Wednesday, July 22, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO, JULY 22 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kitaaluma na kielimu. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746

News Microphone Computer Online Podcast
MWANANCHI
Baada ya vuta vikuvute ya muda mrefu, hatimaye leo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinatarajia kumtangaza mgombea wake wa urais katika mkutano maalumu utakaofanyika jijini Mwanza.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na viongozi wa chama hicho Kanda ya Ziwa Magharibi na makao makuu zilisema kuwa leo mgombea huyo atatangazwa mkoani hapa huku zikibainisha kuwa anayepewa nafasi kubwa ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa.
Taarifa hizo zimekuja wakati kukiwa na tetesi kuwa chama hicho kilikuwa kinafanya mazungumzo na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyekuwa anawania urais kupitia CCM na kutemwa katika hatua za awali, huku vyanzo mbalimbali vikisema mazungumzo hayo yanachukua muda mrefu na kuna uwezekano mkubwa wa kutozaa matunda.
Jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe pamoja na baadhi ya wabunge walikaririwa wakitoa matamko ya kumkaribisha Lowassa kuingia Chadema lakini kwa sharti la kufuata kanuni na taratibu za chama hicho, lakini Dk Slaa alisita kumzungumzia kiongozi huyo akiahidi kuzungumza mambo yatakapokuwa sawa.
Mratibu wa Operesheni za Chadema Kanda ya Ziwa Magharibi, Tungaraza Njugu alisema mgombea huyo (bila kumtaja jina), atatangazwa katika mkutano wa hadhara utakaofanyika kwenye Viwanja vya Magomeni, Ilemela kuanzia saa nane mchana.
Njugu alisema katika mkutano huo, viongozi wakuu wa Ukawa wanatarajia kuwapo na maandalizi yake yamekamilika.
“Kesho (leo) tutakuwa na mkutano mkubwa kwenye viwanja vya Magomeni,” alisema Njugu na kuongeza: “Mgombea urais kupitia Ukawa atajulikana hapo, kwani tunatarajia viongozi wakuu wa Ukawa watamtangaza.”
Katika mazingira tofauti, akihutubia mkutano wa hadhara mjini Geita juzi, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alidokeza jina la Dk Slaa kama mgombea urais wa chama hicho, kitendo kilichoibua hamasa na umati kumshangilia, lakini akawapoza akisema ulimi umeteleza.
Alipoulizwa kuhusu mkutano huo, Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alikiri kuwa leo kulikuwa na mpango wa kumtangaza mgombea wa Ukawa, lakini alidhani ingekuwa Dar es Salaam, hivyo kwa kuwa wameamua iwe Mwanza angefanya utaratibu wa ndege ili aweze kuwahi.
Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia hakupatikana kuzungumzia mkutano huo, lakini Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosena Nyambabe alisema hakuwa na taarifa hizo, hasa kwa kuwa vikao vya mwisho vilivyofanyika Jumapili na Jumatatu vilihusisha wenyeviti wa vyama pekee.
Hata hivyo, alisema ilibidi mgombea huyo atangazwe ama jana au leo. Chama cha CUF kimekwishatangaza kuwa kinasubiri uamuzi wa kikao cha Baraza Kuu la Uongozi litakaloketi Julai 25 kuamua juu ya hatima yake ndani ya Ukawa.
Alipotakiwa kudokeza ni nani atasimama kuwakilisha Ukawa, Njugu alisema jukumu hilo ni la viongozi wa juu na kwamba yeye akiwa kiongozi wa Kanda anatambua mgombea urais wa Ukawa atatangaziwa Mwanza leo.
MWANANCHI
Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa amemrushia kombora kada mkongwe wa chama hicho, Kingunge Ngombale-Mwiru kuwa, hazijui vyema kanuni zinazoongoza mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala.
Huku akinukuu Kanuni za Usalama na Maadili, toleo la mwaka 2012, Msekwa alisema ilitumika ili kupambana na siasa zinazoendeshwa kwa nguvu ya fedha na kuwachuja wagombea ili kupata walio waadilifu.
Kauli ya Msekwa ni mwendelezo wa madai ya Kingunge aliyeitupia lawama CCM kuwa haikutenda haki katika mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM.
Katika mchakato huo, Dk John Magufuli alichaguliwa kuwa mgombea urais akiwashinda Asha-Rose Migiro na Balozi Amina Salum Ali.
Kingunge aliyejitoa kindakindaki kumpigania Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amekuwa akitoa matamko mbalimbali kuhusiana na mchakato huo na zaidi akisema haukutenda haki.
Amekuwa akikaririwa akisema wagombea wote 38 waliojitokeza walitakiwa kuhojiwa na Kamati Kuu, kisha wachujwe na kubaki watano na kupinga kitendo cha Kamati ya Usalama na Maadili kufanya kazi ya kuwachuja wagombea.
Msekwa ni mmoja wa viongozi wa zamani waliotoa mapendekezo yaliyokuwa msingi wa CCM kupata mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu
Msekwa alinukuu vifungu vinavyoeleza majukumu ya Kamati ya Usalama na Maadili na chama hicho, kusisitiza kuwa wanaolalamikia mchakato huo, ama hawajazipitia kanuni hizo au hawazijui.
“Mzee Ngombale amezua madai kwamba eti mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM ulikuwa ni batili, kwa sababu eti ulikiuka kanuni za chama. Madai hayo yamepotosha kabisa ukweli wa jambo hilo. Kwani ukweli wenyewe ni kwamba kanuni za CCM zinazohusika zilifuatwa kwa ukamilifu. Kanuni hizo zilizotumika zinaitwa Kanuni za Usalama na Maadili, toleo la mwaka 2012. Pengine tatizo la mzee huyo ni kwamba hajazipata vizuri.”
Alisema: “Kwa mujibu wa Kanuni namba 3(3)(vii); Kamati ya Usalama na Maadili itachambua kwa makini ubora wa wanachama wanaoomba uongozi, kabla vikao vinavyohusika havijatoa idhini ya kuwaruhusu wateuliwe kugombea uongozi wanaouomba.”
“Kanuni hii ndiyo inaipatia uwezo Kamati ya Usalama na Maadili kufanya uchambuzi wa maadili ya wagombea wote kabla majina yao hayajapelekwa kwenye vikao ninavyofuata vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa.”
Alisema utaratibu uliowekwa na kanuni hiyo ulifuatwa kwa ukamilifu, kusisitiza kuwa haukuwa batili kama inavyodaiwa.
Akizungumzia lengo la kutoa kipaumbele cha kwanza kwa suala la maadili ya viongozi alisema: “Ni vyema ieleweke kwamba kanuni hii ilikusudiwa kupambana na ukosefu wa maadili ya viongozi ambao ni wanachama wa CCM na hususan kupambana na tatizo kubwa la ujio wa money-driven politics (siasa zinazoendeshwa kwa nguvu ya fedha).”
Alisema tatizo la siasa zinazoendeshwa kwa fedha lilijitokeza kwa nguvu wakati wa mchakato wa kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka huu.
MTANZANIA
Vituko vimeanza katika kampeni za kuwania kuteuliwa na CCM kugombea nafasi za Ubunge katika majimbo mbalimbali nchini.
Moja ya vituko hivyo ni kile kilichotolewa na Mbunge wa Dodoma Mjini anayemaliza muda wake Dk.David Mallole ambaye jana wakati akijinadi kwa wanachamawa chama hicho, aliwaomba wamteuwe kwa mara nyingine kwa sababu amesoma darasa moja na mgombea Urais John Magufuli.
Wakati hayo yakijiri Dodoma, Jimbo la Kinondoni msanii Steve Nyerere aliomba achaguliwe kwani ana uwezo wa kupita katika ofisi za mabalozi wa nje waliopo jijini Dar es salaam kuomba misaada.
Kampeni hizo zilianza jana wakati Dar wakati wagombea wakijinadi mbele ya wajumbe kabla ya kupiga kura ya maoni Agosti mosi mwaka huu.
“Wilaya ya Kinondoni ndio inayoongoza kwa kuwa na ofisi nyingi za mabalozi, mkinichagua nitahakikisha nakwenda wenye Ubalozi wa Marekani kuomba misaada kwa ajili ya kuwawezesha vijana…Nitakwenda Ubalozi wa China kuomba atusaidie kuondoa mafuriko yanayolijumba jimbo hili “Steve Nyerere.
Katibu wa CCM,Kinindoni alisema katika Wilaya yake kuna wagombea 60 ambao kati yao wanawake wanne wanawania majimbo ya Kinondoni,Kawe, Ubungo na Kibamba.
NIPASHE
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mkoa wa Dodoma, Mariam Mfaki, alifariki dunia jana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Mtoto wa marehemu, Mohamed Mfaki, alisema mama yake alifariki majira ya saa sita mchana.
Alisema mama yake mpaka kufikwa na mauti hayo alikuwa anasumbuliwa na saratani ya utumbo.
“Alianza kuugua tangu mwaka 2012 vidonda vya tumbo, baadaye utumbo ulipata tatizo lililosababisha saratani ya mapafu na utumbo, baada ya kuendelea na matibabu hayo akapata pia ugonjwa wa moyo,” alisema.
Mohamed alisema marehemu alianza kutibiwa katika Hospitali ya Apollo nchini India mwaka 2012 mpaka mwaka 2014 huku akiwa anaendelea na shughuli zake ikiwamo kuhudhuria vikao vya Bunge.
“Marehemu alizidiwa usiku wa Julai 19 mwaka huu na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya matibabu, ilipofika jana majira ya saa tano asubuhi hali ilibadilika hatimaye saa sita mchana akaaga dunia,” alisema.
Alisema taratibu za mazishi zinaendelea na kwamba wao kama familia wamepanga mazishi yafanyike leo saa 10 jioni shambani kwake maeneo ya Miyuji, Manispaa ya Dodoma.
Alipoulizwa kama ofisi ya Bunge ina taarifa za msiba huo, alisema taarifa wanazo na tayari baadhi ya maofisa walifika nyumbani kwa marehemu Area E.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Ezekiel Mpuya, alithibitisha kutokea kifo hicho na kwamba kilitokea majira ya saa tano asubuhi.
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah, alipotafutwa kwa njia ya simu kuelezea kifo hicho cha Mbunge, simu yake haikupokelewa.
Marehemu alikuwa Mbunge wa Viti Maalum kwa vipindi vitatu kuanzia mwaka 2000 hadi Bunge lilipovunjwa Julai 9, mwaka huu.
Kabla ya kuwa mbunge, alikuwa Afisa Tarafa kwa zaidi ya miaka 20 katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Dodoma. Ameacha mume, watoto sita na wajukuu 10.
NIPASHE
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), leo inatarajia kuanza uandikishaji wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa Teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR) katika Jiji la  Dar es Salaam, huku kukiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu idadi ya mashine zitakazotumika kwa kila kituo.
Hadi jana majira ya mchana, baadhi ya ofisi za kata za Manispaa za Temeke, Ilala za jiji hilo zilikuwa bado hazijapelekewa mashine hizo, isipokuwa Ubungo, katika Manispaa ya Kinondoni ilikuwa na  takriban BVR 14.
Manispaa  ilieleza kuwa  kila kituo kitakuwa na BVR moja, tofauti na maelezo ya awali yaliyotolewa na Nec, kwamba kila kimoja kingekuwa na mashine  mbili.
Katika Ofisi za Manispaa ya Kinondoni, pilikapilika za watu, wakiwamo maofisa watendaji wa Kata, waliofika katika ofisi hizo kufuata mashine hizo.
Ofisa Uchaguzi wa Manispaa hiyo, Valence Urassa, alisema mashine 706 zilikuwa zimepokelewa katika ofisi hizo hadi majira ya jioni.
Kwa mujibu wa Valence, manispaa hiyo ina vituo vya kuandikishia wananchi 706 na kila kituo kimoja kitakuwa na BVR moja.
Ofisa Mwandikishaji Msaidizi wa Manispaa ya Temeke, Waziri Kombo, alisema BVR zote 572 zilikuwa zimepokelewa kwa ajili ya kusambazwa leo asubuhi kwenye vituo 572  na kwamba kila kituo kitakabidhiwa mashine moja.
Ofisa Uchaguzi wa Manispaa ya Ilala,  Baina Hilary, alisema mashine zilizopelekwa katika ofisi yao  zilikuwa 396 ambazo ni sawa na idadi ya vituo vya kuandikishia wananchi katika daftari hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Nec, Julius Malaba, alisema mashine zilizoagizwa kwa ajili ya uandikishaji nchi nzima zipo 8, 000 na zinazotarajiwa kutumiwa kwa Dar es Salaam ni zaidi ya 3,000.
“Hakuna utakakokwenda utakuta BVR mbili… hiyo ni minimum. Eneo linaweza kuwa na vituo zaidi na idadi ya BVR inaweza kuwa vinne, 13 kulingana na eneo.  Siyo kwamba foleni hazitakuwapo lakini tumejiandaa na tutaendelea kuongeza BVR katika eneo lenye tatizo,” alisisitiza.
NIPASHE
Mchakato wa uteuzi wa wagombea ubunge kupitia viti maalum katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) unadaiwa kutawaliwa na hongo.
Habari kutoka vyanzo vyetu mbalimbali ndani ya CCM na Jumuiya zake zinaeleza kuwa kuna baadhi ya vigogo wakiwamo wabunge wanaoshikilia nafasi hizo ambao wanamwaga kiasi kikubwa cha fedha kuwahonga wajumbe wa vikao mbalimbali kuanzia kata, wilaya na mikoa watakaopiga kura.
Mbali na kumwaga kiasi kikubwa cha fedha kwa wajumbe, pia wanadaiwa kuwahonga watendaji ambao wanawatumia kuwaandalia mikutano isiyo rasmi kwa ajili ya kukutana na wapigakura.
Malalamiko mengi ya kumwagwa hongo kwa ajili ya kupata viti maalum yanauhusu Mkoa wa Dar es Salaam ambao vigogo kadhaa wamejitosa kwa ajili ya kusaka nafasi hizo.
Vigogo watatu wanaowania nafasi hizo ndio wanaolalamikiwa zaidi kwa kufuru ya hongo.
Chanzo kimoja kimeeleza kuwa kuna kigogo mmoja mwenye ukwasi mkubwa ambaye anakata dau kubwa kuwashawishi wapigakura na kwamba kwa sasa anatoa hadi Sh. 200,000 kwa kila mjumbe.
Yaani nakwambia sasa hivi napiga raundi ya tatu mkoani. Kuna wajumbe kama 300 hivi, kila mmoja mara ya kwanza aliwapoa Sh. 150,000, lakini juzi hapa baada ya Bunge kuvunjwa ameibuka na anatembeza Sh. 200,000,
Mwanachama huyo aliyeomba kutokutajwa jina lake kwa sababu za kiusalama, alisema kuwa kwa mwelekeo wa sasa ndani ya CCM ni miujiza kama mtu hana fedha za hongo, kuchaguliwa.
Yaani ukifika kwenye ofisa za kata kama hujatoa fedha, hakuna anayekusikiliza. Akija aliyetoa fedha utashangaa anavyoshangiliwa. Jamani CCM imefika hapa kweli,” alilalamika.
JAMBOLEO
Mbunge wa Kasulu Mjini ,Moses Machali amekihama rasmi chama hicho na kujiunga na ACT – Wazalendo huku akiwaeleza wananchi waliofika kumsikiliza katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kiganamo mjini hapa kuwa hatasita kuachana na chama chake kipya endapo kitaonekana kinatetea mafisadi na viongozi wanaokandamiza demokrasia.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa kadi na kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe, Naibu Katibu Mkuu huyo wa NCCR – Mageuzi alisema amejiunga baada ya viongozi wa chama hicho kumhujumu katika harakati zake za kutetea masilahi ya Halmashauri ya Wilaya Kasulu.
“Nilijiunga na NCCR-Mageuzi nikitokea Chadema mwaka 2010 na wananchi mkanichagua kuwa mbunge wa Kasulu Mjini ili tushirikiane kupigania haki na maendeleo ya Kasulu, lakini kwa muda mrefu nimekuwa nazushiwa maneno kwamba mimi ni mkorofi na ndiyo maana sielewani na wataalamu pale halmashauri, lakini vita yangu ilichochewa na kuchukia kwangu rushwa na ufisadi, mambo ambayo kuna wenzetu kule NCCR wanashiriki kuyafanya,” alisema.
Alisema: “Nilifukuzwa bungeni pamoja na wabunge wengine watano wa upinzani kwa vile tulikuwa tunapinga kitendo cha Serikali kuleta miswada muhimu kwa hati ya dharura. Kama Spika, Anne Makinda mwenyewe alikuwa anaogopa muziki wangu, hawa watendaji wa Halmashauri wataniweza? Alitamba Machali.
Mbunge huyo alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake kueleza namna baadhi ya viongozi wa NCCR walivyokuwa wakitumika kuhujumu miradi ya maendeleo, akimtaja mmoja wa madiwani wa Kasulu kama chanzo cha matatizo ndani ya chama hicho.
Zitto licha ya kuwataka wananchi wa Kasulu kujiunga na chama hicho, alisema Machali alishajiunga nao muda mrefu na kwamba alichokuwa anasubiri ni kukabidhiwa kadi. “Tulisema lazima tupate baadhi ya wabunge na viongozi maarufu kutoka vyama vingine, sasa tumeanza na Machali na wengine watafuata,” Zitto.
Viongozi wengine waliojiunga na chama hicho jana ni pamoja na kada wa CCM, Emmanuel Mbwiliza aliyewahi kuwa Diwani wa Kata ya Nyumbigwa hadi mwaka 2010 pia akiwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kuanzia 2007 hadi 2012.
Katika mkutano huo pia viongozi wengine wa NCCR kutoka Kasulu Mjini na Kasulu Vijijini walijiunga na ACT huku wakiahidi kupambana kuhakikisha wanashinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment