Wednesday, May 18, 2016

HADITHI SITASAHAU NILIVYOGEZUWA PAKA SEHEMU YA 18

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572

NILIVYOGEUZWA PAKA (18)

IPOISHIA

"Shikamoo bi Chaurembo" nikamuamkia na Chausiku naye akamuamkia

"Marahaba.Mmekuja kumuamkia bibi yenu?"

"Hayakuhusu bibi.Sema ulilonalo" bibi akamkatiza.

"Mh! ngoja nikae kwanza niseme niliyonayo niondoke, maana leo bibi yenu kawa mkali. Sijui mmemletea pesa!"

Bi Chaurembo aliketi kwenye kiti kilichokuwa pale ukumbini

"Nimekuja kukueleza wewe gunge kwa maana tukiona jambo ni lazima kwanza tuje tukueleze wewe.Una habari kwamba kuna duka jipya la mwaarabu limefunguliwa jana kijijini kwetu?"

"Sina habari.Liko wapi hilo duka?" bibi akamuuliza na kuwa na shauku ya kujua

"Liko jirani na ile shule. Nasikia yule mwaarabu alikuwa akikaa Songe. Huko pia ana duka lakini duka amemuachia mwanawe.Yeye amekuja kuingilia mji wetu bila taarifa.Nimepita leo nimeona duka limejaa khanga tele na kaniki."

"Usiniambie dadaa!" bibi akang'aka

"Utakwenda kuliona mwenyewe.Nataka leo katika pita pita zako uende ujifanye unauliza kitu"

"Utanipeleka wewe.Ukiondioka hapa twende mguu kwa mguu ukanioneshe hilo duka"

"Twende sasa hivi"

"Subiri wageni wangu waondoke twende"

" Kwanza sisi hatukai bibi, tunakwenda zetu.Nataka nikawahi kupika.Ikifika saa sita tu mume wangu anataka kula" mke wangu akamwaambia bibi

"Ehee!" bibi akatoa kicheko cha kajeli  "Si mume wako peke yako dada, ni mume wetu sote.Kama ikifika saa sita anataka kula, mimi nitampikia saa tano"

"Sasa nikuachie niende zangu"

"Kila mtu na zamu yake bibi.Zamu yangu nitakuja kuipanga mwenyewe.Atakula huku atalala huku lakini leo nendeni zenu.Tukutane huo usiku.Nataka niende nikaliangalie hilo duka la mwarabu"

SASA ENDELEA.

Mimi na Chausiku tukaondoka

"Yule bibi yako anachekesha sana.Ananitaka mimi ataniweza?" nikamwaambia Chausiku wakati tunaenda

"Si anakutania tu, kwani anakutaka kweli"

"Siku moja alinivulia nguo kabisa"

"Sasa ndiyo ungemjaribu uone kama anakuweza"

"Anatafuta mauti bure.........."

"Wazee wa zamani wale wamekula miti mingi.Siku moja aliniambia ana umri wa miaka mia moja.Ameshakata karne nzima na bado anaonekana ana nguvu"

"Ni mzee kweli lakini anaonekana katika usichana wake alikuwa hashikiki"

Chausiku akacheka halafu akanyamaza kimya

"Huko kwa mwarabu wanakokwenda kunawahusu nini?" nikamuuliza Chausiku

Chausiku akanitupia jicho kali kama vile hakufurahishwa na swali hilo

"Wenyewe wanajua" akanijibu kwa sauti ya chini halafu akayabadili yale mazungumzo,akaniambia  "Umeona leo umeweza kugeuka paka?"

"Ni kweli,nyinyi mnadawa kali sana "

"Bado kuna mambo mengi atakufundisha"

"Sasa nitaweza kujigeuza paka kila siku au ni leo tu?"

"Utaweza kujigeuza kila siku isipokuwa ufuate masharti.Wewe ni mbishi sana "

"Masharti gani?"

"Wewe hutaki kula nyama za watu mpaka ulazimishwe.Inatakiwa kwa mwezi ule hata mara moja na usiku utoke kama wenzako"

“Na ile dawa uliyonirambisha ilikuwa  ni ya  nini?”

“Ndiyo iliyokupa uwezo wa kujigeuza na ile unatakiwa uirambe kila wiki”

“Na nisiporamba kila wiki sitaweza kugeuka paka?”

“Hutaweza. Ni lazima urambe kila wiki”

Nikanyamaza.Nilichokuwa nikiwaza ni kuwa sikuwa na ulazima wa kuendelea kuramba dawa nisizo zielewa kwani sikupenda kuendelea na ile tabia ya kujigeuza paka

Nilitaka kujaribu tu na nimeona matokeo yake, imetosha. Lakini sikutaka kumwambia Chausiku mawazo yangu kwa sababu nilijua angechukia

Tulipofika nyumbani aliingia jikoni akapika chakula. Chakula kilipokuwa tayari tulikula kisha tukapunzika chumbani


Saa nane usiku Chausiku akaniamsha usingizini.Nilipoamka aliniambia  “Jiandae tutoke”

Usingizi ulikuwa umenikolea.Nilitamani nikatae lakini sikuweza.Nikajilazimisha kunyanyuka kitandani na kujiandaa kwa safari ya kwenda kiwanjani.

Tulipotoka nje akaniambia  “Sasa jigeuze paka twende”

“Wewe je?”

“Mimi pia nitajigeuza”

Nikatia nia ya kujigeuza paka na hapo hapo nikageuka paka.Chausiku aliponiona nimekuwa paka na yeye akajigeuza paka. Tukaenda zetu

Kabla hatujafika kiwanjani tulikutana na mlevi aliyekuwa anakuja upande wetu.Alikuwa akitembea huku akiyumba

Alipofika karibu yetu alisimama na kutuambia

“Nyinyi ndiyo wanga wenyewe.Bibi na bwana mnakwenda kuwanga!” akatuambia kama vile alikuwa anatujua

Hakuishia hapo, aliinama na kuokota jiwe ili atupige.Nikawaza kwamba kama jiwe lile litampata mmoja wetu kichwani ungekuwa ndio mwisho wake.Umezaliwa kama binaadamu  lakini unakufa kama paka!

Mlevi akaliinua juu lile jiwe. Chausiku aliyekuwa mbele yangu alinyanyuka kama ngedere. Akasimama kwa miguu miwili. Mkono mmoja akamnyooshea yule mtu na kumuambia.

“Wewe koma!”

Mlevi alipomuona paka amesimama kwa miguu miwili na akimsemesha kama binaadamu, alilitupa jiwe na kutimua mbio.Tulivyomuona mara ya kwanza alikuwa anayumba lakini sasa baada ya kupata hofu aliweza kukimbia sawasawa huku akipiga kelele  “Jamani nakufaa….jamani nakufaa……!”

“Twende zetu” Chausiku akaniambia

Tukaendelea na safari

Tulipofika kiwanjani tulikuta wenzetu wamekwisha fika.Tulikuwa sisi wawili tu tuliokuwa na miili ya paka.Wenzetu wote walikuwa na miili ya kibinaadamu

Jinsi walivyokuwa wanawahi kufika pale kiwanjani, nilihisi kulikuwa na wengine hawalali majumbani kwao kwa kusubiri saa nane waje pale kiweanjani

“Nilikuwa nawasubiri nyinyi” bibi akatuambia

“Kulikoni bibi?” Chausiku akamuuliza.Tulikuwa bado katika maumbo yaleyale ya paka

“Nataka mimi na nyinyi na bi Chaurembo twende katika lile duka la mwaarabu tukammwagie kimavi. Hatutaki aweke duka lake hapa kijijini kwetu”

“Twendeni” Chausiku akamuambia

Bibi akawageukia wale wachawi wengine tuliowakuta

“Sasa mgawanyike katika vikundi  viwili, mwende katika kazi nilizowatuma” akawaambia

Wachawi hao wakajigawa katika vikundi viwili.Kila kikundi kikashika njia yake.

Kilibaki kikundi chetu cha watu wanne.Bibi akamuambia bi Chauermbo na wao wajigeuze paka kama sisi twende huko kwa mwaarabu

Hapo hapo na wao wakageuka paka. Bibi akatuongoza njia,tukamfuata

Kama mtu yeyote angetokea usiku huo na kutuona tulivyojipanga mstari lazima angeshuku kuwa tulikuwa wanga na angetukimbia

Tulipofika kwenye hiyo nyumba iliyokuwa na duka tulikuta taa ikiwaka nje.Hapo nilijifunza kitu tofauti tukiwa na miili ya kipaka. Tulianza kucheza huku bibi na bi Chaurembo wakitoa sauti za kipaka zinazotisha

Baada ya kucheza kwa karibu dakika tano, tulianza kujipenyeza ndani ya duka hilo.Alianza bibi, akafuatia bibi Chaurembo, halafu mimi na Chausiku. Bibi na bi Chaurembo pamoja na mke wangu walilisotea duka hilo na kujaza kinyesi kila mahali.Wakati wakifanya hivyo walikuwa wakitoa sauti za kunuizia kuharibu biashara katikia duka hilo

“Tunalisotea duka hili liingie nuksi, mwarabu asipate biashara.Asije mtu yeyote kununua kitu hapa.Duka hili life kabisa na mwenyewe afilisike arudi kwao……..”

Ndiyo maneno waliyokuwa wakisema bibi na bi Chaurembo kwa sauti zao za kipaka bila kujali kama kelele zao zilikuwa zinasikiwa.

Tulipotoka hapo dukani tulijipenyeza ukumbini. Huku nako bibi na bi Chaurembo walieneza kinyesi

“Sasa twendeni zetu.Kesho tukija tutawaingilia vyumbani tuwawangie mpaka wahame” bibi akatuambia

Tukarudi kwenye duka kisha tukatoka na kurudi kiwanjani

Tulipofika kiwanjani bibi akajigeuza mtu na kuanza kucheka.Chausiku naye akageuka mtu, nikafuatia mimi kisha bi Chaurembo

Vilikuwa vicheko vitupu.Mimi tu ndio sikuwa nikicheka.Sikuona la kunifurahisha. Bibi na bi Charembo wakawa wanajisifia kuwa watamuonyesha yule mwarabu

Kumbe wachawi baada ya kufanya uovu hufurahia kwa vicheko kama watu waliofanya jambo la maana lenye kuleta tija.

Wachawi wenzetu walipofika, kila kikundi kikawa kinahadithia juu ya kazi waliyokwenda kuifanya.Baadaye bibi akawapa pongezi kisha akaamrisha tucheze ngoma.Tukacheza ngoma yetu ya kichawi.

JE NINI KITAENDELEA KUTOKEA? ENDELEA KESHO usikose kufuatilia hadithi hii ya kusisimua hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment