Friday, May 27, 2016

HADITHI MWANAMKE SEHEMU YA 4

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572

MWANAMKE 4

Ilipoishia

Nilikuwa nikilitupia macho lile jumba, nikataka kumuuliza alikuwa amepangisha chumba au alikuwa akiishi kwao. lakini nilishindwa kumuuliza ili asione ninayachunguza maisha yake.

“Nimepaona” nikamjibu.

“Karibu ndani” akaniambia.

“Asante”

“Karibu” Msichana akanisisitizia.

“Hapa panatosha” nikamwambia nikiwa nimekaa kwenye pikipiki yangu.

“Unataka uishie nje, si vizuri. Tuingie ndani. Ninaishi peke yangu tu usiogope”

“Unaishi peke yako humu ndani?” nikamuuliza.

“Nimejenga mwenyewe kutokana na biashara zangu na ninaishi mwenyewe. Msichana aliniambia huku akifungua geti.

“Karibu”

Kwa jinsi alivyokuwa akinibembeleza ilibidi nishuke kwenye pikipiki. Niliposhuka tu msichana aliishika pikipiki yangu akaikokokota na kuiingiza ndani, nikawa namfuata nyuma.

Tulipoingia ndani msichana aliiegesha pikipiki kando ya mti mkubwa uliokuwa umeota katika ua wa jumba hilo. Aliiacha pikipiki akaenda kufunga geti.

“Karibu” akaniambia huku akitangulia kwenda kwenye mlango wa kuingilia kwenye jumba hilo. Nikamfuata.

SASA ENDELEA

Alifungua mlango akanikaribisha tena, tukaingia ndani. Tulitokea kwenye sebule pana iliyokuwa na makochi ya chini chini ambayo hutumiwa zaidi na watu wenye asili  ya kiarabu. Ilikuwa sebule iliyonakishiwa na kupendeza.

“Karibu ukae” akaniambia.

Nikaa kaa kwenye kochi mojawapo.

“Nikuletee kinywaji gani, cha moto au cha baridi” akaniuliza.

“Hapana, sihitaji kinywaji chochote” nikamwambia.

Msichana akanitazama na kukunja uso kisha akaondoka hapo sebuleni. Nikajua kuwa amekwenda kunichukulia kitabu changu ili niondoke.

Baadaye kidogo akarudi. Alikuwa ameshika chano kilichokuwa na kijibiika kidogo na vikombe viwili vya kahawa. Chano hicho pia kilikuwa na kisahani kilichokuwa na tende.

Akakiweka chini mbele yangu.

Yeye mwenyewe alikuwa amevua baibui na kubaki na dera la mikono mirefu lililoziba kabisa miguu yake. Dera hilo lilikuwa limedariziwa nyuzi zilizokuwa zikimemeta kama hariri.

Pia alikuwa ameiondoa hijabu na badala yake alijitanda mtandio mwepesi uliokuwa unaonya. Uso wake uliweza kuonekana vizuri. Nywele zake ndefu za maboga kama za kiarabu zilikuwa zimefikia kwenye mabega yake.

“Karibu” akaniambia na kuongeza.

“Kunywa kahawa kidogo. Kahawa inachangamsha”

Sikupenda kuikataa ile takirima ingawa nilimwambia sikuhitaji kinywaji chochote.

Msichana akaketi chini karibu yangu akachukua kile kibirika na kunimiminia kahawa kisha akajimiminia na yeye.

Alichukua kikombe hicho akaionja kahawa kisha akakirudisha chini na kuokota tende moja na kuitia midomoni.

Na mimi niliokota tende kwanza, nikaitia midomoni kisha nikainua kikombe cha kahawa kusukumizia.

“Wewe una asili ya kiarabu?” nikamuuliza.

“Nimechanganya uarabu na uswahili”

‘Muarabu ni baba yako au mama yako?”

“Baba yangu ni muarabu wa Ajemi, mama yangu ndio amechanganya. Zamani tulikuwa tunaishi Zanzibar”

“Sasa wazazi wako wako wapi?” nikamuuliza baada ya kutoa kokwa ya tende mdomoni.

“Iweke hapo kwenye sinia” aliniambia akinionesha kile chano.

Nikaiweka ile kokwa kwenye chano hicho kisha nikaokota tende nyingine.

“Baba yangu yuko Zanzibar na mama yangu yuko Ajemi” akaniambia.

“Kwa hiyo wewe unaishi hapa peke yako?” nikamuuliza.

“Ninaishi peke yangu” Msichana akanikubalia kwa haraka.

“Uliniambia hii nyumba uliijenga mwenyewe kwa biashara zako, unashughulika na biashara gani?”

“Ninauza madini”

“Madini gani?”

“Madini ya kila aina”

“Unayapata wapi?”

“Baba yangu ananiletea kutoka Zanzibar”

“Yeye anayapata wapi?”

Msichana akabetua mabega yake.

“Sijui anayapata wapi”

“Ninavyojua mimi Zanzibar hakuna madini”

“Hayatoki Zanzibar, anayapata kutoka nje ya Zanzibar lakini sio Afrika ila mahali penyewe sipafahamu na hajawahi kuniambia”

“Ndiyo yamekuwezesha kujenga nyumba hii?”

“Ndiyo”

“Hongera sana. Sasa kwanini unaishi peke yako?”

“Sijapata mwenzangu wa kuishi naye”

Kahawa aliyonitilia kwenye kikombe nikaimaliza. Akataka kuniwekea nyingine, nikamwambia.

“Imetosha, asante sana”

“Ngoja nikakuchukulie kitabu chako” akaniambia huku akiinuka. Macho yangu yalimsindikiza hadi alipotoka mlangoni.

Kusema kweli baada ya msichana huyo kuondoka sikujua tena kilichotokea kwani usingizi ulinipitia hapo hapo bila kutarajia. Nikalala fofofo.

Nilipokuja kuzinduka nilijikuta nimekaa peke yangu mahali pale pale nilipokuwa. Kile chano cha kahawa na tende kilikuwa kimeondolewa. Kwa kutaka kujua ilikuwa ni saa ngapi nilitazama saa yangu ya mkononi, nikaona ilikuwa saa tisa kasorobo ya usiku.

Nikashituka sana kuona nilikuwa nimelala nyumbani kwa msichana huyo hadi muda huo. Nikataka kuinuka ili nimuite mwenyeji wangu ambaye sikujua alikuwa wapi.

Kabla ya kuinuka nikaisikia sauti yake ikitoke nje ya dirisha la kile chumba. Kisha nilisikia sauti nyingine ya kiume ikijibishana naye. Sauti ile ya kiume ikanishitua kwa sababu yule mwanamke aliniambia alikuwa akiishi peke yake mle ndani.

Nikapenua pazia nakuchungulia uani. Nikaiona pikipiki yangu niliyokuwa nimeiegesha kando ya mti. Mbele ya pikipiki niliona kitu kama kisima cha maji. Wakati tunaingia mle ndani kisima hicho sikukiona.

Maji yaliyokuwa kwenye kisima hicho yalikuwa mekundu kama damu na yalikuwa yakitoa harufu ya damu ya binaadamu mpaka nikahisi yalikuwa ni damu kweli.

Ndani ya kile kisima kulikuwa na watu wawili waliokuwa wakioga na ndio waliokuwa wakizungumza. Mmoja akatoka na kusimama kando ya kisima hicho. Mara moja nikatambua kuwa ni yule mwenyeji wangu lakini safari hii alikuwa na umbile la kutisha sana.

Kwanza nywele zake zilikuwa nyingi na ndefu zilizoteremka na kumfikia kiunoni. Zilikuwa nywele nyeupe kama mvi za bi kikongwe. Yeye mwenyewe ngozi yake ilibadilika na kuwa nyeupe kama ya mzungu. Macho yake yalikuwa ya kijivu na mboni zake zilikuwa nyembamba na zilizosimama kama mboni za paka.

Bado alikuwa ameota manyoya marefu mwili mzima. Nikagundua kwenye miguu yake hakuwa na vitanga vya miguu kama walivyo binaadamu wote bali alikuwa na kwato nyeusi kama za farasi au punda. Hakuwa amevaa chochote. Alikuwa uchi wa mnyama!

Mwenzake naye akatoka kwenye kisima. Yeye alikuwa mwanaume lakini alikuwa na umbile kama la yule msichana. Miguu yake pia ilikuwa na kwato.

Walikuwa wakizungumza kwa lugha ambayo sikuielewa. Kwa kweli nilishituka sana. Nikapata hofu na uoga mpaka mwili wangu ukawa unatetemeka.

Nikahisii kwamba yule msichana aliyenikarisha mle ndani hakuwa binaadamu bali alikuwa jini na pale alikuwa akizungumza na jini mwenzake.

Nikatengeza mawazo kwamba huenda msichana yule aliniingiza katika nyumba ile kwa hila ili wanidhuru kwani ile damu iliyokuwa kwenye kile kisima ilikuwa ni ya binaadamu kama mimi. Na bila shaka waliingizwa mle ndani na kuuawa kikatili.

Hapo ndipo nilipochanganyikiwa nikajua kwamba dakika zangu za kuishi zilikuwa zimekaribia kwisha.

HAYO NDIO MAMBO YA BlOG YA tangakumekucha. SASA KUMEKUCHA KWELI. Sijui jamaa atafanya nini? Kesho si mbali. Tuombe Mungu atuweke hai tukutane tena hapa hapa.

No comments:

Post a Comment