Wednesday, May 25, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU YA 2

HADITHI

SIMULIZI A FAKI A FAKI 0713 340572 0655 340572

MWANAMKE 2

ILIPOISHIA

Hapo hapo taa zikazimwa na filamu ya Dosti ikaanza. Ile filamu ilikuwa ikizungumzia marafiki wawili, mmoja kipofu na mwingine mlemavu wa miguu. Ilikuwa filamu nzuri na ya kusikitisha sana. Ilikuwa na nyimbo nne. Nyimbo tatu ziliimbwa na muimbaji maarufu wa India Mohamed Rafiy ambaye kwa sasa ni marehemu na moja iliimbwa na Usha Mangesh ambaye ni dada wa Lata Mangesh.

Sinema ilipomalizika tuliinuka kwenye viti na kutoka. Kwa vile kulikuwa na watu wengi, nilipotoka sikumuona tena yule msichana, nikaenda kuchukua pikipiki yangu nikaiwasha na kuondoka.

Kutoka Majestic Cinema nilishika barabara ya Eckenford hadi bustani ya Uhuru ambapo nilikata kushoto na kushika barabara ya Pangani. Wakati nalivuka eneo la Tangamano niliona mtu akinipungia mkono mbele yangu. Alikuwa mwanamke na nilihisi alikuwa anataka kuniomba lifti.

Kusema kweli muda ule wa usiku nilikuwa sipakii mtu nisiyemfahamu hata kama ni mwanamke. Kwa hiyo nilitaka kumpita lakini pikipiki ikazimika moto ghalfa. Mwanamke huyo akaona nilisimama kwa ajili yake, akanifuata.

Alipofika karibu yangu nikaona alikuwa ni yule msichana niliyekuwa naye sinema. Nikajiuliza alifikaje pale wakati nilimuacha kule Majestic?

SASA ENDELEA

Nilipomuona nikatabasamu.

“Ni wewe kumbe?” nikamuuliza.

“Ni mimi, naomba unisaidie lifti”

“Unaishi wapi?” nikamuuliza.

Kabla hajanijibu alikuwa ameshakaa nyuma yangu.

“Unaishi wapi?” nikamuuliza tena.

“Mikanjuni” akanijibu.

Nikaguna lakini bila kutoa sauti. Eneo alilolitaja, wakati huo lilikuwa kama pori la miti ya mikanju. Viwanja vilikuwa vikipimwa sasa na kama kulikuwa na nyumba zilikuwa chache na za kienyeji. Kwenda huko usiku ule ilikuwa ni hatari.

Lakini msichana alikuwa ameshakaa nyuma yangu akijisogeza upande wangu ili akae vizuri.

Nikajikuta nikipiga kiki ya pikipiki ili kuiwasha kwani pikipiki ilikuwa imezima moto. Pikipiki ikawaka, nikatia gea ya kwanza ya kuondokea  na kuondoka.

Msichana aliupitisha mkono wake kwenye tumbo langu ili kujizua. Mkono huo uliniletea changamoto na hisia toauti kwenye akili yangu.

“Kama unakaa Mikanjuni kwanini unakwenda sinema za usiku?” nikamuuliza.

“Nimeshazoea” akanijibu. Kidogo aliliminya tumbo langu, pengine ni kwa bahati mbaya, nikashituka.

“Mbona unashituka?” akaniuliza.

“Nilikuwa najiweka sawa”

“Mh!” Msichana akaguna. Sikujua ni kwanini aliguna.

“Ulitegemea ungerudi  nyumbani kwa usafiri gani usiku huu?” nikamuuliza.

“Ninaomba lifti tu kwa watu”

“Ukikosa lifti unakwenda kwa miguu?”

“Naweza kukodi teksi lakini sijawahi kukosa lifti hata siku moja”

Baada ya hapo tukabaki kimya.

Nilikwenda hadi Duga  kisha nikakata kushoto na kushika barabara ya kuelekea Mikanjuni. Hapo ndipo nilipoanza kupita kwenye eneo la vichaka na miti ya mikanju.

Tulipoingia katika eneo la Mikanjuni nikamuuliza.

“Unaishi sehemu gani?”

“Twende tu, nitakuonesha” akaniambia.

“Una maana hatujafika bado?”

“Bado”

Nikaendelea kwenda mbele. Laiti angekuwa mwanaume mwenzangu, ningemshusha hapo hapo nikarudi kwa hofu ya kutaka kunipora pikipiki.

Sasa tulikuwa tunaingia kwenye pori kamili. Kulikuwa na nyumba moja moja tena zikiwa mbali mbali na hazina taa za umeme . Sehemu nyingi vilikuwa ni viwanja vitupu.

“Simama hapa hapa” Msichana akaniambia tulipokuwa tunaupita mti wa muwembe.

Nikasimamisha pikipki. Msichana akashuka.

“Asante sana kaka” akaniambia.

“Unaishi wapi?” nikamuuliza kwa sababu sikuona nyumba karibu.

“Naishi mtaa wa pili” akaniambia. Mtaa huo pia sikuuona lakini nilimkubalia ili niwahi kurudi.

“Uende salama, mimi nakwenda zangu” nikamwambia huku nikiigeuza pikipiki.

Nikamuona msichana akichapuka kuelekea mtaa huo aliosema. Nikatia gea kwa nguvu na kuingia gea ya pili  na kuondoka.

Wakati narudi nilimsikitikia sana msichana yule, alikuwa anaishi pembeni sana na katika mazingira ambayo hayakulingana naye.

Nilipotokea kwenye barabara ya Duga nilikata kulia nikarudi nyumbani kwangu.

Nilifungua mlango nikaingiza pikipiki yangu ukumbini kisha nikaingia chumbani kwangu. Nilivua nguo nikajifunga taulo na kwenda bafuni.

Nilijimwagia maji ya baridi ili kuuosha mwili wangu ulikuwa umetota kwa jasho. Nilipotosheka nilirudi chumbani kwangu na kujiandaa kulala.

Asubuhi kulipokucha nilitoka kwenda kazini kwangu. Baada ya kama wiki moja hivi nilikutana tena na yule msichana. Nilikuwa nimekwenda katika duka moja la vitabu kununua kitabu cha “Mashimo saba ya Mfalme Suleyman”

Mara nyingi niwapo nyumbani hupenda kujisomea vitabu vya hadithi. Katika orodha yangu ya vitabu kitabu hicho hakikuwemo hivyo nikataka nikinunue ili niwe nacho.

Kabla sijaingia kwenye duka hilo nilikiona kitabu hicho kwenye safu ya vitabu vilivyokuwa kwenye kioo. Nilipoingia humo dukani nilimwambia muuzaji kuwa nataka kitabu cha Mashimo Saba ya Malme Suleiman.

“Vimekwisha” akaniambia.

“Kipo kimoja, nimekiona kwenye kioo” nikamwambia.

“Umekiona?” akaniuliza.

“Ndiyo nimekiona”

“Njoja nitazame”

Muuzaji huyo alizunguka nyuma ya kioo akakiona kitabu hicho.

“Ni kweli kipo, kilibaki kimoja tu” akaniambia huku akikifuta vumbi na kunipa.

“Bei gani?”

Akanitajia bei yake nikatoa pesa na kumlipa.

Wakati ninatoka nje ya duka nikakutana na msichana aliyekuwa akiingia dukani humo. Akanishitua aliponiambia.

“Kaka habari ya tangu siku ile?”

Nikaangaza macho yangu kumtazama. Nikamkumbuka. Alikuwa ni yule msichana niliyekutana naye sinema siku ile.

“Oh nzuri! Hujambo?” nilijibu salamu yake.

“Sijambo. Leo tumekutana tena”

“Imekuwa kama bahati. Nilikuwa natoka kununua kitabu”

“Mimi pia nimekuja kununua kitabu. Nilikuwa nahitaji kitabu cha “Mashimo Saba ya Malme Suleiman”

“Vimeisha. Kilikuwa kimebaki kimoja tu nilichonunua mimi” nikamwambia.

“Kumbe wewe pia ulikuja kununua kitabu hicho hicho?”

“Nilikuja kununua kitabu hicho”

Nikakitoa kile kitabu na kumuonesha.

Akakishika na kukitazama.

“Una umuhimu nacho sana kwa leo na kesho?” akaniuliza.

“Ni kwa ajili ya kujisomea tu”

“Basi naomba uniazime kwa siku mbili tu halafu nitakurudishia”

Sikuwa na sababu yoyote ya kukataa. Nilihisi yule msichana alikuwa akikihitaji zaidi.

“Nitakuazima, sasa sijui nitakipata vipi?”

NAAM. MAMBO YANAZIDI KUKOLEA UTAMU. JE NINI KITATOKEA? ENDELEA KUITUPIA MACHO BLOG HII kesho hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment