Monday, May 23, 2016

SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA (MWISHO)

Simulizi za faki a faki 0655 340572

SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA 23

ILIPOISHIA

Nikamdokeza kuwa yule bibi aliyekuja dukani alikuwa ndiye kiongozi wa wachawi hao.

“Kama ile hirizi ungeichanganya na pesa zako, pesa zako zote zingeyayuka na zingekwenda kwa yule bibi” nikamwambia.

Hapo nilimuona yule mwarabu akitikisa kichwa kusikitika.

“Sasa Jana usiku ndio tulifika kwako tukiwa katika maumbile ya paka. Wewe uliponiona ukaniapiza na kweli maapizo yako yakafanya nishindwe kujibadili na kuwa binaadamu.

“Mke wangu alinitesa sana. Alinitia kwenye kapu na kwenda kunitupa. Nikajitahidi kurudi nyumbani. Aliponiona tena alinifungia chumbani na kuhama nyumba. Nilitoka kwa kupanda juu nikaenda kumtafuta.

“Nikamkuta katika nyumba moja akiongea na rafiki yake. Alikuwa akimueleza kuwa yeye ndiye aliyemuua mke wangu wa kwanza kwa kumchoma  kisu ili mimi niende nikamuoe yeye. Jambo hilo lilinishangaza sana. Basi nikamrukia na kumtoboa jicho kisha nikakimbia na ndio nikafika hapa kwako” Nikamaliza kumuelezea yule muarabu mkasa huo.
 
SASA ENDELEA

Mke wake na mwanawe waliokuwa wamekimbia walikuwa wamesogea karibu na kunisikiliza.

Mwarabu baada ya kukisikia kisa changu alitaharuki sana akaniambia.

“Huyo mke wako ni mtu mbaya sana. Sasa umesharudi katika umbile lako la kibinaadamu utamchukulia hatua gani?”

“Nataka niende polisi Handeni nikatoe ripoti kuwa yeye ndiye aliyemuua mke wangu”

“Kwa vile hiki kisa kimenigusa sana, mimi niko tayari kukupatia nguo na kukusindikiza hadi Handeni uende ukamripoti mke wako”

Dakika chache baadaye mimi na mwarabu huyo tukawa kwenye basi linalokwenda Handeni. Alikuwa amenipa shati na suruali.

Tulipofika Handeni tulikwenda kituo cha polisi.

Polisi walipotuuliza tuna shida gani, niliwaeleza kuhusu lile tukio la mauaji  ya mke wangu wa kwanza ambalo lilitokea karibu miaka miwili iliyopita.

Kwa vile niliwatajia jina la marehemu, tarehe, mwezi na mwaka aliouawa, mara moja walilipata faili lake. Baada ya kulisoma faili hilo polisi hao waliniambia.

“Mtuhumiwa ni mume wake na tunaendelea kumtafuta”

“Mume wake nilikuwa mimi. Marehemu aliuawa na msichana anayeitwa Chausiku” nikawambia.

“Wewe ndiye uliyekuwa mume wake?” Polisi mmoja akaniuliza kwa kutaharuki.

Kabla sijamjibu akaniambia “Wewe ndiye tuliyekuwa tunakutafuta!”

Mwarabu kusikia hivyo aliingilia kati akawaeleza polisi jinsi tukio
hilo lilivyotokea.

“Tuna sampuli za alama za vidole tulizozipata kwenye kisu kilichotumika katika mauaji. Tutachukua alama zako sasa hivi” Polisi wakaniambia.

“Sawa chukueni tu”

“Hukugusa kile kisu?” Polisi mmoja akaniuliza.

“Hapana, sikukigusa”

Alama zangu za vidole zilichukuliwa na kwenda kulinganishwa na alama zilizokuwa zimehifadhiwa. Baada ya muda jibu lilikuja kwamba alama zangu sizo zilizokuwemo katika kisu kilichotumika kumuua marehemu.

 Hapo hapo polisi sita wakiwemo polisi wawili wamawake na mimi pamoja na Mwarabu tulipakiwa katika gari la polisi tukaenda kijijini kumkamata Chausiku.

Lakini Chausiku hakupatikana kijijini. Tuliambiwa kuwa alikuwa amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Handeni baada ya jicho lake moja kutobolewa na paka.

Paka mwenyewe nilikuwa mimi!

Tukarudi  tena Handeni hadi katika hospitali ya wilaya. Tulimkuta Chausiku amelazwa wodini, jicho lake moja likiwa limefungwa bendeji. Aliponiona na polisi alishangaa.

Polisi walichukua alama zake za vidole na kumuweka chini ya ulinzi wao.

Siku ile tulilala katika nyumba ya wageni Handeni. Asubuhi tulipokwenda kituo cha polisi tuliambiwa kuwa alama za vidole za Chausiku ndizo zilizokutwa katika kisu kilichomuua marehemu. Hivyo polisi walikuwa wanasubiri aruhusiwe kutoka hospitali wamfikishe mahakamani.

MWISHO

No comments:

Post a Comment