafahamu mpango huo zaidi ya kuitaka CCM isitafute ushindi wa mezani.
“Wangekuwa na wanasheria
wasingefikiria kabisa wala kuzungumza hivyo. Kifungu nilichohukumiwa
nacho hakinizuii kugombea. Wasitafute ushindi wa mezani waje uwanjani,” Mbowe.
Mbowe alisema tayari jopo la mawakili sita wa Chadema, ambao hata
hivyo hakuwataja kwa majina, limeweka mkakati maalumu wa kukata rufaa
kupinga hukumu hiyo aliyodai ni batili.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete
amefanya mabadiliko ya utendaji katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
kwa kumteua aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala wa Tume hiyo, Kailima Kombwey kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Kombwey ambaye aliapishwa jana
jioni, anachukua nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Mallaba, ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Rais Kikwete pia amemteua Jaji Richard Mziray,
kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
pamoja na majaji wengine wapya 13 wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Taarifa hiyo pia imesema kuwa Jaji
Mziray ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania,
kwa sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu, Dar es Salaam.
Majaji wengine wa Mahakama Kuu walioteuliwa na Rais Kikwete ni Ignas Kitusi ambaye ni Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania na Wilfred Dyansobera, ambaye ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu.
Wengine ni Lameck Mlacha ambaye ni Naibu Msajili na Mwenyekiti wa Baraza la Rufani la Kodi; Salima Chikoyo ambaye ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi; Isaya Arufani ambaye ni Naibu Msajili na Katibu wa Jaji Mkuu wa Tanzania na Mallaba.
Pia yumo Adam Mambi ambaye ni Katibu Msaidizi Tume ya Kurekebisha Sheria; Sirilius Matupa ambaye kwa sasa ni Msaidizi wa Rais, Sheria, Ofisi ya Rais, Ikulu; Issa Maige ambaye ni Wakili wa Kujitegemea na Licia Kairo ambaye ni Wakili wa Kujitegemea.
Dk Masoud Shaaban Benhaji, Wakili wa Kujitegemea na Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu Huria, Dar es Salaam pia ameteuliwa kuwa Jaji Mahakama Kuu. Wengine ni Victoria Makani ambaye ni Wakili wa Kujitegemea na Rehema Kerefu ambaye ni Mwanasheria wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
HABARILEO
Baadhi ya vigogo wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na Serikali, waliokuwa wakiwania nafasi ya kuteuliwa kuwa wabunge
wa viti maalumu baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu ujao, wamejikuta
wakishindwa katika kura za maoni.
Kura hizo zilizopigwa juzi na wajumbe wa
mkutano wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ngazi za mikoa yote nchini,
isipokuwa Mkoa wa Dar es Salaam, mbali na kuangusha baadhi ya vigogo,
pia zimeibua majina mapya na kuwapa nafasi za juu, zitakazowapa fursa ya
kuteuliwa kuwa wabunge wa Viti Maalumu na hata pengine uwaziri.
Washindi wawili wa juu katika kura hizo katika kila mkoa, ndio walio na
nafasi ya kuteuliwa kuwa wabunge wa viti maalumu, huku wa kwanza akiwa
na nafasi nzuri zaidi, baada ya kupatikana kwa kura za mgombea urais wa
CCM.
Miongoni mwa vigogo walioangushwa, yupo
Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Shamsha Mwangunga, Naibu Waziri
wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana na viongozi wa mikoa wa UWT, wakuu wa wilaya na wabunge kadhaa wa Viti Maalumu wanaomaliza muda wao.
Mkoani Njombe katika kura za wajumbe wa
Mkutano Mkuu wa UWT, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na
Watoto, Dk Pindi Chana, alijikuta akipoteza fursa ya kurejea bungeni
kupitia uwakilishi wa wanawake wa mkoa huo. Mshindi katika kura hizo ni
Dk Suzan Kolimba, ambaye alijizolea kura 252 na kufuatiwa na Neema Mgaya
213.
Wengine na kura zao katika mabano ni Dk
Chana (164), Erika Sanga (107), Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Rosemary Sitaki
(38) na Magret Kyando (5).
Katika Mkoa wa Iringa, aliyekuwa Mbunge
wa Viti Maalumu na mmoja wa wenyeviti wa Bunge la 10 linalomaliza muda
wake, Lediana Mng’ong’o (58) naye amepoteza fursa ya kurejea bungeni
kupitia dirisha hilo la UWT.
Aliyeongoza katika kura hizo na
kujihakikishia kuingia katika bunge lijalo ni Rose Tweve, aliyezoa kura
240 na kufuatiwa na Mbunge anayemaliza awamu yake ya kwanza ya ubunge
huo wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Ritta Kabati aliyepata kura 199.
Mng’ong’o alijikuta akichukua nafasi ya tatu kwa kupata kura 162 na
kufuatiwa na Shakira Kiwanga (89), Esta Chaula (21), Emma Mwalusamba
(14), Hafsa Mtasiwa (10), Farida Ninje (4) na Agnes Nyakunga (4).
Katika mkoa wa Tabora, ndiko ambako
wabunge waliomaliza muda wao, wamefanikiwa kutetea nafasi yao ya kurejea
bungeni. Uchaguzi uliofanyika mkoani hapo, umeshuhudia Mbunge
aliyemaliza muda wake, Munde Tambwe, akitetea kiti chake kwa kupata
ushindi wa kwanza baada ya kuzoa kura 662. Tambwe alifuatiwa na mbunge
mwenzake aliyemaliza muda wake, Mwanne Mchemba, aliyejizolea kura 342.
Wengine walioshiriki katika uchaguzi huo
na kura walizopata ni Aziza Ally (290), Paskazia Malunde (52),
HamidaThabit (40), Asma Suleiyum (40), Nasalile Mwaipase (16) na Agnes
Mgongo (6).
Mkoani Arusha nako, Mbunge wa Viti
Maalumu anayemaliza muda wake Catherine Magige, amefanikiwa kushinda
baada ya kujizolea kura 409, huku mshindi wa pili akiwa Vaileth Mfuko,
ambaye alipata kura 248.
Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Alphonce
Kinamhala, alitaja wengine katika kundi hilo kuwa ni Flora Zelote (128),
Halima Mamuya (92), Tina Timani (91), Clementina Mollel (44), Rehema
Mroso (9), Nembris Kimbele (44), Catherine Sakaya (6) na Mary Morindet
(51). Katika kundi la wabunge wa Viti Maalumu, aliyeshinda ni Amina
Mollel aliyepata kura 362 na kumbwaga mwenzake katika kundi la walemavu,
Christina Manyenye aliyepata kura (196).
Katika Mkoa wa Mtwara, aliyekuwa Mbunge
wa Viti Maalumu, Anastansia Wambura aliongoza kwa kupata kura 438 na
kufuatiwa na Mbunge mwingine wa Viti Maalumu anayemaliza muda wake,
Agness Hokororo aliyepata kura 316. Hokororo pia ni Mkuu wa Wilaya ya
Tunduru, mkoani Ruvuma. Msimamizi Mkuu wa uchaguzi huo ambaye pia ni
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara na Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT Taifa, Halima
Dendego, alitaja wengine walioshiriki katika uchaguzi huo na kura zao
katika mabano kuwa ni Rukia Swalehe (223), Daisy Ibrahimu (204), Emma
Rashid Kawawa (40), Luckiness Amlima (12), Dk Divana Kaombe (11),Asha
Motto (8) na Thecla Mbuki (1).
Mkoani Singida, mbunge wa Viti Maalum
anayemaliza muda wake, Diana Chilolo, alijikuta akishindwa kutetea
nafasi yake baada ya kuibuka mshindi wa tatu. Mbali na Chilolo, pia
msanii maarufu wa filamu, aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2006, Wema
Sepetu, ambaye alivuma wakati alipochukua fomu, naye alijikuta
akishindwa katika kura hizo. Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo,
Msimamizi Mkuu wa uchaguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko
Kone, alimtaja mshindi wa kwanza kuwa ni Aysha-Rose Matembe aliyezoa
kura 311, huku Mbunge wa Viti Maalumu anayemaliza muda wake, Martha
Mlata, akitetea nafasi hiyo baada ya kuibuka wa pili kwa kupata kura
235.
Wengine walioshiriki katika uchaguzi huo
na kura zao katika mabano ni Chilolo (182), Sepetu (90), Sarah Mwambu
(74), Martha Gwau (44), Rehema Madusa (24), Aziza Ntandu (5), Mary Marco
(3), Sofia Joseph (2), Salome Mpondo (1), Leah Samike (1) na Elizabeth
Lucas (0). Bukoba Mkoani Kagera, Mbunge wa Viti Maalumu anayemaliza muda
wake, ambaye pia amekuwa Mbunge kwa miaka 25, Elizabeth Batenga
ameshindwa kutetea nafasi yake.
Mbali na Batenga, pia Mbunge wa zamani
wa Jimbo la Muleba Kaskazini, Ruth Msafiri, aliyekuwa akiwania kurejea
bungeni kwa kupitia Viti Maalumu, naye ameanguka katika uchaguzi huo.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo jana, Msimamizi Mkuu wa uchaguzi huo
ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongella, alimtaja aliyekuwa
Mbunge wa Viti Maalum mkoa huo kwa miaka mitano iliyopita, Benadetha
Mshashu kuwa ndiye mshindi wa kwanza, baada ya kupata kura 432.
Mshindi wa pili ni Oliva Semguruka
kutoka wilayani Ngara aliyepata kura 314. Wengine walioshiriki katika
uchaguzi huo mbali na Batenga aliyepata kura 255 na Msafiri aliyeambulia
kura 20 ni Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora, Janath Kayandaali (133) na
Mwagen Balaganwa (47). Pia yumo Elizabeth Ngaiza aliyepata kura 16,
Levina Jovin ambaye pia ni Mwenyekiti wa UWT Mkoa huo (16), Grace
Maumbuka (7) na Domina Balyagati (7).
Morogoro Mkoani Morogoro wabunge watatu
wa Viti Maalumu waliomaliza kipindi chao, Sara Msafiri, Dk Christine
Ishengoma na Margaret Mkanga (Kundi la Wenyeulemavu), wametetea nafasi
zao baada ya kushinda katika kura hizo. Msimamizi Mkuu wa uchaguzi huo,
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rajab Rutengwe, aliwataja Dk Chritine
Ishengoma kuwa mshindi kwa kwanza kwa kupata kura 641.
Aliyeshika nafasi ya pili ni aliyekuwa
Mbunge wa Viti Maalumu kupitia UVCCM Mkoa wa Morogoro, Sara Msafiri
ambaye alichaguliwa kwa kura 608. Wagombea wengine katika kundi hilo ni
Harriet Mwakifulefule, Elizabeth Lyimo, Dk Magdalena Kongera, Sarah
Kalaite, Tatu Madikah, Susan Saileni, Mariam Kiamani, Mercy Minja,
Redempta Mushi na Lucy Ngugi.
Katika kinyang’anyiro cha ubunge viti
maalumu kwa watu wenye ulemavu mchuano, ulikuwa mkali kati ya Mbunge
anayemaliza muda wake, Margaret Mkanga ambaye alipata kuwa 424 sawa na
asilimia 55.99 ya kura zote 759 zilizopigwa. Mshindani wake mkubwa
muigizaji wa filamu nchini, Wastara Issa alipata kura 252 sawa na
asilimia 33 ya kura zote huku Chausiku Lukinga akiambulia kura 43.
Mkoani Dodoma, Waziri wa zamani wa
Maliasili na Utalli, Shamsa Mwangunga, alijikuta akishindwa kufurukuta
katika uchaguzi huo, ambao Mbunge wa Viti Maalum anayemaliza muda wake,
Felister Bura, aliibuka kidedea baada ya kupata kura 457. Akitangaza
matokeo hayo, Katibu wa (UWT) Mkoa wa Dodoma, Kaundime Kasesa, alimtaja
mshindi wa pili ambaye naye ana fursa ya kuwa Mbunge wa Viti Maalumu,
kuwa ni Fatma Tawfiq, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Manyoni aliyepata kura
368.
Wengine walioshiriki mbali na Mwangunga
aliyepata kura 27 ni Asia Abdalah (112), Fortunata Njalala (102) na
Neema Majure (78). Pia yumo Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Dodoma, Salome
Kiwaya, Elizabeth Chagwanda, Romana Nyoni na Rahel Baragele. Wengine ni
Mary Chihoma, Sarah Chwamba, Martha Dismas, Aurelia Mamboleo, Nyemo
Masimba, Egla Mwamoto, Judith Muyeya, Mary Mgongo, Safina Mfaki, Mariam
Ndahani, Asha Omary na Stella Mwimba.
Katika mikoa mingine matokeo ya awali
tuliyopata ni Mkoa wa Rukwa ambao aliongoza Silafi Maufi na kufuatiwa na
Bupe Mazengo;Katavi ni Taska Mbogo na Ana Lupembe; Kigoma ni Josephine
Genzabuke na Philipa Mtulano; Kilimanjaro ni Shary Raymond na Betty
Machangu na Tanga ni Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Ummy Mwalimu
akifuatiwa na Sharifa Abebe.
Mkoani Mbeya mshindi ni Mary Mwanjelwa
na Mary Mbwilo; Kaskazini Unguja ni Angelina Malembeka na Mwanajuma
Kassim; Kusini Unguja ni Asha Msimba Jecha na Mwamtum Haji Dau; Mkoa wa
Mjini ni Fakharia Khamis Shomari na Asha Abdallah Juma na Mkoa wa
Mgharibi ni Tauhida Nyimbo na Kaukeb Ally Hassan.
Katika Mkoa wa Songwe, mshindi ni
Juliana Shonza na Neema Mwandabila; Simiyu ni Ester Midimu na Lea
Komanya; Manyara ni Martha Umbulla na Esther Mahawa huku mkoani Mara
washindi ni Agnes Mathew na Christina Samo. Mkoani Ruvuma, mshindi ni
Jackline Mshongozi na Sikudhani Chikambo; Kaskazini Pemba ni Maida Hamed
Abdallah na Asia Sharif Omary.
Katika Mkoa wa Kusini Pemba ni Faida
Mohamed na Asha Moahamed Omary huku Lindi akipita Hamida Mohamed
Abdallah na Honoratha Chitanda. Katika Mkoa wa Geita, mshindi ni Vicky
Kamata na Josephine Chagulla; Mwanza Kemilembe Lwota na Kiteto Koshuma;
Pwani akipita Zaynab Vullu na Subira Mgalu huku Shinyanga akipita Lucy
Mayenga na Azza Hilary.
Imeandikwa na Regina Kumba, Dar es
Salaam, Frank Leonard, Njombe na Iringa; Lucas Raphael,Tabora; Veronica
Mheta, Arusha; Abby Nkungu, Singida; Clarence Chilumba, Masasi; Angela
Sebastian Bukoba; John Nditi, Morogoro na Sifa Lubasi na Grace
Chilongola, Dodoma
HABARILEO
Mgombea urais mteule wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli,
amewaomba wananchi wa mkoa wa Morogoro na mingine nchini, kuchagua
wabunge wachapakazi kama yeye wanaotokana na CCM. Lengo la ombi hilo, ni
ili yeye atakapochaguliwa na Watanzania kuwa Rais, ateue wabunge hao
kwenye nafasi ya uwaziri watakaowatumikia kikamilifu.
Akielezea uzoefu wake, Dk Magufuli
alisema ametumikia nafasi ya ubunge na uwaziri katika miaka 20 na
anajivunia kuwa na rekodi nzuri ya utendaji, hivyo alisema anatumia
fursa hiyo, kuwaomba wananchi wa mkoa wa Morogoro, wachague wabunge
wanaofanana naye wanaotokana na CCM.
Dk Magufuli alisema hayo juzi kwa
nyakati tofauti katika maeneo ya Dumila na Dakawa wilayani Mvomero na
Manispaa ya Morogoro katika viwanja vya Jengo la CCM Mkoa, wakati
akisalimia na kujitambulisha kwa wananchi, wapenzi na wanachama wa CCM.
“Wananchi
wa Morogoro nawaombeni muwachague wabunge wachapakazi wanaotokana na
CCM kama nilivyokuwa mimi, ili nitakapopata ridhaa yenu ya kuchaguliwa
kuwa Rais wenu, niwateue kuwa mawaziri ili wawatumikie kikamilifu hasa
wananchi wa hali ya chini,” alisema mgombea huyo.
Alisema iwapo Watanzania watampa ridhaa
kushika nafasi hiyo katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu, atahakikisha
anamaliza migogoro baina ya wafugaji na uwakulima hapa nchini.
Magufuli alipokewa na umati mkubwa wa
wananchi katika maeneo ya Dumila na Dakawa huku wakimshangilia na
kumpongeza wakimuita ‘jembe’, ambapo wakati akizungumza nao, alisema
anasononeshwa na kero ya kuwepo kwa migogoro ya wakulima na wafugaji.
Aliahidi kuwa akipewa ridhaa ya kuwa
Rais atakomesha jambo hilo. Alisema, migogoro hiyo imekuwa ikigharimu
maisha ya watu na haipaswi kuendelea kuwepo hapa nchini, kwakuwa
Watanzania wote wamekuwa wakiishi kama ndugu bila kujali dini wala
kabila, hivyo ni lazima ikomeshwe ili amani iendelee kuwepo katika
maeneo yote.
Magufuli alisema, kinachotakiwa
kufanyika ni kukutanisha pande zote mbili za wafugaji na wakulima na
kuzungumza pamoja ili kupatikana muafaka pasipo kuangalia itikadi ya
vyama vya siasa, kabila wala rangi.
Awali, Mwenyekiti wa Wazee wa Mkoa wa Morogoro, Kanali mstaafu Isaac Mwisongo
ambaye wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea wa urais kupitia chama
hicho alitangaza hadharani yeye na wazee wenzake, kumuunga mkono Waziri
Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, alisema kuanzia sasa wanaungana na Dk Magufuli.
Alisema yeye pamoja na Mkuu wa Mkoa wa zamani wa Morogoro, Stephen Mashishanga, na Waziri wa zamani aliyeshika nyadhifa mbalimbali katika serikali za awamu ya tatu na nne, Dk Juma Ngasongwa
walipanda jukwaani na kumuunga mkono Lowassa, lakini kutokana na
kumalizika kwa mchakato huo, sasa wameunganisha nguvu zao zote kwa Dk
Magufuli, ambaye ni mgombea urais wa CCM.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment