Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kitaaluma na kielimu. Kituo kipo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
amesema chama chake kimeshindwa kumtangaza mgombea wake wa urais kama
ilivyotarajiwa jana, badala yake kikawaomba Watanzania kutokuwa na
haraka, wasiwasi wala mihemko na kuwa muda ukifika kitamtangaza.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika
Viwanja vya Magomeni Mwanza, Mbowe aliwaomba wananchi kuuvumilia Umoja
wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa sababu viongozi wake wanaendelea na majadiliano na watakapokubaliana watamtangaza mgombea wao.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu
alisema ilikuwa wamtangaze mgombea urais kama ilivyoripotiwa na gazeti
hili, lakini wenzao wa CUF wamewaomba kuwa wanaendelea na vikao vyao vya
chama.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema:
“Wengi wana hamu ya kutaka kujua mgombea urais wa Chadema, naomba
niseme kwamba tumekuja Mwanza kwa mambo mawili, kuja kuwapokea makamanda
hawa wawili na kuitokomeza CCM.
“Ukawa
itamsimamisha mgombea urais ambaye Oktoba lazima aiondoe CCM
madarakani, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Magdalena Sakaya) ametuomba tena
tusubiri hadi tarehe 25 (Jumamosi), kwani watakuwa na kikao cha Baraza
Kuu la chama hicho, hivyo tunawasubiri wenzetu.”
Mbowe aliyetumia mkutano huo kuwakabidhi
kadi wanachama wapya waliotoka CCM na kujiunga Chadema, Mbunge wa
Kahama, James Lembeli na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya, aliweka
msisitizo:
“Muungano wetu wa Ukawa ni wa msingi
sana, kuna changamoto, tunaomba wananchi muwe wavumilivu, tuache mihemko
ili tufikie uamuzi sahihi.
“Tunaomba
mtuvumilie, hatuwezi kumtangaza mgombea wetu kwa sababu tu CCM
wametangaza wa kwao, hapana! Tutamtangaza mgombea wetu na nyote
mtafurahi,” alisema Mbowe huku akishangaliwa na maelfu ya wananchi.
Alisema, Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi
alikuwa ahudhurie mkutano huo lakini kutokana na foleni za Dar es
Salaam alishindwa kuwahi ndege na kwamba, viongozi wengine wa CUF na
NCCR Mageuzi walialikwa lakini walikuwa na vikao vya vyama vyao.
Mbowe alisema Ukawa ni mpango wa
wananchi, siyo wa viongozi na kwamba ulianzishwa Dodoma na viongozi wote
wa upinzani na Kundi la Wabunge 201 wa Bunge Maalumu la Katiba
walihudhuria, lakini baadhi yao walipenyezewa ‘kitu kidogo’ wakaondoka
hivyo kubaki vyama vinne vya siasa.
MWANANCHI
Kasoro za uandikishaji wananchi katika
Daftari la Kudumu la Wapigakura zilizokuwa zikitokea katika mikoa
mbalimbali nchini, zimejitokeza pia jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku
ya kwanza ya kazi hiyo.
Mwananchi ilipita katika maeneo
mbalimbali jana na kushuhudia wananchi wengi wakiwa wamekutana na
changamoto kadhaa kwenye baadhi ya vituo ikiwamo ya kukosekana mashine
za Biometric Voters Registration (BVR).
Wananchi hao walisema licha ya kwamba
Dar es Salaam imepewa siku 10 ya uandikishaji, kama changamoto hizo
hazitachukuliwa hatua kazi hiyo inaweza isikamilike kwa wakati.
Miongoni mwa changamoto nyingine ni
kuharibika kwa mashine zilizopo, ukosefu wa umeme, uchache wa watendaji
na kuelemewa na watu, mtandao usio wa uhakika na nani aanze kuandikishwa
kati ya wenye mahitaji maalumu na wasionayo.
Katika kituo cha uandikishaji cha Shule
ya Msingi Oysterbay ambako kuna vituo vidogo vitano, wakala wa
uandikishaji, Margereth Galway alisema mwitikio wa vijana umekuwa mkubwa
kiasi kwamba inakuwa shida kuwapa nafasi ya upendeleo wazee, viongozi,
walemavu au wajawazito na wanaonyonyesha.
“Eneo
hili lina wazee na viongozi wengi wa chama na Serikali. Mwitiko mkubwa
wa vijana unatufanya tushindwe kuwasaidia watu hao,”Galway.
Alisema wasimamizi wote wa kituo hicho
wamekubaliana kuwa kuanzia leo, wateue mashine moja na itengwe kwa ajili
ya wenye mahitaji maalumu ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi
wanaokuwa wamesimama kwenye foleni muda mrefu.
“Tayari wameshakuja Warioba (Jaji
Joseph), Msekwa (Pius) na Butiku (Joseph) wakiwa na wake zao na
kujiandikisha. Pamoja na kufahamika kwao bado vijana hawakuwa radhi
kuwapisha wakitaka wajipange jambo ambalo ni gumu kulitekeleza.
“Kama
tutafanikiwa kuwashawishi waandikishaji basi foleni za watu wa kawaida
zitakuwa nne na moja itaachwa kwa ajili ya wenye mahitaji muhimu,” alisema.
Katika Kituo cha Shule ya Msingi Kawe A,
wazee wengi walikutwa wamekaa kwenye madawati, nje ya madarasa
wakisubiri kuandikishwa baada ya vijana kutokubali kuwapisha wakidai
waandaliwe utaratibu ambao hautoingilia foleni iliyopoo.
Katika Shule ya Msingi Hekima iliyopo
wilayani Kinondoni, kulikuwa na malalamiko kama hayo na wananchi
wakaiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuweka utaratibu maalumu.
Mmoja wa waliofika kujiandikisha,
Mwanaidi Abdallah alisema katika uandikishaji huo wanawake wamekuwa
wakipata shida kutokana na utaratibu mbovu.
Alisema inachukua muda mrefu kupata huduma kwa sababu baadhi ya vijana wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kujiandikisha.
Katika kituo cha Mtendaji kilichopo Mtaa
wa Mzimuni, Kata ya Kawe, wananchi walikutwa wakiwa nje saa 8:00 mchana
wakisubiri mashine ili uandikishaji uanze licha ya kutangaziwa kazi
hiyo ingeanza asubuhi.
Kitu pekee kilichokuwa kinaendelea ni
wananchi kujiorodhesha kwenye daftari na kupewa namba ya foleni hadi
mashine zitakapoletwa.
HABARILEO
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli
amesema akifanikiwa kuchaguliwa kuwa kiongozi wa juu wa nchi hii,
atahakikisha anatekeleza ipasavyo Ilani ya Uchaguzi wa chama hicho.
Alisema hayo mjini hapa jana jioni
alipokuwa akisalimiana na mamia ya wananchi, walioenda kumwona akiwa
safarini kutoka nyumbani kwake Chato mkoani Geita kuelekea Dodoma.
Alisema ni kwa kutekeleza kikamilifu Ilani hiyo, ndipo maendeleo ya
kweli nchini yatapatikana.
Hata hivyo, alisema kuwa atahakikisha analeta maendeleo kwa watu wote bila ubaguzi wa dini, rangi, kabila wala itikadi.
“Maendeleo
hayana Chama. Nikifanikiwa kuwa Rais nitaleta maendeleo kwa kila mtu…
Kwa wana-Chadema, Wana-Cuf na hata kwa wale wasio na Chama,” Dk Magufuli.
Aidha, alisema akifanikiwa kuwa Rais,
atakuwa mtumishi wa watu na kuhakikisha anachagua serikali ya watu
makini wasioonea wananchi.
“Namwomba Mwenyezi Mungu nisije kuwa Rais wa kujikweza, wa kujivuna na wa kusahau watu wangu” Dk Magufuli.
Dk Magufuli aliwakosha wananchi na
kushangiliwa kwa nguvu pale alipotiririka kwa salamu za makabila mbali
mbali nchini, kuanzia Kaskazini hadi Kusini, Mashariki hadi Magharibi
mwa Tanzania “Huo ndio Utanzania wetu,” aliwaambia wananchi baada ya
kumaliza na kuongeza kuwa atahakikisha anazingatia na kudumisha misingi
yote mizuri, iliyoachwa na waasisi wa Taifa hili na marais waliopita.
NIPASHE
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)
lipo katika mchakato wa mwisho wa kuanzisha kampuni ya kutengeneza
nguzo za umeme za zege, ikiwa ni mkakati wa uboreshaji huduma kwa wateja
wake, kupunguza matumizi ya nguzo za miti na kudhibiti uharibifu wa
miundombinu hiyo.
Mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba,
alisema kampuni hiyo ambayo itakuwa chini ya shirika hilo inatarajiwa
kuanza kazi mwishoni mwa mwaka huu mchakato wa kuisajili kwa Wakala wa
Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) utakapo kamilika.
Alisema hatua ya shirika hilo kuanza
kutumia nguzo za zege badala ya za miti ni moja ya mikakati ya shirika
ilo kuhakikisha linatoa huduma bora na za uhakika kwa wateja wake kwani
mara nyingi nguzo za miti zimekuwa hazidumu na kulazimika kubadilishwa
mara kwa mara kutokana na uchakavu.
“Teknolojia
inakuwa kila siku na kurahisisha huduma kwa wananchi na hata wakati
mwingine kupunguza gharama, tutakapoanza kuzalisha nguzo za zege
tutapunguza kero nyingi kwa wateja wetu kwani nguzo za miti huharibika
haraka hasa kipindi cha mvua pamoja nyingine kuungua moto unapotokea,” alisema.
Mramba alisema kutumika kwa nguzo hizo
za zege pia kutabadilisha mandhali ya miji na kuongeza kuongeza fursa za
ajira kwa Watanzania.
Kuhusu uboreshaji wa huduma ya umeme kwa
jiji la Dar es Salaam, Mramba alisema ujenzi wa vituo vidogo vitano vya
usambazaji na upozaji wa umeme unaendelea vizuri pamoja na changamoto
mbalimbali zilizojitokeza katika eneo la Mbagala na Vijibweni na
kusababisha kazi hiyo kuchelewa kukamilika.
Alisema vituo hivyo vilitakiwa kuwa
tayari mwezi ujao lakini kutokana na changamoto hizo sasa vitakamilika
mwishoni mwa mwaka huu na kwamba kituo cha Kinyelezi na City Centre
vinategemewa kukamilika Agosti, mwaka huu.
NIPASHE
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa
Morogoro Imemkuta na makosa mawili ya uchochezi ya kujibu Katibu wa
Jumuiya na Taasisi za Kislamu Tanzania, Shekh Ponda Issa Ponda.
Kutokana na hali hiyo, Agosti 7, mwaka huu, imepanga kuanza kusikiliza utetezi wake.
Sheikh Ponda atajitetea dhidi ya makosa mawili kati ya matatu yaliyokuwa yakimkabili.
Hakimu wa Mahakama hiyo, Mary Moyo,
alisema baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka, Mahakama
imemuona mshtakiwa huyo ana kesi ya kujibu katika shtaka la pili na la
tatu.
Alisema katika kosa la kwanza mahakama
hiyo imeona Ponda ana kesi ya kujibu kwa kuwa shtaka hilo lilitolewa
uamuzi na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam baada ya kutupa ombi lake
la kufutiwa kesi hiyo hivi karibuni.
Alisema maamuzi yanayotolewa na Mahakama za juu hayawezi kupingwa na mahakama za chini yake.
Alisema mahakama hiyo imeridhika na
ushaidi wa upande wa mashtaka ambao ulipeleka mashahidi, mkanda wa video
uliorekodiwa katika eneo aambako mshtakiwa huyo alidaiwa kutoa maneno
ya uchochezi na nyaraka mbalimbali.
Wakili wa upande huo wa utetezi, Juma
Nassoro, alikubaliana na uamuzi wa mahakama hiyo na kuahidi kuwasilisha
mashahidi siku hiyo.
Kwa upande wa mashtaka ukiongozwa na
Wakili Sunday Hyera, uliiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine ya
kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa utetezi kwa madai kuwa Wakili
Kiongozi wa Serikali, Bernard Kongola hakuwapo mahakamani kutokana na
dharura.
Ponda alifikishwa kwa mara ya kwanza
mahakamani hapo Agosti 18, mwaka juzi na kusomewa mashtaka hayo matatu
na Wakili Kiongozi wa Serikali, Bernard Kongola.
Kongola alidai kuwa Agosti 10, mwaka
2013 alitoa maneno ya uchochezi katika eneo la Kiwanja cha Ndege
Manispaa ya Morogoro kwa kuwaambia Waislamu wasikubali kuunda kwa kamati
za ulinzi na usalama za misikiti kwa kuwa zimeundwa na Baraza Kuu la
Waislamu Tanzania (Bakwata) ambao ni vibakara wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na serikali.
Aliendelea kudai kuwa Ponda aliwaambia
Waislamu hao kuwa kama watajitokeza watu hao na kujitambulisha ni kamati
za ulinzi na usalama za misikiti, wafunge milango na madirisha ya
msikiti na kuwashambulia kwa kipigo.
Alidai mshtakiwa huyo pia alikiuka amri
ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya Mei 9, mwaka 2013 ya kumtaka
kuhubiri amani ndani ya mwaka mmoja wakati akitumikia kifungo cha
mwaka mmoja nje.
Alidai Agosti 10, mwaka juzi katika
eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro, Sheikh Ponda aliwaambia
Waislamu kuwa serikali ilipeleka jeshi mkoani Mtwara kudhibiti vurugu
zilizotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa
sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu, lakini haikufanya hivyo
kwa Loliondo walipokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji
kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo.
Alidai maneno hayo ni ya uchochezi kwa sababu yalikuwa yakiumiza imani za watu wengine kinyume cha sheria.
NIPASHE
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema atafuta umiliki kwa maeneo nchini ambayo yametekelezwa kwa zaidi ya miaka 10 bila ya kuendelezwa.
Lukuvi alitangaza mpango huo katika
Kijiji cha Tungamalenga kilichopo Wilaya ya Iringa mkoani hapa,
alikokwenda kusikiliza mgogoro wa ardhi baina ya wananchi, wawekezaji ,
wafugaji na wakulima.
Alisema ametoa agizo hilo nchi nzima kwa
watu walionunua ardhi za vijiji zaidi ya hekari 50 na kushindwa
kuziendeleza hivyo kugeuka mapori.
Alisema amewaagiza maofisa wa ardhi wa
halmashauri na wizara yake kufuatilia ili kujua watu hao wamenunua ardhi
hiyo kwa malengo yapi, lini na wameendeleza kwa kiasi gani hadi sasa.
Lukuvi ambaye pia ni Mbunge wa Ismani
anayemaliza muda wake, alisema kabla ya kufuta umiliki wa maeneo hayo,
maofisa hao watatakiwa kuwapa notisi wamiliki waliyoshindwa
kuyaendeleza.
“Kazi
ya kuweka akiba ya ardhi haiwezi kuwa kazi yenu ninyi lakini
haiwezekani ukatoka jijini Dar es Salaam ukanunua ekari 100 Tungamalenga
ukasema unajiwekea akiba ya miaka 20 ijayo mimi sitakubali, “ alisema na kusisitiza kuwa:
“Serikali ya kijiji lazima iwe na akiba
ya ardhi kwa vizazi vijavyo na sisi kama serikali kuu lazima tuwe na
akiba ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa kitaifa.
Akijibu malalamiko ya wakazi wa kijiji
hicho, Lukuvi aliwaagiza maofisa Ardhi wa Halmashauri ya wilaya hiyo
kwenda kutoa ufafanuzi wa eneo ambalo limepangwa na serikali kuu na
lililoachwa kama akiba ya kijiji.
Kwa upande mwingine aliwaonya viongozi wa vijiji wasiuze ardhi yote kwa wawekezaji ili kudonoa migogoro kwenye maeneo yao.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment